Makusudio sahihi ya Aliyekunja uso 

 

Muhammad Faraj Salem Al Saiy

 

Imepokelewa kuwa siku moja Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa amekaa na wakubwa wa Ma-Quraysh akiwalingania Diyn kwa hima kubwa akitaraji kuwa wakisilimu wakubwa hao, na wanyonge wao watafuata kwa sababu wengi kati ya wanyonge walitaka kusilimu lakini walijizuia kwa kuwaogopa wakubwa wao hao

Wakati huo akatokea kipofu mmoja aliyesilimu tokea zamani aitwaye Ibn Ummi Maktuum (Radhiya Allaahu Anhu), na bila kujua kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) ameshughulika akawa anampigia kelele kumwambia: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, nifunze na mimi katika aliyokufunza Mwenyezi Mungu.

Akawa anayarudia maneno hayo, na kwa vile Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ameshughulika kutaka kuwasilimisha viongozi wale wakubwa, akamfinyia uso yule kipofu wala asimsikilize, ndipo Mwenyezi Mungu Alipomteremshia aayah za mwanzo za Suuratu-Abasa. Mwenyezi Mungu Anasema:

ٰ ﴿١﴾

Alikunja (Mtume) uso akageuka

ٰ ﴿٢﴾

Kwa sababu alimjia kipofu

ٰ﴿٣﴾

Na nini kilichokujulisha (ya kuwa huyo Swahaabah kipofu hahitaji mawaidhah mapya), huenda yeye atatakasika (kwa kusikia mawaidha yako).

ٰ ﴿٤﴾

Au atakumbuka ukumbusho huo upate kumfaa

ٰ ﴿٥﴾

Ama ajionaye hana haja

ٰ ﴿٦﴾

Wewe ndiye unayemshughulikia.

ٰ ﴿٧﴾

Na si juu yako kama hakutakasika.

ٰ ﴿٨﴾

Lakini anayekukimbilia

ٰ ﴿٩﴾

Naye anaogopa

ٰ ﴿١٠﴾

Wewe unapuuza (Usifanye hivyo)

﴿١١﴾

Sivyo! Hakika hii (Qur-aan) ni nasaha

﴿١٢﴾

Basi kila apendaye atawaidhika

 

Shiah wanasema kuwa makatazo ndani ya aayah hizi si kwa ajili ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) kwa sababu si yeye (Swalla Llaahu alayhi wasallam) aliyekunja uso na kugeuka na kwamba yeye (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) hawezi kukunja uso wala kukosolewa, bali aliyekosea na kukosolewa ndani ya aayah hizo ni Uthmaan (Radhiya Allaahu Anhu).

Tatizo ni kuwa baadhi yao hawana uoga hata kidogo, na wako tayari kubadilisha maneno ya Mwenyezi Mungu (Subhaanahu Wa Taala), kwa ajili ya kutaka kuiuza bidhaa yao mbovu.

Sisi Tunasema: Lau kama aliyeteremshiwa aayah hizi ni Uthmaan (Radhiya Allaahu Anhu), basi hii ni sifa kubwa kwake, kwa sababu mtiririko wa aayah unatujuulisha kuwa aliyekatazwa ni mtu aliyekuwa akiwalingania watu katika Diyn, na hii ni sifa nzuri hata kama atakatazwa au kukaripiwa kidogo na Mola wake (Subhaanahu wa Taala).

Mwenyezi Mungu Anasema:

{{Alikunja uso na akageuka. Kwa sababu alimjia kipofu. Na nini kilichokujuulisha (ya kuwa huyo Swahaabah kipofu hahitaji mawaidhah mapya), huenda yeye atatakasika (kwa kusikia mawaidha yako).}} [Abasa: 1-3]

Kutokana na aayah hizi, (kwa rai ya Shiah) inaleta maana kuwa kipofu (Abdullaah mwana wa Ummi Maktuum), hakumuendea Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam), wala hakumuendea Aliy bin Abi Twaalib wala Maswahaabah (Radhiya Llaahu anhum) waliokuwepo mahali hapo, bali alimuendea Uthmaan (Radhiya Allaahu Anhu) kwa ajili ya kutaka kupata mawaidhah na uongofu kutoka kwake. Kwa sababu aliyekunja uso ni Uthmaan (Radhiya Allaahu Anhu) na si Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam).

Huu ni ubabaishaji wa maneno, kwa sababu aayah zinatufahamisha kuwa aliyejiwa ndiye aliyekunja uso, na haiwezekani kwa mwana wa Ummi Maktuum kumuacha Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) akamuendea Uthmaan (Radhiya Allaahu Anhu).

Kama wangelitafakari kidogo tu kabla ya kuandika maandishi yao haya yenye sumu, wangeligundua kuwa maneno yao ni utovu wa adabu dhidi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam).

Hadiyth sahihi zinasema kuwa kipofu yule alimuendea Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) huku akimuambia: Nifundishe katika yale Aliyokufundisha Mwenyezi Mungu. Akawa anaendelea kuyakariri maneno hayo, na kwa vile yeye ni kipofu, hakuelewa kuwa wakati ule Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ameshughulika kutaka kuwasilimisha wakubwa wa Ma-Quraysh waliokuwa naye akiwa na tumaini kuwa huenda mmoja wao atasilimu. Ndipo alipokunja uso na hakumjibu, na hapo ndipo zilipoteremshwa aayah za kumkosoa (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam).

Na hili ni jambo la kawaida kwa mtu yeyote anayekatwa maneno wakati akizungumza, na hili ni funzo kwetu kutoka kwa Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) kuwa tusiwakate watu maneno wanapozungumza kwa sababu hili ni jambo linalokera.

Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) hakumdharau kipofu yule wala hakumkaripia kwa kumuambia kwa mfano: Nyamaza! au Ondoka hapa! bali alikunja uso wake tu bila kumjibu. Lakini Mwenyezi Mungu (Subhaanahu Wa Taala) alimkaripia Mtume wake na kipenzi chake (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya kuwa kipofu yule hawezi kuuona uso wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) wala kujua kuwa amekasirikiwa.

Ikiwa aayah hizi ameshushiwa Uthmaan (Radhiya Allaahu Anhu), kwa nini basi asikaripiwe kwa unafiki na ukafiri wake kama Mashiah wanavyoamini kuwa yeye ni mnafiki. Wakati kitendo cha unafiki ni kikubwa zaidi na kinachostahiki zaidi kukaripiwa kuliko kukunja uso.

Wengine wakasema kuwa eti mwana wa Ummi Maktum hakuwa akiuliza mambo ya Diyn, bali ni mambo ya kidunia tu ndiyo maana akamuendea Uthmaan!

Enyi Shiah! Hebu zingatieni vizuri mtiririko wa hizi aayah:

Mwenyezi Mungu Anasema:

Lakini anayekukimbilia. (Ewe Uthmaan?) Naye anaogopa (Anaogopa nini?). Wewe unapuuza (Usifanya hivyo, sivyo! Hakika hii (Qur-aan) ni nasaha huenda yeye atatakasika (Akatakasika na nini?).

Kama aayah hizi ametereshiwa Uthmaan (Radhiya Allaahu Anhu), basi ni sifa kubwa kwake kwa kukimbiliwa na kutakiwa amsikilizishe kipofu yule mawaidhah apate kuongoka.

Kwa kila mwenye kupenda haki, musikubali kudanganywa na tafsiri kama hizi zenye kubadilisha maneno ya Mwenyezi Mungu na kupotosha.

Hii si mara ya mwanzo kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) kukosolewa ndani ya Qur-aan tukufu. Na sisi tunaamini kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) hakosolewi kwa kuwa amefanya kitendo cha dhambi, bali hukosolewa kutokana na kujitahidi kwake sana au kwa ajili ya huruma nyingi aliyonayo au kwa ajili ya kuwataka watu waingie haraka ndani ya Diyn ili waepukane na Moto kama ilivyoelezwa katika Suuratul-Kahf.

Mwenyezi Mungu Anasema:

ٰ ٰ

{{Labda unajiangamiza nafsi yako kwa kusikitikia hali yao kuwa hawaziamini Hadiyth hizi. Usijihuzunishe hivyo, kama hawataki kuamini basi.}} [Al-Kahf: 6]

Ifuatayo ni mifano mingine michache:

Mwenyezi Mungu Anasema:

ۖ ۚ

{{Ewe Nabii! Kwa nini unaharimisha Alichokuhalilishia Mwenyezi Mungu? Unatafuta kuwaridhi wake zako. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.}} [At-Tahriym: 1]

Na Akasema:

ٰ

{{Haimpasii Nabii na wale walioamini kuwatakia msamaha washirikina, ijapo kuwa ni jamaa zao, baada ya kwisha bainika kuwa hao ni watu wa Motoni.

At-Tawbah -113

Na Akasema:

.

Haimfalii Nabii yeyote kuwa na mateka mpaka awe ameshinda baraabara katika nchi. Munataka vitu vya dunia, na Mwenyezi Mungu anataka Akhera. Na Mwenyezi Mungu ni Mtukufu Mwenye nguvu Mwenye hikima.}} [Al-Anfaal: 67]

Sisi tunaamini kuwa hizi ni sifa njema na fahari kubwa kwa kiumbe kusemeshwa na kufundishwa na Mola wake (Subhaanahu wa Taala), na kukosolewa kwa ajili ya huruma zake na wala si sifa mbaya. Lakini wanayoyatambua haya ni wenye akili peke yao.

Mwenyezi Mungu Anasema:

﴿١٢٨﴾ ٰ ۖ ۖ

{{Amekufikieni Mtume aliye jinsi moja na nyinyi; yanamhuzunisha yanayo kutaabisheni; anakuhangaikieni sana, kwa Walioamini ni mpole na mwenye huruma. Basi wakidumu kukengeuka (hao makafiri), sema: Mwenyezi Mungu Ananitosheleza. Hapana wa kuabudiwa ila Yeye tu. Namtegemea Yeye, na Yeye ndiye Mola wa (hiyo) Arshi iliyo kubwa kabisa.}} [At-Tawbah: 128-129]

Ndani Ya Vitabu Vya Kishiah

Tafsiri sahihi kuwa aliyekusudiwa ni Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) zimo hata ndani ya vitabu vyao na tafsiri za Maulamaa wao wakubwa na maarufu, na zinakubaliwa na wanavyuoni mbali mbali wa Shiah kuwa aliyekusudiwa ni Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) .

Anasema At-Tubrusiy ambaye ni mmoja katika Maulamaa wakubwa wa Shiah Ithna-Ashariyah: Kule kuambiwa Mtume alayhis salaam kuwa aliukunja uso wake siyo tuhuma, kwake. [Tafsiyr Majmaal Bayaan, ukurasa 266 Juzuu ya 10]

Tembelea tafsiri ya At-Tubrusiy katika anuani hii: http://www.holyquran.net/cgi-bin/majma.pl

Anaendelea kusema At-Tubrusiy:

Aayah hii imeteremshwa kwa ajili ya Abdullaah mwana wa Ummi Maktuum na jina lake ni Shurayh bin Maalik bin Rabiyah Al-Fahary, anayetokana na kabila la Bani Aamir bin Luay. Aliyemjia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) na wakati huo alikuwa akiwalingania Utbah bin Rabiyah na Abu Jahal bin Hishaam na Al-Abbaas bin Abdil Muttwalib na Umayah bin Khalaf akiwalingania wamuamini Allaah, akitarajia kusilimu kwao. Akasema (Mwana wa Ummi Maktuum): Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, nifunze na mimi katika Aliyokufunza Mwenyezi Mungu. Akawa anamuita huku akiyakariri maneno yale bila kujua kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ameshughulika na watu wengine. Mpaka kuchukizwa na kukabainika usoni mwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) kutokana na kukatwa maneno yake kila anapotaka kusema. Ikampitikia nafisini mwake kuwa wakubwa wa makafiri hawa watasema kuwa wafuasi wake ni vipofu na watumwa, akageuka asimjibu na kuwaelekea wale aliokuwa akiwalingania, ndipo zilipoteremka aayah.

Akawa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya siku ile akimkirimu na kila anapomuona, husema: Karibu ewe ambaye kwa ajili yake Amenikosoa Mola wangu. Kisha humuuliza: Una haja yoyote?: Na alimpa ugavana wa mji wa Madiynah mara mbili.

Anaendelea kusema At-Tubrusiy ambaye ni mmoja wa Maulamaa wakubwa wa Shiah akijibu hoja za wenye madai hayo:

Kutajwa kuwa Mtume (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa amekunja uso siyo tuhuma kwake. Kama mtu atasema: Ikiwa kweli amekosolewa, hii ina maana kuwa kumkunjia mtu uso ni dhambi?

Jawabu: Kukunja uso au kutabasamu mbele ya uso wa kipofu si kitendo cha dhambi kwa sababu kitendo hicho hakimdhuru, na kwa ajili hiyo si kitendo cha dhambi.

Huenda ikawa Mwenyezi Mungu Amemkosoa Mtume wake (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) ili awe na tabia bora kupita zote na kumtanabahisha juu ya utukufu wa Muislamu anayetafuta uongofu na kumjuulisha kuwa kumuongoza Muislamu apate kuthibiti katika imani yake ni bora kuliko kutegemea kusilimu kwa mshirikina.

(Mwisho wa kunukuu maneno ya At-Tubrusiy)

Mwanachuoni mwengine wa Kishiah aitwae Al-Jibaiy anasema: Ndani yake mna fundisho kuwa hapo mwanzo kitendo cha kukunja uso hakikuwa cha dhambi, mpaka amri ya kukataza ilipoteremka.

Anaendelea kusema:

Imepokelewa kuwa Mtume (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa kila anapomuona Abdullaah mwana wa Ummi Maktuum humuambia: Karibu karibu, hapana Wallah! Mwenyezi Mungu Hatonikataza tena juu yako. Na alikuwa mpole sana kwake.

Maneno kama haya pia yamenukuliwa kutoka mmoja katika Maulamaa wakubwa wa Shiah Muhammad Haadi Al-Yuusufiy kutoka kwa At-Tubrusiy katika kitabu chake Encyclopedia ya Taariykh Juzuu ya 1, ukurasa 494.

Na maneno hayo pia yameandikwa na mwanachuoni wa Kishiah Al-Majlisiy katika Bihaar al Anwaar, juzuu ya 17, ukurasa wa 78.

Yamenukuliwa maneno kama haya pia kutoka kwa mwanachuoni mkubwa wa Kishiah katika wakati wetu huu Muhammad Husayn Fadhlullah katika tafsiri yake Wahyul Qur-aan.

Atakaye anaweza kuutembelea ukurasa huo katika mtandao wake unaopatikana penye anuani ifuatayo: http://arabic.bayynat.org.lb/books/quran/abas1.htm

Hebu tumsikilize Ayatullah Muhammad Husayn Fadhlullah akiwajibu Mashiah wenzake wanaosema kuwa waliokusudiwa katika aayah zile ni Uthmaan au mtu katika watu wa kabila la Bani Umayyah. Anasema mwanachuoni huyu wa Kishiah:

Riwaya inayonasibishwa na Imaam Asw-Swadiq (Radhiya Allaahu Anhu) kuwa aayah imeteremshwa kwa ajli ya mtu wa kabila la Bani Umayyah haikubaliani na mtiririko wa aayah. Kwa sababu ni wazi kuwa kusudi la aayah hizo ni kuwa aliyekusudiwa ni mtu mwenye kumiliki sehemu muhimu katika kuifikisha risala na kwamba mtu huyo anabeba jukumu la kuwatakasa na kuwafundisha wale waliokwisha hidika na kuikubali risala hiyo kwanza, ili wawe na msingi mzuri na uwezo wa kuifikisha Dini kwa watu, kinyume na wale wasiohidika ambao hawastahiki kupewa juhudi kubwa.

(Mwisho wa maneno ya Muhammad Husayn Fadhlullah)

Kutokana na haya, tunaona kuwa waliosema kuwa aliyekusudiwa katika aayah zile ni Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) si Masunni peke yao. Bali pia yamesemwa na Maulamaa wakubwa wa Kishiah ambao ni At-Tubrusiy, Al-Majilisy, Al-Yuusufiy na Muhammad Husayn Fadhlullah kama tulivyoona.

Na hii chini ni anuani ya mtandao unaoitwa Az-Zahraa wa mwanachuoni wao aliyesema uongo juu ya aayah hizi, na ndani ya mtandao huu zimo hotuba mbili za Muhammad Fadhlullah akitamka kuwa aayah hizo ziliteremshwa kwa ajili ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam).

http://www.mezan.net/sounds_files/sounds1/7/r007.html