KWA ELIMU YAO WALITAMBA

Imeandikwa katika kitabu kiitwacho 'Tuhufatul Ahawazi kilichoandikwa na mwanachuoni maarufu AlMubarak Furry - mlango wa 1804 kama ifuatavyo;

 

"Yafuatayo ni maelezo yaliyoandikwa na Ibnu Salah katika utangulizi wa hadithi alizosimuliwa na Al Zuhuriy kuwa alimwambia;

"Nilikwenda kwa Abdul Malik bin Marawan (Khalifa wa Waislam wakati wa utawala wa Bani Umayyah) akaniuliza;

'Unatokea wapi ewe Al Zuhuriy?'

Nikamwambia;

'Natokea Makkah'

Akaniuliza;

'Umemuacha nani mwenye kupendwa na mwenye kufuatwa huko Makkah?'

Nikamwambia;

"Ataa bin Abu Rabah.'

Akaniuliza;

"Ni katika waarabu huyu au katika watumwa walioachwa huru?'

Nikamwambia;

'Ni katika watumwa walioachwa huru.'

Akaniuliza;

'Sababu gani zilizomfanya apendwe na kufuatwa?'

Nikamwambia;

'Elimu yake ya dini na riwaya.'

Akasema;

'Hakika wenye elimu ya dini na riwaya ndio wanaopaswa kupendwa na kufuatwa.'

Akaniuliza tena;

'Nani mwenye kupendwa na kufuatwa katika nchi ya Yemen?'

Nikamwambia;

'Taus bin Kiysan'.

Akaniuliza;

'Ni katika waarabu huyu au katika watumwa walioachwa huru?'

Nikamwambia;

'Ni katika watumwa walioachwa huru.'

Akaniuliza;

'Sababu gani zilizomfanywa apendwe na kufuatwa?'

Nikamwambia;

'Sababu zile zile zilizomfanya Ataa apendwe na kufuatwa.'

Akaniuliza;

'Nani mwenye kupendwa na kufuatwa huko Misiri?'

Nikamwambia;

'Yazid bin Abu Hubayb.'

Akaniuliza;

'Ni katika waarabu huyu au katika watumwa walioachwa huru?'

Nikamwambia;

'Ni katika watumwa walioachwa huru.'

Akaniuliza;

'Nani mwenye kupendwa na mwenye kufuatwa huko Syria?'

Nikamwambia;

'Makahool.'

Akaniuliza;

'Ni katika waarabu huyu au katika watumwa walioachwa huru?'

Nikamwambia;

'Ni katika watumwa walioachwa huru, alikumwa mtumwa katika Wanubi aliyeachwa huru na mwanamke wa kabila la Hudhayl.'

Akaniuliza;

'Nani mwenye kupendwa na kufuatwa katika Bara ya Arabu (Arabian peninsula)?'

Nikamwambia;

'Maymun bin Maharan'

Akaniuliza;

'Ni katika waarabu huyu au katika watumwa walioachwa huru?'

Nikamwambia;

'Ni katika watumwa walioachwa huru.'

Akaniuliza;

'Nani mwenye kupendwa na kufuatwa huko Khurasan?'

Nikamwambia;

'Al Dhahaaq bin Muzahim.'

Akaniuliza;

'Ni katika waarabu huyu au katika watumwa walioachwa huru?'

Nikamwambia;

'Bali katika watumwa walioachwa huru.'

Akaniuliza;

'Nani mwenye kupendwa na kufuatwa katika nchi ya Basra?'

Nikamwambia;

'Al Hassan bin Abul Hassan'.

Akaniuliza;

'Ni katika waarabu huyu au katika watumwa walioachwa huru?'

Nikamwambia;

'Bali katika watumwa walioachwa huru.'

Akaniuliza;

'Nani mwenye kupendwa na kufuatwa katika nchi ya Al Koufa?'

Nikamwambia;

'Ibrahim Al Nakhaiy'.

Akaniuliza;

'Ni katika waarabu huyu au katika watumwa walioachwa huru?'

Nikamwambia;

'Ni katika waarabu.'

Akanambia;

'Umenipumzisha ewe Al Zuhriy! wallahi waliokuwa watumwa watatamba na kusikilizwa na kuwashinda waarabu mpaka utafika wakati wao watapanda juu ya membari na waarabu watakuwa chini yao wakiwasikiliza.'

Nikamwambia;

'Ewe Khalifa wa Waislamu! Hii ni amri ya Mwenyezi Mungu. Mwenye kuihifadhi ndiye atakayefuatwa na mwenye kuipoteza ataanguka.'