AL  I M A N. 1

UTANGULIZI WA MFASIRI. 2

UTANGULIZI WA WATUNGAJI. 2

IMANI NI ITIKADI NA MATENDO.. 5

AMALI (Matendo) NI AINA NYINGI. 6

IMANI HUZIDI NA KUPUNGUA.. 6

KUZITAKASA NYOYO. 7

MOYO MSAFI NI MOYO WA MWENYE KUAMINI. 7

KUUPENDA UKWELI NA KUUFUNGULIA MOYO UISLAMU. 7

KUITIKIA MWITO WA IMANI NA KUPENDA KUIONGEZA. 8

KUJIKUMBUSHA. 9

YAKINI. 9

KULAINISHA NYOYO KWA KUMDHUKURU MWENYEZIMUNGU. 10

KUFUATA QURANI NA SUNNAH.. 11

KUMWAMINI MWENYEZI MUNGU. 12

ELIMU NI NJIA YA IMANI. 12

DALILI ZA KIELIMU ZINAZOITHIBITISHA IMANI JUU YA MWENYEZIMUNGU. 13

a)MSINGI WA MWANZO. 13

ALIYEKUWEPO.. 13

b) MSINGI WA PILI. 13

UKIICHUNGUZA BIDHAA ITAKUJULISHA BAADHI YA SIFA ZA MTENGENEZAJI. 13

ALIYE HAI - AMBAYE YUPO MILELE - (AL HAY). 14

MWENYE KUJUWA (Kila kitu) - (AL ALIYM). 15

MWENYE HIKIMA - (AL HAKIYM). 16

AZ ZUKHRUF - 84. 17

MWENYE UJUZI WA KILA JAMBO - (AL KHABIYR). 17

MTOAJI WA RIZIKI - (AL RAZZAAQ). 18

MWENYE KUONGOZA - (AL HAADIY). 19

MLINZI (AL HAAFIDH). 20

SIFA NYINGINE. 21

MMOJA TU ALIYE PEKEE (AL WAAHIDUL AHAD). 22

NANI MWENYE SIFA ZOTE HIZI?. 23

MSINGI WA TATU - ASIYEKUWA NA KITU HAWEZI KUTOA.. 23

NI NINI HAYA MAUMBILE?. 23

MAMBO YANAYOBABAISHA WATU  NA MAJIBU YAKE. 24

KUJIBU UPOTEVU WA MANASARA.. 24

ANAYEMJIBU ALIYEDHIKIKA ANAPOMUOMBA.. 25

MSIMAMO WA MAKAFIRI DHIDI DALILI ZA IMANI. 26

KUIGIZA KATIKA KUKUFURU, 26

UZUSHI WA MAMBO YANAYOBABAISHA.. 26

KUWEKA MASHARTI ILI WAAMINI. 28

KUMJUA MWENYEZIMUGU KWA MAJINA YAKE NA SIFA ZAKE. 28

WAHYI NDIYO NJIA BORA KATIKA KUYAJUA MAJINA NA SIFA ZA MWENYEZIMUNGU. 29

KUMTAKASA MWENYEZIMUNGU KWA KUTOMFANANISHA NA VIUMBE. 30

KUYAAMINI MAJINA NA SIFA ZA MWENYEZI MUNGU KAMA YALIVYO.. 30

KATIKA QURANI NA SUNNAH.. 30

HAIWEZEKANI KUUJUWA MFANO WAKE. 31

AKILI NA KUFIKIRIA.. 31

MAJINA MAZURI MAZURI. 32

USHAHIDI KWAMBA MUHAMMAD(SAW) NI MTUME WA MWENYEZIMUNGU. 32

MUUJIZA WA QURANI. 33

UFASAHA WA QURANI NA KUTOKUCHOSHA KWAKE. 33

QURANI YAELEZA MAMBO YA GHAIBU. 34

MIUJIZA YA SAYANSI KATIKA QURANI. 36

 

AL  I M A N

 

UTANGULIZI WA MFASIRI

Nashuhudia kuwa hapana Mola anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Allah na kwamba Muhammad(SAW) ni Mtume Wake . Ameufikisha ujumbe, ameituwa amana aliyopewa na akapigana Jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu kama alivyopaswa, basi Sala na Salam zimfikie Yeye na Aali na Masahaba wake watukufu.

Amma Baad,

Hii ni tafsiri ya kitabu kilichoandikwa na Sheikh Abdul Majeed Al Zindani akishirikiana na wanavyuoni wengine watano nao ni;

Abdullah Al Wadh-aaf

Ahmed Salama

Feisal Abdul Aziz

Hizam Al Bahluli

Tawhid Abdul Hameed

Kitabu hiki kwa lugha ya kiarabu kimepitiwa na wanavyuoni mia moja, na majina yao yameandikwa ndani ya kitabu hicho cha  "Al Iman".

Hiki ni kitabu kilichojaa faida nyingi sana .

Sheikh Abdul Majeed  Al Zindani ni miongoni mwa wanavyuoni wakubwa wa Kiislamu na anajulikana sana kwa umahiri wake katika uwanja wa mada za 'Miujiza ya Sayansi katika Qurani'. Ameshiriki katika utafiti, tahakiki, mikutano, majadiliano na pia ametunga vitabu vingi sana kuhusu mada hiyo.

Hivi sasa (wakati wa kukifasiri kitabu hiki) yeye ni Mkuu wa baraza la Shuura huko Yemen, na pia ni mjumbe wa kudumu katika baraza kuu la 'Miujiza ya Sayansi katika Qurani ulimwenguni', na makao yake ni huko Misri.

Nilimpigia simu Sheikh Al Zindani na kuzungumza naye kuhusu kukifasiri kitabu hiki kwa vile yeye ni mtungaji na mwenye haki za kupiga chapa akanijibu;

"Vitabu vyangu vyote ni Wakfu kwa Waislamu wote, na mimi sina haki yoyote ndani yake, nakuruhusu kukifasiri na kuuza tafsiri yako unapotaka, isipokuwa tu usiwauzie ndugu zako kwa bei ya ghali'.

 

MUHAMMAD FARAJ SALIM AL SAAIY

 

 

UTANGULIZI WA WATUNGAJI

Hakika shukurani zote anastahiki Mwenyezi Mungu, tunamuomba atusaidie katika shida zetu, atusamehe madhambi yetu, atukinge na shari za nafsi zetu na shari za amali zetu ovu. Atakaye Mwenyezi Mungu kumuongoza hakuna awezaye kumpoteza na anayeachiwa basi hana uongofu.

Nakiri kwamba hapana apasaye kuabudiwa isipokuwa Mwenyezi Mungu pekee asiye na mshirika, na ninakiri kwamba Muhammad (SAW) ni Mtume wake na mjumbe wake.

Wa - baad,

Wajibu wa kwanza wa kila mwanadamu ni kumjua Mwenyezi Mungu kwa njia ya Ilimu. Mwenyezi Mungu anasema :

"Juwa ya kwamba hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu".

 ( Muhammad - 19 )

Wajibu wa pili ni kumjua Mtume wa Mola wake, na ukweli wa ujumbe wake, kwa njia ya Ilimu inayompelekea kuwa na yakini.

 Mwenyezi Mungu anasema:-

"Jee anayejua kwamba yaliyoteremshwa kwako kutoka kwa Mola wako ni haki (akayafuata basi) ni kama aliyekipofu? Wenye akili ndio wanaozingatia".

(  Al - Raad -19)

Kila mwanadamu lazima aijue hikima (sababu) ya kuumbwa kwake katika dunia hii, na ajue mwisho wa safari yake hii anayokwenda na aijue Dini ya Mola wake ambayo ameamrishwa kuifuata".

Iwapo ubora wa Ilimu unajulikana kutokana na somo lenyewe basi Ilimu ya Imani ni somo linalohusiana na kumjua Mwenyezi Mungu na Mtume wake(SAW) na kuijua dini yake.

Na kama ilivyo, umuhimu wa kazi yo yote ile unaambatana na faida inayopatikana na kazi hiyo, pamoja na hatari ambayo nafsi hujikinga kwa Ilimu hiyo, basi Ilimu ya Imani inampatia binaadamu furaha na ushindi mkuu duniani na akhera. Mwenyezi Mungu amewaahidi wale waloamini mambo mengi hapa duniani.

 

Ushindi Juu Ya Maadui Zao. -

 Mwenyezi Mungu anasema :

"Na ni wajibu juu yetu kuwanusuru wale walioamini."

(  Al-Ruum - 47)

 

Kuwakinga.   -

 Mwenyezi Mungu anasema:-

"Hakika Mwenyezi Mungu huwakinga wale wanaoamini."

(Al - Hajj - 38)

 

Kuwalinda. -

 Mwenyezi Mungu anasema:

   "Mwenyezi Mungu ni Mlinzi wa wale walioamini."

(Al-Baqarah- 257)

 

Kuwaongoza. -

 Mwenyezi Mungu anasema:

"Na kwa yakini Mwenyezi Mungu ndiye awaongozaye wale walioamini katika njia iliyonyooka."

(Al-Hajj - 54)

 

Kutoshindwa na Makafiri. -

 Mwenyezi Mungu anasema:

"Na Mwenyezi Mungu hatawajaalia makafiri njia ya kuwashinda Waislamu."

(An- Nisaa - 141)

 

Kusimamisha Dini Yao Na Kuwafanya Makhalifa. - 

Mwenyezi Mungu anasema;

"Mwenyezi Mungu amewaahidi wale walioamini miongoni mwenu na kufanya vitendo vizuri kuwa atawafanya Makhalifa katika ardhi kama alivyowafanya makhalifa wale waliokuwepo kabla yao, na kwa yakini atawasimamishia dini yao aliyowapendelea na atawabadilishia  amani baada ya hofu yao "

(Al-Nur-55)

 

Riziki Njema .-

 Mwenyezi Mungu anasema :-

"Na lau kama watu wa miji wangeliamini na kuogopa kwa yakini tungeliwafungulia baraka za nbinguni na ardhini"

(Al aaraf 96)

 

Utukufu. -

 Mwenyezi Mungu anasema:-

"Na utukufu hasa ni wa MwenyeziMungu na Mtume wake na wa Waislamu"

(Al Munafiqun-8)

 

Maisha Mema. -

Mwenyezi Mungu anasema :-

"Wafanyaji mema wanaume na wanawake, hali ya kuwa wao ni Waislamu, tutawahuisha maisha mema "

 (Al-Nahli-97)

 

 Haya ni baadhi ya mambo watakayopata Waislamu hapa duniani, na haya ndio waliyoyapata wenzetu waliotangulia, walioamini kikweli.

Ama kuhusu Nyumba ya Akhera, Mwenyezi Mungu anasema:

"Kwa yakini walioamini na kufanya vitendo vizuri makazi yao yatakuwa hizo Pepo za Firdausi. Watakaa milele humo hawatataka kuondoka."

(Al-Kahf -107-108)

Na akasema:

"Bila shaka wale walioamini na wakafanya vitendo vizuri, zitakuwa kwao mabustani ya neema (peponi).Watakaa humo milele ni ahadi ya Mwenyezi Mungu iliyo haki na Yeye ndiye Mwenye Nguvu (na) Mwenye Hekima."

(Luqman 8-9)

 

Anayechunguza hali za Waislamu leo, ataona kwamba yale ambayo Mwenyezi Mungu amewaahidi Walioamini hapa duniani hawajayapata, huu ni uthibitisho kwamba Imani zao ni dhaifu au wamepoteza sifa nyingi za Imani, na hii ndio sababu ya kupoteza yale waliyoahidiwa na Mola wao hapa duniani kama vile Ushindi juu ya maadui, Kuwakinga, Kuwalinda, Uongofu, Kuwa Watukufu ulimwenguni, Kutoshindwa na makafiri, Riziki njema, Utukufu na Maisha mema.

Atakayendelea na hali hii basi atayakosa hata yale ambayo MwenyeziMungu amewatayarishia Walioamini, huko Akhera, na kama walivyokula hasara hapa duniani,  basi huenda wakapata hasara ya kuingizwa katika Moto wa Jahannam.

 

Kwa hivyo lazima tuitie nguvu Imani, tuithibitishe na kuiongezea nguvu mara kwa mara kwa njia ya kueneza Ilimu ya Imani baina ya Waislamu, na kufuata Sheria za Dini.

Ni wajibu wa Ma-Ulamaa kujitolea na kusimamia wajibu huu, hasa wakiwa wanaona namna wale wasioamini Mungu wakiwashambulia Waislamu na kujaribu kuwaingiza katika dini zao, na pia wakiwa wanaona namna zinavyoenea itikadi zisizo na msingi wa Kiislamu na mambo yaliyo batili ambayo hao wanaoyaeneza wanajaribu kuyanasibisha maovu hayo na Uislamu.                

 

Kwa hivyo kitabu hiki cha Imani tunakiweka mikononi mwa Waislamu kikiwa ni miongoni mwa vitabu vinavyofunza wajibu wa Dini na tunamuomba MwenyeziMungu akijaaliye kiwe ni kwa ajili Yake tu, na kiwafae Waislamu .

Nasi tunamuomba kila mwenye kuionea uchungu Dini yake afanye kila juhudi ili ajifunze na awafunze watu wake, jirani zake pamoja na Waislamu wengine, na MwenyeziMungu ndiye anayefanikisha .

 

WATUNGAJI

 

 

IMANI NA UHAKIKA WAKE

MwenyeziMungu amekwishawabainishia waja wake Imani gani inayokubaliwa na kuwafanya wayapate yale waliyoahidiwa na Mwenyezi Mungu

 

IMANI NI ITIKADI NA MATENDO

MýwenyeziMungu anasema;-

"Wenye kuamini kweli kweli ni wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake kisha wakawa si wenye shaka na wakaipigania dini ya Mwenyezi Mungu kwa mali zao, hao ndio wenye kuamini".

(Al-Hujurat- 15)

Kutokana na aya hii, tunaona kuwa Imani inayokubaliwa na iliyo ya kweli, ni itikadi isiyochanganyika na shaka, pamoja na kuipigania Dini kwa mali na nafsi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.

Hii ni kwa sababu kuamini kwa moyo peke yake tu hakutoshi kukubaliwa kwa Imani, kwani Iblisi alikuwa akiamini kuwepo kwa Mwenyezi Mungu, kama ilivyoandikwa katika Qurani kwamba alitamka akasema:-

"Mola wangu nipe nafasi ya kuishi nisife mpaka siku watakayofufuliwa viumbe".

(Sad 79). 

Juu ya hayo, MwenyeziMungu amekwishampa sifa ya ukafiri kwa sababu ya kutakabari kwake kwa kukataa kufuata amri ya Mola wake.

MwenyeziMungu anasema:-

"Isipokuwa iblisi akakataa na akajivuna na (tokea hapo) alikuwa katika makafiri".

(Al- Baqarah-34).

 

Kwa Hivyo Imani Ya Haki Ni Ile Iliyokusanya yafuatayo:-

1)      Itikadi iliyo thabiti na isiyokuwa na shaka.

2)      Matendo yanayosadikisha Imani hiyo, nayo ni matunda yake.

 

AMALI (Matendo) NI AINA NYINGI.

·                    Matendo ya Moyo, - kama vile kumuogopa Mwenyezi Mungu, kumuelekea na kumtegemea Yeye peke Yake.

·                    Matendo ya Ulimi, - kama vile kutoa shahada mbili kumtukuza na kumuomba maghfira Mwenyezi Mungu, pamoja na kuwalingania watu katika njia Yake.

·                    Matendo ya Kiwiliwili, - mfano wa Sala, Kutoa Zaka, Kufunga, Kupigana Jihadi katika njia ya MwenyeziMungu, kutafuta Ilimu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, kufanya biashara, kulima na kutengeneza vitu viwandani ili kuihakikishia amri ya MwenyeziMungu ya kuwafanya watukufu katilka ardhi kutokana na mafunzo ya Kiislamu.

 

IMANI HUZIDI NA KUPUNGUA

Zipo sababu zenye kuzidisha Imani, -

MwenyeziMungu anasema:-

"Na wanaposomewa aya zake huzidi Imani".

(Anfal -2).

Na katika kumuasi Mwenyezi Mungu Imani inapungua.

Mtume (SAW) anasema:-

"Na wala hazini mzinifu wakati anapozini akawa yeye ni mwenye Imani (Muumin)".

Na maana yake ni kama ifuatavyo;

'Pale mtu anapozini, huwa hana sifa ya Imani'.

 

 

Tukitaka kufanikiwa kuipata Imani ya kweli, hatuna budi kuisimamisha Imani hiyo kwa njia zifuatazo:-

1)       Kuisadikishe nyoyoni kwa njia ya Ilimu .

2)      Kutafakari katika  dalili za MwenyeziMungu zilizomo ulimwenguni na zilizomo katika Qurani, pamoja na kujikumbusha ahadi aliyotupa MwenyeziMungu juu ya Pepo, pamoja na maonyo (juu ya Moto).

3)     Matendo ya Ulimi , - Kama vile kumtaja MwenyeziMungu sana, kutamka maneno ya haki na kulingania watu katika njia ya MwenyeziMungu pamoja na kuamrisha mema na kukataza mabaya, kujielimisha pamoja na kuelimisha na kuusiana katika kufuata haki na kuusiana katika kushikamana na subira.

4)      Matendo ya viungo, - kama vile kutekeleza nguzo za Uislamu, jitihada kwa ajili ya kusimamisha neno la MwenyeziMungu kwa hali na mali pamoja na kuilazimisha nafsi itii amri za MwenyeziMungu na kukaa na wale walio wema:

MwenyeziMungu amesema :-

"Na ujiweke pamoja na wale wanaoabudu Mola wao asubuhi na jioni, hali ya kuwa wanataka radhi Yake, wala macho yako yasiwavuke (hawa ukawatafuta wengine) kwa kutaka pambo la maisha ya dunia wala usiwatii wale ambao tumezighafilisha nyoyo zao wakafuata matamanio yao, na mambo yao yakawa yamepita mipaka.

Na sema "huu ni ukweli uliotoka kwa Mola wenu, basi anayetaka  na aamini na  anayetaka na akufuru".

(Al-Kahf 28-29).

 

Haya yote yanahitajia kuongoka kwa nyoyo na kuzisafisha kutokana  na maradhi yanayomzuia mtu asipate hidaya ya Mola wake.

 

 

KUZITAKASA NYOYO.

 

Mwenyezi Mungu anasema;

"Siku ambayo hayatofaa mali wala watoto isipokuwa mwenye kuja kwa MwenyeziMungu na moyo msafi. (huyu ndie atakaepata ya kumfaa)."

(Al-Shuraa-88).

 

MOYO MSAFI NI MOYO WA MWENYE KUAMINI.

Kama vile ardhi inayofaa kulimiwa ina sifa zake, na moyo wa aliyeamini pia una sifa zake nazo ni:

1)      KUIKUBALI HAKI.

Kuikubaili haki ni Jambo linalompelekea mtu kuujua ukweli na kuufuata.

MwenyeziMungu amesema :-

"Habari njema (bushara njema) ni zao.Basi wape habari njema waja wangu (hawa) ambao husikiliza kauli nyingi zinazosemwa. Wakafuata zile zilizo njema . Hao ndio aliowaongoa MwenyeziMungu na hao ndio wenye akili .

(Azzumar-17).

Ama nyoyo zilizokufuru-zenye maradhi utaziona daima zinaipinga haki, hubaki na ujinga na wala haziongoki.

MwenyeziMungu amesema:-

"Na haiwafikii hoja yoyote katika hoja za Mola wao ila wanakengeuka (wanaibishia).

(Al-An-Am - 4).

 

KUUPENDA UKWELI NA KUUFUNGULIA MOYO UISLAMU.

Mwenye moyo msafi daima huwa anaipenda haki na anaupenda ukweli na moyoni mwake huipenda Dini na hutaka kusoma juu ya Dini ya Kiislamu. Kwa hivyo mtu wa namna hiyo anaistahiki Hidaya ya MwenyeziMungu.

Ama mwenye moyo ulio na maradhi huichukia haki na huona dhiki kifuani pake anaposikia juu ya Uislamu. Kwa ajili hiyo anajitakia mwenyewe adhabu ya MwenyeziMungu kutokana na kujipotosha yeye mwenyewe.

MwenyeziMungu amesema:-

"Basi yule ambaye MwenyeziMungu anataka kumuongoza, humfungulia kifua chake Uislamu; na yule ambaye MwenyeziMungu anataka kumhukumu kupotea humfanya kifua chake kizito kinaona taabu kubwa (kufuata huo Uislamu); kama kwamba anapanda mbinguni (kusikokua na pumzi).

(Al-An-Am -125).

Na hii ni kwa sababu ya kuichukia kwao haki.

MwenyeziMungu anasema:-

"Basi amewajia (Nabii Muhammad ) kwa haki na wengi katika wao wanaichukia haki"

Al-Muumin - 70).

 

KUITIKIA MWITO WA IMANI NA KUPENDA KUIONGEZA.

Mwenye moyo msafi huuitikia mwito wa Imani, kama alivyoeleza MwenyeziMungu juu ya wenye nyoyo safi aliposema;

"Mola wetu tumemsikia mwitaji anayeita mwito wa Imani kwamba "Muaminini Mola wenu" Tukaamini, Mola wetu tusamehe madhambi yetu na utusamehe makosa yetu na utufishe na watu wema".

(Al-Imran - 193)

Mwislamu, siku zote hupenda Imani yake izidi.

MwenyeziMungu anasema  :-

"Na inapoteremka sura (mpya ya Qurani ) wako miongoni mwao (watu wanafiki) wasemao, "Ni nani miongoni mwenu (sura hii) imemzidishia imani?" Ama wale walioamini inawazidishia imani nao wanafurahi. Ama wale wenye ugonjwa nyoyoni mwao basi inawazidishia ubaya (mpya) juu ya ubaya waliokuwa nao."

(Al -Tawba- 124-125).

Ama wenye nyoyo zenye maradhi utawaona daima wanawazuilia watu njia ya MwenyeziMungu .

MwenyeziMungu anasema:-

"Wale wanaofadhilisha maisha ya dunia kuliko akhera na wakawazuilia (watu) njia ya MwenyeziMungu na wanataka kuipotoa (na hali ya kuwa si potofu) hao wamo katika upotofu (upotevu ) ulio mbali na haki".

(Ibrahim - 3).

Wenye nyoyo safi utawaona siku zote wanatafakari katika nafsi zao, na namna zilivyoumbwa mbingu na ardhi, na wanatafakari katika uongofu  uliowajia kutoka kwa Mola wao, ukiwafahamisha hikima ya kuishi kwao na ya kufa kwao, walikotokea na wanakoelekea pamoja na Pepo aliyowatayarishia MwenyeziMungu waja wake walioamini, na adhabu inayowasubiri makafiri, na wanatafakari juu ya miujiza ya Mtume (SAW) na juu ya ushahidi wa ukweli aliokuja nao na jinsi ya kutekeleza yale aliyowaamrisha ili wajipatie furaha ya dunia na ya akhera na ili wajiepushe na adhabu ya motoni.

MwenyeziMungu anasema:-

"Ambao humkumbuka MwenyeziMungu wakiwa wima na wakikaa na wakiwa wamelala na hufikiri katika kuumbwa mbingu na ardhi (wakasema) Mola, hukuviumba hivi bure utukufu ni wako basi tuepushe na adhabu ya moto.

(Al -Imraan 191)

Lakini makafiri wameyafunga masikio yao na akili zao, hawavitumii viungo hivyo katika kazi zake zilizoumbiwa ambayo ni kutafakari, kwa hivyo hawatakiri mpaka iwafikie siku ya majuto (siku ya kiama ) .

 

MwenyeziMungu anasema juu yao:-

"Na watasema; Kama tungelikuwa tunasikia na tungelikuwa na akili hatungekuwa katika watu wa motoni. Wakakiri dhambi zao (lakini hapana faida) basi kuangamia kumewastahikia watu wa Motoni (leo)".

 

KUJIKUMBUSHA.

Binaadamu husahau, lakini mwenye moyo msafi hukumbuka na kuiona njia.

MwenyeziMungu anasema :-

"Wale wanaomuogopa MwenyeziMungu zinapowagusa pepesi za shetani (wakaasi) mara hukumbuka, tahamaki wamekwisha ona njia".

(Al -Aaraf-201).

Ndio sababu MwenyeziMungu akaamrisha kukumbushana, akasema;

"Endelea kuwakumbusha, maana ukumbusho huwafaa wanaoamini."

(Al- Dharia 55).

Na akasema :-

"Basi waidhishe ikiwa utafaa waadhi. bila shaka atakumbuka mwenye kumuogopa (MwenyeziMungu), na mwingi wa mateso atajitenga nayo hayo (mawaidha) ambaye atauwingia moto mkubwa. Kisha humo hatakufa wala hatakuwa hai"

(A -Alaa 10 - 13)

Ama wenye nyoyo zilizo na maradhi utawaona wameghafilika wala hawaamini.

MwenyeziMungu amesema:-

"Na uwaonye siku ya majuto wakati amri (ya kuingia Peponi na Motoni) itakapokatwa. Nao hapa duniani wapo katika ghafla wala hawaamini"

("Maryam - 39 ).

 

Baadhi ya walioghafilika unapowakumbusha juu ya siku ya kiama huenda wakakuambia;

"Unakuja leo kunifundisha Uislamu? Mimi ni Mwislamu bora kuliko wewe".

 

YAKINI     

Mwenye moyo msafi, mwenye kutafakari na kujielimisha na Kujikumbusha utamuona keshaifikia Yakini kama alivyobainisha Mola wetu katika kauli yake:-

"Bila ya shaka katika mbingu na ardhi zimo alama kubwa (za kuonyesha kuwa yupo MwenyeziMungu) kwa ajili ya wanaoamini. Na katika umbo lenu na katika viumbe alivyovitawanya zimo alama (vile vile) kwa watu wenye Yakini".

(Al - Jathiyah -3-4)

Ama yule aliyeghafilika, anayebisha utamuona siku zote yumo katika shaka.

MwenyeziMungu anasema:-

"Lakini hao makafiri wamo katika shaka na wanacheza tu".

(Al Dukhan -9).

Na wala hawaijui yakini isipokuwa kama alivyosema  MwenyeziMungu:-

"Na ungaliwaona waovu wakiinamishwa vichwa vyao mbele ya  Mola wao, (Na kusema) tumekwishaona na tumekwisha sikia basi turudishe tufanye vitendo vizuri, hakika (sasa) tumeyakinisha (ungaliwaona katika hali hiyo ungaliwaona dhila yao")

(As -Sajdah -12)

 

KULAINISHA NYOYO KWA KUMDHUKURU MWENYEZIMUNGU.

Wenye nyoyo safi, nyoyo zao na ngozi hulainika kwa kumkumbuka MwenyeziMungu pamoja na kutafakari juu ya dalili Zake.

Ama makafiri nyoyo zao huwa ngumu na hazilainiki kwa dalili zozote zile.

MwenyeziMungu anasema :-

"Je! Mtu ambaye MwenyeziMungu amemfungulia (amemfungua) kifua chake kuukubali uislamu akawa yumo katika nuru itokayo kwa Mola wake (ni sawa na mwenye moyo mgumu?) Basi adhabu kali itawathibitikia wale wenye nyoyo ngumu wasimkumbuke MwenyeziMungu. Hao wamo katika upotofu (upotevu) ulio dhahiri, MwenyeziMungu ameteremsha hadithi nzuri kabisa (kwa kuteremshwa) kitabu chenye maneno yanayowafikiana, (yasiyopingana) na yanayokaririwa (bila kuchosha) husisimka kwayo ngozi (miili) za wale wanaomuogopa Mola wao, ikisha ngozi zao na nyoyo zao huwa laini kwa kumkumbuka Mola wao."

(Az-Zummar -22-23)

 

   Na utawaona wenye nyoyo ngumu hizo wanajivuna na wanakuwa wakaidi pamoja na kukanusha dalili za Mola wao.

MwenyeziMungu anasema :-

"Na wakazikanusha na hali ya kuwa nafsi zao zina yakini nazo, wanazikanusha kwa dhulma na kujivuna”.

(Al - Naml -14).

 

Na hawa wanaotakabari wataadhibishwa.

MwenyeziMungu anasema:-

"Nitawaepusha na (kuzingatia) Aya zangu wale wanaotakabari katika nchi pasipo na haki".

(Al -Aaraf 146).

Haya ni malipo yao hapa duniani, ama siku ya kiama malipo yao yatakuwa kama alivyosema MwenyeziMungu:-

"Na (wakumbushe) siku watakapowekwa waliokufuru mbele ya moto (waambiwe) mlipoteza vitu vyenu vizuri katika maisha yenu ya duniani (basi hamtavipata leo hapa) Nyinyi  mlijifurahisha navyo (huko) basi leo mtapewa adhabu ya fedheha kwa sababu ya kule kujivuna kwenu bure duniani na kwa sababu ya kule kuasi kwenu."

(Al - Ahqaf 20).

 

KUFUATA QURANI NA SUNNAH

Utamuona mwenye moyo msafi ni mtiifu wa Mola wake na kwa Mtume wa MwenyeziMungu na utamuona kila jambo lake hulifanya kama kinavyoamrisha kitabu cha MwenyeziMungu (Qurani) na Sunnah (Mafundisho) ya Mtume wake (SAW).

 

MwenyeziMungu anasema:-

"Wale wanaoamini wanaume na wanawake, ni marafiki wao kwa wao. Huyaamrisha yaliyo mema na huyakataza yaliyo mabaya na  husimamisha Sala  na kutoa Zaka na humtii MwenyeziMungu na Mtume wake, hao ndio MwenyeziMungu atawarehemu, hakika MwenyeziMungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hekima ".

(Al - Tawba -71).

 

Mtu wa aina hii huwa kesha tii amri ya MwenyeziMungu isemayo:-

"Enyi mlioamini ! Mtiini MwenyeziMungu na Mtume".

(An -Nisaa -59).

 

Na ile isemayo:-

"Na anachokupeni Mtume basi pokeeni, na anachokukatazeni jiepusheni nacho, na muogopeni MwenyeziMungu, kwa yakini MwenyeziMungu ni mkali wa kuadhibu".

(Al - Hashir -7).

Hii ni kwa sababu kumtii Mtume (SAW) ni kumtii MwenyeziMungu.

MwenyeziMungu. Anasema:-

"Mwenye kumtii Mtume amemtii MwenyeziMungu (kwani anayoamrisha Mtume yametoka kwa MwenyeziMungu)”.

Annisaa- 79

Ama mwenye moyo ulio na maradhi utamuona akimfuata kila shetani  mwenye kuasi na hufuata matamanio yake na kujiabudia wengine wasiokuwa MwenyeziMungu, huyo atakuja kujuta, lakini siku hiyo majuto hayatosaidia kitu (majuto mjukuu).

MwenyeziMungu anasema:-

"Siku ambayo nyuso zao zitapinduliwa pinduliwa (zitapounguzwa) Motoni watasema "Laiti tungemtii MwenyeziMungu na tungemtii Mtume".

(Al -Ahzab -66).

 

Nyoyo zetu zikiwa na sifa njema zilizotajwa hapo mwanzoni, ndipo tutakapokuwa miongoni mwa wenye nyoyo safi, njema, zinazoweza kumea ndani yake mti wa Imani na kustawi kisha na kutoa mazao ya amali njema.

Iwapo katika nafsi zetu hatuoni amali njema, basi hii inatokana na udhaifu wa mti wa Imani uliomea ndani ya nyoyo zetu na ambao haujatimiza sifa za moyo mwema.

 

Na iwapo hatutofanya haraka kuzisafisha nyoyo zetu basi hali zetu hazitobadilika. 

MwenyeziMungu amesema:-

"Hakika MwenyeziMungu habadili yaliyoko kwa watu mpaka wabadili wao yaliyomo katika nafsi zao".

(Ar -Raad -11)

 

Na Mtume (SAW) amesema:-

'Ndani ya kiwiliwili mna kipande cha nyama, kikitengenea, basi mwili wote hutengenea, na kikiharibika, basi mwili wote unaharibika, kitu hichi ni moyo'.

Na moyo hautengenei isipokuwa kwa kuongezeka Imani ndani yake na kuimakinisha.

 

KUMWAMINI MWENYEZI MUNGU

Kumwamini MwenyeziMungu Ni Wajibu Wa Kila Mwanadamu

Mwanadamu akizingatia kidogo atagundua kwamba MwenyeziMungu aliyemuumba amemjaalia viungo ili aweze kujielilmisha navyo elimu zote za dini na za dunia, na bila ya vyombo hivyo hawezi kujielimisha chochote.

 MwenyeziMungu amesema :-"Na MwenyeziMungu amewatoeni matumboni mwa mama zenu hali ya kuwa hamjui chochote, na amekujaalieni masikio na macho na nyoyo ili mupate kushukuru.

(Al -Nahli -78).

 

Jambo la mwanzo la kumshukuru MwenyeziMunguni ni kuvitumia viungo hivi vya kujielimisha alivyotupa Mola wetu kwa ajili ya kumjua Yeye.

MwenyeziMungu anasema:-

"Jua ya kwamba hakuna aabudiwaye kwa haki isipokuwa MwenyeziMungu na omba maghfira kwa dhambi zako".

(Muhammad -19).

 

Bila ya kumjua Muumba wake, binaadamu hawezi kuitambua na kuifuata njia ya Mola wake itakayompa furaha hapa duniani na akhera, na kwa hivyo atakuwa miongoni mwa waliopata hasara. Kwa ajili hiyo wajibu wa mwanzo kwa binaadamu ni kumjua MwenyeziMungu.

 

 

ELIMU NI NJIA YA IMANI.

Mwanadamu akiitaka Imani iliyo sahihi, hana budi kujielimisha.

MwenyeziMungu anasema:-

"Jee anayejua ya kwamba yaliyoteremshwa kwako kutoka kwa Mola wako ni haki (akayafuata, basi) ni kama aliye kipofu? Wenye akili ndio wanaozingatia."

(Ar -Raad - 9).

Hii ni kwa sababu Imani ya kuiga tu, (bila ya elimu) hutetereka mara inapopambana na mtihani au inapopambana na mikanganyo (mambo yanayobabisha).

Mwenyezi Mungu anasema:-

"Sema. Jee! wanaweza kuwa sawa wale wanaojua  na wale wasiojua? Wanaotanabahi ni wale wenye akili tu".

(Az - Zummar -9)

Na akasema:-

"Na katika watu wako wanaomuabudu MwenyeziMungu ukingoni. Ikiwafikia kheri, hutuliya kwayo, na ikiwafikia fitina (msukosuko) hubwatika juu ya uso wake (akasunukia hataki kuuona tena huo Uislamu) amepata hasara ya dunia na akhera. Hiyo ndiyo hasara iliyo dhahiri".

(Al - Hajj -11).

 

 

DALILI ZA KIELIMU ZINAZOITHIBITISHA IMANI JUU YA MWENYEZIMUNGU

 

Misingi Ya Kiakili

a)MSINGI WA MWANZO.

ASIYEKUWEPO HAWEZI KUUMBA KITU.

ALIYEKUWEPO

Tukivizingatia viumbe vinavyozaliwa kila siku, kuanzia binaadamu, wanyama na mimea, na tukitafakari juu ya kila kinachotokea katika ulimwengu, mfano wa upepo, mvua, usiku, mchana, na tukitazama yanayotokea kila wakati kwa mpangilio ulio na nidhamu, nidhamu ya jua na mwezi, nyota na sayari, tukivizingatia hivi, pamoja na kuzingatia juu ya mabadiliko yaliyojaa hekima yanayotokea ulimwenguni kila wakati, tutaona kuwa akili ya mwanadamu huhakikisha kwamba vitu hivi havijaumbwa na ‘Asiyekuwepo’, bali vimeumbwa na ‘Muumbaji’ ambaye ‘Yupo - Subhanahu wa Taala’.

MwenyeziMungu anasema:-

"Jee wameumbwa pasipo na kitu au wao ndio waliojiumba. Au wameumba mbingu na ardhi? Bali hawana yakini (ya jambo lolote)”.

(At -Tur -36).

 

b) MSINGI WA PILI

 

UKIICHUNGUZA BIDHAA ITAKUJULISHA BAADHI YA SIFA ZA MTENGENEZAJI

Kila kilichokuwemo ndani ya bidhaa yoyote kinafahamisha uwezo au sifa alizonazo yule aliyeitengeneza bidhaa hiyo, na hii ni kwa sababu haiwezekani kuwepo kitu ndani ya bidhaa ikiwa mtengenezaji hana uwezo au sifa za kumwezesha kukitengeneza.

Kwa mfano:-

Unapouona mlango wa mbao umetengenezwa kwa ufundi kamili, utaelewa kuwa aliyeutengeneza anazo mbao, na kwamba anao uwezo wa kuzikata kiasi atakacho (saizi aitakayo), pamoja na uwezo wa kuzilainisha mbao hizo ziwe kama kioo (kwa kupiga randa), na utaelewa kwamba anayo misumari na kwamba ni hodari wa kuziunganisha mbao hizo kwa misumari.

Unapoiona tundu iliyotobolewa kwa mpango maalum katika mlango huo, (kwa ajili ya ufunguo) inatuthibitishia kwamba fundi huyo anao uwezo wa kuutoboa mlango kwa ustadi na kwamba ana mpango ulio thabiti katika kazi yake.

Kwa njia hii tutaona kuwa kila kitu kilichotengenezwa kinathibitisha uwezo na sifa alizonazo mtengenezaji, maana haiwezekani kuwepo kitu katika  bidhaa isipokuwa mtengenezaji anao uwezo au sifa zinazomwezesha kukitengeneza kitu hicho.

Kwa njia hii tunatambua kuwa ukikichunguza chochote kilichotengenezwa utapata baadhi ya sifa za yule aliyekitengeneza. Na kwa kufuata msingi huu tunaelewa kwamba tukivichunguza viumbe tutapata baadhi ya sifa za Muumbaji.

MwenyeziMungu anasema:-

"Bila ya shaka katika mbingu na ardhi ziko alama kubwa (za kuonyesha kuwa yupo MwenyeziMungu) Kwa ajili ya wanaoamini na katika umbo lenu na katika viumbe alivyovitawanya zimo alama (vile vile) kwa watu wenye yakini. Na katika kupishana (kufuatana) usiku na mchana na katika riziki aliyoteremsha MwenyeziMungu kutoka mawinguni (mvua) na akaifufua kwayo ardhi baada ya kufa kwake na katika mabadiliko ya upepo zimo alama pia kwa watu wenye akili. Hizi aya za MwenyeziMungu tunakusomea kwa ukweli basi hadithi gani watakayoiamini (baada ya kupuuza hadithi ya MenyeziMungu na aya zake?")

(Al -Jathiya -3-6).

 

Tukichunguza na kutafakari juu ya viumbe, vitatuelimisha juu ya alama za MwenyeziMungu ndani yake kwa kutujulisha baadhi ya sifa Zake zilizomo ndani ya viumbe hivyo.

MwenyeziMungu anasema:-

“Sema’; tazameni nini yanayotokea katika mbingu na ardhi".

(Younus -101).

Na akasema :-

"Jee hawatazami ufalme wa mbingu na ardhi na vitu alivyoviumba MwenyeziMungu? (Hawatazami wakarejea kwa Mungu kwa kuona) kuwa pengine ajali yao iko karibu. Basi baada ya maneno haya hadithi gani nyengine watakayoiamini?".

(Al -Aaraf -185).

 

ALIYE HAI - AMBAYE YUPO MILELE - (AL HAY)

Chakula tulacho hakina uwezo wa kusikia wala kuona wala hakitaharuki wala hakikuwi, hakivuti pumzi wala hakioi, hakilali wala hakiamki. Kinapoingia mwilini, hubadilika kuwa sehemu ya kiwiliwili kilicho na uhai na hubeba sifa zilizotajwa hapo mwanzo.

Pia katika mada mfano wa maji, udongo, na hewa ambavyo ni vyakula vya mimea, vitu hivyo havikui wala havizai wala havivuti pumzi wala havili chakula, lakini vinapoingia ndani ya sehemu za miti hugeuka kuwa sehemu ya hiyo miti iliyo hai na  kusitawi.

Uhai huu unaoenea katika kila kiwiliwili iwapo ni cha mti au mnyama au binaadamu kila siku na kila wakati, unashuhudia kuwa umetengenezwa na Mtoaji wa uhai.

    Binaadamu alijaribu kuumba uhai akashindwa. Na wataalamu kutoka Mashariki na Magharibi ya ulimwengu wamekwishatangaza kushindwa kwao kuumba uhai.

   Na akasadikisha MwenyeziMungu aliyesema:-

"Enyi watu! Unapigwa mfano, basi usikilizeni; hakika wale mnaowaomba badala ya MwenyeziMungu hawawezi kuumba (hata) nzi, wajapokusanyika kwa jambo hili. Na kama nzi akiwanyang'anya kitu hawawezi kukipokonya kwake. Amedhoofika kweli kweli huyu mtaka (kupokonya) na mtaka (kupokonywa), (atakaye na anayetakiwa). Hawamuadhimishi MwenyeziMungu kama anavyostahiki kuadhimishwa. Hakika MwenyeziMungu bila ya shaka ni Mwenye nguvu na Mwenye kushinda."

(Al - Hajj -73-74).

 

    Naam, na wanadamu wanashindwa kukipata chochote alichokichukua nzi, na hii ni kwa sababu mara tu baada ya kukichukua,  hukitemea mate na kukibadilisha haraka sana kuwa kitu kingine na haiwezekani kukipata tena.

Hakika uhai uliopulizwa na unaoendelea kila wakati kupuliziwa viumbe hauwezi kupatikana isipokuwa kutokana na Aliye Hai, Mwenye Kudumu milele (Subhanahu wa Taala).

     Kila uhai unatishwa na mauti kila inapokuja sababu ya kifo (kama kuumia, kuumwa, n.k.), lakini Muumba wa hizo sababu hadhuriki na sababu, kwani Yeye ndiye Aliye Hai Mwenye kudumu milele Ambaye hafi.

 

 MwenyeziMungu amesema:-

"Ufalme wa mbingu na ardhi ni wake. Anahuisha na kufisha, na Yeye ni Mwenye uweza juu ya kila kitu."

 (Al -Hadiyd -2).

 

Na akasema:-

"Na umtegemee ( MwenyeziMungu) wa milele ambaye hatakufa."

(Al-Furqan -58)

 

MWENYE KUJUWA (Kila kitu) - (AL ALIYM)

Ukikizingatia kiumbe chochote, utaona kuwa macho yake  yanaumbwa akiwa bado yumo ndani ya tumbo la uzazi la mama yake kabla hajazaliwa, mahali penye kiza kizito, juu ya kuwa jicho halioni isipokuwa penye mwangaza nje ya tumbo hilo. Hii ni dalili kwamba aliyeumba macho anaelewa kuwa kiumbe kile kitatoka katika dunia penye mwangaza. Na vivyo hivyo kuumbwa kwa mbawa za ndege angali yumo ndani ya yai lake kunathibitisha kwamba Muumbaji anaelewa kuwa ndege huyo atakapotoka nje atataka kuruka katika anga, ndiyo maana akamuumba akiwa na mbawa kabla hata hajazaliwa. Na hivi ndivyo ilivyo katika kila kiumbe kabla hakijazaliwa kishatayarishwa kuambatana na hali atakayoishi nayo baada ya kuzaliwa kwake.

Hata mbegu za miti MwenyeziMungu hutayarisha ndani yake sehemu zitakazokuwa majani na matawi, na sehemu zitakazoingia ndani ya ardhi (mizizi), ili iweze kunyonya maji na udongo (wenye chumvi chumvi). Hawezi kufanya hayo isipokuwa Mwenye Kujuwa kwamba mti utahitajia maji na udongo na mwangaza na hewa.

Viumbe vya kiume vikiumbwa, utaona kwamba Muumbaji keshatayarisha idadi ya kike kiasi cha kutosheleza idadi ya kiume. Hii inathibitisha kwamba hii ni kazi ya "Mjuzi" (Mwenye Kujuwa) Subhanahu wa Taala.

MwenyeziMungu anasema:-

"Na katika kila kitu tumeumba dume na jike ili mpate kufahamu."

(Al -Dhariyaat 49).

 

Maji matamu yaliyotulia huharibika, lakini MwenyeziMungu mwenye kuyaelewa hayo amejaalia maji ya bahari kuwa ya chumvi na kuyafanya yawe na mawimbi ili kuwe na harakati na ili yasije maji hayo yakaharibika na kuharibu maisha katika ardhi.

 

    Haya, na yote yaliyomo katika ulimwengu huu yanashuhudia kuwa;

Muumba wa ulimwengu huu anakielewa kila anachokiumba.

Na Yeye ndiye aliyesema:-

"Oh! Asijue aliyeumba! naye ndiye avijuaye visivyojulikana na vinavyojulilkana".

(Mulk -14).

 

    Na elimu ya Mwenyezi Mungu imekizunguka kila kitu, haiguswi na ujinga wala kusahau.

Mwenyezi Mungu amesema:-

"Ili mjue kwamba MwenyeziMungu ni mwenye uwezo juu ya kila kitu, na kwamba MwenyeziMungu amekizunguka kila kitu kukijua (vilivyo kwa ilimu yake)."

(Al Talaq -12).

 

MWENYE HIKIMA - (AL HAKIYM)

Ukizingatia sura za viumbe utaona kwamba Mwenyezi Mungu ameviumba katika kila jinsi viumbe vilivyofanana (vyenye sura aina moja) kwa hekima yake. Kwa mfano:-

Binaadamu ana macho mawili na pua baina ya hayo macho na mikono ipo katika pande zake mbili na miguu ipo chini.

Hukuti jicho likawa gotini au mkono kutokeza juu ya kichwa. Hii inathibitisha kwamba ni kazi ya Mwenye Hikima aliyeumba binaadamu kwa hikima kubwa sana.

Ameumba kila aina ya mnyama au mmea kwa hikima pia, na ameviumba katika sura na mfano mmoja.

Ni nani basi aliyepanga sura hizi isipokuwa yule aliyesema:-   

"Yeye ndiye anaye kutengenezeni sura matumboni jinsi apendavyo hakuna aabudiwaye ila Yeye Mwenye nguvu na Mwenye Hikima.

(Aali - Imran -6).

    Ukiichunguza hewa tuivutayo utaona kwamba unaitumia hewa safi (Oxygen) na kuigeuza kuwa hewa chafu (carbon dioxide) lakini kiasi cha hewa safi hakipungui katika anga kwa sababu muumbaji ameiamrisha mimea iibadilishe hewa hiyo uliyoichafua ipate kuwa safi tena kwa kiasi maalumu ili kiasi cha hewa kibaki kwa kadiri maalumu kisizidi wala kisipungue.

     Jee haithibitishi kwamba hii ni kazi ya Mwenye Kujuwa, Mwenye Hikima?

    Ukiitazama pua yako utaiona imeumbwa kwa hekima ili ikubaliane na kazi yake. Hewa huingia kupitia tundu mbili zilizopo baina ya macho, lakini Mjuzi, Mwenye Hikima amezifunika tundu mbili hizo kwa ngozi ya pua, na akaijaalia sehemu ya juu ya pua kuwa ni fupa ili upepo ukiwa mkali usije ukaibonyeza nyama ya pua na kuzibana tundu za ndani ya pua ukashindwa kuvuta pumzi. Fupa hilo husaidia pia katika kuyakinga macho (mtu akianguka pua na kipaji cha uso hutangulia, na kwa njia hiyo huyakinga macho), na pia kuiacha pua iwe wazi wakati wote ili hewa iweze kupita.

   Lau kama pua yote ingelikuwa ni fupa tupu, basi tusingeweza kupenga kamasi.

    Akajaalia pua iwe imepinda ili upepo unapoingia ndani uwe ukigonga ukuta wa pua uliopinda na kuurudisha katika vikwazo vya ndani ili vigongane na kugusana na vikwazo hivyo pamoja na kamasi zilizo kwenye mianzi ya pua na kuvigandisha (kuzuwia) vijidudu (germs) pamoja na vumbi ili usafike upepo kabla haujaingia ndani ya mwili.

(Upepo hauingii puani kuelekea katika mapafu moja kwa moja).

   Siku za baridi damu hujikusanya puani hata rangi ya pua hugeuka nyekundu ili ipate kuupa joto upepo unapoingia. Ama siku za joto pua hufanya kazi ya kuirowesha pua (jasho linapotoka) na kuuburudisha upepo mkavu au umoto unaoingia.

   Jee yote haya si ushahidi kwamba hii ni kazi ya Mwenye Kujuwa, Mwenye Hikima?

   Na hivi ndivyo ilivyo tukizingatia katika kuumbwa kwa kila kitu Ardhini au Mbinguni tutagundua kwamba kimeumbwa kwa Hikima ya hali ya juu.

   Hekima iliyo ndani ya kila kitu ni ushahidi kwa kila mwenye akili kwamba hii ni kazi ya Mwenye Hikima, Mwenye Elimu, Utukufu ni wake Mwenyezi Mungu aliyesema:

  "Na Yeye ndiye anayeabudiwa mbinguni na anayeabudiwa ardhini; Naye ni Mwenye Hikima, Mwenye Elimu" .

   AZ ZUKHRUF - 84

 

MWENYE UJUZI WA KILA JAMBO - (AL KHABIYR)

Kizingatie vizuri chakula tunachokula. Ingawaje kimetokana na udongo na maji namna moja, lakini vinapatikana ndani ya mchanganyiko huo wa udongo na maji vyakula vya aina mbali mbali na vya rangi mbali mbali. Hii inakuthibitishia kwamba hii ni kazi ya Mjuzi wa kila jambo, ambaye kutokana na asili moja anatoa aina mbali mbali kwa Hikima ya hali ya juu kabisa.

Zingatia jinsi gani kutokana na chakula hiki Mwenyezi Mungu anavyoumba nyama, damu, mifupa, shahamu, maziwa, ngozi, nywele, vidole, makucha, mishipa ya hisia na maji maji ya aina mbali mbali.

Kisha zingatia uso wako, jinsi gani mate hutokea mdomoni na kamasi hutokea puani na machozi hutokea machoni na taka za masikio kutokea masikioni, ingawaje vitokaji vyote hivi vinatokana na chakula kimoja, ikikuthibitishia kwamba hii ni kazi ya Mwenye Ujuzi Subhanahu wa Taala.

Ingekuwaje kama mate yangetokea puani, na kamasi zingetokea mdomoni? Taka za masikio zingetokea machoni, na machozi yakatokea masikioni?

Nani aliyeuchagua mpango huu? Na nani aliyechagua sehemu za kutokea? Hakuna mwingine isipokuwa yule Mwenye Elimu, Mjuzi, Mwenye Hikima.

   Na tone ambayo kwayo Binadamu ameumbiwa, ameijaalia Mwenye Elimu, Mjuzi Suhanahu wa Taala iwe na viungo mbali mbali na vyombo vilivyo na mpango vikishirikiana kumhudumia binadamu.

   Samaki baharini anahitajia hewa ili aweze kuvuta pumzi, Mjuzi akamyeyushia hewa kisha akaiingiza pamoja na tone tone za mvua zinazoanguka baharini na akamjaalia samaki awe na chombo maalumu (mashavu ya kuvutia pumzi) ili aweze kuitumia hewa hiyo iliyoyeyushwa ndani ya maji.

   Ukifikiri na ukichunguza vizuri utaona kwamba kila kitu katika ulimwengu kimetengenezwa kwa ujuzi wa hali ya juu kabisa ikishuhudia kwamba hii ni kazi ya Mjuzi wa kila kitu, Aliyetukuka Subhanahu wa Taala.

 

MTOAJI WA RIZIKI - (AL RAZZAAQ)

    Mwanadamu anapokuwa amefungika ndani ya kiza cha tumbo la uzazi, hapana yeyote anayeweza kumsaidia kwa chochote, si kwa maji wala kwa chakula. Hata baba yake au mama ambaye ndani yake mwili huo unaumbika, pia hawawezi kumsaidia isipokuwa kwa rehema yake Mtoaji wa Riziki ambaye humfikishia chakula kikiwa kimewiva kimekwisha lainishwa kupitia kwenye bomba ambalo ni kamba za kitovu (cha mama yake).

  Mara baada ya mtoto kuzaliwa kamba hizo hukatika, lakini Mtoaji wa riziki humtolea chakula chake mtoto huyo kifuani pa mamake akiwa tayari keshajulishwa namna ya kukitoa chakula hicho (maziwa) kwa kunyonya matiti wakati bado hajaanza hata kuona, kusikia wala kufahamu.

   Baada ya kukuwa MwenyeziMungu huwapa riziki viumbe vyake kutokana na mimea na miti ambayo hutengeneza vyakula kutokana na maji, udongo na hewa.

MwenyeziMungu hulitiisha jua kwa ajili ya miti ili ikamilishe kazi ya kutengeneza chakula ambacho huhitajiwa na binaadamu na wanyama.

         Chakula kisingeweza kupatikana lau kama MwenyeziMungu hajayaleta maji matamu na kutayarisha udongo unaofaa kwa kilimo na kufanya iwepo hewa pamoja na hali inayonasibiana na utengezaji wa chakula kutoka kwenye miti.

MwenyeziMungu anasema:-

"Hebu mwanadamu na atazame chakula chake, hakika sisi tumemmiminia maji kwa nguvu kutoka mawinguni. Tena tukaipasua pasua ardhi, kisha tukaotesha humo (vyakula vilivyo) chembe chembe. Na mizabibu na mboga na mizeituni na mitende na mabustani (mashamba) yenye miti iliyosongana barabara. Na matunda na malisho kwa ajili ya kukustarehesheni nyinyi na wanyama wenu."

(Abasa - 24 -32).

     Mwanadamu au mnyama anapokula chakula na kusagika chakula hicho katika mfumo wa kusaga chakula ambao MwenyeziMungu amemjaalia  kuwa nao kila kiumbe, basi Mtoaji wa riziki hiyo hukisambaza chakula hicho kuelekea katika kila sehemu ya mwili wa kiumbe kilicho hai. Hukifikisha mpaka katikati ya ubongo au sehemu ya chini ya ngozi au katika (ubongo wa mafupa).

 

Na MwenyeziMungu amesadikisha alivyosema:-

"Au nani ambaye atakupeni riziki kama akizuia riziki yake (MwenyeziMungu)? bali wao wanaendelea tu katika uasi na chuki."

(Almulk -21).

 

 Mtoaji Riziki Subhanahu wa Taala amekwisha dhamini riziki ya kila kiumbe, akapeleka riziki ya samaki katika sehemu za chini kabisa za bahari, akaipeleka riziki ya baadhi ya vijidudu na kukifikisha mpaka ndani ya mawe, akafikisha riziki za watoto wachanga wakiwa ndani ya kiza cha matumbo ya uzazi ya mama zao, na akakifikisha chakula cha mimea ndani ya mbegu.

MwenyeziMungu amesema:-

"Na hakuna mnyama yoyote (yaani kiumbe chochote) katika ardhi ila riziki yake iko juu ya MwenyeziMungu. Na anajua makao yake ya milele na mahali pake pa kupita tu (napo ni hapa duniani).Yote yamo katika kitabu kinachodhihirisha (kila kitu)".

 (Hud -60.)

Na akasema:-

"Enyi watu! Kumbukeni neema za MwenyeziMungu zilizoko juu yenu. Jee yuko Muumba mwengine asiyekuwa MwenyeziMungu anayekupeni riziki kutoka mbinguni na ardhini? Hakuna aabudiwaye kwa haki ila Yeye tu basi wapi mnakopinduliwa".

(Fatir -3 ).

Mwenye yakini kwamba riziki yake inatokana na Aliyemuumba, na kwamba yeyote hatoweza kumchukulia riziki yake, hatamwogopa yeyote katika riziki yake isipokuwa MwenyeziMungu Peke Yake.

 

MWENYE KUONGOZA - (AL HAADIY)

    Ukizichunguza kope na nyusi, utaona kuwa nyusi zinaelekea juu na kope zimeelekea chini. Ingekuwa kinyume cha hivyo (yaani nyusi zingeelekea chini na kope  kuelekea juu) mwanadamu asingeweza kuona vizuri.

Ni nani basi anayeongoza kila unywele (wa nyusi na kope na nywele nyengine) uelekee kila mmoja mahali pake kama si Mwenye Kuongoza, Al Haadiy MwenyeziMungu Subhanahu Wataala?

Nani mwenye kuyaelekeza meno ya chini yakaelekea juu na ya juu kuelekea chini? Na nani aliyeyaongoza meno membamba ya mbele yakachomoza mahali pake sawa sawa na meno ya pembeni mahali pake na magego yakaota penye magego?

 Ni nani mwengine isipokuwa Mwenye Kuongoza?.

Mwenyezi Mungu anasema;

ý"Aliyeumba (kila kitu) na akakitengeneza na akakikadiria (kila kimoja jambo lake) na akakiongoza (kufanya jambo hilo)."

(A'laa -3-4ý)

 Nani aongozaye kila sehemu ya kiwiliwili katika mimea au wanyama au binaadamu mpaka kikawepo mahali pake sawa sawa mwilini, kisha kikakuwa kwa kiasi kadiri inavyotakikana kikikubaliana na mahali pake?

Nani mwenye kuiongoza mbegu ikaweza kupasua udongo chini ya ardhi na kuelekea juu wakati inapomea na kuielekeza mizizi chini ya ardhi, na vigogo pamoja na majani kuelekea juu? Kwa nini isipatikane hata mbegu moja ikimea kinyume na hivyo?

Jee haya yote hayawi dalili kwa kila mwenye akili kwamba hii ni kazi ya Mwenye Kuongoza – Al Haadiy Subhanahu wa Taala?

Nani anayeongoza majani ya miti yakagawika katika sehemu mbali mbali za vigogo au katika matawi wakati linapochomoza jani upande mmoja wa mti, jani lengine huchomoza upande wa pili?

Nani aliongozaye jua, mwezi na nyota katika njia zake na akawaongoza ndege wanaosafiri kuelekea makwao mbali kabisa?

Ni Mwenye Kuongoza aliyesema:-

"Aliyeumba (kila kitu) na akakitengeza na akakikadiria kila kimoja jambo lake na akakiongoza (kufanya jambo hilo)".

(Al - Aalaa -3-4)

   Mwenyezi kukiongoza kila kitu, nywele na mbegu na majani, kisha akakamilisha uongofu wake kwa binadamu kwa kumpelekea wajumbe (Mitume) ili kuwabainishia uongofu utokao Kwake.

     Mwenye yakini kwamba MwenyeziMungu ni Mwongofu na Mwenye Hikima, hakubali fikra yoyote yenye kupingana na uongofu wake Subhanahu wa Taala, na msemo wake siku zote huwa ile kauli ya MwenyeziMungu isemayo:-

"Sema uongozi khasa ni uongozi wa MwenyeziMungu".

(Al -An -Am -71).

 

MLINZI (AL HAAFIDH)

Yule aliyekulinda na kila hatari huku ukiwa unaumbika ndani ya tumbo la mama yako ndiye yule yule anayeulinda ubongo wako ulio dhaifu akautia ndani ya kisanduku kigumu ndani ya fupa la bufuru la kichwa chako, na ndiye Yule yule anayeyalinda macho yako kwa kuumba fupa la paji la uso na ufupa wa paji la pua na mashavu, na ndiye anayeulinda moyo wako na mapafu yako kwa kuizungushia mifupa ya kifua (mbavu).

Ni Yeye anayeulinda uhai wako na akakurahisishia mahitajio ya kuishi mfano wa chakula, maji, hewa, mwangaza, joto na venginevyo.

Ni Yeye ambaye hakupatishi tabu ya kui ingiza hewa ndani ya mwili wako na kuitoa unapokuwa umelala au unapokuwa umacho. Lau kama angelikukalifisha wewe kazi hiyo ya kuingiza na kuitoa hewa, basi usingekuwa na wasaa wa kufanya jambo lolote lingine katika maisha yako yote isipokuwa kuiingiza na kuitoa tu, na usingizi ukikuchukua ghafla, basi usingeipata hewa na ukafa.

Hakika Mlinzi Subhanahu wa Taala ndiye anayeyaendesha mawingu yaliyo juu yako, kisha hayamimini maji ya mvua yaliyojikusanya katika mawingu hayo kwa wingi yakaangamiza mashamba na mimea, bali huyamimina kwa njia ya mvua inayomwagika mfano wa maji ya marashi.

Hakika Mlinzi, (MwenyeziMungu) ndiye aliyeizungushia dunia yetu (sayari "earth") mkanda wa hewa na michanganyiko mingine (Ozone layer) unaozuia miale ya jua na ya nyota iangamizayo isiweze kutufikia  na kuangamiza maisha na kila kinachoishi, na akajaalia kuwepo mkanda huo kuwa ni kinga yetu kwa kuviangamiza vimondo (shooting star), ambavyo huangukia ardhini kwa mamilioni kila wakati usiku na mchana. Na Yeye ndiye aliyeithibitisha ardhi isiweze kuyumbayumba chini ya miguu yetu kwa kuyaingiza majabali ndani ya ardhi yakawa kama vigingi.

    Kwa nini basi tusimshukuru Mola wetu Subhanahu Wataala ambaye ametuhifadhi ndani ya miili yetu na juu yetu na chini yetu?

MwenyeziMungu amesema kweli aliposema:-

"Ana (kila mtu) kundi (la Malaika) mbele yake na nyuma yake wanamlinda (na kuyadhibiti anayoyafanya) kwa amri ya MwenyeziMungu”.

(Al - Raad -11).

Na mwenye yakini kwamba MwenyeziMungu ndiye anayemuhifadhi, basi hawezi kudhurika na yeyote yule awe yupo mbinguni au ardhini isipokuwa kwa aliyekwisha kadiriwa na MwenyeziMungu, na msemo wake siku zote ni kauli ya  MwenyeziMungu:-

"Sema "Halitotusibu ila alilotuandikia MwenyeziMungu".

(At - Tawba -51)

 

SIFA NYINGINE.

    Ukichunguza chakula kimoja kinacholiwa na ukoo mmoja, utaona kuwa anapokula mwanamume hugeuka kuwa mwili wa kiume,  na chakula hicho hicho anapokila mwanamke hugeuka kuwa mwili wa kike, na katika mwili wa mtoto hugeuka mtoto na anapokula chakula hicho hicho paka, basi hugeuka kuwa mwili wa paka. Anapokula panya au mbwa hugeuka kuwa ni sehemu ya mwili wa panya au mbwa, wakati chakula ni hicho hicho kimoja, basi Utukufu ni wake Mwenye Kutengeneza sura kama apendavyo Subhanahu wa Taala.

Na ukiichunguza huruma ya mama na namna anavyowaonea huruma wanawe, yote sawa iwapo mama huyo ni mwanadamu au mnyama, utamauona namna gani anavyojitolea mhanga kwa ajili ya kuwalinda wanawe.

Hata kuku ambaye kwa kawaida huogopa hata sauti ya mtoto mdogo, utamwona namna anavyokasirika na kumshambulia yeyote anayejaribu kuvidhuru au hata kuvisogelea vifaranga vyake.

    Hakika rehema hizi ambazo hujaaliwa kuwa nazo hata viumbe vidogo vidogo, ni ushahidi mkubwa kuwa hii ni kazi ya Mwenye Kuneemesha neema ndogo ndogo na Mwenye Kuneemesha neema kubwa kubwa Mwingi wa Rehma.

    Ukivichungua viumbe vikubwa kama vile nyota ambazo ni kubwa kuliko dunia yetu kwa mara milioni nyingi, na ukivichunguza viumbe vidogo kabisa vinavyoweza kujikusanya kwa mamilioni ndani ya tone moja ya maji, kisha ukajiuliza mwenyewe ilikuwaje viumbe vyote hivi vikasalimu amri kwa kufuata amri moja na nidhamu aina  moja yenye kuongozwa barabara na iliyopangika sawa sawa?

Hapo ndipo utakapo pata jibu kwamba hii ni kazi ya Mwenye Nguvu, Mwenye kuyaendesha Mwenyewe mambo Yake, Subhanahu Wataala.

 

MMOJA TU ALIYE PEKEE (AL WAAHIDUL AHAD)

Kila kitu duniani kinashuhudia kwamba kimeumbwa na Mmoja tu Aliye Pekee.

Chakula chako kwa mfano, hutegemea kazi ya tumbo (kwa usagaji wa chakula). Na madaktari wanasema kuwa usagaji wa chakula unategemea mzunguko wa damu, na damu ili ifanye kazi yake vizuri huitegemea hewa na uvutaji wa pumzi, na ili ipatikane hewa safi inategemea kazi ya miti (ambayo ndiyo inayoisafisha hewa hiyo), na ili miti iweze kufanya kazi yake sawa inalitegemea jua, na jua ili libaki linazitegemea sayari zilizoizunguka pamoja na nyota nyengine.

Kwa hivyo utaona kwamba kila kitu ili kiwepo na ili kiweze kufanya kazi yake vizuri, kinategemea kitu kingine. Kama tulivyoona jinsi tumbo lilivyoshikamana na nyota zilizo mbinguni.

Hii inathibitisha kwamba kila kitu kimeumbwa na Mungu Mmoja.

MwenyeziMungu anasema:-

"MwenyeziMungu hakujipatishia mtoto wala hakuwa pamoja naye mungu (mwengine). Ingekuwa hivyo basi kila mungu angaliwachukuwa aliowaumba. Na baadhi yao wangeliwashinda wengine, MwenyeziMungu ameepukana na sifa Wanazomsifu (nazo zisizokuwa ndizo)".

(Al -Muumin -19)

 Na akasema:-

"Sema; "Yeye ni MwenyeziMungu ni Mmoja (tu). MwenyeziMungu tu ndiye anayestahiki kukusudiwa (na viumbe vyake vyote kwa kumuabudu kumuomba na kumtegemea) hakuzaa wala hakuzaliwa".

(Ikhlas -1-3)

Na kama pangalikuwepo na mungu mwengine basi mapambano yangelitokea baina yao juu ya kuviendesha viumbe hivi, na hapo ufisadi ungelienea ardhini na mbinguni.

 

MwenyeziMungu anasema:-

"Lau kwamba wangalikuwepo humo (mbinguni na ardhini) waungu wengine isipokuwa MwenyeziMungu, bila shaka zingeharibika (hizo mbingu na ardhi). Na ametakasika MwenyeziMungu Mola wa Arshi (yu mbali) na yale wanayomsifu."

(Al -Anbiyaa -22)

 

NANI MWENYE SIFA ZOTE HIZI?

   Kutokana na yaliyotangulia tumeona kuwa unapotafakari juu ya ulimwengu na viumbe tunavyoishi navyo, utagundua kuwa Muumba wa vitu hivi ni Muumbaji, Aliye Hai, Mwenye Ujuzi, Mwenye Kutoa Riziki, Mwenye Kuongoza, Mlinzi, Mtengenezaji wa sura, Mwenye Kurehemu, Mwenye Nguvu, Mwenye Uwezo, Mmoja tu Aliye Pekee.

     Na kama kilivyoshuhudia kila kilichokuwepo duniani kwa ushahidi huu, kwa hivyo Muislamu amesalimu amri pamoja na ulimwengu huu huku akiikariri shahada hii, akiwa anaelewa na ana yakini huku akisema:-

"ASH - HADU AN LAA ILAAHA ILLA LLAH"

"Nashuhudia kwamba hapana Mola apasae kuabudiwa isipokuwa Mwenyezi Mungu".

    Na iwapo katika msingi wa mwanzo tumeelewa kwamba ASIYEKUWEPO HAWEZI KUUMBA KITU, na katika na msingi wa pili tukazielewa BAADHI YA SIFA ZA MUUMBAJI.

Basi katika msingi wa tatu tutaelewa kwamba sifa hizi hazimfai yeyoye yule isipokuwa (ALLAH), MwenyeziMungu Asiye na mshirika.

 

 

MSINGI WA TATU - ASIYEKUWA NA KITU HAWEZI KUTOA

Asiyekua na mali watu hawamuombi mali, na asiyekuwa na elimu hawezi kuelimisha, na hii ni kwa sababu asiye na kitu hawezi kutoa (KWA SABABU HANA KITU).

     Kwa kuyazingatia haya tumepata dalili na ushahidi katika kila kiumbe inayotujulisha baadhi ya sifa za Muumbaji - Subhanahu wa Taala. Na tunapotambua sifa, tunamjua mwenye sifa hizo.

Sasa wale wanaodai kuwa maumbile ndio yaliyowaumba, wamekwenda kinyume na akili na wameupiga vita ukweli, na hii ni kwa sababu ulimwengu wote unashuhudia kwamba aliumba ni Mwenye Hikma, Mwenye Ilimu, Mwenye Ujuzi, Mwenye Kuongoza, Mtoaji wa Riziki, Mlinzi, Mwenye Kurehemu, Mmoja Aliye Pekee.

    Hayo maumbile yasiyoweza kusema, yaliyokauka, yasiyokuwa na elimu wala hikima, hayana uhai wala rehma wala uwezo, vipi  basi wajinga wakawaza namna hii (kuwa hayo ndiyo yaliyowaumba?)  wakati ASIYEKUWA NA KITU HAWEZI KUTOA.

 

NI NINI HAYA MAUMBILE?

Maumbile ni hivi viumbe pamoja na sifa zinazobeba. Wanaoabudu viumbe toka zamani waliabudu baadhi ya viumbe kama vile jua, mwezi, nyota, moto, mawe na pia waliabudu watu.

Na hawa wanaoabudu viumbe wa siku hizi (wana wa maumbile) wanadhania kuwa vitu hivi vilivyokuwa vikiabudiwa hapo zamani (maumbile) kuwa ndiyo vilivyowaumba, wakati ambapo maumbile hayana hata akili na wao wanazo akili, maumbile hayana ilimu, na wao wanayo ilimu!!! Maumbile hayana ujuzi  wao wanao ujuzi !!! maumbile hayana uwezo na wao waonao uwezo.

    Jee hawaelewi kuwa ASIYEKUWA NA KITU HAWEZI KUTOA?

MwenyeziMungu amesema:-

"Enyi watu unapigwa mfano basi usikilizeni hakika wale mnaowaomba badala ya MwenyeziMungu hawawezi kuumba hata nzi japo wakikusanyika kwa jambo hilo, na kama nzi akiwanyang'anya kitu hawawezi kukipokonya kwake.

Amedhoofika kweli kweli huyu mtaka (kupokonya) na mtakwa (kupokonywa).

Hawakumuadhimisha MwenyeziMungu kama anavyostahiki kuadhimishwa hakika MwenyeziMungu bila shaka ni Mwenye nguvu na Mwenye kushinda."

(Al - Hajj -73-74).

 

MAMBO YANAYOBABAISHA WATU  NA MAJIBU YAKE.

Baadhi ya wasioamini MwenyeziMungu wanadai kuwa eti maumbile ndiyo yenye kuumba wakitegemea ushahidi wao juu ya kutokeza kwa vijidudu (funza n.k) kutokana na takataka na mizoga ya wanyama na maiti ya wanadamu.

    Elimu iliposonga mbele ikawaelimisha watu kwamba wadudu hawa wanaotokeza penye mizoga na sehemu nyingine wanatokana na mayai madogo sana ambayo hayaonekani kwa macho. Pakawezekana  kuonekana hayo kwa kwa njia ya darubini (Microscope).

Kisha wakadai tena kwamba eti ikiwa vijidudu hivyo vinatokana na vijidudu vingine vilivyotangulia vilivyotokana ndani ya vijiyai vidogo ambavyo hatuvioni, basi germs ambao husababisha chakula kuoza na kuharibika wanatokana na maumbile na kwamba hawatokani na vijidudu vingine vilivyokuwepo kabla yao.

Lakini madai haya pia yakashindwa kiasi cha miaka Themanini iliyopita wakati watalamu walipogundua njia ya kuhifadhi chakula bila ya kuharibika kwa kuviingiza kwa ustadi ndani ya makopo, na vijidudu vikafa kwa joto la kupikwa au miale ya joto kisha kikafunikwa kwa ustadi ili hewa (inayobeba vijidudu hivyo) isiweze kuingia ndani na kusababisha kuingiza vijidudu wengine.

Kwa njia hii ikajulikana kuwa viumbe vyote vinatokana na viumbe vilivyokuwa kabla yao. Na kwamba havitokani na maumbile kama wanavyodai wajinga wasioamini kuwepo kwa MwenyeziMungu.

       Utashangaa ewe Mwislamu, kwamba miongoni mwa viongozi wasioamini kuwepo kwa MwenyeziMungu wanayajua haya tokea miaka themanini iliyopita, lakini wanashikilia kueneza habari hizo za kijinga za kutoaamini Mungu ambazo hazidumu ila na wajinga.

 

KUJIBU UPOTEVU WA MANASARA

MwenyeziMungu alipomwokoa Nabii Issa (AS) kutokana na vitimbi vya maadui wake na kumnyanyua kwake, maulamaa wa Kinasara waliobaki waliingizwa katika vitisho vya Warumi, na wengi wao wakatoweka na wengine wakauawa na  ujinga ukaenea baina ya Manasara.

    Injili ya Nabii Issa (AS) ikapotea, wakaibadilisha kwa Injili walizozitunga wao wenyewe na kila mtungaji akaandika jina lake katika Injili yake inayohitalifiana na  nyingine, wakawa  na Injili nyingi kama vile Injili ya Matayo, Injili ya Yohana, Injili ya Maiko, Injili ya Luka, Injili ya Barnaba, hata idadi yake ikafikia zaidi ya Injili Sabini.

Kisha ukafanywa mkutano wa Manasara wakazichagua nne tu miongoni mwa hizi Injili na kuziunguza zilizobaki.

Kisha wakadai kwamba MwenyeziMungu amegawika sehemu tatu na kwamba Issa ni mwana wa Mungu, wakati MwenyeziMungu yuko mbali juu kabisa na hayo wanayomsingizia.

Kisha baadaye wakasema kwamba MwenyeziMungu ni mmoja lakini wakaanza kuamini mambo yasiyoingia akilini nayo ni kwamba Mungu ni mmoja lakini wakati huo huo ni watatu (amegawika sehemu tatu).

 Mshairi maarufu Albusiyri, alisema:-

"Wamefanya watatu kuwa ni mmoja, lau wangeongoka wasingeweza kuifanya idadi kubwa kuwa moja".

Kisha wakadai kwamba mungu (Nabii Issa(AS), amekufa msalabani, - ingawaje wanaamini kwamba Malaika hawafi - na kwamba binaadamu (Mayahudi na Warumi) ndio waliomuuwa. Injili yao inasema kwamba baadhi ya wafuasi wake walimuona akiwa  hai baada ya kusulubiwa kwake.

Na MwenyeziMungu anasema:-

"Hawakumuua wala hawakumsulubu bali walibabaishiwa na kwa hakika wale waliokhitilafiana katika (hakika) hiyo wamo katika shaka, hawana yakini juu ya hili isipokuwa wanafuata dhana tu. Na kwa yakini hawakumwua bali MwenyeziMungu alimnyanyua kwake na MwenyeziMungu ni Mwenye Nguvu na Mwenye Hekima."

(Al -Nisaa - 157-158).

Kuhusu madai yao kwamba Issa (AS) kwa vile hana baba kwa hivyo hii ni dalili kuwa baba yake ni Mwenyezi Mungu. Qurani imekwishawajibu.

MwenyeziMungu anasema:-

"Bila ya shaka hali ya Issa kwa MwenyeziMungu ni kama hali ya Adam alimwumba kwa udongo kisha akamwambia; "Kuwa", basi akawa."

Aal -Imran -59).

MwenyeziMungu amekwisha bainisha kuwa Issa (AS) ni mwanaadamu na alikuwa akila chakula, na anayekula hana budi kufanya haja (ndogo na kubwa).

Vipi basi awe Mungu yule ambaye hana budi kula, kunywa na kufanya haja?

MwenyeziMungu anasema:

"Masihi bin Maryam si chochote ila ni Mtume, bila shaka Mitume wengi wamepita kabla yake na mama yake ni mwanamke mkweli. Wote wawili walikuwa wakila chakula. Tazama jinsi tunavyobainisha aya, kisha tazama jinsi wanavyogeuzwa".

 (Al -Maidah- 75).

 

ANAYEMJIBU ALIYEDHIKIKA ANAPOMUOMBA

Kila mtu anaweza kumjua Mungu wake kwa urahisi kwa njia ya kuona jinsi dua inavyojibiwa. Mara ngapi Waislam walitoka kwa nyoyo tiifu, zilizotubu, wakimuomba Mola wao awanyeshee mvua, na majibu ya dua zao hupatikana hapo hapo?’ Mvua hunyesha katika kijiji au mji, mahali ambapo watu walitoka wakimuomba MwenyeziMungu awaletee hiyo mvua wakati ambapo vijiji na miji ya jirani haipati mvua hiyo. Wangapi waliokuwa na dhiki wakapata faraja baada ya kumuomba Mola wao?

MwenyeziMungu amesema:-

“Áu yule anayemjibu aliyedhikika amwombapo na kuondoa dhiki yake na kukufanyeni wenye kuendesha dunia. Jee yupo Mungu pamoja na MwenyeziMungu? Ni kuchache kuwaidhika kwenu."

 

MSIMAMO WA MAKAFIRI DHIDI DALILI ZA IMANI.

Dalili za imani juu ya kuwepo kwa MwenyeziMungu ni nyingi, na idadi yake ni sawa na idadi ya viumbe vyote vilivyopo duniani, kwa sababu kila kiumbe kinatujulisha sifa za Muumbaji wake. Lakini makafiri hawajanufaika na dalili hizi kwa sababu nyoyo zao zina maradhi, haziko tayari kuyakubali maongozo,  kinyume na nyoyo zilizoamini.

Kama tulivyobainisha hapo mwanzo, kafiri siku zote anapinga dalili za MwenyeziMungu na anabishana bila ilimu.

MwenyeziMungu anasema:-

"Na katika watu wako wanaojadiliana juu ya MwenyeziMungu bila ilimu wala uongozi wala kitabu chenye nuru."

(Al - Hajj -8).

Utamwona pia akizifanyia kiburi dalili za MwenyeziMungu.

MwenyeziMungu anasema:-

"Na wakazikanusha hali ya kuwa nafsi zao zina yakini nazo (kuwa ni kweli, lakini walizikanusha) kwa dhuluma na kujivuna."

(An - Naml -14)

Na utamwona anachanganya haki na batili.

MwenyeziMungu anasema:-

"Wala msichanganye haki na batili na mkaficha haki na hali mnajua."

(Al  -Baqarah -42)

 

Na utamwona anazuia watu wasifuate njia ya MwenyeziMungu.

MwenyeziMungu anasema:-

"Hakika wale waliokufuru na kuzuilia (watu) njia ya MwenyeziMungu bila shaka wamepotea upotofu ulio mbali (na haki)."

(An - Nisaa -167).

 

KUIGIZA KATIKA KUKUFURU,

Miongoni mwa sifa za ukafiri ni kwamba wakati wanaikataa Imani juu ya kuwepo kwa dalili zilizo wazi, badala yake wanaielekea (wanaikubali) kufru bila ya dalili yoyote, wanafuata tu mfano wa kipofu.

Mwenyezi Mungu anasema;

"wanapoambiwa 'Njooni katika hukumu alizoziteremsha MwenyeziMungu na (anazozisema) Mtume, husema yanatutosha yale tuliyowakuta nayo baba zetu'. Jee hata kama baba zao walikuwa hawajui kitu na wala hawakuongoka (watawafuata tu)?"

(Al - Maidah -104).

 

UZUSHI WA MAMBO YANAYOBABAISHA

Miongoni mwa vitimbi vya makafiri katika kutaka kuwapoteza Waislamu ni kuzusha mambo yanayobabaisha yanayoweza kumpoteza asiyeielewa Itikadi yake na asiyejijengea ngome (ya ilimu ya dini yake) kwa ajili ya kujilinda na ubabaishaji wa wale wasioamini Mungu.

Miongoni mwa maneno wanayoyatumia ni yale waliyosema wana wa Israil (tokea zamani) kumwambia Musa (AS), kama ilivyoelezwa ndani ya Qurani:-

"Na mliposema "Ewe Musa! hatutakuamini mpaka tumwone MwenyeziMungu wazi wazi".

(Al - Baqarah - 55)

Ingawaje makafiri hao wanaamini kuwepo kwa akili inayoweza kufikiri, kuwepo kwa hewa, na kuwepo kwa nguvu ya mvutano inayovuta kila kitu kuelekea ardhini na wanaamini kuwepo kwa mawimbi ya sauti yanayowafikia kutoka sehemu za mbali, juu ya kuwa vyote hivyo hawavioni kwa macho yao, lakini wanaiona athari ya akili kutokana na wenye akili na wanaiona athari ya hewa kutokana na kutikisika kwa matawi ya miti na venginevyo, na athari ya nguvu ya mvutano inaonekana kutokana na kuvutika kwa kila kitu kuelekea ardhini, na wakaamini kuwepo kwa mawimbi ya sauti baada ya kuiona athari yake kwa njia ya sauti zinazosikika kutoka kwenye vyombo vya idhaa n.k.

Kwa hivyo wameamini kuwepo kwa akili, hewa na nguvu za mvutano juu ya kuwa macho yalishindwa kuviona kwa udhaifu wake, lakini akili ikatambua kutokana na athari zake walizozishudia.

Laiti wale wasioamini wangeacha kutakabari na hizo nguvu zao za kuona zilizo dhaifu, zisizo na uwezo, zisizoweza kuiona hewa wanayoigusa au kukiona kitu kilichokuwepo nje ya pale walipo. Wangelitafakari wangeligundua kwamba wao pamoja na vilivyomo ulimwenguni, zikiwemo ardhi na mbingu, si chochote isipokuwa ni dalili na ushahidi ulio wazi ukiwajulisha kuwepo kwa Muumba wao Subhanahu Wa Taala.

Uwezo huu wa kuona ulio dhaifu hauna nguvu ya kuziona nyota kwa ukamilifu. Nyota ambazo ni pambo tu la mbingu ya dunia, vipi basi wataweza kumuona Yule Aliye juu kabisa kwenye Arshi Yake?

 (Mbingu zote saba zikilinganishwa na kiti Chake (Mwenyezi Mungu) ni sawa na senti ndogo saba ukizitia ndani ya ngao (ya kujikingia katika vita). Na Kiti kikilinganishwa na Arshi Yake MwenyeziMungu ni mfano wa pete ndogo iliyotupwa jangwani).

Iwapo macho ya binaadamu katika dunia hii hayawezi kuvumilia kulitazama jua moja kwa moja, vipi basi yatakuwa na uwezo wa kuiona Nuru ya MwenyeziMungu Aliyetukuka, Aliye juu ya yote?

MwenyeziMungu angejidhihirishia kwa viumbe vyake duniani, basi kujidhihirisha huko kungeliwalazimisha watu kumfuata, na huko kungeifanya dunia isiwe mahali pa kufanyiwa mtihani maana kumuamini Mungu wakati huo kungekuwa ni kwa njia ya kulazimishwa na kwa hivyo pangeondowa ile maana ya Majaribio au Mtihani.

Nabii Mussa(AS) hapo zamani alimwomba amuone Mola wake.

MwenyeziMungu anasema:-

"Basi Mola wake alipodhihirisha baadhi ya Nuru Yake katika jabali alifanya lenye kuvunjika vunjika na Musa akaanguka hali ya kuzimia ".

(Al  Aaraf -143).

Watu wote wakiwemo makafiri, wanawasadiki madaktari na wenye ujuzi pamoja na walimu wanapowaeleza juu ya mambo wasiyoweza kuyaona kwa macho yao. Hii ni kwa sababu wenye ujuzi hawa wanasadikiwa na wasikilizaji wao.

Basi hao makafiri wangeacha kiburi chao, wao pia wangelimjua Mola wao kwa njia ya kuwasadiki Mitume wa MwenyeziMungu wasemao kweli, ambao kwa miujiza na ushahidi waliokuja nao unawafanya kuwa ni watu wanaofaa kusadikiwa zaidi kupita wote duniani kutoka na wanayoyasema juu ya Mola wao.

 

KUWEKA MASHARTI ILI WAAMINI

Wapo wengine wanaomwekea masharti MwenyeziMungu ili wamuamini.

Utawasikia wakisema kwa mfano;

"Iwapo Mungu anataka nimuamini, basi afanye hiki au kile". Na huu ni mfano wa makafiri uliotajwa katika Qurani:-

"Na walisema (makafiri wa kikureshi kumwambia Mtume) hatuwezi kukuamini mpaka utububujishie (utupitishie) chemchemu katika ardhi. Au uwe na bustani ya mitende na mizabibu ikisha ububujishe mito katikati yake kwa mabubujiko makubwa. Au utuangushie mbingu vipande vipande kama ulivyodai, au utuletee MwenyeziMungu na Malaika uso kwa uso."

Israa( Bani Israil) 90 - 92.

Na kama MwenyeziMungu angefanya njia ya kuaminiwa iwe kwa kutimiza masharti ya binaadamu, basi wangelitokea wenye masharti mbali mbali, wengine wangeomba mchana uwe usiku na jua kuwa mwezi, na wengine wangetaka ardhi iwe mbingu na wanaume kuwa wanawake, na wengine kinyume cha hivyo. Wengine wangeshurutisha auliwe mtu fulani au kuangamizwa nchi fulani na wengine kinyume cha hivyo; Na kwa njia hiyo ardhi na mbingu zingefisidika.

MwenyeziMungu anasema:-

"Na kama "Haki" (MwenyeziMungu) angefuata matamanio yao, zingeliharibika mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake".

(Al Muumin - 71

MwenyeziMungu amesimamisha dalili nyingi katika viumbe vyake, na akatupa uwezo wa kusikia na kuona, akatupa nyoyo ili tuweze kuzijua dalili hizo na kwa njia hii ukweli unasimama na kubabaika kunaondoka.

 

KUMJUA MWENYEZIMUGU KWA MAJINA YAKE NA SIFA ZAKE

Umuhimu Wa Kuyajua Majina Yake Na Sifa Zake

Unapoambiwa kuwa mtu fulani ni karimu na kwamba moja kati ya sifa zake ni kumpa kila muhitaji, bila shaka unapokuwa na shida utategemea kupata uyatakayo kutoka kwake, na utamheshimu mtu huyo moyoni mwako kwa kuwa yeye ni mkarim, na utafaidika kutokana na kuijua sifa yake hii ya ukarimu pale unapohitaji.

Na kinyume chake pale unapoelewa kuwa mtu ni bakhili, (Hutotegemea kuyapata mahitajio yako kutoka kwake kwa sababu ya ubakhili wake wa kuogopa kupungukiwa na mali yake).

Unapoambiwa kuwa serikali fulani ina uadilifu katika kuhukumu kwake na kwamba inawashughulikia wanaoishi ndani ya nchi hiyo na kuwatia adabu wasiofuata kanuni, watu watamiminika katika nchi hiyo ili wafaidike na sifa za huduma zake pamoja na kufaidika na sifa ya uadilifu wake na sifa ya kuiheshimu kwake sheria. Utawaona watu hao wanaipenda serikali hiyo kutokana na sifa njema iliyo nayo, huku wakijaribu kila njia kujiepusha na kuvunja sheria ili wasije wakahukumiwa na kutiwa adabu.

MwenyeziMungu ndie mwenye sifa tukufu zaidi. Kwa mwenye kuzijua sifa za Mola wake na majina Yake mazuri mazuri, elimu yake juu ya MwenyeziMungu Mwenye Ufalme wa mbingu na ardhi inaongezeka, na mwenendo wake huwa unalingana na elimu aliyonayo juu ya Majina na Sifa za MwenyeziMungu.

Ama makafiri, MwenyeziMungu amesema juu yao yafuatayo:

"Hawakuamuadhimisha MwenyeziMungu kama anavyostahiki kuadhimishwa. Hakika MwenyeziMungu bila shaka ni Mwenye Nguvu Na Mwenye Kushinda”.

(Al -Hajj 74)

Na Qurani imetuhadharisha juu ya kubadilisha majina ya MwenyeziMungu.

MwenyeziMungu anasema:-

"Na MwenyeziMungu ana majina mazuri mazuri basi muombeni kwa hayo. Na waacheni wale wanaoharibu utakatifu wa majina yake karibuni hivi watalipwa yale waliokuwa wakiyatenda ."

(Al -Aaraf -180)

Qurani pia imekwisha onya juu ya kumpa MwenyeziMungu sifa zisizolingana Naye.

Mwenyezi Mungu anasema;

"MwenyeziMungu hakujipatishia mtoto wala hakuwa pamoja  naye mungu (mwengine). Ingekuwa hivyo basi kila Mungu angewachukua aliowaumba, na baadhi yao wangeliwashinda wengine. MwenyeziMungu ameepukana na sifa wanazomsifu nazo (zisokuwa ndizo)."

(Al -Muumin 91.)

 

WAHYI NDIYO NJIA BORA KATIKA KUYAJUA MAJINA NA SIFA ZA MWENYEZIMUNGU

Elimu ya mwanadamu juu ya viumbe vya MwenyeziMungu ina mpaka wake na mwanadamu hawezi kujua kila kitu juu ya Mola wake.

Kwa mfano mbingu zote saba zikilinganishwa na Kiti Chake MwenyeziMungu, ni sawa na senti ndogo saba ukizibandika juu ya ngao kubwa, na hicho Kiti ukikilinganisha na Arshi ya MwenyeziMungu ni sawa na pete ndogo iliyotupwa jangwani.

(Mwenyezi Mungu anacho Kiti (Kursy) na anayo Arshi - hivi ni vitu viwili tofauti , na Arshi ni kubwa sana kuliko Kiti).

MwenyeziMungu anasema:-

"Ndiye Mungu mwenye rehma aliyetawala juu ya Ashi yake".

(Taha -5).

Ilimu yetu haiwezi kuizizunguka na kuzijua nyota ambazo ni pambo la mbingu ya dunia, kwa hivyo hatuna uwezo wa kuizunguka kwa kujua kila kitu juu ya Mola wetu.

MwenyeziMungu anasema:-

"Wala hawalijui lolote katika elimu yake ila alipendalo. Enzi yake imeenea mbingu na ardhi wala kuvilinda hivyo hakumshindi na Yeye peke Yake ndiye Aliye juu na ndiye Aliye Mkuu."

(Al -Baqarah -255).

Kwa hivyo sisi wanadamu hatuna ilimu ya kutuwezesha kumjua Allah kama alivyo, isipokuwa kwa ilimu itokayo kwake, na kwa vile umekwishatujia kutoka kwa MwenyeziMungu ubainifu na ilimu, na Akatujulisha juu Yake na juu ya sifa Zake, kwa hivyo tusimame hapo hapo bila ya kuongeza mengine kutoka kwetu, na tumtukuze MwenyeziMungu kwa.

 

KUMTAKASA MWENYEZIMUNGU KWA KUTOMFANANISHA NA VIUMBE

Inaposemwa kwamba; "Mfalme fulani ni karimu na mlinzi wake ni karimu na mwanawe ni karimu", Bila shaka asikiaye hayo atatofautisha baina ya ukarimu wa mfalme, ukarimu wa mlinzi, na wa mtoto wa mfalme ingawaje wote hao ni wanaadamu.

Na utakapoambiwa kuwa; "MwenyeziMungu ni Karimu", bila shaka utajuwa kuwa ukarimu wake MwenyeziMungu aliyetukuka haufanani hata kidogo na ukarimu wa viumbe vyake  alowamiliki na walio dhaifu.

Hivi ndivyo ilivyo katika sifa zake zote MwenyeziMungu Subhanahu wa Taala.

Elimu Yake ni tofauti na elimu ya viumbe vyake, na Hikima Yake inatofautiana na hikima ya viumbe vyake na Rehema Zake juu ya walioamini na Ghadhabu Zake juu ya waliokufuru ni tofauti na rehema na ghadhabu za viumbe vyake. Vyote hivyo na venginevyo Yeye amekamilika navyo ukamilifu wa hali ya juu kabisa usio na mfano wowote;

MwenyeziMungu anasema:-

"Hakuna chochote mfano wake nae ni mwenye kusikia, na mwenye kuona."

(Al-Shuraa 11)

    Kwa hivyo upungufu unapatikana kwa asiyekuwa Yeye, ama Yeye (MwenyeziMungu) Pekee ndiye Aliyekamilika.

 

 

KUYAAMINI MAJINA NA SIFA ZA MWENYEZI MUNGU KAMA YALIVYO

KATIKA QURANI NA SUNNAH

Miongoni mwa fadhila za MwenyeziMungu juu yetu ni kwamba kwa Ilimu Yake na kwa Hikima Yake ametujulisha ni nani Yeye, ametufundisha hayo kupitia katika kitabu chake na katika mafundisho ya Mtume wake (SAW). Akatujulisha kwamba ana majina yaliyo bora kabisa na sifa za ukamilifu, na kwamba haiwezekani kwa Mwislamu kubadilisha katika sifa alojipa Mwenyewe Subhanahu Wataala.

    Mwanamke mmoja wa kizungu ambaye mumewe ni Mwislamu alikwenda kujadiliana na Sheikh Al Hakim. Huyu ni Sheikh aliyemsilimisha mumewe bibi huyo.

Majadiliano yalikuwa kama yafuatavyo:-

Bibi: Mimi siamini kuwepo kwa MwenyeziMungu mpaka nimuone kwa urefu na mapana. (Astaghafiru llah).

Sheikh:- Jee wewe unampenda mumeo?

Bibi :-  ndiyo.

Sheikh  :- Mimi sisadiki.

Bibi :- Kwa nini?

Sheikh:- Siamini kama unampenda mumeo mpaka niyaone hayo mapenzi kwa marefu na mapana na uzito na rangi yake.

Bibi :- Mapenzi yapo lakini haiwezekani kuyaona kama yalivyo.

Sheikh :- Basi MwenyeziMungu ni mfano ulio bora zaidi, sisi tunaamini kuwa yupo ingawaje hatuna uwezo wa kumjua jinsi alivyo. Na vingapi tunaviamini ingawaje havionekani. Usingizi unatujia na sisi hatuujuwi jinsi ulivyo na wala hatujuwi vipi na wapi unatokea. Kuamka pia, furaha na hata kuna wengi ambao hawaelewi umeme ukoje lakini wanaamini kuwepo kwake na kuna mambo mengi ya aina hiyo.

 

HAIWEZEKANI KUUJUWA MFANO WAKE

Kwa dalili za kiakili na za kunukuu tunaelewa kwamba MwenyeziMungu ni tofauti na viumbe Vyake, na kwa ajili hiyo sifa zake lazima zitofautiane na sifa za viumbe vyake, kwa sababu kila kiumbe kina upungufu wa sifa, lakini yeye Subhanahu Wa taala ndiye aliyekamilika.

Kutoka Kwake tumejulishwa Wasfu Wake pamoja na ubainifu, kwa hivyo tuziamini na kufuata kama alivyotujulisha katika kitabu chake kitukufu pamoja na Mafundisho ya Mtume wake (SAW) bila kuuliza juu ya mfano Wake.

MwenyeziMungu anasema:-

 "Hakuna chochote mfano Wake Naye ni Mwenye kusikia na Mwenye kuona."

(Al -Shuraa -11)

Kwa hivyo Yeye ni Mwenye Kusikia na Mweye Kuona lakini kuona na kusikia kwake si kama kuona na kusikia kwa viumbe vyake na sisi hatuna ilimu ya kumzunguka na kumjua  vilivyo na Yeye ndiye Aliye Mkuu Aliye Juu.

 

AKILI NA KUFIKIRIA

MwenyeziMungu amemuumba binaadmu akiwa na akili, ili aweze kutambua uhakika wa mambo, na kwa akili hiyo aweze kupambanua baina ya haki na batili na aweze kuelewa kinachomdhuru na chenye manufaa naye. Ndiyo sababu aliyepoteza akili akawa amenyanyuliwa kalamu (haandikiwi dhambi wala thawabu). Mwenyezi Mungu akaipa akili hiyo uwezo wa aina nyingi.

MwenyeziMungu amempa binaadamu uwezo wa kufikiria juu ya mambo mbali mbali ili uwezo huo umsaidie katika kupanga mambo yake na kuyafikiria.  Lakini uwezo huo (wa kufikiria) una udhaifu na pia una mipaka yake.

Mfano; ukisifiwa ju ya mji, utaanza kufikiria mambo mengi juu ya mji huo, lakini unapokuja kuuona mji huo utaona kwamba sio kama vile ulivyokuwa ukiufikiria.

Mfano mwingine; Mlango ukigongwa utajua kwamba yupo mtu anayegonga mlango, lakini uwezo wako wa kufikiria unashindwa kumjua ni nani anayegonga mlango huo, urefu wake, upana wake, rangi yake nk.

Kwa hivyo Nguvu za Akili zimevuka mpaka wa mlango na kuweza kujuwa kuwa yupo anayegonga, lakini Uwezo wa Kufikiria umeshindwa kuupenya mlango na kumjua mgongaji.

(MwenyeziMungu Ndiye Mwenye Sifa Tukufu) Akili inaamini kuwa yupo Mwenyezi Mungu, lakini Uwezo wa Kufikiria unashindwa kufikiria jinsi MwenyeziMungu alivyo.

"Hakuna chochote mfano Wake Naye ni Mwenye Kusikia na Mwenye Kuona".

As Shuura- 11

 

 

MAJINA MAZURI MAZURI

MwenyeziMungu ana majina mazuri mazuri tisini na tisa, atakayeyahifadhi (na kutimiza wajibu wa majina hayo) ataingia Peponi. Na Mtume (SAW) ametujulisha juu ya majina mengine mbali ya hayo.

MwenyeziMungu anasema:-

"Na MwenyeziMungu ana majina mazuri mzuri muombeni kwayo."

(Al -Aaraf -180).

Miongoni mwa majinaa Yake mazuri ni haya yafuatayo:-

Al Waahid - Mmoja Aliyepekee.

Al Ahad - Mmoja.

Assamad - Anayetegemewa Kwa Kila Mahitaji Naye Hana Shida Ya Kitu

Al Qayyum - Anayesimamia Kila Jambo.

Al Khaliq - Muumbaji.

Al Musawwir - Mfanyaji Wa Sura Za Kila Aina Ya Viumbe

Al Rahman - Mwenye Kuneemesha Neema Kubwa Kubwa

Al Rahim - Mwenye Kuneemesha Neemesha Ndogo Ndogo.

Al Latif - Mpole

Al Razzaq - Mtoaji Wa Riziki.

Al Waasi-a  -  Ambaye Rehema Na Elimu Yake Imeenea Kila Mahali

Al Adhiym - Aliye Mkuu

Al Aziz - Mshindi Asiyedhalilika

Al Hakiym - Mwenye Hikima

Al Aliym - Ajuwaye Kila Kitu

Al Haafidh - Mwenye Kuhifadhi (Kulinda).

Al Haadi - Mwenye Kuongoza.

Al Muhu-yi - Mwenye Kuhuyisha

Al Mumiyt - Mwenye Kufisha

Al Waarith - Atayebaki Baada Ya Kutoweka Viumbe Vyote

 

 

USHAHIDI KWAMBA MUHAMMAD(SAW) NI MTUME WA MWENYEZIMUNGU

Dalili Zilizo Wazi Juu Ya Ukweli Wa Utume Wa Muhammad (SAW)

MwenyeziMungu huwapa Mitume wake ushahidi (Miujiza) wa kuthibtisha ukweli wa ujumbe wao ili wasikanushwe na watu.

MwenyeziMungu anasema:-

"Kwa hakika tuliwapeleka Mitume wetu kwa dalili waziwazi (Miujiza)".

Al Hadiyd -25

Na MwenyeziMungu amempa Mtume Muhammad (SAW) ushahidi ulio wazi kabisa pamoja na dalili zisizo na shaka ambazo ni Miujiza, ikiwemo ifuatayo:

 

MUUJIZA WA QURANI

MwenyeziMungu ameijaalia miujiza ya Muhammad(SAW) iwe ya daima ili iwe ni hoja kwa watu wote hadi siku ya kiama na akaijaalia Qurani tukufu kuwa ni muujiza wenye nguvu kupita zote,  na akaihifadhi isiweze kubadilishwa (maneno yake).

MwenyeziMungu anasema:-

"Basi jee mtu aliye na dalili wazi itokayo kwa Mola wake (naye ni Nabii Muhammad) na anaifuata (dalili hiyo) shahidi atokaye kwake MwenyeziMungu (Nayo ni Quran) na kabla yake kilikuwa kitabu cha Musa kilichokuwa kiongozi na rehema (nayo ni Taurat ambayo ilitaja habari za Nabii Muhammad)(anaweza kuwa muongo? Hawezi kuwa muongo), basi hao (walioongoka) wanamuamini yeye, na atakayemkataa katika makundi (ya maadui) basi moto ndio mahali pa miadi yao".

(Hud -17)

Ushahidi huu wa Qurani upo wa aina nyingi zinazothibitisha miujiza yake, na tutazitaja baadhi yake.

 

UFASAHA WA QURANI NA KUTOKUCHOSHA KWAKE

Maandishi ya Qurani yanatokana na herufi za 'hija-a' (alfabeti), (Alif, Be, Te, Thee …….)

Na maneno ya wanaadamu yatokana na herufi hizi hizi, lakini ufasaha wa Qurani  umewafanya wanadamu na majini washindwe kuleta sura ndogo za mfano wa Qurani.

Unaposikia hotuba iliyotolewa kwa ufasaha au nyimbo nzuri, zinakupendeza, lakini ukishasikiliza mara nyingi, hamu yake inaondoka, hii ni kwa sababu maneno yanayosemwa na wanadamu kwa kawaida huchosha kuyasikia yanapokaririwa mara kwa mara.

Lakini Waislamu mara ngapi na ngapi wanaisoma SuratulFatiha au Sura ndogo ndogo za Qurani, au mara ngapi wanahitimisha Msahafu na kurudia tena na tena bila kuchoka wala kutokwa na hamu. Hii ina maana gani? Bila shaka hii ni dalili iliyo wazi kwa kila mwenye akili kwamba Qurani ni maneno ya MwenyeziMungu yasiyochosha (juu ya kukaririwa kwake).

Na Qurani imewabishia wanaoukanusha ukweli wake, walete sura moja yenye mfano wake.

MwenyeziMungu anasema:-

"Na mkiwa mna shaka kwa hayo tuliyomteremshia Mtumwa wetu basi leteni sura moja (iliyofanywa na mtu) mfano wake na muwaite waungu wenu wasiokuwa MweyeziMungu (wakusaidieni) ikiwa mnasema kweli. Na msipofanya, na hakika hamtafanya kamwe, basi uogopeni moto ambao kuni zake ni watu na mawe, uliowekewa makafiri."

(Al - Baqrah -23-24)

 

QURANI YAELEZA MAMBO YA GHAIBU

Hapana aijuwae ghaibu isipokuwa MwenyeziMungu, na Qurani imeeleza habari nyingi za ghaibu. Na hii ni dalili kwamba Qurani imetoka kwa MwenyeziMungu na kwamba Muhammad (SAW) aliyekuja nayo ni Mtume wa MwenyeziMungu.

1)  Zifuatazo ni miongoni mwa habari za ghaibu zilizoelezwa katika Qurani tukufu:-

Wakati Wafursi (Iran) waliokuwa wakiabudu moto (na masanamu) walipowashinda Warumi waliokuwa watu wa Kitabu, katika nchi ya Palastina, washirikina wa Makka (waliokuwa wakiabudu masanamu kama wao) walifurahi sana na wakawa wanawaambia Waislamu (kwa kuwatisha), kwamba mwisho wao utakuwa kama mwisho wa Warumi.

 Habari hizi ziliwahuzunisha sana Waislamu (ambao pia ni watu wa kitabu, Qurani). Ndipo MwenyeziMungu alipoteremsha aya isemayo:-

"Aliyf Laam Mym.

Warumi wameshindwa katika nchi iliyo karibu na (na nchi ya bara Arabu nayo ni Shamu), nao baada ya kushindwa kwao watashinda.

Katika miaka michache. Amri hii ni ya MwenyeziMungu kabla (yake) na baada (yake) na siku hiyo Waislamu watafurahi.

Kwa nusura ya MwenyeziMungu. Humnusuru Amtakaye Naye ni Mwenye Nguvu na Mwenye Rehema.

 (Hii ni) ahadi ya MwenyeziMungu, MwenyeziMungu havunji ahadi Yake lakini watu wengi hawajui."

(Al Rum - 1-6).

Zilipoteremshwa aya hizi Waislamu wakawa wanazisoma mara kwa mara wakiwadhihaki washirikina kwa vile walivyowatabiria kwamba na wao Waislamu watashindwa kama walivyoshindwa Warumi.

Mmoja katika makafiri akashindana na Abubakar (RA) kwa mali (dau), akidai kwamba Wafursi hawatoweza kushindwa kwa muda huo mchache. "(BIDHI-I-SINIYN)", neno lililotumika katika aya hiyo maana yake ni  baina ya miaka mitatu na tisa, sio zaidi, na Abubakar(RA) alikubali kushindana na kafiri huyo kwa dau, na hii ilikuwa kabla haikuharamishwa kushindana kwa mali (dau), na Mtume (SAW) aliruhusu ushindani huo.

Makafiri wakasimama pamoja na kafiri mwenzao aliyeingia katika ushindani, na Waislamu wakawa wanaingoja ahadi iliyotolewa na MwenyeziMungu itimie, na Mtume(SAW) akasema kuwa (BIDHI_I) ni baina ya tatu na tisa.

Unabii (wa Mtume(SAW)) uliingizwa katika mtihani mkubwa, kwa sababu umekuja na habari kutoka kwa MwenyeziMungu zikibashiri ushindi wa Warumi ambao hivi karibuni tu walishindwa vibaya sana, na hapakuwa na dalili kuwa wangeweza kushinda tena. isitoshe waadi uliowekwa (kuwa watashinda) ulikuwa chini ya miaka kumi. Na habari hizo zimeelezewa kwa njia ya kuwafahamisha watu kuwa Warumi watashinda bila shaka yoyote ile;

"Ahadi Ya Mwenyezi Mungu Ambae Havunji Ahadi Yake Lakini Watu Wengi Hawajui".

Na Makafiri wote wanaelewa kwamba Muhammad (SAW) ni mwenye akili timamu kupita wote, na kwamba asingejiingiza katika mtihani kama huu angekuwa hana uhakika utokao kwa Mola wake pamoja na Imani aliyo nayo juu ya Mola wake.

Haikupita miaka saba na ahadi ya MwenyeziMungu ikatimia. Wafursi walishindwa, Waislamu wakafurahi, na ukweli wa Mtume(SAW) ukadhihiri, na watu wengi wakaamini na kuingia katika dini ya MwenyeziMungu.

 

2) Majaribio mengi yalifanywa na Washirikina wa Makka pamoja na Mayahudi ya kutaka kumuuwa Mtume(SAW), kivita, na kwa kufanya hila mbali mbali. Juu ya hayo, MwenyeziMungu akateremsha aya katika Qurani zikimhakikishia Mtume wake (SAW) kwamba maadui wake hawawezi kumdhuru.

Mwenyezi Mungu anasema;

"Na kumbuka tulipokwambia 'Hakika Mola wako amekwisha wazunguka hao watu (wabaya)"

(Al - Israa -60).

Na akasema:-

"Ewe Mtume!  Fikisha uliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wako na kama hutofanya basi hukufikisha ujumbe wake na MwenyeziMungu atakulinda na watu."

(Al -Maidah -67)

Baada ya kuteremka aya hizi, Mtume (SAW) akawaamrisha Masahaba waliokuwa wakimlinda (RA) kwa kuwaambia;

"Enyi watu! towekeni msinilinde tena, maana MwenyeziMungu Aliyetukuka keshatoa waadi wa kunilinda na hakuna awezaye kunidhuru".

Ibnu Jarir, Al Tirmidhy na Al Hakim.

 

Ingawaje mbinu nyingi zilifanywa za kutaka kumuuwa  Mtume(SAW), lakini MwenyeziMungu alizishinda kama alivyoahidi.

Baada ya kufa kwa Mtume(SAW), watatu miongoni mwa Makhalifa wanne Waongofu (Al Rashidiyn, nao ni, Omar Othman na Ali (R.Anhum)), wote waliuliwa, ingawaje wakati huo Uislamu ulikuwa na nguvu zaidi na ukafiri ulikuwa umekwisha toweka na amani ilikuwa imeenea kwa ajili ya usalama wa Makhalifa hao, na wakati Mtume(SAW) hapakuwepo na amani kama hiyo, lakini Ulinzi Wake MwenyeziMungu ndio uliomwokoa Mtume (SAW) aliyekuwa na uhakika juu ya ahadi hiyo na akaendelea kuwalingania watu, akawaondoa walinzi wake na MwenyeziMungu akamtimizia yale Aliyomuahidi.

 

3)   Mitume (Alayhimu Ssalaam), hapo mwanzo walikuwa wakiteremshwa mmoja baada ya mwengine, lakini baada ya kuja kwa Mtume (SAW), hakuteremsha Mtume mwengine,  na hii inasadikisha kauli ya MwenyeziMungu isemayo:-

"Muhammad si baba wa yeyote katika wanaume wenu bali yeye ni Mtume wa MwenyeziMungu na mwisho wa Mitume. Na MwenyeziMungu ni Mjuzi wa kila kitu."

Haa Miym Sajdah -53 (Fusilat)

Hii ni ahadi inayozungumzia Ghaybu iliyosadikishwa na karne nyingi zilizokuja baada ya Mtume Muhammad (SAW) ikisadikisha kuwa hapana Mtume baada ya "Mwisho wa Mitume" (Muhammad (SAW)).

 

MIUJIZA YA SAYANSI KATIKA QURANI

Mwenyezi Mungu anasema;

"Tutawaonyesha (ukweli wa) maneno yetu haya katika nchi za mbali na katika nafsi zao wenyewe mpaka IWABAINIKIE kwamba haya ni kweli. Je! Haikutoshi kwa Mola wako kuwa Yeye ni mjuzi wa kila kitu?"

Ha Miym Sajdah - 53 (Fusilat)

Ahadi ya Mola wetu imetimia katika wakati wetu huu. Makafiri ambao bado HAUKUWABAINIKIA ukweli wa dalili za Mwenyezi Mungu, wakaziona dalili za MweyeziMungu katika kuumba kwake, katika sehemu mbali mbali za dunia. Hawakuweza kuyaona hayo isipokuwa kwa kutumia vyombo na njia za kisasa kabisa, mfano wa ndege, manowari zinazozama baharini (Submarine), vyombo ambavyo hapo zamani wanadamu hawakuwa wakivimiliki.

Ikawabainikia kwamba MwenyeziMungu ndiye aliyempa Muhammad(SAW) siri hizo katika kuumba (akaweza kuzijua tokea miaka elfu moja mia nne aliyopita), wakati hapakuwa na vyombo vya kufanyia uchunguzi wa kielimu (maabara) na pia hapakuwa na ndege wala manowari  zinzozama baharini na hii ikawa ni namna nyingine ya miujiza ya  Qurani ikiwabainishia makafiri ukweli wa ujumbe aliokuja nao Mtume Muhammad (SAW) na ukweli wa dini  hii.

Miongoni mwa miujiza hiyo ni :-

1) Hapana aliyekuwa akijua kwamba asili ya sayari zote pamoja na nyota zake ni moshi, mpaka zana za uchunguzi wa sayansi zilipoendelea sana na wachunguzi kuona mabaki ya moshi katika hali ya kubadilika zikigeuka kuwa nyota hadi wakati wetu huu.

Na MwenyeziMungu anasema :-

"Kisha akazielekea mbingu na zilikuwa moshi basi akaziambia mbingu na ardhi. "Njooni mkipenda msipende". Vyote viwili vikasema; 'Tumekuja hali ya kuwa wenye utiifu".

Haa mym Sajdah- 11.

 

2) Wachunguzi hivi karibuni tu wamegundua kuwa nyota bado zinaendelea kuumbwa na kwamba mikusanyiko ya nyota (Galaxies) inazidi kubaidika kila moja mbali na nyingine na kwa njia hii ikajulikana kuwa nyota zilizo angani zingali zinatawanyika na kuwasaika na kuenea mbali zaidi.

MwenyeziMungu amesema:-

"Na mbingu tumezifanya kwa kudra yetu na hakika sisi ndio wenye uwezo wa kuzieneza".

(Al - Dhariyyat -47).

 

3) Wachunguzi hivi karibuni pia wamegundua kwamba hapo mwanzoni mwezi ulikuwa ukiwaka na kutoa mwangaza wenyewe bila ya kumulikiwa na jua na hatimaye mwangaza huo ukafutika na kwamba mwangaza tunaoupata kutoka mwezini wakati wa usiku asili yake ni mwangaza wa jua unapoumulika mwezi kisha mwangaza huo unaturudia sisi.

MwenyeziMungu anasema:-

"Kisha tumeifuta (tumeuondosha mwangaza) ishara ya usiku na tukaifanya ishara ya mchana yenye mwangaza."

Bani -Israil - 12  (Israa).

Maulamaa wa tafsiri wamesema (Ishara ya usiku ni mwezi na Ishara ya mchana ni jua) na Ibni Abbas (RA) amesema;

"Mwezi ulikuwa ukitoa mwangaza kama jua".

Maulamaa wa tafsiri wamesema;

"Maana ya kauli yake MwenyeziMungu;

"Tumeifuta ishara ya usiku"  ni

(Tumeufuta mwangaza wake).

Kisha Qurani ikataja juu ya mwezi na taa yake (jua )

MwenyeziMungu anasema:-

"Ni mwenye kuleta baraka yule aliyezijaalia nyota mbinguni na akajaalia humo taa (jua ) na mwezi unaonga'ra".

(Al -Firqan -61).

Zingatia! MwenyeziMungu amesema "(TAA)" (Siraajan), na lau kama mwezi unatoa mwangaza kama jua (ambalo lenyewe linawaka na kutowa mwangaza), basi MwenyeziMungu angalisema "TAA MBILI" (Siraajayni) na asingelisema "TAA moja"(Siraajan).

4)  Watu, hapo zamani walikuwa wakidhani kwamba anayepaa kueleka anga za juu huvuta pumzi kwa raha zaidi, lakini  baada ya mwanadamu kuunda ndege za kisasa na kuruka angani akagundua kwamba anayepaa juu, kifua chake hudhikika  na kufikia  hali ya juu ya kudhikika  na hii ni kwa sababu hewa hupungua kila anapopaa na kuelekea juu zaidi.

 

MwenyeziMungu anasema:-

"Basi yule ambaye MwenyeziMungu anayemtaka kumuongoza hukifungulia kifua chake Uislamu; na yule ambaye MwenyeziMungu anataka kumhukumu kupotea hufanya kifua chake kizito kinaona taabu kubwa (kufuata huo Uislamu) kama kwamba anapanda mbinguni (kusikokuwa na pumzi) ".

(Al - An -am -125)

 

5) Hakuna aliyekuwa akifikiria kwamba jabali limezama ndani ya ardhi kama vigingi mpaka wataalamu walipogundua kwamba chini ya ardhi hii ngumu tunayoishi juu yake, pana tabaka laini mfano wa tope zito na kwamba kila jabali lina (mfano wa) mizizi sehemu ya chini  inayopiga mbizi ndani ya tabaka hizo laini na kuizuia ardhi ngumu hii tunayoishi juu yake isije ikazama katika ardhi laini iliyo chini yetu .

MwenyeziMungu amesema:-

"Na milima kuwa kama vigingi vya ardhi ".

(A n  -Nabaa -7)

"Na tukaweka katika ardhi milima (yenye kuthibiti barabara katika ardhi) ili isiwayumbishe".

(Al _Anbiyaa -31).

 

6) Wataalamu wakagundua pia kwamba maji yanapoteremka ndipo mmea unapoota na kwamba mmea hutoa mada yenye rangi ya kijani yenye kutengeneza punje na matunda. Na kutokana na mada hii ya kijani matunda na punje za nafaka hupatikana.

MwenyeziMungu anasema:-

"Na yeye ndiye aliyeteremsha maji kutoka mawinguni, na kwayo tunaotesha mimea ya kila kitu. Kisha tunapeleka kuchipua (majani ya) kijani (mada ya kijani 'chlorophyl'). Katika (mimea) hiyo tukatoa ndani yake punje zilizopangana."

(Al _Anam -99)

1)                                                                                                                                                                   Wachunguzi pia wamegundua kwamba mimea yote ipo dume na jike, na haya hayakuwa yakijulikana hapo mwanzoni.

MwenyeziMungu anasema:-

"Ametukuka MwenyeziMungu alieumba dume na jike katika (vitu) vyote. Katika vile vioteshayo ardhi na katika nafsi zao (wanaadamu) na katika vile wasivyovijua."

(Yaasin -36)

 

8) Madaktari wamegundua kwamba mishipa ya hisia (nerves) inayohisi maumivu ya kuungua na inayohisi ukali wa baridi ipo penye ngozi tu, kama ilivyo mishipa mengine ya hisia. (yote imo penye ngozi). Na hii ndio sababu inayomfanya mtu ahisi maumivu ya sindano anayopigwa na daktari pale inapoingia ngozini, ama sindano ikishazama ndani ya mwili (katika nyama) maumivu hutoweka.

Na Qurani imebainisha kwamba maumivu ya kuungua hupatikana penye ngozi tu. MwenyeziMungu anasema:-

"Hakika wale waliozikataa aya zetu tutawaingiza katika moto. Kila ngozi zao zitakapowiva tutawabadilisha ngozi nyengine badala ya zile ili wawe wanaonja uchungu wa adhabu (maisha). Hakika MwenyeziMungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hekima.

(An -Nisaa -56).

 

9) Wataalamu pia wakagundua kwamba maziwa ya wanyama hukamilika utengenezaji wake baada ya kupita baina ya mavi ndani ya utumbo mdogo wa mnyama huyo (small intestine), na vibakiavyo humo hutoka vikiwa mfano wa kinyesi. Wakati hapo mwanzoni mabaki hayo yalikuwa mfano wa choo maji maji. (mfano wa matapishi). Baada ya kupita katikati ya mavi yaliyo ndani ya utumbo mdogo, maziwa hupitia katika damu (ili yasafike kutokana na uchafu wa kinyesi), na yanapotoka katika damu husafishwa maziwa hayo kutokana na damu katika matiti.

 

 

MwenyeziMungu anasema:-

"Na bila ya shaka katika wanyama mna mazingatio makubwa kwa ajili yenu. Tunakunywisheni katika vile vilivyomo matumboni mwao (vikitoka) baina ya choo na damu (nayo ni maziwa tukakunywisheni), maziwa safi mazuri kwa wanywao".

(Al - Nahli -66).

 

10) Hapana aliyekuwa akijua kwamba chini ya bahari kuna mawimbi ya ndani mbali ya mawimbi ya juu tuyaonayo, na watu hawakuwa wakijuwa kwamba sehemu za chini ya bahari (kubwa) ni giza (totoro). MwenyeziMungu amewaumba samaki wanaoishi sehemu za chini ya bahari kubwa wakiwa na (mfano wa) taa ili iwaangazie njia katika viza hivyo.

Na hapana aliyekuwa akijua kwamba mawimbi, kwa sababu ya kutotulia kwake huirudisha juu miale ya mwangaza na kusababisha miale hiyo isifike chini ya bahari, na kwa hivyo hupatikana giza lnalozidi kila uendapo chini ya bahari mfano wa mawingu yanapozuwia mwangaza wa jua kufika juu ya ardhi.

Siri zote hizi MwenyeziMungu amezieleza katika aya moja tu.

MwenyeziMungu anasema:-

"Au (amali zao zile mbaya) ni kama giza katika bahari yenye maji mengi inayofunikwa na mawimbi na juu yake kuna mawimbi na juu yake (kuna) mawingu. Giza hili juu ya hili, (hata) anapoutoa mkono wake anakaribia asiuone (kwa kiza kilivyoshtadi ) na ambaye MwenyeziMungu hakumjaalia nuru hawi na nuru."

(An - Nur -40)

Siri hizi na nyenginezo zilizomo katika anga za juu, chini ya bahari, chini ya ardhi, ndani ya matumbo ya wanyama, ndani ya miti na jinsi binaadamu alivyoumbika, binaadamu hawakuwa wakizijua isipokuwa katika zama hizi za karibu na baada ya kuunda vyombo na ala za kisasa zilizomwezesha kuzijua siri hizi.

Basi ni nani aliyemjulisha Muhammad(SAW) siri hizi miaka elfu na mia nne iliyopita wakati ambapo siku hizo hapakuwa na ndege wala submarine wala hapakuwa na uvumbuzi wa kisayansi?

Haya yote yanamthibitishia kila mwenye akili akiwa yupo Amerika au Urusi. Bara hindi au Uchina, Ulaya au Australia kwamba Qurani hii imeteremshwa kwa ujuzi wa MwenyeziMungu.

MwenyeziMungu anasema:-

"Sema'; Ameteremsha haya yule ajuaye siri za mbinguni na ardhini."

Al Furqan - 6

Huu pia ni ushahidi kwa kila mwenye akili kwamba Muhammad(SAW) ni Mtume wa MwenyeziMungu.