HASADA NA MADHARA YAKE

Na Ali Said Arafa

       Katika makala hii tumeonelea tuelezane kwa mukhtasari ubaya wa hasada na madhara yake na zaidi kwa kuwa karibuni hivi tumetoka katika mwezi mtukufu wa Ramadhan ambao tulijituma kwa ibada mbali mbali na pia hivi sasa tumo katika miezi mitukufu ambapo pia tunatakiwa tuwe na hima ya kutenda amali mbali mbali wanavyuoni wametwambia: “Bora ya mawaidha ni yale yenye kumpelekea mja kumcha Mungu na bora ya elimu ni ile yenye kumpelekea awe mnyenyekevu na mzuri wa tabia”.

        Masikitiko makubwa katika nyoyo za watu wengi wanapofikiwa na mwezi wa Ramadhan huwa na hima ya kujitakasa na maasi mbali mbali ya nyoyo n.k. lakini baada ya kumalizika tu mwezi wa Ramadhan masikini tunatekwa na Bilisi pamoja na nyoyo zetu kwa kutenda maasi mbali mbali na hapana dhambi ambayo Bilisi ameipandisha katika nyoyo za watu wengi na wa matabaka mbali mbali kama hasada, gonjwa hili la hasada limewasibu vijana wadogo baina yao, watu wazima, masikini na matajiri, wasio kuwa na elimu na hata hao wenye elimu nao ndio zaidi.

       Mtume (S.A.W) amesema katika hadithi aliyosimulia sahaba Bwana Abi Malik (R.A) ambayo imepokewa na Imam Muslim “Twahara ni nusu ya imani…” wanavyuoni wenye elimu za batini wemefasiri kuwa twahara iliyokusudiwa hapo ni mtu ajisafishe na maradhi ya nyoyo nayo ni hasada, kibri, choyo, bughudha, jeuri n.k akishajisafisha na magonjwa hayo hapo ndio mja huyo atakuwa na nusu ya imani.

       Wamesema baadhi ya watu wenye hikima kuwa “Madhambi makubwa yenye kumuangamiza mja mwenyewe ni matatu hasada, kibri na pupa” ubaya na uzito wa dhambi hii ya hasada ni kuwa mtu mwenyenayo anakuwa anaingilia utawala wa Mwenyezi Mungu (S.W) pasina mwenyewe mtu huyo kujijuwa na kujitambua, kwa vile tu kuchukiwa kwake mja huyo, kubughudhi na kuhoji kwa nini Fulani karuzukiwa hivi na miongoni mwa sifa za Mola wetu (S.W) ni kuwa yeye hakuna wa kumuhoji na kumtia ila kama alivyotwambia katika aya ya 16 ya Suratul-Buruji: “Yeye Mwenyezi Mungu (S.W) ni mwingi wa kutenda alipendalo na wala hakuna wa kumuhoji kwa hali zote”.

Maadui wa neema za Mwenyezi Mungu (S.W).

      Kila mtu mwenye hasada anahisabika mbele ya Mwenyezi Mungu (S.W) kuwa ni adui wa neema zake kwa waja wake na haya ameyesema Mtume (S.A.W): “Hakika ya neema za Mwenyezi Mungu (S.W) zina maadui” Masahaba walimuuliza “Nani hao maadui wa Mwenyezi Mungu (S.W)” Mtume (S.A.W) aliwajibu: “Hao ni wale ambao wanawahusudu watu katika neema walizoruzukiwa na Mwenyezi Mungu (S.W)”.               Ukirejea katika historia za Mitume mbali mbali na wafuasi wao, historia za wanasiasa mbali mbali na wananchi, tofauti na mabara mbali mbali utaona athari za hasada ziliziathiri Qaumu zote hizo, mayahudi (L.A) walikataa kumuamini na kumfata Mtume (S.A.W) si kwa lolote ila ni kwa sababu ya husda yao tu juu ya Mtume (S.A.W) na haya ameyasimulia Mwenyezi Mungu (S.W) katika Qur-a! n aya ya 53-54 ya Suratu-Nnisai:        “Au wanayo sehemu ya ufalme wa (Mwenyezi Mungu (S.W), basi wanahamaki kwa nini kupewa mtu kitu pasina amri yao?”. Basi hapo wasingaliwapa watu hata kokwa ya tende. Au wanawafanyia watu hasada kwa yale aliyowapa Mwenyezi Mungu (S.W) kwa ukarimu wake? Basi tuliwapa (vile na vile) watoto wa (Sayyidna) Ibrahim kitabu na hikima na tukawapa ufalme mkubwa”.

Ubaya wa hasada katika Jamii

      Hasada inapotawala katika jamii yoyote kwanza jamii hiyo itambue kuwa ishafikiwa na msiba mkubwa sana usiokuwa na mithali na athari za jamii hiyo itasibiwa na matatizo, ya majanga yakiwemo watu, hawatopendana, hawatosaidiana, hawatoheshimiana, hawatokuwa na maendeleo yoyote tokea mtu mmoja  mmoja hadi jamii yao nzima na maisha yao watakuwa madhalili na mafukara na mwisho jamii hiyo ima iwe katika kiambo chao, kijiji chao au nchi yao itakuja kutawaliwa na kuongozwa na wageni ambao hawana hata tone la ikhlsai na wao katika nyanja zote wao na vizazi vyao.

      Mtume (S.A.W) kwa kuielewa uzito na madhara ya gonjwa hili la hasada katika jamii na inavyofarikisha umoja na kufuta mapenzi katika nyoyo za waja, na kila saa akisema “Siye katika miongoni mwangu (mtu yeyote) mwenye hasada, msengenyi na yeyote wa watu wenye sifa hizo” baada ya kusema maneno hayo alisema aya ya 58 ya Suratul-Ahzab: “Na wale wanaowaudhi wanaume waislam na wanawake waislam pasipo wao kufanya kosa lolote, bila shaka (watu hao wanye kuwaudhi) wamebeba dhulma kubwa na dhambi zilizo dhahiri”.

       Maovu ya hasada yakishakushamiri katika jamii yoyote athari yake ya mwisho inaua na kukata udugu wa damu na wa nasaba na hii ndiyo hali katika ulimwengu wa leo iliyozifika familia za kiislam, watu wamekatanakatana, mtoto hamjui mjomba wala shangazi, maami nao hali kadhalika sasa mapenzi, mahaba na huruma yatapatikana vipi ikiwa jamii yenyewe imesibiwa na hali hii?

        Mtume (S.A.W) amesema: “Hawatoacha watu kuwa katika kheri (na furaha za maisha) muda wa kwamba hawakuhusudiana” kama wakihusudina basi ndio wakuwa washajifisidi katika maisha yao wao na vizazi vyao na jamii yao nzima.

Madhara na maafa yatakayomfika mtu mwenye hasada duniani na akhera.

        Kwa hakika mtu mwenye hasada atafikiwa na mambo mengi ambayo yatamfikisha na kumdumisha katika maisha yake na wala hatofikia daraja ya kuwa mwema na wala hatokuwa ni mwenye kutunukiwa za kheri na Mwenyezi Mungu (S.W) na yatosha maneno aliyosema Mtume (S.A.W): “Nakutahadharisheni na hasada, hakika hasada inakula mema ya mtu kama moto uanavyokula kuni” hiyo ni alama yenye  kutujulisha kuwa mtu mwenye hasada hafikili katika utukufu na daraja za juu iwe duniani au Akhera.   Sayyidha Luqmanul-Hikma (R.A) katika miongoni mwa wasia aliomuusia mwanawe kama alivyotwambia Mwenyezi Mungu (S.W) katika Qur-an katika sura ya Luqman aya ya 18 alimwambia hivi “Wala usiwatazame (usiwafanyie watu jeuri) kwa upande mmoja wa uso wala usende katika ndhi kwa maringo, hakika Mwenyezi Mungu (S.W) hampendi kila ajivunae na ajifakharishaye”.

       Mmoja wa wanavyuoni ameilezea hasada kuwa mtu mwenye kuwa nayo atafikiwa na mambo manane: atafisidika katika umri wake wote, atakuwa na tabia mbaya na chafu zisizo na mfano, atakosa shifaa ya Mtume (S.A.W), ataingia motoni, atapatwa na joto la moyo(presha) na atakufa kiroho, atakuwa kipofu wa moyo hafahamu chochote katika hukumu za Mwenyezi Mungu (S.W), atanyimwa tunuku na neema mbali mbali na Mwenyezi Mungu (S.W) na wala hatofikia katika mustakbali mwema katika maisha yake, hatotajwa kwa wema baada ya kufa kwake.

Kujilinda na hasada.

       Ili mtu asifikwe na gonjwa la hasada itampasa ajilee katika mwenendo mwema, kwa kusoma elimu njema na pia asuluhiane katika maisha yake na watu walio wema na shifa kubwa ya kuepukana  na gonjwa hilo ni wajibu awe anaizingaita sana ile hadithi ya Mtume (S.A.W). Aliposema: “Unapoangalia neema za Mwenyezi Mungu (S.W) basi watizame alio chini yako…” yaani usiwatizame watu waliokupita kwa uwezo wa maisha n.k, bali unavyotakiwa uwatizame wale walio chini yako uliowapita pengine wewe una Baskeli, laikini wangapi leo hawaimiliki, pengine wewe una saa ya morio ambayo wewe unaiona si nzuri na si ya kisasa lakini kumbuka kuna wangapi wanatamani sa! a hiyo hiyo uliyokuwa nayo wewe lakini hawaimiliki hawana uwezo wa kuinunua na wangapi Mwenyezi Mungu (S.W) amewatunuku uwezo mkubwa wa maisha na wana uwezo wa kununua saa za bei ghali lakini masikini hawana mkono wa kuvalia saa.

     Kwa hiyo ni neema kubwa sana mja kushukuru na kujikinai kwa kile alichotunukiwa na Mwenyezi Mungu (S.W).

      Wasia mwengine ni mtu awe na dhana nzuri na wenziwe, akimuona mwenzake maisha mazuri basi asijenge dhana kuwa ni mustahiki wa kuwa hivyo, au pia akisikia mwenziwe kateuliwa cheo fulani pia ajenge dhana njema kuwa imemstahiki fulani kupata cheo hicho n.k, yaani mtu ajitahidi lisimtawale tamko la kwa nini fulani kupata hivi na hivi katika maisha yake, ataangamia asifanye maskhara.

Nani hasa gonjwa hili la hasada limewakabili?

        Gonjwa la hasada limewasibu watu wote ila hasa lilowakabili na saa yoyote linaweza kuwadhuru kwa upesi sana ni wanavyuoni pamoja na kuwa wao ni wajuzi sana na haya ameyathibitisha Mwenyezi Mungu (S.W) tokea katika Zaburi ya Sayyidna Daud (A.S) na pia Mtume (S.A.W) ametwambia katika hadithi mbali mbali, hasa katika ile hadithi iliyotaja aina sita za watu na sababu za wao kuingizwa motoni: “Aina sita za watu wataingizwa motoni kabla ya hisabu” masahaba walimuuliza : “Nani hao ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu (S.W)” Mtume (S.A.W) aliwajibu: “…Wanavyuoni wataingia motoni kwa sababu ya hasadi”. Ama katika kitabu cha Mawaidhaul-baligha, Mwenyezi Mungu (S.W) amesema “Ewe mtoto wa adamu inapokuwa vingozi wataingia motoni kwa sababu ya jeuri, na watu wanaokaa nje ya mji (ndani mashamba huko) wataingia motoni kwa maasi, na wanavyuoni kwa hasada, na wafanya biash! ara kwa khiyana, na wapiganaji kwa ujinga, na mafundi kwa ghushi, n a wafanya ibada kwa riya, na matajiri kwa kibri na amafukara kwa kusema uongo, basi nani ataipata pepo (yangu) na wala hamuingii peponi ila isipokuwa kwa rehma zangu”.

       Hapa tuanpata faida kuwa Iblisi kila kundi la waja amewauzia bidhaa zake za uovu sasa cha kufanya ni kuwa kila mtu ajitahidi awe kila saa anausafisha moyo wake ili hili gonjwa la hasada pamoja na maradhi mengine yote ya moyo yamuepuke Inshaallah kwa rehma za Mwenyezi Mungu (s.W) na kwa jaha ya Mtume (S.A.W).

Maneno waliyoyasema baadhi ya MaBwana wema kuhusu hasada akiwemo Bwana wetu, shifaa wa nyoyo zetu na Mtume wetu Sayyidna Muhammad (S.A.W) ili iwe ni ibra na mazingatio kwa kila msomaji wa makala hii:

Mtume (S.A.W) amesema: “Haikusanyiki katika moyo wa muislam imani na hasada”

        Imam Sayyidna Hasan bin Al bin Abitalib (R.A) amesema: “Maangamizi ya watu yapo katika vitu vitatu; kibri, pupa na hasada, kibir ndio maangamizi ya dini na kwa hili amelaaniwa Iblisi (L.A), pupa ni adui wa roho na kwa hili alitolewa Sayyidina Adam (A.S) peponi na hasada ndio kiongozi wa maovu yote na kwa hili Kaabil alimuuwa Habil”.

         Imam Sufyan bin Uyayna (R.A) amesema: “Usiwe hasidi utapata baraka na furaha ya maisha na utakuwa mwepesi wa kufahamu elimu mbali mbali na mambo tofauti”.

         Imam Shafi (R.A) amesema: “Watu wote nilioishi nao nimewafurahisha ila mahasidi zangu sijui niwafanyie nini ili niwafurahishe”.

Sayyid Abdulwarith (R.A) kila saa akitawambia: “Hasidi hafuzu”.

        Maalim Shaaban Robert, mwanawe mwanamke na kuolewa alimtungia utenzi wa kumuawidh kuhusu maisha na jinsi ya kujiepusha na maradhi ya moyo ili awe nuru kwa watu, kwa wakwe zake, kwa watoto wake na kwa jamii nzima katika baadhi ya beti alimuusia kwa kumumbia hivi:

Majivuno hayafai

Yanaleta uadui

Japo mtu humjui

Kumdunisha hatia

Usishiriki uongo

Ijara upate hongo

Mtu muongo msungo

Masuto mengi hupewa

Masuto si mazuri

Yanapunguza kadiri

Jitihada kujibariki

Mbali na madoa.

        Inshaallah Mwenyezi Mungu (S.W) atuwafikishe tuwe na akhlaqi na atutunuku ilhamu ya kujitengeneza nyoyo zetu ili tufikilie katika ukamilifu wa tabia njema kwa jaha ya Mtume (S.A.W) Amin.