KUHITILAFIANA

Inajulikana wazi kabisa na kila mtu kuwa; Watu wanahitilafiana katika fikra zao. Mwanadamu tokea alipoumbwa alikuwa akiutizama ulimwengu kwa mtazamo wake, kila mmoja kwa mtazamo wake na kwa falsafa yake. Na kwa ajili hiyo wakakhitilafiana katika mtazamo wao, katika kupenda kwao na katika kuchukia kwao. Na kila ulimwengu unapopiga hatua katika maendeleo, katika majenzi, katika kupanuka kwa miji, hitilafu za wanadamu zinaongezeka na kupanuka. Na kwa ajili hiyo zikatokea hitilafu mbali mbali za ki Madhehebu ya kifalsafa, hitilafu za kijamii na za kiuchumi.

Mmoja katika wana falsafa wa zamani anasema;

“Haki yote, haiwezekani ikamilikiwa na upande mmoja , wala kukosewa yote na upande mwingine, bali kila upande husibu sehemu yake. Mfano wake ni mfano wa kundi la watu vipofu waliotakiwa kwa muda mfupi sana wamwendee tembo na kumgusa, kisha wamuelezee jinsi alivyo.

Yule aliyeshika mkongwe, akasema;

“Mwili wa tembo uko duara mfano wa gogo la mti”,

Aliyeushika mgongo akasema;

“Mwili wa tembo upo mfano wa jabali dogo”,

Aliyeshika sikio akasema;

“Mwili wa tembo mpana pana duara na laini”.

Na hivyo hivyo kila mmoja atauelezea mwili wa Tembo kiasi alivyodiriki kuugusa. Kila mmoja kati yao anasema kweli, lakini anaelezea kinyume na mwenzake na kudhani kuwa anavyojuwa yeye ni sahihi na kwamba wenzake wamekosea.

Tizama jinsi gani ukweli ulivyowaunganisha na tizama jinsi gani kukadhibishana kulivyowatenganisha.

Kila mmoja alivyoisibu sehemu tu ya haki na kudhani kuwa yeye ndiye mwenye kuijua yote.”

Hitilafu husababishwa na mambo mengi, yakiwemo kupenda, matamanio ya nafsi, mielekeo ya elimu, ya kifikra, kuiga waliotangulia, kupenda umaarufu, kupenda ukubwa, hitilafu za ustaarabu na ziko sababu nyingi nyingine na maelezo yake ni mengi sana tutayazungumzia siku za usoni Inshaallah itapohitajika.

 

MUHAMMAD FARAJ SALEM AL SAIY