NYUMBA YA KIISLAM

Inasikitisha kuona kwamba kila tunapopiga hatua moja mbele katika elimu za kisasa tunapiga hatua mbili nyuma katika elimu ya dini yetu. Kila tunapoendelea katika haya yanayoitwa maendeleo ya kisasa tunarudi nyuma katika maendeleo ya dini yetu. Kila tunaposonga mbele katika kuyavamia maisha ya kisasa tunazidi kusalimu amri kwa kuacha baadhi ya mafundisho ya dini yetu.

Makafiri wamefanikiwa kiasi kikubwa kutubabaisha na kutuingiza kwa nguvu katika ulimwengu wao kiasi ambacho wakati huu yule anayeshikamana na dini yake akikataa kutetereshwa na uvamizi huu basi huitwa ‘Wenye siasa kali’, na yule anayelingania dini, huonekana kama ni mtu aliye mbali kabisa na fikra za kisasa, mtu aliye nyuma kabisa, isipokuwa kwa wale wachache aliowarehemu Mola wao.

Tumeiacha nuru alokuja nayo Mtume wetu mtukufu (SAW) na kufuata yale waliyokua wakitaka makafiri tokea zamani tuyafuate.

Wao wanaelewa vizuri kuwa si rahisi kumtoa Muislam katika dini yake na kufuata dini yao, kwa sababu Alhamdulillah ukweli ushadhihiri na uwongo ushajitenga. Lakini baada ya kushindwa kutuingiza katika dini yao, hivi sasa lengo lao kubwa ni kututoa katika dini yetu tu, si muhimu kwao iwapo tutafata dini yao au hatutofuata, muhimu kwao kutupotosha mbali na njia ya haki. Kutupotosha mbali na mafundisho ya Qurani na ya Mtume wetu Muhammad (SAW).

Mwenyezi Mungu wetu ni Mungu wa Haki

Mtume wetu ni Mtume wa Haki

Dini yetu ni dini ya Haki

Na kitabu chetu ni kitabu cha Haki

Sasa kuna nini basi badala ya kufuata Haki isipokuwa upotevu tu?

Mshairi anasema;

Mayahudi walikuwa wakijua fika kuwa Muhammad(SAW) ni Mtume wa kweli, walikuwa wakimjua kama wanavyowajua watoto wao, bali walijua hata wakati wake wa kufika kuwa umeshakaribia, lakini alipokuja yule walokuwa wakimjua, wakamkanusha na kumkataa, na kwa ajili hiyo Mwenyezi Mungu akawalani.

Mayahudi walokuwa wakiishi pale Madina walijijengea ngome za kuwalinda wakati wa vita, na walikuwa daima wakiwagombanisha waarabu na kufaidika kwa vita vilivyopiganwa baina yao, kwani walikuwa wakinunua mateka wao na kuwauzia silaha zao.

Walifikiri kuwa kwa uhodari wao huo na kwa ngome zao hizo hawataweza kufikiwa na chochote.

Wakamkanusha Mtume(SAW), na kuvunja kila ahadi walizokubaliana baina yao, na kwa ajili hiyo Mwenyezi Mungu akawadhalilisha na kuwafanya wabomoe nyumba zao kwa mikono yao wenyewe.

Mwenyezi Mungu anasema;

“Yeye ndiye aliye watoa walio kufuru miongoni mwa Watu wa Kitabu katika nyumba zao wakati wa uhamisho wa kwanza. Hamkudhani kuwa watatoka, nao walidhani kuwa ngome zao zitawalinda na Mwenyezi Mungu. Lakini Mwenyezi Mungu aliwafikia kwa mahali wasipo patazamia, na akatia woga katika nyoyo zao. Wakawa wanazibomoa nyumba zao kwa mikono yao na mikono ya Waumini. Basi zingatieni enyi wenye macho!”

Al Hashar – 2

Na maana ya aya hii ni kuwa;

Yeye Mwenyezi Mungu ndiye aliyewatoa walio kufuru miongoni mwa Watu wa Kitabu, nao ni Mayahudi wa ukoo wa Banu Nadhir, kutoka kwenye majumba yao wakati wa kuwatoa mara ya kwanza katika Bara Arabu. Kwa sababu mara ya pili walitolewa nje kabisa ya Bara Arabuni na Sayiduna Omar bin Khatab(RA). Enyi Waislamu! Hamkudhania kuwa watatoka kwenye nyumba zao kwa sababu ya nguvu zao. Na wao wenyewe walidhani kwamba ngome zao zitawalinda na mashambulio ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu akawatokea katika upande wasio utarajia, na akawatia katika nyoyo zao fazaa (hofu) kubwa, wakawa wanabomoa nyumba zao kwa mikono yao ili zibaki kuwa magofu tu, na kwa mikono ya Waumini wapate kuzivunja zile ngome. Basi enyi wenye akili, chukueni somo katika haya yaliyo washukia hawa.

Hakuna sababu nyingine iliyotufikisha katika unyonge na udhalili huu Waislamu isipokuwa ni kwenda kinyume na mafundisho ya dini yetu.

Sudan imepigwa, Iraq inaendelea kuangamizwa, Chechnya inaunguzwa, Afghanistan inangoja zamu yake, maangamizi yanaendelea, Waislam wanatizama macho tu, hawana la kufanya, bali hawana uwezo wa kufanya lolote.

Mtume(SAW) amesema;

“Hivi karibuni mtakuja zungukwa na mataifa, mfano wa walaji wanavyokizunguka chakula chao”

Wakamuuliza;

“Nikwa sababu ya uchache wetu ewe Mtume wa Mwenyezi Mung?”

Akajibu;

“La! Bali nyinyi siku hiyo mtakuwa wengi sana lakini

Nini sababu ya yote hayo?

Sababu kubwa kabisa ya yote hayo ni kuwa nyumba zetu zimekuwa ni nyumba za kumtii shetani, na kuzipiga vita amri za Al Mannani Subhanahu wa Taala..

 

Waislam lazima warudi kwa Mola weo na kuirudisha ile shani waliyokuwa nayo wale waliokuja kabla yetu?

Imam Malik bin Anas anasema;

‘Hakuna kuwatengeneza umma wa mwisho isipokuwa kwa yale yaliyowatengeneza umma wa mwanzo’

Kila mtu lazima ajaribu kuifanya nyumba yake iwe nyumba ya Kiislam kikweli, na kila nyumba ikiweza kusimamisha amri ya Mwenyezi Mungu, itakuwa mfano wa tufali moja likingoja tufali jengine, na tufali baada ya tufali mpaka nyumba itamalizika.

Nyumba za Waislam ni nyumba za kumtii Mwenyezi Mungu na si za kufanya maasi

Wallahu waliyu ttawfiyq

MUHAMMAD FARAJ SALEM AL SAIY