ARUSI

 

Bisimilahi naanza

Jina la Mola Muweza

Tupate kuyatimiza

Haya tulokusudiya

 

 

Bisimilahi Karimu

Mola wetu Muadhamu

Sherehe tuihitimu

Na furaha kutimiya

 

 

Arusi yetu ifane

Wazee wasikizane

Wote washirikiane

Na waliohudhuriya

 

 

Tupate kufarajika

Tufurahi na kucheka

Vifijo na hekaheka

Sote tukishangilia

 

 

Bi arusi kanawiri

Bwana arusi mzuri

Wan'gara kama qamari

Mwezi unapotimiya

 

 

Mola uwape fanaka

Wazidishiye Baraka

Uwape wanavyotaka

Vya akhera na duniya

 

 

Ya Rabi Mola Karimu

Waja wako wakirimu

Watuze kila adhimu

Daima na abadiya

 

 

Waowane wapendane

Huruma waoneane

Waishi wasikizane

Kwa uwezo wa Jaliya

 

 

Rabi wajaze furaha

Waepushe na karaha

Waishi waone raha

Wawe mbali na udhiya

 

 

Nyumba uijaze kheri

Iwe baidi na shari

Na ibada zikithiri

Faradhi na sunnah piya

 

 

Uwaruzuku na wana

Wengi wenye kupendana

Waishi na kuwaona

Wajukuu na dhuriya

 

 

Watoto wenye bashasha

Wengi wanofurahisha

Wacheze na kuchekesha

Na wazee kuridhiya

 

 

Watoto wawe kathiri

Wenye imani wa kheri

Wenye kutii amri

Yako Allah na Nabiya

 

 

Na haki zitambulike

Za mume na mwanamke

Wazijuwe wazishike

Zisije zikapoteya

 

 

Nasiha kwako bibiye

Tuliya uyasikiye

Tena uyazingatiye

Haya ninayokwambiya

 

 

Mumeo usimuudhi

Haja zake uzikidhi

Siri zake zihifadhi

Mtu usije mwambiya

 

 

Uso uwe mkunjufu

Maneno yawe latifu

Kwake uwe mtiifu

Pasipo na maasiya

 

 

Asikalie kitanda

Mumeo asompenda

Katu usifanye inda

Maudhi kumleteya

 

 

Hayo ukijihimiza

Na swala ukatimiza

Janna atakuingiza

Mola Atakuridhiya

 

 

Ya Rabi Mola Karima

Waishi wote kwa wema

Kwa mawada na rehema

Nyumba yote kueneya

 

 

Na wewe bwana arusi

Usijifanye mkwasi

Mkeo ukamtusi

Kiburi kumfanyiya

 

 

Usije mtia dhiki

kwani huyo makhluki

Aso kile ana hiki

Hapana alotimiya

 

 

Huyo ni kwako amana

Ulopewa ewe bwana

Kwa neno la Subuhana

Mke ulimpokeya

 

 

Umpe  kila naimu

Mkirimu muheshimu

Asokirimu laimu

Ni muovu wa tabiya

 

 

Haki yake umlishe

na kwa wema umvishe

Umlishe umvishe

Na wema kumtendeya

 

 

Msipende kubishana

Wala kulaumiana

Na pia kununiana

Baraka inakimbiya

 

 

Ukipenda kulaumu

Wapunguza hitiramu

Hapana mwana adamu

Mja asiyekoseya

 

 

Ghadhabu hazina kheri

Ndani yake mna shari

Udhaifu wa bashari

Shetani anaingiya

 

 

Zinapozidi ghadhabu

Murudi kwa wenu Rabu

Madhambi yenu mutubu

Mola atawaridhiya

 

 

Ugomvi wote nyumbani

Unaletwa na shetani

Kwa haraka mumlani

Na murudi kwa Jaliya

 

 

Ili apate ondoka

Mutawadhe kwa haraka

Muziswali mbili raka

Mbiyo atatokomeya

 

 

Rabi wajaze imani

Waipende Quruani

Maneno yaso kifani

Mola ulotuleteya

 

 

Wasikiapo mwadhini

Waende misikitini

Wasiziswali nyumbani

Swalatu za far'dhiya

 

 

Kuswali msikitini

Bora kuliko nyumbani

Ni saba uishirini

Daraja wajipatiya

 

 

Muzifuate kwa wema

Hizi ni nasaha njema

Bwana pia mwanamama

Hallah hallah nausiya

 

 

Ya Rabi Uwaongoze

Nyoyo zao Uzipoze

Ya nje wasisikize

Siri ziwe dakhiliya

 

 

Nyumba yao isitiri

Nyuso zao zinawiri

Miili iwe tahiri

Siha njema na afiya

 

 

Imani ijizatiti

Na nyoyo ziwe thabiti

Shetani wamdhibiti

Asiweze kuwangiya

 

 

Rabi jicho la hasidi

Liweke mbali baidi

Kwao lisipige hodi

Wala hata kusogeya

 

 

Amina Rabi amina

Amina Rabi amina

Amina Rabi amina

Dua tutakabaliya