Maneno ya Hekima

 

Mwenyezi Mungu asipoombwa hughadhibika

Mwanadamu anapoombwa hukasirika

Wacha kumuomba mwenye kusikitika

Umuombe yule ambaye milango Yake iwazi wala haitofungika

Ali bin Abu Talib (RA)

 

 

Amali bora kupita zote ni Sala kwa wakati wake

Hadithi ya Mtume (SAW)

 

 

 "Nilipotambua kuwa amali zangu hawezi kunifanyia mwengine, nikapania kuzifanya mwenyewe.

    Na nilipotambua kuwa riziki yangu hawezi kuichukuwa mwengine, moyo wangu ukapata utulivu.

    Na nilipotambua kuwa Mola wangu ananiona, nikaona haya asinione nikimuasi".

Al Hassan al Basry

 

 

NAMNA YA KUHUKUMU BAINA YA WATU

Omar (RA) alimuandikia Abi Musa Al Ash ary (RA) yafutayo akimfundisha hekima za kuhukumu baina ya watu kwa uadilifu;

“Kutoka kwa Mja wa Mwenyezi Mungu Amiri wa Waislamu kwa Abdullahi bin Qays; kwa hakika kuhukumu baina ya watu ni fardhi iliyo wazi na mwenendo unaowajibika kufuatwa. Fahamu pale unapotolewa ushahidi na uamue unapokubainikia ukweli, kwani haki bila ya kuamuliwa haina faida. Wapoze watu katika majlis yako, ….Mwenye kudai anawajibika kutoa ushahidi, na mwenye kukanusha wajibu wake kula kiapo.

Suluhu ni bora baina ya Waislamu, lakini isiwe suluhu inayohalalisha haramu na kuharamisha halali.

Usije ukakuzuwia uamuzi ulouamuwa jana, kisha Mwenyezi Mungu akakuongoza ukatambua kuwa ulikosea katika uamuzi ule, ukakufanya uogope kuiweka sawa haki, kwani haki ni haki na haibatilishwi na chochote. Na kuirudisha haki kwa wenyewe ni bora kwako kuliko kuendelea kuinyamazia batili.

Ushahidi wa Waislamu baina yao ni haki, isipokuwa yule aliyewahi kuhukumiwa kupigwa mjeledi kwa kosa kubwa au aliyewahi kutoa ushahidi wa uwongo au anayetiliwa shaka kwa sababu ya kumpendelea mshitaki au mshitakiwa kwa ajili ya undugu wa nasaba, (hawa ushahidi wao haukubaliwi), na Mwenyezi Mungu ndiye ajuwae siri za moyoni.

Usiwatishe watu au kuingiza uwoga nyoyoni mwao, kwani yule anayeihusisha nia kwa ajili ya kumridhisha Mwenyezi Mungu basi Mwenyezi Mungu anamtosheleza. Ama mwenye kuamua kinyume na haki kwa ajili ya kutaka kujipendekeza kwa watu, MwenyeziMungu humuacha alivyo, na iko siku atamfedhehesha. Unaonaje mtu akizikimbilia thawabu za Mola wake na Rehema Zake?

Wassalaam”.

Omar bin Khattab (RA)

 

Luqman mwenye Hekima

Siku moja mfalme wa Luqman mwenye hekima "Luqman al Hakiym" alichinja mbuzi wawili na kumtaka Luqman achaguwe kutoka katika mbuzi wawili hao vipande viwili vibaya kupita vyote na viwili vingine vizuri kupita vyote

Luqman akachagua moyo na ulimi kutoka katika kila mbuzi. (yaani alitoa kutoka katika mbuzi wa kwanza moyo na ulimi, na kutoka katika mbuzi wa pili akatoa pia moyo na ulimi).

Mfamle akamuuliza;

"Nilikwambia uchague kutoka KILA mbuzi sehemu mbili, mbona umechagua mbili hizi tu (Moyo na ulimi)?"

Akajibu;

"Hakuna vibaya kuliko hivi vikiharibika na hakuna vizuri kuliko hivi ikitengenea".

 

FUNGUO ZA KHERI

Kheri yote inapatikana pale Mwenyezi Mungu anaporidhika na mja wake, na funguo za kheri zimo katika Dua pamoja na unyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu na kuonesha kumpenda kwa kutenda yale yanayomridhisha na pia kumuogopa kwa kuepukana na makatazo yake.

Mja anapokabidhiwa na Mola wake funguo hizi basi ajue kuwa Mola wake anamtakia kheri, na anaponyimwa basi ajue kuwa amefungiwa milango ya kheri.”

Omar bin Khatab(RA) anasema;

“Mimi sijishughulishi na majibu ya dua yangu, bali najishughulisha na kuomba Dua, wakati wowote Mola wangu anaponikabidhi funguo za dua, basi huwa na uhakika kuwa majibu yake yatakuja tu”