MTOTO UMLEAVYO NDIVYO AKUAVYO

 

 

Muhammad Faraj Salim Al Saaiy

Tembelea http://mawaidha.info

 

Mtoto Umleavyo. 1

Mwangi 2

Faatwimah (Radhiya Llaahu Anha) 2

Mifano Mbali Mbali 3

Mtoto Ni Mfano Wa Chombo. 4

Uadilifu Baina Yao. 7

Kuwapa Moyo. 8

Kudekeza Sana. 9

Usia. 9

Ghadhabu. 11

Al-Ahnaf Bin Qays (Radhiya Llaahu Anhu) 12

Sababu Za Kuharibika Kwa Tabia. 12

 

 

Mtoto Umleavyo

 

Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo ni msemo maarufu, na wengine wanasema Mtu huvuna kile alichopanda.

 

Watoto wetu ndio vijana wa siku za mbele na viongozi wa mustakbal. Ni mababa wa watoto watakaokuja baada yetu. Ukiwalea vizuri kwa mafundisho mema, unalea umma uliochipukia katika malezi mazuri, tabia njema, hekima pamoja na Tawhiyd. Umma unaostahiki kuuongoza ulimwengu. Umma alioutaja Mwenyezi Mungu Aliposema:

Nyinyi ndio Umma bora kuliko Umma zote zilizodhihirishiwa watu (ulimwenguni) mnaamrisha yaliyo mema na manakataza yaliyo maovu na mnamuwamini Mwenyezi Mungu. Na kama wale waliopewa kitabu wangaliamini, ingelikuwa bora kwao. Miongoni mwao wako wanaoamini na wengi wao wanatoka katika taa ya Mwenyezi Mungu.

Aali Imraan 110

 

Mwangi

Mtoto mdogo aliyekuwa akitembea alijikuta yupo nje ya mji karibu na pango, akaamua kukaa juu ya ardhi, na kilipomjia kikohozi akaisikia sauti ya kikohozi chake kikimrudia mwenyewe (mwangwi wake echo-). Kwa vile ni mara yake ya mwanzo kusikia sauti ikimrudia, akadhani kuwa pana mtoto mwengine upande wa pili au ndani ya pango anajaribu kumwigiza.

Akauliza kwa ukali: Nani wewe?!

Sauti yake mwenyewe ikamrudia: Nani! Wewe?

Nakuuliza nani wewe? Sauti ikamrudia tena kama mwanzo.

Akasema kwa ukali zaidi: Nakuuliza nani wewe usokuwa na adabu?

Sauti ikamrudia tena kwa maneno yale yale aliyotamka.

Mtoto alikasirika sana akarudi nyumbani akiwa na ghadhabu, akamhadithia mama yake juu ya mtoto jeuri aliyekuwa akimuigiza maneno yake.

Mama yake akamwambia: Mwanangu, huo ni mwangi wako mwenyewe. Ni sauti yako mwenyewe ikikurudia, na wala hapana mtoto aliyekuwa akikuigiza. Na kama wewe ungelitamka maneno mazuri, basi yangelikurudia maneno mazuri.

Mfano huu unafaa kutumika katika mambo mengi sana, na hasa katika malezi mema, kwa sababu ukilea vyema utapata matunda mema, na ukilea vibaya utavuna kile ulichopanda.

 

 

Faatwimah (Radhiya Llaahu Anha)

Anasema mama wa Waislam Bibi Aaishah (Radhiya Llaahu anha):

Faatwimah (Radhiya Llaahu anha), amefanana sana na baba yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wasallam). Alikuwa anapokuja kumtembelea baba yake, Mtume (Swalla Llaahu alayhi wasallam) akimuinukia, kisha humsalimia kwa kumpa mkono wake mtukufu, kisha humbusu mwanawe penye kipaji chake, kisha humpisha akakaa mahali pake.

Na Mtume (Swalla Llaahu alayhi wasallam) anapokwenda kumtembelea binti yake huyo nyumbani kwake, Bibi Faatwimah (Radhiya Llaahu anha) naye hufanya kama anavyofanya baba yake (Swalla Llaahu alayhi wa sallam). Humuinukia, kisha humsalimia kwa mkono wake, kisha humbusu baba yake juu ya kipaji chake, kisha humpisha baba yake na kumuacha akae mahali pake.

 

Haya ni mafundisho matukufu, kutoka kwa watukufu wawili, Mmoja akiwa ni mbora wa viumbe vyote (Swalla Llaahu alayhi wasallam), na wa pili ni Bibi wa mabibi wa Peponi (Radhiya Llaahu anha), yakitufundisha juu ya heshima na uhusiano unaotakiwa baina ya mzazi na wanawe na namna mzee anavyoweza kuvuna kile anachopanda.

Mtume (Swalla Llaahu alayhi wasallam) amesema:

Hayuko pamoja nasi asiyemheshimu mkubwa wetu na kumhurumia mdogo wetu.

 

 

Mifano Mbali Mbali

Siku moja Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Llaahu anhu) alipoingia nyumbani kwa Mtume (Swalla Llaahu alayhi wasallam) alimkuta amewaweka Al-Hassan na Al-Husayn (Radhiya Llaahu anhum) mgongoni pake, akasema:

Utukufu ulioje wa ngamia aliyepandwa.

Mtume (Swalla Llaahu alayhi wasallam) akamjibu:

Na utukufu ulioje wa wapandaji wake (ngamia huyo).

 

Mtu mmoja aliingia nyumbani kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) na kumkuta akiwabusu wajukuu zake, akasema: Hivyo nyinyi Mnawabusu watoto wenu?

Mtume (Swalla Llaahu alayhi wasallam) akamuuliza:

Kwani nyinyi mnawafanyaje watoto wenu?

Yule mtu akasema:

WaLlaahi nina watoto kumi na sikupata hata siku moja kumbusu mmoja kati yao.

Mtume (Swalla Llaahu alayhi wasallam) akamwambia:

Nifanye nini ikiwa Mwenyezi Mungu Ameondoa rehma katika moyo wako. Hakika Mwenyezi Mungu huwahurumia wale wenye huruma.

 

Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Llaahu anhu) siku moja alikuwa amelala juu ya ardhi huku wanawe wanacheza na kuruka ruka kifuani pake. Akaingia mmoja katika Magavana wake aliyekuwa akihukumu katika mojawapo ya mikoa ya dola ya Kiislam na kumuona katika hali ile, akashangaa na kusema:

Umar! Simba wa Mwenyezi Mungu unafanya hivi na wanao?

Umar (Radhiya Llaahu anhu) akamuuliza:

Kweni wewe unafanyaje na wanao?

Akasema:

Mimi nikiingia nyumbani mfano wa simba, kila mmoja anajificha kwenye pango lake.

Umar (Radhiya Llaahu anhu) akamwambia:

Bora jiuzulu, usiifanye tena kazi yetu (ya Ugavana).

Yule mtu akauliza:

Kwanini ewe amiri wa Waislam?

Umar akamwambia:

Ikiwa wanao unawafanyia hayo, watakuwa katika hali gani Waislam walio chini ya utawala wako?

 

Hii ni mifano michache ndani ya mafundisho mengi yanayopatikana kutoka kwa Mtume (Swalla Llaahu alayhi wasallam) na Sahaba zake (Radhiya Llaahu anhum), yakitufundisha namna gani walivyowalea watoto wao kwa mapenzi na huruma, watoto waliokuja kuwa wanaume kweli wakaweza kuzifungua nchi mbali mbali Mashariki ya ardhi na Magharibi yake.

 

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) (Swalla Llaahu alayhi wasallam) anasema:

Mwenyezi Mungu Akiwatakia watu wa nyumba kheri, basi huingiza mapenzi baina yao.

 

Mtoto Ni Mfano Wa Chombo

Wataalamu wanasema: Akili ya mtoto, ni mfano wa chombo kitupu kinachosubiri kujazwa, na usipokijaza mwenyewe kitajazwa na wengine, na hapo usiilaumu isipokuwa nafsi yako.

Usingoje akili ya mwanao ikatawaliwa na marafiki wabaya waliojaa nje.

Waarabu wanasema:

Watoto wetu ni maini yetu yanayotembea juu ya ardhi.

 

Mwenyezi Mungu Akitujulisha namna gani waliotutangulia walivyokuwa wakivijaza vyombo hivyo, Anasema:

ٰ ٰ ٰ

Je! Mlikuwapo yalipomfikia Yaakubu mauti, alipowaambia wanawe Je, mtamuabudu nani baada yangu? Wakasema; Tutamwabudu Mola wako na Mola wa baba zako, Ibrahimu na Ismaili na Ishaka; Mungu Mmoja tu, na sisi tunanyenyekea kwake

Al-Baqarah 133

 

Siku moja Mtume (Swalla Llaahu alayhi wasallam) alipanda mnyama na alimpakia nyuma yake Abdullaah bin Abbaas (Radhiya Llaahu anhu), ambaye wakati huo alikuwa bado mdogo.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) (Swalla Llaahu alayhi wasallam) akamwambia:

Ewe kijana! Mimi ninakufundisha maneno, uyahifadhi (vizuri). Unapoomba, umuombe Mwenyezi Mungu (Allaah) (tu), ukitaka msaada, uuombe kutoka kwa Mwenyezi Mungu (Allaah) (tu), na ujue (ya kuwa) hata kama umma wote utajumuika kutaka kukunufaisha kwa jambo, basi hauwezi kukunufaisha isipokuwa kwa kile Alichokwisha kukuandikia Mwenyezi Mungu (Allaah). Na ikiwa watajumuika kutaka kukudhuru kwa jambo, basi hawatoweza kukudhuru, isipokuwa kwa kile Alichokwisha kukuandikia Mwenyezi Mungu (Allaah), kalamu zimekwisha nyanyuliwa na uwino umeshakauka.

 

Hivi ndivyo tunavyotakiwa tuwalee watoto wetu, kwa kuizamisha imani ya Tawhiyd nyoyoni mwao, mtoto aijue dini yake, ajuwe ya kuwa hapana wa kumuomba isipokuwa Allaah, hapana wa kumtegemea isipokuwa Allaah, hapana wa kumkimbilia wakati wa shida isipokuwa Allaah. Amuogope na kumtii MwenyeziMungu (Allaah), na hii ni kwa sababu kumjua na kumuogopa Mwenyezi Mungu ndiyo elimu bora kupita zote. Asiyemuogopa Mwenyezi Mungu hana maana wala hana mwamana hata kidogo, na anayemuogoga Mola wake kati yenu ni yule anayemjua Mola wake kama Anavyopaswa kujulikana.

Mwenyezi Mungu Anasema:

Kwa hakika wanaomwogopa Mwenyezi Mungu miongoni mwa waja Wake ni wale wanachuoni (Maulamaa).

Faatwir 28

 

Mtu mmoja alikwenda kumshitaki mwanawe kwa Sayyiduna Umar (Radhiya Llaahu anhu) kuwa alimpiga kofi la uso. Umar akamuuliza:

Mwanao huyu umemfundisha Qur-aan?

Yule mtu akajibu: Sijamfundisha

Umemfundisha mafundisho ya Mtume?

Sijamfundisha

Umemfundisha tabia njema za waarabu?

Sijamfundisha.

Umar akamwambia: Mwanao huyu alikufananisha na ngombe, ndiyo maana akakupiga.

 

Juu ya kuwa kuwafanyia wema wazee wawili ni jambo tukufu sana na jambo lililofaradhishwa na Mwenyezi Mungu, lakini kwa upande mwingine, wazee wenyewe ndio wanaotegemewa kuipanda na kuilea mbegu hii. Kwa sababu kile watakachopanda ndicho watakachovuna.

 

Siku moja Mtume (Swalla Llaahu alayhi wasallam) alipokuwa amekaa pamoja na Sahaba zake (Radhiya Llaahu anhum), aliletewa maji, akanywa na kubakisha mengine ili wenzake nao wapate kunywa. Kuliani pake alikaa mtoto mdogo, na kushotoni watu wazima. Kwa mujibu wa sheria shariah (tutofautishe sheria (za wanaadam) na shariah (za Allaah [Dini]), ugawaji lazima uanze upande wa kulia na kuendelea upande huo huo wa kulia bila kujali ukubwa wa mtu au umri wake.

Ili Mtume (Swalla Llaahu alayhi wasallam) aweze kuwapa maji watu wazima walioko kushotoni pake kwanza, ilibidi amuombe ruhusa mtoto yule aliyekaa kuliani kwake kwa kumwambia:

Ikiwa utaniruhusu nitawapa hawa kwanza (watu wazima walio kushotoni pangu).

Yule mtoto akasema:

Hapana WaLlaahi, sijitolei haki yangu itokayo kwako (baraka zako) kumpa mtu yeyote yule.

 

 

Uadilifu Baina Yao

Hapana kitendo kibaya kuliko mtu kutokuwa muadilifu baina ya watoto wake. Kumpendelea mmoja wao na kuwaacha wengine wakitizama ni dhulma na kujenga uadui baina yao, uadui ambao taathira yake mbaya itaanza kuonekana kuanzia utotoni mpaka ukubwani.

 

Na kama itabidi kupendelewa zaidi, basi mdogo mpaka akue au anayeumwa mpaka apone au aliyesafiri mpaka arudi, na upendeleo huo usipindukie mpaka, kwa sababu watoto wanahisi kuliko unavyowafikiria.

 

Mtume (Swalla Llaahu alayhi wasallam) alipomuona mtu mmoja amempakata mwanawe wa kiume, na amemweka wa kike mbele yake juu ya ardhi, akamwambia:

Si bora ungefanya uadilifu baina yao?

 

Mtu mmoja alitaka kumpa sehemu ya mali yake mmoja tu kati ya wanawe, na alitaka mkewe awe shahidi juu ya jambo hilo. Mkewe, akamwambia:

Mimi sikubali mpaka kwanza umtake shauri Mtume wa Mwenyezi Mungu.

Mtume (Swalla Llaahu alayhi wasallam) akamuuliza:

Jee na wanao wengine pia utawaandikia sawa na mtoto huyu?

Yule Mtu akajibu:

Hapana, namtakia huyu mmoja tu

Mtume (Swalla Llaahu alayhi wasallam) akamwambia:

Mimi siwi shahidi katika (jambo la) dhulma.

 

 

Kuwapa Moyo

Wazee mara nyingi huwa na tabia ya kuwavunja moyo watoto kwa kuwashutumu na kulaumu kila wanapotenda makosa madogo madogo, na kwa ajili hiyo watoto huingiwa na uwoga ndani ya nyoyo zao na kuendelea na uwoga huo hadi ukubwani wakajihisi kuwa wana kasoro mbele ya wenzao.

Mtoto anapokosea hukosolewa kwa hekima kwa niyah ya kumjulisha kosa lake, na siyo kumshutumu na kumvunja moyo na kuingiza uoga (ima kote iwe uoga au uwoga) ndani ya moyo wake akaogopa tena kujaribu kufanya jambo.

 

Alipotawazwa Umar bin Abdil-Aziyz (Radhiya Llaahu anhu) kuwa Khalifa wa Waislam, wajumbe na watu kutoka sehemu mbali mbali za dola ya Kiislamu walikwenda kumpa hongera na kufungamana naye. Mojawapo ya makundi hayo likiongozwa na kijana mdogo liliwasili katika qasri ya Umar bin Abdil-Aziyz. Kijana aliinuka na kuanza kuhutubia kwa kumpa hongera Umar mbele ya hadhara ya watu waliomzidi umri.

Umar akamwambia:

Mbona umeinuka wewe mdogo wao, si bora mungelimchaguwa kiongozi aliye mkubwa wenu kwa umri?

Yule kijana akasema:

Kama uongozi ni kwa umri, basi wako wanaostahiki zaidi kuwa Makhalifa kuliko wewe.

Umar bin Abdil-Aziyz alifurahi sana kwa ushujaa na uhodari wa kijana yule, akasema:

                      

Na maana yake ni:

Jifunze, kwani mtu hazaliwi akiwa na elimu. Na aliye na elimu hawezi kuwa sawa na asiyekuwa na elimu.

Kisha akasema: Wameongoka watu waliokuchaguwa uwe kiongozi wao.

 

 

Kudekeza Sana

Kwa upande mwingine, kudekeza sana watoto hasa wa kiume na kuwaendekeza kupita kiasi hadi kuwavalisha vidani na kukata mikato ya nywele za watoto wa kiume kama wanawake na kuvaa nguo zilizofanana na za kike au kuigiza staili za makafiri ni jambo lisilopendeza. Kuwaachia moja kwa moja bila ya kuwakosoa wanapokosa au kuwaongoza wanapopotea njia si katika malezi mazuri.

 

Malezi yanatakiwa yawe kati na kati, kama alivyosema Muawiyah bin Abi Sufyaan (Radhiya Llaahu anhu): Lau kama baina yangu na baina ya kaumu yangu upo unywele (vuta nikuvute), basi sitouacha ukatike. Wakikaza nitaregeza na wakiregeza nitakaza.

 

Mwanamume wa Kiislamu anatakiwa awe na sifa ya ushujaa na ucha Mungu, na ushupavu.

Mwenyezi Mungu Amewasifia wanaume kwa ushujaa wao na uwanaume wao Aliposema:

Wapo watu (wanaume kweli kweli) miongoni mwa walioamini, waliotimiza ahadi waliyoahidiana na Mwenyezi Mungu

Al-Ahzaab - 23

 

Usia

Luqmaan mwenye hekima alikuwa na tabia ya kumuusia mwanawe mara kwa mara na kumfundisha tabia njema.

Mwenyezi Mungu Anasema:

Na (wakumbushe), Luqman alipomwambia Mwanawe; na hali ya kuwa anampa nasaha. Ewe mwanangu! Usimshirikishe Mwenyezi Mungu maaana shirki ndiyo dhulma kubwa.

Luqmaan- 13

 

Na Akasema:

Wala usiwabeuwe watu, wala usitembee katika nchi ardhi kwa maringo. Hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila anayejivuna na kujifakhirisha.

Luqmaan 18

 

Haya ni mambo mawili ambayo mtoto wa Kiislamu anatakiwa afunzwe kujiepusha nayo, Ushirikina na Kiburi.

Ushirikina ni dhambi isiyosameheka, na Kiburi ni tabia Asiyoipenda Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala).

 

Anasema mshairi:

 

Ikiwa umeumbika, kwa uzuri ulotimu,

Au umetajirika, pesa nyingi tasilimu,

Kiburi ukajivika. vazi lenye uhasimu,

Kiburi kwa mwanaadamu, Si kitu chema kiburi.

 

Mola mwenye madaraka, Ndiye Mwenye kurehemu

Kukupa na kukupoka, ndiyo kaziye Karimu.

Humpa Anayetaka, jamii ya wanaadamu,

Kiburi kwa mwanaadamu, Si kitu chema kiburi.

 

Waringa na hekaheka, wenzio kuwashutumu,

Kwa kuziona fanaka, Mola Alokukirimu,

Wazimu ukakushika, ukawa huna fahamu,

Kiburi kwa mwanaadamu, Si kitu chema kiburi.

 

Kwanza ziondowe taka, nduguzo kuwahasimu.

Usiipige mipaka, wazazi kuwalaumu,

Zinduka ndugu zinduka, wewe Sio marehemu,

Kiburi kwa mwanaadamu, Si kitu chema kiburi.

 

Kiburi ni mbaya shuka, kuivaa ni haramu.

Yapendeza kukumbuka, msemo wenye kudumu,

Mpanda ngazi hushuka, alacho kikawa sumu.

Kiburi kwa mwanaadamu, Si kitu chema kiburi.

 

Na mwanaadamu yataka, bongo lake kuhitimu.

Wazee walotamka, maneno yalo muhimu,

Kulonama huinuka, laini huwa kigumu.

Kiburi kwa mwanaadamu, Si kitu chema kiburi.

 

Kituoni nimefika, nazikomesha nudhumu,

Yatosha naloandika, kiburi ni jahanamu,

Ashikae atashika, asoshika Si lazimu,

Kiburi kwa mwanaadamu, Si kitu chema kiburi.

 

Ghadhabu

Mara nyingi mtu anaporudi kutoka kazini akiwa amebeba kichwani matatizo yake ya kazini, na anapowasili nyumbani na kukuta mambo yameparaganyika, mke mkali, watoto wanafanya zogo, kazi zao za skuli hawakuzifanya, wanapigana, na mengi katika matatizo yanayotokea mara kwa mara majumbani, wakati huo mzigo unakuwa mzito sana juu yake, na ghadhabu zake zote alizokuja nazo kutoka kazini huwamiminia watoto wake kwa kuwapiga vibaya sana.

Kuwapiga watoto kwa ghadhabu kunaweza kuleta madhara kuliko manufaa.

 

Mtu anaporudi na akahisi kuwa siku hiyo amekumbana na matatizo mengi na akaona kuwa ghadhabu zake ziko karibu karibu, ni bora aanze kuomba msaada wa Mola wake kwa kusoma ile duaa aliyotufundisha Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wasallam):

Allaahumma inniy abduka wabnu abdika wabni amatika naaswiyatiy biyadika maadhin fiyyaa hukmuka adlun fiyyaa qadhaauka as-aluka bikulli smin huwa lak sammayta bihi nafsika aw anzaltahu fiy kitaabika aw allamtahu ahadan min khalqik aw istaatharta bihi fiy ilmil ghaybi indak an tajala l Qur-aana rabiya qalbiy - wa nuura sadry wa jalaa-a huzniy wa dhahaaba hammiy.

 

Hapo Mwenyezi Mungu Atamuondolea dhiki na huzuni zake, na badala yake Atampa furaha na ataweza kuyakabili matatizo ya nyumbani kwa utulivu na bila ya ghadhabu.

 

 

Al-Ahnaf Bin Qays (Radhiya Llaahu Anhu)

Muaawiyah alimuuliza Al-Ahnaf bin Qays (Radhiya Llaahu anhum):

Ewe Aba Bahr! Unasemaje kuhusu watoto?

Al-Ahnaf akasema:

Ewe Amiri wa Waislam, wao ni uti wa migongo yetu, matunda ya nyoyo zetu, kipumbazo cha macho yetu, kwa ajili yao tunawashinda adui zetu, na wao ndio watakaokuwa wazazi wa watakaokuja baada yetu, kwa hivyo uwe kwao, mfano wa ardhi laini, na uwe mfano wa mawingu yanayowaletea kivuli. Wakikuomba, uwape, wakikuomba msamaha, uwasamehe, na wala usiwanyime ulichonacho mpaka wakakuchukia na kukuona unachelewa kufa (ili wakurithi).

Muaawiyah (Radhiya Llaahu anhu) akasema:

WaLlaahi ewe Aba Bahr, wao ni kama ulivyowaelezea.

 

Usiku mmoja Waislam waliokuwa safarini kupigana Jihaad wakiwa wamejipumzisha huku wakisikiliza hotuba ya Abdullaah bin Mubaarak (Radhiya Llaahu anhu) ambaye ni mmoja katika Maulamaa wakubwa wa Kiislam, akiwatia moyo pamoja na kuwajulisha umuhimu wa kupigana Jihaad.

Mmoja kati ya waliohudhuria akamuuliza:

Ewe Abdullaah, ipo amali yoyote iliyo bora kuliko hii tuliyokuwa nayo sisi? Tumo safarini kwa ajili ya Jihaad na wakati huo huo tupo katika majlis ya elimu.

Abdullaah bin Mubaarak akamwambia:

Naam ipo. Yule aliyeamka usiku, akaenda kuwatizama wanawe waliolala, na kuwafunika vizuri wale wasiojifunika.

 

Haya ndiyo mapenzi na rehma tunayotakiwa kuwafanyia watoto wetu ili nao wakue, wawe na huruma na ili wapate kuhurimiana ndugu kwa ndugu, Waislam kwa Waislam na kuieneza rehma baina yao.

 

 

Sababu Za Kuharibika Kwa Tabia

Baada ya kufanya utafiti kwa kuwahoji waalimu, baadhi ya wazee, na watoto waliolazwa mahospitali kwa ajili ya kutibiwa ili wasirudie kutumia unga na mihadarati, pamoja na wale waliotiwa jela kwa ajili ya kujishughulisha na biashara hii ovu, wataalamu wamegundua yafuatayo kuwa ni miongoni mwa sababu muhimu za kuharibika kwa mwenendo wa watoto:

 

1.  Ugomvi usiokwisha baina ya wazee mbele ya watoto (Watoto wasipopata mfano mwema wa kuufuata katika wazee wao basi huutafuta mfano huo nje, na kwa ajili hiyo huwafanya waimbaji, wana michezo, na wababe wa sinema kuwa ni mfano kwao bora wa kuigwa, na kuanza kuvaa kama wao na kuchana michano yao pamoja na kutembea kama wao n.k.)

 

2.  Kuoana baina ya watu wa mataifa yasiyolingana ustaarabu wao.

 

3.  Baba na mama wanapoacha kuifanya kazi yo vizuri kwa kutofuatilia habari za watoto wao kutaka kujua nini wanachofanya wakiwa shuleni au nje wanapocheza na wenzao. Mshairi maarufu aitwae Ahmad Shawqiy anasema: Yatima si yule aliyefiwa na wazee wake, bali yatima ni yule mwenye mama aliyeiacha kazi yake na baba asiyejishughulisha naye.

 

4.  Kuruhusiwa watoto kuwaiga na kuwapenda bila kipimo waimbaji na wababe wa sinema n.k. katika mavazi yao na mwenendo wao. Na moja katika dalili kubwa za kusalimu amri mbele ya njama za adui, ni pale adui anapoanza kufaywa kuwa ni mfano mwema wa kuigwa.

 

5.  Marafiki wabaya wana sehemu kubwa ya kuharibika kwa mwenendo wa watoto. Kuwazuia watoto wasiende kwa rafiki zao ni jambo gumu sana, lakini mtu anaweza kumuelimisha mwanawe na kumkumbusha mara kwa mara juu ya umuhimu wa tabia njema na umuhimu wa kumtii Mola wake, ili mtoto nae kwa upande wake aweze kuwaongoza rafiki zake.

 

6.  Kuwaruhusu watoto kutizama na kufuatilia filamu za fujo na zile zenye kuonyesha utovu wa adabu.

 

7.  Kutokujishughulisha kwa mzee kupekua mikoba ya mwanawe ili ajue ni vitabu vya aina gani anavyosoma. Kwa sababu marafiki wabaya wanaweza kumpa vitabu vya utovu wa adabu na kuviingiza nyumbani na kusababisha ndugu zake wengine nao kuviangalia.

 

8.  Kutotembelea skuli za watoto wao kwa ajili ya kujua mwenendo wao pamoja na matatizo yao, na ili kuweza kuepusha matatizo kabla ya kutokea.

 

9.  Kutojishughulisha na matokeo ya mwanawe katika mitihani, ikiwa amefeli au amepasi yote kwake ni sawa tu, hii humfanya mtoto asiyashughulikie sana masomo yake au hata kuyachukia na kukimbia skuli.

 

10.      Kutendewa vibaya na waalimu pia kunawafanya watoto kutoipenda skuli.

 

11.      Ushirikiano baina ya skuli na wazee ni jambo muhimu sana.

 

12.      Wazee kuwapenda watoto wengine na kutowashughulikia wengine.