KUKUNJA MIKONO KATIKA SALA

Muhammad Faraj Salem  Al Saiy


 
Kukunja mikono si kitendo kilichotendwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallahu Llahu alayhi wa Sallam) peke yake, bali alikuwa akisisitiza na kuwasahihisha wale waliokuwa wakikunja mikono yao ndani ya Sala kinyume na inavyotakiwa.
Anasema Imam Malik (Mwenyezi Mungu amrehemu) katika kitabu cha Al Muwatta, na huyu ni Imam wa watu wa Madina mji alioishi na kusali ndani yake Mtume wa Mwenyezi Mungu zaidi ya miaka kumi, na Masahaba wake watukufu (Radhiyallahu 'anhum) wakaendelea kusali hapo miaka mingi iliyofuata.
Katika ukurasa wa 122 na 123 mlango wa "Mwenye kusali aweke mkono mmoja juu ya mwengine",  imeandikwa katika kitabu hicho cha Imam Malik katika hadithi nambari 133 kama ifuatavyo;
"Katika maneno ya Mitume ni kuwa usipokuwa na haya basi fanya utakalo, na
pia (katika maneno ya Mitume) ni kuweka mkono mmoja juu ya mwengine katika Sala.
"
Haya ni maneno ya Imam Malik ndani ya kitabu chake cha Al Muwatta.
Na katika kitabu hicho hicho cha Al Muwatta Imam Malik ameandika hadithi
kutoka kwa Sahl bin Saad Al Saaidiy kuwa; Watu walikuwa wakiamrishwa kuweka mkono wao wa kulia juu ya mkono wa kushoto katika Sala."
Anasema Abu Hazim;
"Naelewa kuwa anakusudia hapa wakati wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallahu Llahu alayhi wa Sallam)".
Bukhari Juz. 1 ukurasa wa 397 Imam Malik katika Muwataa na Imam Ahmed katika
Musnad
Na katika kuisherehesha hadithi hiyo amesema Imam Malik (Mwenyezi Mungu amrehemu);

"Kuweka (mkono) wa kulia juu ya kushoto na kuharakisha futari na kuchelewesha daku."

Haya ameyasema katika kuisherehesha hadithi iliyotangulia ya Abil Mukhariq.

 

Abil Mukhariq

Baadhi ya watu wakasema kuwa katika hadithi iliyomo ndani ya Muwatta yumo Abil Mukhariq na huyu anajulikana kuwa ni dhaifu katika elimu ya hadithi, lakini inaeleweka pia katika elimu ya hadithi kuwa udhaifu wa wapokeza unakhitalifiana darja, na kwamba daraja inayokubalika hadithi zao katika madhaifu ni wale waliodhoofishwa kwa ajili ya udhaifu wao wa kuhifadhi ikiwa wao si watu waongo wala si wenye kupenda kuongeza maneno.

Madhaifu wa aina hii anasema Dr. Mohd Ajjaj al Khatib katika kitabu chake cha 'Al Mkhtasar al wajiyz fiy Uluum al Hadiyth kuwa;

"Mtu aliyedhoofishwa kwa ajili ya kuhifadhi kwake, au kwa ajili ya kutoweza kudhibiti maneno vizuri, ikiwa hatuhumiwa kwa ila nyingine, na ikiwa zitapokewa hadithi zake kwa njia nyingi, basi hadithi itapanda na kufikia darja ya hadithi 'Hassan', na kwa ajili hiyo udhaifu wake unatoweka kwa kupokelewa hadithi kwa njia nyingine."

Anasema Imam Muhammad bin Al Hassan Al Sheibaniy kuwa;

"Anatuhumiwa Abil Mukhariq kwa udhaifu wake wa kuhifadhi tu."

 

Isitoshe ndani ya kitabu hicho cha Al Muwatta ipo pia hadithi iliyosimuliwa na Ibni Abbas (Radhiyallahu 'anhu) na kunukuliwa pia na Maimam Ahmed na Bukhari na wengineo, inayosema;

"Watu (wakati wa Mtume (Swallahu Llahu alayhi wa Sallam)) walikuwa wakiamrishwa kuweka mikono yao ya kulia juu ya kushoto katika Sala."

 

Hapana hadithi sahihi hata moja kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallahu Llahu alayhi wa Sallam) inayosema kuwa alikuwa akifanya kinyume cha hivyo, na hii ni kauli ya wengi sana katika Masahaba na Attabiina (Radhiyallahu 'anhum) na haya ndiyo aliyonukuu Imam Malik katika Muwattaa na hapana aliyenukuu maelezo kuwa Imam Malik alikuwa hafungi isipokuwa Ibnil Qassim.

 

Bidayatul Mujitahid

Yaliyoandikwa ndani ya kitabu cha Bidyatul Mujtahid si kukanusha kufunga mikono bali ni kuthibitisha, isipokuwa tu imenukuliwa ndani ya kitabu hicho kuwa Imam Malik amejuzisha kukunja katika sala ya Sunnah na hakujuzisha katika sala ya Fardhi akihofia watu wasiwe wanafunga kwa ajili ya kujipumzisha tu na wasidhani kuwa ni nguzo mojawapo ya Sala na kwamba Sala inabatilika iwapo mtu atafanya kinyume cha hivyo. (hii ikiwa kweli imethibiti kuwa Imam Malik amesema hayo), lakini yaliyomo ndani ya kitabu chake cha Al Muwatta ni kinyume na hayo.

 

Hadithi za Kukunja Mikono

Ama hadithi zinazoeleza juu ya kukunja mikono ni nyingi sana na zinapatikana katika kitabu 'Sifat Salaat Al Nabiy' cha Sheikh Al Albaniy (Mwenyezi Mungu amrehemu). Na pia ndani ya kitabu cha 'Al Qawl al Mubiyn fiy Akhtwaa al Musalliyn) kilichoandikwa na Sheikh Mashahur Hassan Suleiman na pia ndani ya kitabu cha Fiqhil Sunnah cha Sayed Sabiq na ndani ya vitabu vingi sana vya Fiqhi na vya Hadithi sahihi.

 


Na katika Sunan za Abu Daud hadithi iliyosahihishwa na Ibni Khuzaymah
inasema;
"Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallahu Llahu alayhi wa Sallam) alikuwa akiweka mkono wake wa kulia juu ya mkono wa kushoto."
Na katika hadithi iliyopokelewa na Attabarani na Ibni Habban, anasema
'Bahari ya elimu' Ibni Abbas (Radhiyallahu 'anhu) kuwa;
"Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallahu Llahu alayhi wa Sallam) amesema;

"Sisi Mitume tumeamrishwa kuharakisha kula futari zetu na kuchelewesha kula
daku letu, na kuweka mikono yetu ya kulia juu ya kushoto ndani ya Sala
."

Imepokelewa pia kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallahu Llahu alayhi wa Sallam) alipomuona mtu mmoja akisali huku ameuweka mkono wake wa kushoto juu ya mkono wa kulia, akauondoa na kuuweka wa kulia juu ya kushoto."
Ahmed na Abu Daud.
Na imepokelewa kutoka kwa Sahaba Abu Hurairah (Radhiyallahu 'anhu) kuwa katika Sala ya maiti Mtume wa Mweyezi Mungu alinyanyua mikono yake juu akasema 'Allahu Akbar', kisha akauweka mkono wake wa kulia juu ya wa kushoto."
Attirmidhiy katika 'Baab maa jaa fiy rafail yadayni.

Imepokelewa katika Sahih Muslim na kutoka kwa Imam Ahmed na Attabarani kuwa;
"Na alikuwa akiuweka mkono wake wa kulia juu ya sehemu ya nyuma ya mkono wa kushoto."

Katika mlango huu zimepokelewa hadithi zaidi ya ishirini kutoka kwa Masahaba kumi na nane pamoja na waliowafuatilia (Attabiina), zote hizo zikitoka moja kwa moja  kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallahu Llahu alayhi wa Sallam)

(Nanukuu kutoka katika kitabu cha 'Akhtaal Musalliyn' (makosa yanayofanywa
katika Sala) kilichoandikwa na Mashahur Hassan Suleiman) anasema:
Imepokelewa pia kutoka kwa Wail bin Hajar kuwa amesema;
"Kama kwamba namtizama Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallahu Llahu alayhi wa Sallam) namna alivyokuwa akisali", akasema:
"Nikamtizama! akatoa takbir, kisha akanyanyua mikono yake mpaka ikakaribia
masikio yake, kisha akauweka wa kulia juu ya upande wa nyuma wa mkono wa
kushoto
."
Ibni Khuzaymah katika sahih yake na Annasai na Abu Daud katika Sunan yake na Ahmad katika Musnad yake 4/318 na Ibni Majah katika Sunan yake 1/266 na Addarimiy katika Sunan yake 1/314 na Ibnil Jarood katika Al Muntaqa hadithi nambari 208 na katika vitabu vingi vingine".

Nadhani dalili hizi zinatosha kutujulisha kuwa kukunja mikono ni Sunnah
iliyothibiti ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallahu Llahu alayhi wa Sallam), lakini pia ninapaswa
kuhakikisha kuwa nimepitia vitabu vingi vya Fiqhi na sijaona hata mahali
pamoja palipoandikwa kuwa kutokunja mikono kunabatilisha sala.
Kukunja mikono si katika Masharti ya Sala wala si katika Nguzo zake wala si
katika Fardhi zake, bali hiyo ni katika Sunnah zake, mwenye kukunja anapata
thawabu na asiyekunja hapati dhambi, na Sala yake ni sahihi mia fil mia.
Wallahu taala aalam