NYOYO

Nyoyo zina njia zake sita. Tatu katika hizo ni ovu, na tatu nyengine ni njema.

Zilizo ovu, siku zote;

Zinapambiwa na dunia, au

Zinaidanganya nafsi yake na Kuadhibika katika dunia, au

Huwa zina adui anayezijaza wasi wasi na kuisababishia adhabu hiyo.

Ama njia tatu njema, ni zile

Zinazotenda mema na kuonekana natija yake, au

Zenye kuwa na akili inazoziongoza, na

Zenye kumjua Mola wake ili zimuabudu kama anavyopaswa kuabudiwa.

Nyoyo zote zinatembea katika njia hizi.sita.

Kufuata matamanio ya nafsi, na kuwa na matumaini ya kuishi mda mrefu, ni

katika sababu kubwa ya kufisidika kwa moyo, na kufuata matamanio ya

nafsi kunasababisha kuupofosha moyo huo usiweze kuuona ukweli na usiweze kuiona haki.

Kufuata matamanio ya nafsi kunamfanya mtu asipate raha, na siku zote hupenda

kujishambulia au kushambulia wenzake.

Kuwa na tamaa ya kuishi mda mrefu hapa duniani, kunamfanya mtu aisahau

akhera yake na kumzuwia asijitayarishe nayo..

Mwenyezi Mungu anapomtakia mja wake kheri, humjaalia kuwa ni mtu

anayekubali kuwa yeye ni mtenda madhambi na kujizuwia kufuatilia madhambi ya

wenzake.

Humjaalia pia asipende kuwanyima wenzake kile alicho nacho katika mambo ya kheri, na kutopenda kufuatilia vya wenzake.

Na iwapo Mwenyezi Mungu hamtakii mja wake kheri, basi huyageuza mambo, na kuyafanya yawe kinyume na hivyo.

Mtu anapoiona kheri katika nafsi yake, basi amshukuru Mwenyezi Mungu.

Ama anapoona kinyume cha hivyo, basi ailaumu nafsi yake.

Kwa hivyo mtu anatakiwa ajaribu kuzijuwa zile sifa njema ili aweze kuzifuata na kuzipenda.

Na pia anatakiwa atambuwe neema alizopewa na Mola wake ili aweze kumshukuru

kwa kuongeza utiifu.

 

SIFA ZA NAFSI YA HALI YA JUU

Shaqiyq Ibrahim Al Balkhiy, mmoja katika wanavyuoni wakubwa aliyefariki katika mwaka wa 194H. alisema;

"Watu wa aina sita hufungiwa milango ya kufanikiwa;

Wanaojishughulisha na neema wakasahau kumshukuru aliowaneemesha.

Wenye kujishughulisha kutafuta elimu kisha wasiifanyie kazi.

Wepesi wa kufanya madhambi na wazito wa kutubia.

Wanaopenda kufuatana na watu wema wakaacha kufuata mwenendo wao.

Wanaoikimbilia dunia na hali dunia inawakimbia, na

Wanaoikimbia akhera wakati akhera inawakimbilia wao".

Ama Ibnil Qayim, yeye anasema;

"Yote hayo yanatokana na kutokuwa na uoga - uoga wa kumuogopa Mwenyezi Mungu - na asili yake hasa ni upungufu wa yakini na upungufu wa ilimu - ilimu ya kumjua mtu Mola wake, na asili yake hasa ni mtu kuwa na nafsi dhalili na nafsi duni inayokubali kubadilisha kile kilichokuwa duni kwa kile kilichokuwa bora, ama sivyo kama nafsi ingekuwa tukufu inayojiheshimu, basi isingeridhika na kilichokuwa duni".

Heshima Ya Nafsi

Anaendela kusema Ibnil Qayim;

"Kwa hivyo asili ya kheri yote imo katika kuiheshimu mtu nafsi yake hiyo na katika kuitukuza kwake na katika kuitakasa kwake. Na asili ya shari yote imo katika kuidharau mtu nafsi yake na katika kuiviza na katika kutoiheshimu.

Mwenyezi Mungu anasema;

"Bila shaka amefaulu aliyeitakasa (nafsi yake) Na bila shaka amejikhasiri aliyeiviza (nafsi yake)".

Suratush shams - 9-10

Na maana yake aya hii ni kuwa; 'Imefuzu nafsi ya yule aliyeilea katika kumcha Mungu na katika kuitakasa na katika kuikuza kwa kumtii Mwenyezi Mungu. Na imekula hasara nafsi ya yule aliyeilea katika kumuasi Mwenyezi Mungu na katika kuichafua na kuidogosha.

Kwa hivyo nafsi zinazojiheshimu haziridhiki isipokuwa kwa yaliyo matukufu na yaliyo bora na yenye mwisho mwema. Na nafsi zilizo duni ziku zote zinayazungukia zungukia yaliyo duni na kuyaangukia kama nzi wanavyoangukia uchafu.

Kwa ajili hiyo nafsi zinazojiheshimu haziridhiki na dhulma wala haziridhiki na uchafu wala wizi wala khiyana. Na hii ni kwa sababu nafsi hizo ziko juu na zimetakasika mbali kabisa na mambo kama hayo.

Ama nafsi dhalili zisizojiheshimu zinakwenda kinyume kabisa na hayo, kwani kila nafsi inaelekea kule inakopendezwa nako.

Na hii ndiyo tafsiri ya kauli yake Subhanahu wa Taala aliposema;

"Sema; "Kila mmoja anafanya (amali yake) kwa njia yake."

Bani Israil -84

Yaani anafanya kazi kwa njia ile anayonasibiana nayo, kwani anafanya kufuatana na vile anavyopenda na kunasibiana na mwenendo na tabia zake. Na kila nafsi inakwenda katika njia yake na mwenendo wake inaoupenda na kuuelekea.

Kwa hivyo mtu asi anafanya amali zile zinazonasibiana na mwenendo wake katika kuzilipa neema alizoneemeshwa nazo kwa uasi na kwa kwenda kinyume na yule Aliyemneemesha. Na Muislam aliyeamini kikweli anafanya amali zake zinazonasibiana na mwenendo wake katika kumshukuru na kumpenda yule Aliyemneemesha, na pia katika kumsifia na kumtukuza na kumuadhimisha na kujipendekeza kwake na kumuonea haya pamoja na kuchunga asimuasi. "

 

MUHAMMAD FARAJ SALEM AL SAIY