Bidah Inayopambana Na Sunnah

 

Muhammad Faraj Salem Al Saiy

 

 

 

 

Shukrani zote ni Zake Allaah Subhanahu wa Taala, tunamshukuru, tunategemea kwake msaada, na tunajikinga kwake kutokana na shari za nafsi zetu na amali zetu ovu. Yule ambaye Mwenyezi Mungu Atamuongoza basi hapana wa kumpoteza, na yule Atakayemhukumu kumpotosha (kwa kukataa kwake uongofu), basi hapana wa kumuongoza.

Nashuhudia kuwa hapana anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Allaah, Pekee Asiye mshirika, na kwamba Muhammad (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) ni Mtume wake na mjumbe wake na kipenzi chake na mbora wa viumbe vyake.

Amma baad,

Hakika ya maneno ya kweli kupita yote ni kitabu cha Mwenyezi Mungu, na muongozo ulio bora ni wa Muhammad (Swalla Llaahu alayhi wa sallam), na shari ya mambo ni kuzuwa mepya katika dini, na kila uzushi ni Bidah na kila Bidah ni upotovu na kila upotovu mahali pake ni Motoni.

 

Wenye Kupinga Bidah

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alikuwa mwanzo wa hutuba zake akitamka maneno haya: "Na shari ya mambo ni kuzuwa mepya (katika dini), na kila uzushi ni Bidah na kila Bidah ni upotovu na kila upotovu mahali pake ni Motoni."

Na hii ni dalili ya hadhari aliyokuwa akiichukuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kwa kuwakataza umati wake kuzuwa mambo mepya katika dini.

Waislamu wote wanakubaliana kuwa tumekatazwa kufanya kitendo cha Bida'h, nayo ni kuzuwa mambo katika dini ambayo Mwenyezi Mungu hajayatolea amri Yake. Hitilafu iliyokuwepo ni kuwa wengine wanasema ipo Bida'h njema na Bida'h potovu, wakati wengine wanasema kuwa Bida'h zote ni potovu kwa sababu Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema: "Kila uzushi ni Bidah."

 

Kutoka kwa Al-Irbaadh bin Saariyah (Radhiya Llaahu anhu) kuwa amesema:

"Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) alitutolea mawaidha yaliyotutoa machozi na kuzilainisha nyoyo. Tukamuuliza: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, haya ni (mfano wa) mawaidha ya kutuaga, kwa hivyo nini unatuusia?" Akasema: "Nimekuacheni juu ya weupe, (juu ya kitu kisafi) usiku wake sawa na mchana wake, hapotoki akatoka humo isipokuwa mwenye kuangamia. Na atakayeishi miongoni mwenu ataona khitilafu nyingi, basi fuateni mliyokwishayajuwa katika Sunnah yangu (mafundisho yangu), na mafundisho ya Makhalifa wema waongofu watakaokuja baada yangu. Yakamateni kwa magego."

(At-Tirmidhiy, Abu Daawuud, Imam Ahmad na wengine.)

 

Na akasema:

"Atakayezusha katika amri yetu hii (dini yetu) lisilokuwemo anarudishiwa. (halikubaliwi).

(Al-Bukhaariy na Muslim)

 

Wenye kupendelea kufanya sherehe za Maulidi wanatafsiri kitendo cha wenzao wenye kuyapinga kwa kukataa kuisherehekea siku hii kuwa ni watu wasiompenda Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam).

Bila shaka kadhia hii si nyepesi kama inavyodhaniwa, na pia kukifasiri kitendo cha kukataa kuisherehekea Maulidi kuwa ni kutompenda Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) ni katika mambo ya ghushi na kuufumbia macho ukweli.

Ukweli ni kuwa mwenye kukataa kuisherehekea siku hii anakataa kwa ajili ya kuogopa kufanya kitendo cha uzushi ambacho yeye mwenyewe (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) hajapata kukifanya.

Ni kitendo kinacholeta khitilafu nyingi baina ya Waislamu, na si katika Sunnah yake (mafundisho yake) kama alivyotamka Swalla Llaahu alayhi wa sallam, na hakijawahi kutendwa na yeyote kati ya Makhalifa wema waongofu waliokuja baada yake.

 

Mwenye kuacha kufanya kitendo kilichozushwa kwa sababu ya kuhofia kuingia makosani, bila shaka huyo hawezi kutuhumiwa wala kulaumiwa, bali kinyume chake ni kuwa mtu huyo yupo katika usalama kuliko mwenye kufanya kitendo ambacho asili yake hata kama atakiacha hatopata dhambi, kwa sababu hapana amri yoyote katika dini juu kitendo hicho.

 

Katika hadithi niliyotangulia kuitaja, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) alisema:

"Nimekuacheni juu ya weupe, (juu ya amri kisafi) usiku wake sawa na mchana wake, hapotoki akatoka humo isipokuwa mwenye kuangamia."

 

Kwa hivyo mwenye kuiacha sherehe hiyo au kitendo chochote kingine kilichozushwa katika dini kwa ajili ya kuogopa asije akaingia katika Bidah, huyo anajiepusha na "khitilafu nyingi" alizozitaja Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam), na anasalimika, kwa sababu anajiweka juu ya weupe aliotuwachia juu yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam).

 

Kauli Za Baadhi Ya Maulamaa

Mwenyezi Mungu Anasema:

(( )) [: 3].

Leo nimekukamiliishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni UISLAMU uwe ndiyo Dini.

(Al-Maaidah: 3)

 

Maulamaa wanasema: "Kile ambacho siku ile ilipoteremshwa aya hii hakikuwemo katika dini, basi leo hakiwezi kuwemo pia. Mwenyezi Mungu keshaikamilisha dini yake na hakiwezi kukubalika tena kipya isipokuwa kile tu aliochotuletea Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam)."

 

Amesema Imam Ash-Shawkaaniy:

"Ikiwa Mwenyezi Mungu Keshaikamilisha dini Yake kabla hajaichukuwa roho ya Mtume Wake, sasa ni kipi tena hiki wanachokizuwa baada ya kukamilika kwake?

Na ikiwa wanaamini kuwa ni katika dini, basi huko ni kutuhumu kuwa dini haijakamilika.

Na ikiwa wanaamini kuwa si katika dini, basi pana faida gani kujishughulisha na (kuliendeleza) jambo lisilokuwemo katika dini?"

(Qawl al Mufiyd uk. 38)

 

Bidah Njema Na Bidah Ovu

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) amesema:

"Kila uzushi ni Bidah na kila Bidah ni upotovu."

 

Na akasema:

"Atakayeanzisha mwenenedo mwema " katika Uislamu atapata ujira wake na ujira wa atakayetenda wema huo hadi siku ya Qiyaamah bila ya kupungua kitu katika ujira wa waliotenda, na atakayeanzisha mwenendo mbaya atapata madhambi yake na madhambi ya atakayetenda madhambi hayo hadi siku ya Qiyaamah bila ya kupungua kitu katika madhambi yao ".

(Muslim na At-Tirmidhy na An-Nasaiy na wengine)

 

Wengine wakaifahamu vibaya hadithi hii, wakadhani kuwa; kwa vile pana kitu kinachoitwa: " Sunnatun Hasanah (Sunnah njema), kwa hivyo bila shaka mkabala wake ipo pia Bidatun Hasanah' (Bidah njema), wakati ukweli ni kuwa hapana kitu kama hicho katika dini.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) amesema: "Kila uzushi ni Bidah." Kisha akarudia tena, akasema: "Na kila Bidah ni upotovu."

Amelitamka neno 'KILA' mara mbili katika sentensi moja, kwa ajili ya kusisitiza juu ya umuhimu wake, kwani angeliweza kusema: 'Kila Bidah ni uzushi na upotovu.' Bila ya kulirudia neno 'KILA' mara ya pili.

 

Inaeleweka wazi kuwa katika hadithi hii Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) anazungumza juu ya Sunnah njema na siyo Bidah njema, kwa hivyo hapana haja ya kuiunganisha hadithi hii na mambo mawili haya yenye kutofautiana.

 

Huenda ikawa wanajaribu kuiunganisha hadithi hii na ile kauli ya Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Llaahu anhu) aliposema: "Niimat al Bidah haadhihi", (kauli ambayo tutaisherehesha kila tukiendelea mbele InshaAllaah).

 

Baadhi ya Maulamaa wakasema: "Mtu atakayeisimulia hadithi hii ya "Atakayeanzisha mwenendo mwema ... kwa nia ya kuipitisha Bidah yake, kisha asikielezee kisa kilichomfanya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) ayatamke maneno haya, basi huyo anakuwa sawa na mtu aliyeisoma kauli ya Mwenyezi Mungu:

Basi ole wao wanaoswali

Kisha akanyamaza, asiikamilishe kauli hiyo kwa kusoma:

 

Ambao wanapuuza Swala zao

 

Ili kuifahamu vizuri hadithi hii lazima tukisimulie kisa kilichomfanya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) atamke maneno yale.

 

Kutoka kwa Jurayr bin AbdiLlaah (Radhiya Llaahu anhu) amesema:

"Lilikuja kundi la watu wa kabila la kibedui (kabila la Madhr) wakiwa wamevaa nguo zilizoraruka, hawana viatu, na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) akaiona hali yao kuwa walikuwa na shida. Akamuamirsha Bilaal aadhini, kisha ikaqimiwa Swalah, na baada ya kuswali Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) akawahutubia watu na kuwahimiza kuwapa sadaka watu hao. Watu wakakawia kufanya hivyo mpaka ilionekana (huzuni) katika uso wake. Kisha mtu mmoja katika watu wa Madiynah akatoa sadaka Dinari zake na wengine wakaanza kutowa Dirham na wengine nguo zao na wengine pishi za ngano na wengine tende, kisha mwengine akaleta bahasha aliloshindwa kulibeba kisha watu wakafuatiliana mmoja baada ya mwingine mpaka yakaonekana marundu mawili ya nguo na chakula mpaka nikauona uso wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) ukingara kwa furaha ndipo aliposema:

"Atakayeanzisha mwenendo mwema " katika Uislamu atapata ujira wake na ujira wa atakayetenda wema huo hadi siku ya Qiyaamah bila ya kupungua kitu katika ujira wa waliotenda, na atakayeanzisha mwenenedo mbaya atapata madhambi yake na madhambi ya atakayetenda madhambi hayo mpaka siku ya Qiyaamah bila ya kupungua kitu katika madhambi yao ".

(Muslim na At-Tirmidhy na An-Nasaaiy na wengine)

 

Anasema Imam Ash-Shaatwibiy:

"Katika hadithi hii, neno kuanzisha hakujakusudiwa kwa maana ya kuvumbuwa au kuzusha, bali kumekusudiwa kuhuisha matendo yaliyothibiti kuwa yamewahi kutendwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam), na dalili ni kuwa kilichomfurahisha Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) ni kitendo cha kutoa sadaka kwa wingi, na la pili ni aina ya sadaka; marundu ya nguo na marundu ya vyakula.

Kwa hivyo sadaka haiwezi kuwa katika uzushi (Bidah), kwa sababu uzushi ni katika matendo yasiyokubaliana na sheria, kinyume na sadaka."

(Imam Ash-Shaatwibiy Al-Itiswaam juz. 1, uk. 233)

 

 

Basi Na Hii Bidah Pia

Haiwezekani pasemwe kuwa pana Bidah njema katika dini, kwa sababu vitu hivi viwili haviwezi kwenda sambamba hata siku moja haviwezi kukubaliana, hasa kwa vile Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) keshatamka kuwa:

"Kila uzushi ni Bidah na kila Bidah ni upotovu."

 

Kauli hiyo imetamkwa na kiumbe mwenye ulimi fasaha kupita ndimi zote zilizoumbwa na Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala), na ni kiumbe mwenye kuelewa vizuri kile anachokitamka. Kwa hivyo haikubaliki tena aje mtu atuambie kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) hajakusudia kuwa Kila uzushi ni Bidah, bali ipo Bidah njema na nyengine potovu.

Huenda mtu akaliona jambo lake kuwa ni zuri akadhania kuwa ni Bidah na lisiwe Bidah, au huenda akaipenda Bidah yake akiona kuwa ni njema lakini haiwezi kuwa njema. Lakini mtu anapokiri kuwa kitendo fulani ni Bidah, kisha aseme kuwa ni Njema, hilo ni jambo lisilowezekana.

 

Mwengine atasema: "Kujenga shule pia ni Bidah hasanah, kwa sababu wakati wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) hapakuwa na shule." Tunamuambia kuwa kweli hilo ni jambo jema, lakini hicho sicho alichokusudia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam), bali alichokusudia ni Bidah katika mambo ya dini aliposema: "Atakayezusha katika amri yetu hii (na maana yake ni amri ya dini yetu)."

Kujenga shule ni katika wasila, ni njia ya kuifikisha elimu na siyo elimu yenyewe ambayo ni ibada, kama vile microphone 'kipaza sauti' ni wasila, njia ya kuifikisha sauti ya Qur-aan na hotuba kwa watu, na Qur-aan na hotuba ndiyo ibada, na watu wanapopanda gari kwenda Makkah, hilo gari ni wasila, njia ya kuwafikisha watu, lakini siyo ibada, ibada ni kule kuhiji na kufanya Umrah.

Kwa hivyo mtu anapojenga shule hakusudii kuwa lile jengo ni ibada, bali jengo ni njia ya kuifikisha elimu kwa wanafunzi, na anapoingiza vipaza sauti Msikitini hakusudii kuwa chombo kile ni ibada bali ni njia tu ya kuwafikishia watu sauti, kama vile mtu anapopanda gari kwenda kuhiji, anajua kuwa gari lile si ibada bali ni njia ya kumfikisha kwenye ibada anayoitaka. Na hii ndiyo njia wanayotumia Maulamaa katika kutoa hukmu.

 

Wakati mwenye kuleta Bidah yake, huyo anakusudia kuwa ni ibada, kwa kuiwekea njia yake ya kufanya na makatazo yake na kuvumbua ndani yake mambo mengi yasiyoteremshiwa amri ya Mwenyezi Mungu juu yake.

 

 

"Niimat Al-Bidah Haadhihi"

Kutokana na ile kauli ya Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Llaahu anhu) aliposema: "Niimat al-Bidah haadhihi" Mtu anaweza kusema kuwa ipo Bidah njema.

Ukweli ni kuwa Umar hapa alilikusudia neno Bidah kwa maana ya kilugha na si kwa maana ya Fiq'hi. Inajulikana kuwa katika kamusi ya Fiq'hi, neno Bidah lina maana nyingine tofauti na maana ya neno hilo katika kamusi ya lugha.

Neno 'Bidah' katika lugha ni neno zuri sana, kwani maana yake ni uvumbuzi wa mambo, kama vile madawa na mambo ya idara na ziraa nk. Lakini neno hilo hilo 'Bidah' katika dini maana yake ni mbaya, lakini katika mambo ya kidunia, Bidah ni kitu kizuri. Ndiyo maana mtu katika dini akiambiwa kitendo ulichofanya ni Bidah hukasirika, lakini anapoanzisha kitu kipya katika mambo ya kidunia akaambiwa "Ni Bidah nzuri sana hiyo," hufurahi sana.

Inajulikana pia kuwa katika lugha ya Kiarabu neno moja linaweza kubeba maana moja katika kamusi ya lugha, na neno hilo hilo likabeba maana nyingine katika kamusi ya Fiq'hi ya dini, kwa mfano:

Neno Swalah, katika lugha ya Kiarabu maana yake ni duaa, na neno hilo hilo katika kamusi ya Fiq'hi maana yake ni; ibada inayoanza kwa takbira na ina maneno na vitendo maalum ndani yake na inamalizika kwa kutoa salaam.

Neno Zakaah, katika kamusi ya lugha ya Kiarabu maana yake ni kujitakasa, na neno hilo hilo katika kamusi ya Fiq'hi ni ile; mali anayopewa masikini baada ya kukamilisha muda maalum. Katika maudhui haya, sisi tunazungumza juu ya Bidah katika kamusi ya dini.

Zipo sababu mbali mbali zinayoifanya ile kauli ya Umar (Radhiya Llaahu anhu) kuwa aliikusudia kilugha, na siyo kidini:

Sababu ya kwanza ni kuwa kitendo cha Umar kuirudisha tena Swalah ya Taarawiyh katika mwezi wa Ramadhaan si kitendo cha Bidah kisheria kwa sababu kitendo hicho kilifanywa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) alipowaswalisha Maswahaba muda wa siku tatu, kisha akaacha kwa sababu alihofia isije ikafaridhishwa na kuwa nzito kwao. Baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) kufariki dunia, Umar (Radhiya Llaahu anhu) akairudisha tena Swalah ile kwa sababu hapakuwepo tena na ile hofu ya kufaridhishiwa, ndipo Umar alipofurahi alipowaona watu wote wamesimama nyuma ya Ubay bin Kaab wakiswali jamaah, akasema: "Niimat al-Bidah haadhihi." Hii haikuwa Bidah kisheria, bali ilikuwa ni kuihuisha Sunnah iliyoanzishwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) aliyewahi kuwaswalisha mara tatu kisha akaacha kwa sababu iliyotoweka baada ya kufariki kwake (Swalla Llaahu alayhi wa sallam), na yeye Umar akaweza kuirudisha tena.

 

Na sababu ya pili ni kuwa kitendo cha Umar (Radhiya Llaahu anhu) hakiwezi kuwa cha Bidah hata kama kitendo hicho atakianzisha yeye, na hii inatokana na kauli ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) katika hadithi iliyotangulia kutajwa aliposema:

"Fuateni mliyokwishayajuwa katika Sunnah yangu (mafundisho yangu), na mafundisho ya Makhalifa wema waongofu watakaokuja baada yangu. Yakamateni kwa magego."

Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Llaahu anhu) ni katika Makhalifa wema waliokuja baada yake, kwa hivyo Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) ameturuhusu kufuata mafundisho yao.

 

Tunamaliza kwa kusema kuwa Bidah ya kisheria, Bidah katika dini, kwa maana ya kuzusha jambo jipya ambalo Mtume (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) hakuwahi kulitenda haiwezi kuwa njema hata siku moja.

 

Anasema Mwanachuoni Faqiyh, Muhammad bin Swaalih bin Uthaymiyn (Mwenyezi Mungu Amrehemu):

"Mtu aingie msikitini kwa mfano, awakute watu wanaswali Sunnah zao kila mmoja peke yake kama kawaida wakimsubiri Imam awaswalishe jamaah, kisha mtu huyo awaambie watu: 'Jamani mnaonaje tukaswali Sunnah jamaah kwa pamoja badala ya kila mtu peke yake."

Watu bila shaka watamuambia: "Unataka kutuletea uzushi gani tena?" Yule mtu atawaambia: "Hapana, si uzushi kwani tunamswalia nani? Si tunamswalia Mwenyezi Mungu? Isitoshe, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) keshawahi kuswali Swalah za Sunnah jamaah, kama vile Swalah za Tahajjud na aliwahi pia kuswali Taarawiyh na akaswali Swalah za kupatwa kwa jua na pia mwezi na aliswali Swalah za Iyd jamaah, na zote hizo ni Sunnah."

Watu bila shaka watamjibu: "Lakini jambo hili unalotuita ndani yake halijawahi kufanywa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam)."

Na hapa ndipo penye hekima yote," anaendelea kusema Mwnachuoni huyo Ibn Uthaymiyn (Mwenyezi Mungu Amrehemu), "nayo ni kuwa kitendo chochote katika dini asichowahi kukifanya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) au kutuamrisha kukifanya basi hiyo ni baatwil, hata kama ni Swalah ya kumswalia Allaah!