Haaruwn Ar-Rashiyd - Kiongozi Aliyezuliwa Mengi

 

Imeandaliwa Na: Muhammad Faraj Salem Al Saiy

 

 

 

YALIYOMO

Nasaba yake

Kutawala kwake

Kupenda kwake wanavyuoni

Kulia kwake kila anaposikia mawaidha

Misimamo isiyosahaulika

Misimamo yake alipokuwa kiongozi

Kifo chake

 

 

 


Juu ya kuwa Haaruwn Ar-Rashiyd alikuwa Kiongozi wa dola ya ‘Abbasiyyah aliyepigana Jihaad mara nyingi zaidi kupita Viongozi wote wa utawala wa bani ‘Abbaas, akateka miji mingi zaidi kuliko Viongozi wote wa kabila lake. Akajishughulisha zaidi na elimu pamoja na kuwaheshimu Maulamaa kupita Viongozi wote wa dola hiyo, hata hivyo huyu ni Kiongozi aliyezuliwa uongo mwingi kupita Viongozi wote wa Kiislamu.

 

Wamemzulia kuwa alikuwa akijishughulisha na wanawake na ulevi, wakamtungia visa vingi visivyosadikika isipokuwa tu kwa wale wenye maradhi ya kusadiki kila wanachokisoma.

 

Katika waandishi waliompa sifa zinazomsitahikia Kiongozi huyu ni Ahmad bin Khalkan aliyeandika yafuatayo ndani ya kitabu chake 'Wafiyat Al-‘Aayaan'. Aliandika:

 

"Haaruwn Ar-Rashiyd alikuwa miongoni mwa Viongozi wenye sifa njema, wanaoheshimika, mwingi wa kusali na kuhiji na kupigana Jihaad na kuteka. Alikuwa shujaa na mwenye rai yenye kusibu."

 

Sifa zake njema nyingi juu ya kupenda kwake kuinusuru haki na kuwaheshimu Maulamaa na kusikiliza na kufuata nasaha zao zimeandikwa ndani ya vitabu mbali mbali vya historia, na hayakanushi haya isipokuwa tu mwenye kupenda kusoma maneno yaliyobadilishwa na kugeuzwa kwa ajili ya matamanio ya nafsi.

Rudi Juu

 

 

Nasaba Yake

 

Jina lake ni Abu Ja’afar – Haaruwn Ar-Rashiyd bin Al-Mahdi Muhammad al Mansuwr Abu Ja’afar ‘Abdullaah bin Muhammad bin ‘Aliy bin ‘Abdillaah bin ‘Abbaas Al-Haashimy Al-‘Abbaasiy.

 

Alizaliwa katika mji wa Ar-Riy katika mwaka wa 148 Hijri na wakati huo baba yake ndiye aliyekuwa gavana wa mji huo pamoja na mji wa Khurasan, na mama yake alikuwa akiitwa Ummu Khayzaran ambaye pia ni mama wa Al-Haadiy, kaka yake Haaruwn Ar-Rashiyd.

 

Haaruwn Ar-Rashiyd alikuwa bado mtoto mdogo alipochukuliwa na baba yake ambaye wakati huo alikuwa mkuu wa jeshi lililofanikiwa kulishinda jeshi la Roma.

 

Rudi Juu

 

 

Kutawala Kwake

 

Haaruwn Ar-Rashiyd alipewa uongozi baada ya kufariki ndugu yake Al-Haadiy usiku wa Jumamosi tarehe 16 Rabiy’ul Awwal mwaka wa 170 Hijri kama alivyousia baba yao, na wakati huo Haaruwn alikuwa na umri wa miaka 22.

 

Ndani ya usiku huo huo Allaah alimruzuku Haaruwn Ar-Rashiyd mtoto wa kiume aliyepewa jina la ‘Abdullaah Al-Maamuwn, na haijapata kutokea siku katika historia ya Kiislamu ambayo ndani yake siku hiyo hiyo alifariki Kiongozi akatawazwa Kiongozi na akazaliwa Kiongozi.

 

Haaruwn Ar-Rashiyd alikuwa mfasihi wa lugha, mwenye elimu na hekima nyingi katika mambo yanayohusu uendeshaji wa nchi, na alikuwa mwingi wa kuswali na mwingi wa kutoa sadaka.

 

Alikuwa akipenda watungaji mashairi na alikuwa akiwalipa vizuri, na alikuwa akipenda kurusha mikuki na kupanda farasi.

 

Rudi Juu

 

 

Kupenda Kwake Wanavyuoni

                  

Haaruwn Ar-Rashiyd alikuwa akiwapenda sana Maulamaa na kuwaheshimu na alikuwa akiheshimu kila kinachohusiana na Dini na alikuwa hapendi mijadala isiyo na maana na pia hakuwa akipenda maneno mengi yasiyo na faida.

 

Anasema Al-Qaadhi Al-Fadhl:

 

"Sijapata kusikia juu ya Kiongozi aliyesafiri kwa ajili ya kutafuta elimu isipokuwa Haaruwn Ar-Rashiyd aliyesafiri pamoja na wanawe wawili Al-Amiyn na Al-Maamuwn mpaka Madiynah kwa Imaam Maalik (Allaah amrehemu) kwa ajili ya kusikiliza sharhi yake ya kitabu cha Al-Muwattwaa.”

 

Alihuzunika sana zilipomfikia habari za kifo cha ‘Abdullaah bin Al-Mubaarak, na mmoja katika Maulamaa aitwae Abu Mu’aawiyah ambaye ni kipofu alisema:

 

"Kila ninapomtaja Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) mbele ya Haaruwn Ar-Rashiyd humsikia akimswalia akisema 'Allahumma swalli ‘alaa sayyidiy', na siku ile nilipomsomea Hadiyth ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) inayosema: ((Natamani nipigane vita katika njia ya Allaah, kisha niuliwe kisha nihuishwe tena ili nipigane tena na niuliwe tena)). Haaruwn Ar-Rashiyd alilia kwa huzuni sana."

 

"Siku moja baada ya kumaliza kula", anaendelea kusema Abu Mu’aawiyah (Kipofu), "Mtu mmoja alikimbilia kunimiminia maji kwa ajili ya kuosha mikono yangu huku akiniuliza: "Unajua nani anakumiminia maji? Ni Mimi Haaruwn Ar-Rashiyd, kwa kwa ajili ya kuiheshimu elimu yako."

 

Rudi Juu

 

Kulia Kwake Kila Anaposikia Mawaidha

 

Anasema Mansuwr bin ‘Ammaar: "Sijapata kuona mtu anayelia sana anaposikia mawaidha kupita watu watatu hawa, Al-Fudhayl bin ‘Iyaadh na Haaruwn Ar-Rashiyd na mtu mmoja mwingine."

 

Na siku ile Al-Fudhayl bin ‘Iyaadh alipomwambia Haaruwn Ar-Rashiyd; 'Wewe ndiye mbebaji jukumu la Ummah huu." Haaruwn alilia sana mpaka akawa anahema.

 

Imenukuliwa kutoka kwa Imaam Al-Qurtubiy katika tafsiri yake kuwa mwanamke wa kiyahudi aliyekuwa na shida alijaribu mara nyingi sana kutaka ruhusa ya kuingia katika kasri ya Kiongozi Haaruwn Ar-Rashiyd apate kumuelezea shida zake, lakini walinzi hawakumruhusu kuingia, na siku moja akabahatika kumuona Haaruwna Ar-Rashiyd akitoka akiwa juu ya farasi, akamsogelea na kumwambia:

 

"Muogope Allaah ee Haaruwn Ar-Rashiyd!"

 

Kusikia maneno hayo Haaruwn Ar-Rashiyd akateremka moja kwa moja kutoka juu ya farasi wake na kusujudu, kisha akaamrisha mwanamke huyo akidhiwe haja zake zote.

 

Watu wakamuuliza:

 

"Ee Amiri wa Waislamu, umeteremka kutoka juu ya farasi wako kwa ajili ya maneno ya mwanamke wa kiyahudi?"

 

Haaruwn akasema:

 

"Sivyo, bali nimeteremka nilipoikumbuka kauli ya Allaah isemayo: {{Na wanapoambiwa: "Mcheni Allaah," mori wao huwapeleka zaidi kwenda kufanya madhambi hayo. Basi Jahannam inawatosha (kuwatia adabu). Napo ni mahali pabaya kabisa pa kutengenezewa kiumbe.}} [Al-Baqarah: 206]

 

Imepokelewa kuwa siku moja Ibn Sammaak alipokuwa akimimina maji katika gilasi ya Haaruwn Ar-Rashiyd akamuuliza:

 

"Ee Kiongozi wa Waislamu! Iwapo duniani hapana maji mengine isipokuwa haya utakuwa tayari kuyanunua kwa kiasi gani?"

 

Haaruwn Ar-Rashiyd akasema: "Nusu ya mali yangu yote."

 

Akamwambia: "Kunywa Allaah akubariki nayo."

 

Na alipomaliza kunywa akamuuliza: "Ikiwa maji haya uliyokunywa yatazuilikia tumboni mwako yasiweze kutoka utakuwa tayari kutoa kiasi gani ili yatolewe?"

 

Akasema: "Ufalme wangu wote."

 

Akamwambia: "Ufalme thamani yake maji na mkojo sina haja nao."

 

Haaruwn Ar-Rashiyd akalia sana.

 

Anasema Ibn Al-Jawziy:

 

"Siku moja Haaruwn Ar-Rashiyd alimwambia Shaybaan: 'Niwaidhi.' Shaybaan akamwambia:

 

'Upate sahibu mwenye kukutisha ukasalimika ni bora kuliko kuwa na sahibu mwenye kukusifia akakutia mashakani.'

 

Haaruwn Ar-Rashiyd akamwambia: "Nishereheshee."

 

Akamwambia: "Mwenye kukuambiwa: Wewe ndiye mbebaji jukumu la raia hawa kwa hivyo muogope Allaah ni bora kwako kuliko mwenye kukuambia: Nyinyi watu wa Ahlul-Bayt mmekwisha samehewa madhambi yenu na kwamba nyinyi ndiyo wenye haki ya kutawala."

 

Haaruwn akalia kwa furaha.

 

Rudi Juu

 

Misimamo Isiyosahaulika

 

Katika mwaka wa mia na themanini na saba (187) ilimfikia Haaruwn Ar-Rashiyd barua kutoka kwa mfalme wa wa Roma Naghfur ikivunja mkataba na ahadi waliyokubaliana baina ya Haaruwn Ar-Rashiyd na mfalme wa Roma mwanamke aitwae Rene aliyetawala kabla yake.

 

Barua hiyo iliandikwa ifuatavyo:

 

"Kutoka kwa Naghfur mfalme wa Roma kumfikia Haaruwn Ar-Rashiyd mfalme wa Waarabu. Amma ba’ad, kwa hakika mfalme aliyetawala kabla yangu alikuwa akikupa wewe mali nyingi na akijipa nafsi yake starehe nyingi, kama unavyojua udhaifu wa wanawake na ujinga wao, basi ukishaisoma barua yangu rudisha mali yote aliyokuletea, ama sivyo basi kitakachohukumu baina yetu ni panga."

 

Uso wa Haaruwn Ar-Rashiyd ulibadilika kwa ghadhabu baada ya kuisoma barua hiyo hata waliokuwa pamoja naye katika majlis ile walianza kutawanyika kwa hofu, baada ya kumuona Haaruwn Ar-Rashiyd akiinuka, na kumwita waziri wake huku akimuambia:

 

"Lete kidawati cha uwino na kalamu kisha andika yafuatayo:

 

"Bismillahir Rahmaanir Rahiym, kutoka kwa Haaruwn Ar-Rashiyd Kiongozi wa Waislamu, imfikie Naghfur Mbwa wa Roma! Nimeisoma barua yako ewe mwana wa kikafiri na jawabu utaiona na wala hutoisikia."

 

Haaruwn Ar-Rashiyd akatayarisha jeshi kubwa na kuondoka nalo mpaka alipoufikia mji wa Heracles na kuuteka, kisha akamlazimisha Naghfur atie sahihi ya kulipa fidia kila mwaka.

 

Imepokelewa kutoka kwa As-Sauly kutoka kwa Ya’quwb bin Ja’afar kuwa katika mwaka aliotawazwa Haaruwn Ar-Rashiyd alimuota Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akimwambia:

 

"Mambo yatakuendea vizuri, kwa hivyo teka miji, nenda kahiji na uwagawie mali watu wa Makkah na Madiynah.”

 

Haaruwn Ar-Rashiyd akafanya kama alivyoambiwa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), akaifunga safari katika mwezi wa Sha’abaan mwaka wa mwanzo wa uongozi wake, akateka miji mingi ya Roma kisha akaelekea moja kwa moja mpaka Makkah kwa ajili ya kuhiji, kisha akaenda Madiynah, na kote huko aligawa mali nyingi sana kwa wote wanaostahiki

 

Rudi Juu

 

Misimamo Yake Alipokuwa Kiongozi

 

Amehiji mara nyingi na ameteka miji mingi ya makafiri.

 

Anasema Al Masuudiy katika kitabu chake 'Muruuj Adh-Dhahb':

 

"Haaruwn Ar-Rashiyd alikuwa na nia ya kuendelea kuteka na kuifanya dola ya Kiislamu kuwa kubwa kuanzia bahari ya Roma hadi bahari ya Qalzam."

 

Katika mwaka wa 175 Hijri alimchaguwa Al-Ghatrif bin ‘Atwaa kuwa gavana wa Khurasan na akamchaguwa Ja’afar Barmaki kuwa gavana wa Misri, na katika mwaka huo vilishtadi vita baina ya makabila ya Al-Qisiya na Al-Yamaniyah katika nchi ya Shaam na chuki baina yao iliongezeka.

 

Majeshi ya Haaruwn Ar-Rashiyd yakiongozwa na Yahya Al-Barmaki yalifanikiwa kuiteka miji ya Qazwin na miji iliyo karibu na nchi ya Urusi.

 

Katika Ramadhaan ya mwaka 179 Hijri, Haaruwn Ar-Rashiyd alifanya ‘Umrah na akabaki Makkah mpaka musimu wa Hijjah, akahiji akitembea kwa miguu kutoka Makkah mpaka ‘Arafah na Muzdalifah na Minaa n.k.

 

Kutoka hapo akaingia vitani tena na kufanikiwa kuiteka miji mingine ya Roma, akauteka mji wa Safsaf na Ankara, kisha mwaka uliofuata akahiji tena akifuatana na wanawe wawili Al Amin na Al Maaamun, na baada ya hapo Ja’afar Al-Barmaki pamoja baba yake wakafanya khiana juu ya kuwa Haaruwna Ar-Rashiyd aliwaokowa walipotaka kuuliwa kisha akawapa vyeo vikubwa katika uongozi wake, akahukumu Ja’afar auliwe na baba yake atiwe jela.

 

Na katika mwaka huo huo majeshi ya Haaruwn Ar-Rashiyd chini ya uongozi wa ‘Abdur-Rahmaan bin ‘Abdil-Malik bin Swaalih Al-‘Abbaas yaliuteka mji wa Dibsah.

 

Na katika Ramadhaan ya mwaka 179 Haaruwn Ar-Rashiyd alifanya tena ‘Umrah na akabaki na nguo zake za Ihraam mpaka ulipoingia msimu wa Hijjah, akahiji tena kwa miguu yake kutoka Makkah hadi ‘Arafah na kurudi tena Makkah.

 

Rudi Juu

 

Kifo Chake

 

Haaruwn Ar-Rashiyd alifariki dunia akiwa vitani katika mji wa At-Tuss uliopo Khurasaan siku ya tarehe tatu mwezi wa Jumaadal Aakhirah mwaka wa 193 Hijri akiwa na umri wa miaka 45, na zipo riwaya zinazosema kuwa alikuwa na umri wa miaka 48, akazikwa huko na kuswaliwa na mwanawe Swaalih.