Tamaa

Tembelea http://mawaidha.info

Muhammad Faraj Al Saiy

 

Imepokelewa katika Athar kuwa Nabii Issa (Alayhi ssalaam) siku moja alipokuwa safarini alikutana na mtu aliyemuomba afuatane naye, na Nabii Issa alikubali.

 

Walipokuwa njiani Nabii Issa alinunua mikate mitatu, akala mmoja, akampa mwenzake mkate mwingine, kisha akamwambia:

"Na mkate huu wa tatu tuubakishe, utatusaidia mbele ya safari."

 

Usiku ulipoingia na Nabii Issa (Alayhi ssalaam) alipojipumzisha na usingizi kumchukuwa, yule mtu aliuchukua ule mkate wa tatu uliobaki akaula.

Alipoamka akamuuliza:

“Uwapi mkate tuloubakisha

Yule mtu akajibu:

“Sijuwi”

 

Walipokuwa wakiendelea na safari wakatokezewa na mnyama mkali sana, na maisha yao yakawa hatarini, Nabii Issa (Alayhi ssalaam) akanyanyua mikono juu na kuomba dua, na yule mnyama akatoweka.

Nabii Issa (Alayhi ssalaam) akamwambia mtu yule:

“Kwa utukufu wa Yule Aliyetuokoa na hatari ya mnyama mbaya huyu, niambie nani aliyekula mkate

Yule mtu akajibu kama alivyojibu pale mwanzo:

“Sijuwi”.

 

Wakaendelea na safari, na walipowasili kandokando ya bahari. Nabii Issa (Alayhi ssalaam) alimuomba Mola wake, akaanza kutembea juu ya bahari pamoja na mwenzake yule, na walipokuwa katika hali ile akamuuliza tena:

“Kwa utukufu wa aliyetuwezesha kutembea juu ya bahari, tafadhali niambie nani aliyeula mkate ule?”.

Yule mtu akajibu vile vile:

“Sijuwi”.

 

Baada ya kuvuka bahari, wakatembea kidogo, kisha wakapumzika karibu na jabali, na Nabii Issa (Alayhi ssalaam) akamuomba Mola wake na lile jabali likageuka kuwa dhahabu, kisha akamuambia mtu yule:

“Jabali hili la dhahabu tutaligawa sehemu tatu. Sehemu moja itakuwa yangu, moja yako, na sehemu moja tutampa yule aliyekula mkate”.

Yule mtu akasema:

“Mimi ndiye niliyekula mkate!”.

Nabii Issa (Alayhi ssalaam) akamuambia:

“Basi dhahabu yote chukua wewe”.

 

Yule mtu alipokuwa amekaa chini ya jabali lake la dhahabu huku akitafakari, wakapita majambazi wawili.

Majambazi:

“Dhahabu ya nani hii

“Yangu”.

“Dhahabu yote yako peke yako

“Ndiyo”.

Majambazi:

“Unaonaje tukagawana sehemu tatu, kila mmoja wetu achukue sehemu moja

Yule mtu baada ya kuwahisi kuwa ni watu wabaya, akawakubalia, kisha akawaambia:

“Sote tuna njaa, mnaonaje nikienda kununua mikate tupate kula, kisha tusikilizane namna ya kuichukuwa dhahabu yetu

Majambazi wakakubali.

 

Baada ya yule mtu kuondoka, majambazi wakaanza kupanga ukhabithi wao.

“Unaonaje akirudi tu, tumshambulie kwa visu na mapanga, tumuulie mbali kisha tuichukuwe sisi dhahabu yote

Wakakubaliana.

 

Na yule mtu alipokuwa akienda kununuwa mikate akawa anawaza na kufikiri;

“Kwa nini nigawane nao dhahabu ile, wakati nimepewa peke yangu? Ah! Bora nitawatilia sumu katika mikate hii, wafe, kisha niichukue dhahabu yote peke yangu”.

Alipowasili na mikate yake ya sumu, wale majambazi walimvamia na kumshambulia kwa visu na mapanga na kumuua, kisha wakakaa chini ya mti na kuanza kula mikate ile iliyotiwa sumu. Wakafa wote watatu.

 

Nabii Issa (Alayhi ssalaam) siku ya pili alipokuwa akirudi safarini akifuatana na wanafunzi wake, alipita mahali pale na kuona maiti tatu, akasema kuwaambia wanafunzi wake;

“Tamaa ndiyo iliyowauwa watu hawa”.