FADHILA ZA SIKU KUMI ZA DHUL-HIJJA*

 

Inatupasa tumshukuru Allaah kwa neema Aliyotujaaliya ya kutuwekea miezi mitukufu, au siku tukufu au nyakati tukufu  ambazo vitendo vyake vyema huwa na thawabu nyingi sana .  Na hivi tunakaribia kabisa kuingia katika mwezi mwingine mtukufu wa Dhul-Hijja Katika mwezi huu, siku kumi za mwanzo ni siku bora kabisa katika dunia na zina fadhila  kubwa kutokana na aya na hadithi zifuatazo:

 

  1. Allaah Ameziapia "Naapa kwa alfajiri -  Na kwa masiku kumi"  Suratul-Fajr 89:1-2

  2. "Ili washuhudie manufaa yao na kulitaja jina la Allaah katika siku zinazojulikana Suratul-Haj 22:28

Ibn Abbas kasema hizo ni siku kumi  za Dhul-Hijja 

 

Hadithi Inatokana  na Ibn Abbas (Radhiya Llahu anhuma). Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) amesema:  Hakuna  siku ambazo  vitendo vyake vyema  Anavipenda  Allaah kama siku kumi hizi (siku kumi za mwanzo wa mwezi wa Dhul-Hijja) Akaulizwa  je, hata  Jihaad katika njia ya Allah?  Akajibu  (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) “hata jihaad katika njia ya Allaah isipokuwa mtu aliyekwenda  na maisha yake na mali yake ikawa  hakurudi na kimojawapo”  (Al Bukhari)

 

Vitendo  vyema vya kufanya katika siku kumi hizi

1. Kutimiza Hajj na Umra (kwa mwenye uwezo)

2. Kuomba Toba ya kweli

3. Kumkumbuka sana Allaah kwa Tasbih, Tahmid,  Tahlil, , Takbir yaani

Subhana Allaah, Alhamdulillah,  Laa Ilaaha Illa Allah,  Allaahu Akbar

Inavyopasa kufanya takbir : Allahu Akbar, Allahu Akbar, Laa Ilaha Illa Allaah Wa-Allaahu Akbar, Allahu Akbar Walillahil-hamd

Takbir hii ni aina mbili :

1)  Wakati wote usiku au mchana  tokea unapoingia mwezi wa Dhul-Hijja na inaendelea mpaka  siku ya mwisho ya siku za Tashriq.  

2)  Takbir baada ya kila swala na huanza asubuhi ya siku ya Arafat  mpaka siku ya mwisho ya Tashriq .

Wanaume  waseme kwa sauti ili kuwakumbusha wengine kurudisha sunna ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam)  na wanawake waseme kimya kimya isipokuwa wakiwa na mahaarim wao.    

Hadithi : Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) kasema "Atakayemuongoza mwenzake  kufanya jambo jema atapata thawabu sawa sawa na za yule atakayetenda hilo jambo jema" Muslim .

Imesemekana kuwa ukiandama mwezi wa Dhul-Hijja Ibn 'Umar na Abu Hurayrah walikuwa wakienda sokoni na kufanya takbir kwa sauti ili kuwakumbusha watu.

4. Kufunga siku hizi hasa siku ya Arafah.  

                 

5. Kuzidisha vitendo vyema mbali mbali kama kusali sunna zaidi, kusoma Qur’an, sadaqa, duaa , kutii wazazi, kuwasiliana na jamaa (kuunga undugu), kufanya wema na jirani, kuambizana yaliyo mema na kukatazana yaliyo maovu, kufanyiana wema na ihsani .

  

6. Kuchinja baada ya swala ya Eid  Kasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) "Basi Swali kwa ajili ya Mola wako na uchinje " Suratul Kawthar 108:2   Ibada  hii ya kuchinja ni sunna iliyosisitizwa hata baadhi ya wanachuoni wameona kuwa ni wajib kwa kila aliyekuwa na uwezo.

Yanayompasa kufanya mwenye kutaka kuchinja

Baada ya kutia nia ya kuchinja, usikate nywele wala kucha mpaka umalize kuchinja kutokana na hadithi:  Ukiandama mwezi wa Dhul-Hijja  na ikiwa  yuko anayetaka kuchinja basi asikate kucha wala nywele wala kutoa kitu katika ngozi yake mpaka akimaliza kuchinja" Muslim

Hii ni fadhila na neema kwetu kuwa tuwe katika hali yaihraamkama waliyokuwa  kwenye Hijja. Ikiwa umesahau na mfano ukakata kucha basi endelea tu na nia yako mpaka umalize kuchinja.

7. Kuhudhuria sala ya Idi  -Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam)  amewahimiza mpaka wanawake walio katika hedhi na wazee kwenda kusikiliza hutba ya swala, wakati wa swala ukifika wanawake hao wenye hedhi wajitenge kando hadi itakapomalizika na kisha wajiunge na wenzao kusikiliza khutba. Na ijulikane kuwa swala ya Eid huswaliwa kiwanjani kwani hiyo ndio sunnah kutoka kwa Mtume wetu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam).

 

SIKU YA ARAFAH  ni siku ya tisa ya Dhul-Hijja

Siku hii tukufu ni siku iliyokamilika dini yetu.

Thawabu za kufunga siku hii ni kufutiwa madhambi ya miaka miwili.  Imetoka kwa Abi Qatada (Radhiya Llahu anhu) (Kasema mjumbe wa Mwenye Enzi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala) kuhusu saumu ya Arafah  kuwa inafuta madhambi ya mwaka uliopita na  uliopo) Muslim

Vile vile inapasa kumtaja sana Allaah siku hii kama alivyosema Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kuwa "Dua bora kabisa ni katika siku ya Arafah,  na yaliyo bora kabisa niliyosema mimi na Mitume kabla yangu niLaa Ilaaha Illa Allaah Wah-dahu la sharika lahu, lahul-mulku walahul-hamdu wa huwa 'alaa kulli shay-in qadir’ "

 

SIKU YA KUCHINJA  ni siku ya Eid Kubwa

Kasema Mtume: "siku iliyo tukufu kabisa kwa Mwenye Enzi Mungu ni siku ya kuchinja, kisha siku ya kutulia"  (yaani siku ya kukaa Mina)  Abu Dawud

 

SIKU ZA TASHRIQ : Siku ya kumi na moja na kumi na mbili na kumi na tatu ya Dhul-Hijja yaani baada ya siku ya Eid. Na siku hizi tatu zimeitwa siku za Tashriiq kwa sababu watu walikuwa wakikatakata nyama na kuzianika juani. Siku za kuanika (nyama) juani. Na pi siku hizi hujulikana kwa 'siku za Minaa'.

 

Namuomba Allaah atupe umri na afya na uwezo wa kuweza kufanya mengi ya kumridhisha katika siku hizi tukufu na siku zote nyingine ili tujipatie thawabu nyingi na  Atujaaliye tuwe  katika wale wanaosikiliza kauli  na daima wakafuata zile zilizo njema  .     Amin.