Kusamehe

 

Vijana watatu walikwenda mbele ya Khalifa  wa  Waislamu Umar bin Al Khattab (Radhiya Llahu anhu) wakiwa wamemkamata mtu waliyemfunga kamba. Wakasema kumwambia Umar (Radhiya Llahu anhu):

"Mtu huyu amemuuwa baba yetu na amekiri juu ya jambo hilo, isipokuwa ametuomba tumpe siku tatu ili aweze kusafiri kwa wanawe kwa ajili ya kuwajulisha juu ya hazina aliyoifukia mahala ambapo hapana anayepajuwa isipokuwa yeye peke yake".

 

Sahaba mmoja aitwae Abu Dhar Al Ghafariy (Radhiya Llahu anhu) akamdhamini mtu huyo juu ya kuelewa kwake vizuri kuwa iwapo mtu huyo hatorudi basi atauliwa yeye badala yake.

 

Mtu huyo hakurudi mpaka baada ya kukaribia sana kumalizika muda wa siku tatu hizo, na watu wakawa na wasi wasi asije Abu Dhar (Radhiya Llahu anhu) akauliwa badala yake.

Dakika za mwisho za siku ya tatu akawasili mtu huyo akiwa amejaa vumbi na huku uso wake ukionesha dalili za kuchoka sana.

Umar (Radhiya Llahu anhu)akamuuliza:

"Ilikuwaje ukarudi wakati ungeweza kukimbia?"

Akajibu:

"Nilihofia pasije pakasemwa kuwa; Watu wenye ahadi za kweli hawapo tena."

 

Kisha Umar (Radhiya Llahu anhu)akamgeukia Abu Dhar (Radhiya Llahu anhu)na kumuuliza:

"Na wewe ilikuwaje ukakubali kumdhamini mtu huyu wakati humjuwi?"

Abu Dhar (Radhiya Llahu anhu)akasema:

"Nilihofia pasije pakasemwa; Wakarimu na wenye moyo wa kishujaa hawapo tena."

 

Ndipi wale vijana watatu wakasema:

"Na sisi tumemsamehe mtu huyu ili pasije pakasemwa; 'Hawapo tena watu wenye kusamehe juu ya kuwa na uwezo wa kulipa kisasi."