Kufaridhishiwa kwake

Amma baad,

Mwenyezi Mungu anasema:

"Na Mwenyezi Mungu amewawajibishia watu wafanye Hija katika Nyumba hiyo; yule awezaye kufunga safari kwenda huko. Na atakayekanusha (asende na hali anaweza) basi Mwenyezi Mungu si mhitaji kuwahitajia walimwengu ."

Aali Imran - 97

 

Maulamaa wote wamekubaliana kuwa Hija ni moja katika nguzo tano za Kiislamu, na ni fardhi ijulikanayo kuwa ni ya lazima. Atakayeikanusha anakuwa kafiri aliyertadi na kutoka katika dini ya Kiislamu.

Wanavyuoni wengi wanasema kuwa ibada ya Hija imefaradhishwa katika mwaka wa sita baada ya Hijra, (baada Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam)  kuhamia Madina.

Mwanachuoni maarufu Ibnul Qayyim katika kitabu chake kiitwacho Zaadul Ma-ad, amesema kuwa Hija imefaridhishwa mwaka wa tisa, pale ilipoteremshwa aya isemayo:

"Na timizeni Hija na Umra kwa ajili ya MwenyeziMungu".

Al Baqarah - 196

 

Amali bora

Amesimulia Abu Huraira (Radhiya Llahu anhu) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) aliulizwa:

"Amali ipi iliyo bora?"

Akasema:

"Imani juu ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake."

'Kisha ipi?'

Akasema:

"Kisha Jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu".

"Kisha ipi?"

Akasema:

"Kisha Hija iliyokubaliwa".

 

Anasema Al Sayed Sabiq, mwandishi wa kitabu ‘Fiq-hil Sunnah’;

"Hija iliyokubaliwa ni ile isiyochanganyika na maovu" .

 

Al Hassan Al Basry anasema:

"Hija iliyokubaliwa ni pale anaporudi aliyehiji akiwa anaipenda akhera yake kuliko dunia yake".

 

Wajumbe wa Mwenyezi Mungu

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) amesema:

"Mahujaji na wenye kufanya Umra ni wageni wa Mwenyezi Mungu. Wakimuomba anawapa na wakimuomba maghufira anawaghufiria".

Annasai, Ibni Majah, Ibni Khuzaymah na Ibni Haban.

 

Kila mwenye kuifunga safari ya kwenda kuhiji akumbuke kuwa tokea pale alipoamua, alikwisha ingia katika kundi la wale waliochaguliwa na Mwenyezi Mungu kuwa mgeni wake katika sehemu hizo tukufu ndani ya siku hizo tukufu.

Kwa ajili hiyo anayehiji anatakiwa ajitahidi awe mwenye kustahiki kuwa mjumbe na mgeni wa Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala. Na anapokuwa katika Ibada hiyo tukufu asigombane wala kuzozana na Mahujaji wenzake, kwa sababu zimepokelewa hadithi nyingi zenye kutujulisha kuwa atakayehiji bila kufanya maovu wala kujadiliana (katika mambo ya kipuuzi na ya kidunia) wala kuzozana, hapana zawadi anayoistahiki isipokuwa Pepo.

 

Inawajibika hapo hapo

Maimamu Abu Hanifa na Malik na Ahmad bin Hanbal na baadhi ya wanafunzi wa Imam Shafi wanasema:

"Hija inamwajibika mtu pale anapokuwa na uwezo. Kwa sababu Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) amesema:

"Anayetaka kuhiji basi aharakishe, kwa sababu huenda akaumwa, au mnyama wake akazeeka au akapatwa na shida.(akazitumia pesa zake)."

Na katika hadithi nyengine:

"Fanyeni haraka mkahiji, maana hajui mmoja wenu atapambana na nini" (Maradhi au shida nk.).

Ahmed, Al Bayhaqi, Al Tahawiy na Ibni Majah.

 

Mali ya kukopa

Kutoka kwa Abdullah bin Abu Aouf (Radhiya Llahu anhu) amesema:

“Nilimuuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) juu ya mtu asiyewahi kuhiji iwapo anaweza kukopa kwa ajili ya kuhiji?”

Akaniambia:

“Hapana, (asifanye hivyo)”.

Al Baihaqiy

 Mali ya haramu

Imepokelewa kutoka kwa Al Tabarani kuwa Abu Huraira (Radhiya Llahu anhu) amesema; kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) amesema:

"Anapotoka anayehiji kwa pesa njema akauweka mguu wake juu ya kipandio cha mnyama wake, akasema: "Labbayka llahumma labbayk", hujibiwa na msemaji kutoka mbinguni, "Labbayka wa Saadayka, mzigo wako (chakula na vifaa vyako) ni vya halali na mnyama wako wa halali na hija yako inakubaliwa na haina madhambi".

Lakini anapotoka anayeihiji kwa pesa za haramu akauweka mguu wake juu ya kipandio cha mnyama wake na kusema: "Labbayka llahumma labbayk", hujibiwa kutoka mbinguni, "(Laa labbayaka walaa saadayaka) Hakukubaliwi kuitikia kwako wala hutolipwa mema, kwa sababu vifaa vyako ni vya haramu na pesa zako za haramu na hija yako ni ya dhambi na wala haikubaliwi".