Hija ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam)

(Kama ilivyohadithiwa na Jabir bin Abdillah (Radhiya Llahu anhu)

 

Muhammad Faraj Salem Al saiy

 

Anasema Imam Muslim:

"Nimehadithiwa na Abubakar bin Abi Shaibah na Ishaq bin Ibrahim, wote pamoja. Na kutoka kwa Hatim amesema kuwa Abubakar amesema;

'Nimehadithiwa na Hatim bin Ismail Al Madani, kutoka kwa Jaafar bin Muhammad, kutoka kwa baba yake (Radhiya Llahu anhum) kuwa alisema:

"Tulimwendea Jabir bin Abdillah (Radhiya Llahu anhu), akaanza kutuuliza majina yetu mmoja mmoja mpaka akaishia kwangu. Nikamwambia:

'Mimi ni Muhammad bin Aliy bin Hussain". Akakivamia kichwa changu, kisha akanifungua kifungo changu cha juu kisha cha chini yake, kisha akauweka mkono wake kifuani pangu, na wakati huo nilikuwa bado kijana. Akaniambia;

"Marhaban (karibu) ewe mwana wa ndugu yangu. Uliza unalotaka kuuliza".

Nikamuuliza, na wakati ule alikuwa kipofu, na wakati wa Swala ulipowadia aliinuka huku akiikusanyakusanya nguo yake, kila akijifunika nayo upande mmoja wa bega lake, upande wa pili inaanguka kwa sababu ya udogo wake.

Akatuswalisha, kisha nikamwambia:

"Tuhadithie juu ya Hija ya Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam)".

Jabir (Radhiya Llahu anhu) akasema:

"Watu walipoarifiwa kuwa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) atahiji mwaka huu, walianza kumiminka mjini Madina kwa wingi sana, kila mmoja akitamani aongozwe na Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) na afanye kama atakavyofanya.

(Ilipowadia siku ya safari) Tukaondoka naye mpaka tulipowasili Dhul Hulaifa (Abaar Ali - mikati ya watu wa Madina), Asmaa binti Umays akamzaa Muhammed bin Abubakar Al Siddique (Radhiya Llahu anhu), akamtuma mtu kwa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kumuuliza nini afanye. Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akamwambia:

"Oga, kisha weka kitambaa na utie nia ya Ihram (nia ya kuhiji)".

Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akaswali msikitini kisha akampanda ngamia wake anayejulikana kwa jina la Al Qaswaa, na alipokuwa katikati ya jangwa nikainua kichwa changu kutizama waliokuwa mbele ya Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam), nikaona watu wengi sana, upeo wa macho yangu wakiwemo waliopanda wanyama na wanaokwenda kwa miguu, kisha nikatizama kuliani kwake, nikaona hivyo hivyo, kisha upande wake wa kushoto nikaona hivyo hivyo, na nyuma yake hivyo hivyo, na Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akiwa pamoja nasi huku wahyi ukimteremkia, huku akituhadithia, na kila anachokifanya, sisi tulikuwa tukimfuata.

Kisha akaanza kusema;

"Labbayka llahumma labbayka, labbayka laa shariyka laka labbayka. Innal hamda wa neamata laka wal mulk, laa shariyka laka".

Na watu wakawa wanasema kama anavyosema".

 

Jabir bin Abdillah (Radhiya Llahu anhu) akaendelea kusema:

"Hatukuwa tukitia nia nyingine isipokuwa nia ya Hija, (hatukuwa tukijuwa aina nyingine za Hija), hatukuwa tukijuwa juu ya Umra. Tukaendelea na safari mpaka tulipoifikia Al Kaaba tukiwa pamoja naye, akaligusa jiwe jeusi kisha akaanza kutufu. Katika mizunguko mitatu ya mwanzo alikuwa akenda kwa kukazana, na katika minne iliyobaki akenda mwendo wa kawaida. Alipomaliza akenda penye Maqamu Ibrahim Alayhi ssalaam, akasoma:

"Wattakhidhu min maqami Ibrahima musalla"

Al Baqarah - 125

Na maana yake (Na mahali alipokuwa akisimama Ibrahim pafanyeni pawe pa kuswalia).

Akaelekea kibla na kuswali rakaa mbili mahali hapo, akasoma katika rakaa ya mwanzo (alhamdu pamoja na) Qul ya ayuha l kafirun na katika rakaa ya pili akasoma (alhamdu pamoja na) Qul huwa llahu ahad, kisha akarudi penye jiwe jeusi, akaligusa kisha akatokea mlangoni kuelekea Safa.

Alipokaribia Safa akasoma:

"Inna Safaa wal Marwata min shaairi llahi - abdau bimaa badaa llahu bihi"

Na maana yake ni:

(Hakika Safa na Marwa (Majabali mawili yanayofanyiwa ibada ya Saa'yi huko Makka) ni katika alama za kuadhimisha dini ya Mwenyezi Mungu - naanzia pale alipoanzia Mwenyezi Mungu).

Akaanzia Safa, akaupanda mlima huo mpaka alipoweza kuiona Al Kaaba akaelekea kibla akasema:

"Laa ilaha illa llahu - allahu akbar",

Kisha akasema:

"La Ilaha Illa Llahu Wahdahu Lashariyka Lahu lahul mulku walahul hamdu Wahuwa Alaa Kulli Shay-In Qadiir. La Ilaha Illa Llahu Wahdau, anjaza waadahu, wa nasara abdahu, wahazamal Ahzaaba Wahdah”.

Kisha akaomba dua, kisha akarudia kusema hivyo mara tatu, kisha akashuka kuelekea Marwa, alipofika katikati ya bonde akawa anakwenda mwendo wa kukazana, na alipolifikia jabali la Marwa akalipanda kwa mwendo wa kawaida, na alipolifika juu yake akasoma na kufanya kama alivyofanya alipokuwa juu ya Safa.

Akaendelea hivyo mpaka tawafu yake ilipomalizikia Marwa akasema:

"Lau kama amri niliyopewa (hivi sasa) ningelipewa kabla, nisingechukuwa pamoja nami mnyama na ningeijaalia (tawafu yangu na saayi yangu) kuwa Umra, na kama yupo kati yenu asiyekuwa na mnyama basi avue nguo za Ihram na aijaalie iwe Umra".

Akainuka Suraka bin Malik bin Jaathum (Radhiya Llahu anhu) akasema:

"Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, (hukmu hii) ni kwa ajili ya mwaka huu tu au milele?"

Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akaviingiza vidole vyake vya mkono wa kulia ndani ya vidole vya mkono wa kushoto na kusema:

"Umra na Hija zishaingiliana" akasema hivyo mara mbili, kisha akasema; "La bali milele".

Aliy (Radhiya Llahu anhu) akawasili kutoka nchi ya Yemen akiwa na ngamia wa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam), akamkuta Fatma (Radhiya Llahu anhu) amekwishavuwa nguo za Ihram na kuvaa nguo za kawaida za rangi rangi na ametia wanja. Akamkataza, kwa ajili hiyo, lakini Fatma (Radhiya Llahu anhu) akamwambia:

"Baba yangu ameniamrisha kufanya hivi".

Akaenda kwa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kumshtaki Fatma kwa vile alivyofanya (kuvua nguo za Ihram na kupaka wanja) na kwa kule kusema kwake kuwa Baba yake ndiye aliyemuambia, akamjulisha kuwa yeye alimkataza kwa kufanya kwake vile.

Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akamjibu:

"Ni kweli, (na) wewe umetia nia gani ya kuhiji ulipokuwa unakuja?"

Akasema:

"Nilisema; 'Allahumma mimi natia nia ile ile aliotia Mtume wako".

Akamwambia:

"Basi mimi ninaye mnyama, kwa hivyo tusivuwe (nguo za Ihram)".

Idadi ya wanyama aliokuja nao Aliy (Radhiya Llahu anhu) kutoka Yemen ikichanganywa na idadi ya wanyama aliokuja nao Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) ikafikia ngamia mia moja.

Watu wote wakavua Ihram zao na kukata nywele isipokuwa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) na wachache waliokuja na wanyama wao.

Ilipofika siku ya Tarwiya - siku ya tarehe 8 Dhul Hija, watu wakaondoka kuelekea Mina wakitia nia ya Hija, na Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akampanda mnyama wake na kuelekea huko pamoja nao. (Walipowasili Mina), wakaswali Adhuhuri, Alasiri, Magharibi, Isha na Alfajiri (Qasran, kila Sala katika wakati wake).

(Baada ya kuswali alfajiri) Akasubiri kidogo mpaka jua lilipochomoza akaamrisha lisimamishwe hema mahali paitwapo Namira, - karibu na Arafat -. Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akaondoka kuelekea Namira na akapitiliza Muzdalifa bila ya kusimama penye Mash-ari l haram, juu ya kuwa Makureshi walidhania atasimama hapo kama walivyokuwa wakifanya wakati wa Ujahilia.

Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) hakusimama mpaka alipowasili Arafat, akaliona hema lishasimamishwa pale Namira kama alivyoamrisha, akashuka na kupumzika hapo mpaka ulipoingia wakati wa adhuhuri, akaamrisha aletwe ngamia wake Al Qaswaa, akampanda na kwenda moja kwa moja mpaka alipofika katikati ya bonde la Arafat akasimama na kuwahutubia watu akasema:

"Hakika ya damu zenu na mali zenu (ni tukufu sana kwa hivyo) ni haramu baina yenu (kumwaga damu zenu na kudhulumiana baina yenu) kama ulivyokuwa utukufu wa siku yenu hii, katika mwezi wenu huu, katika mji wenu huu, visasi vyenu vyote vya wakati wa ujahilia viko chini ya mguu wangu - nishavibatilisha - na kisasi cha mwanzo cha kumwaga damu yetu ninachokibatilisha ni kisasi cha (kumwaga) damu ya Ibni Rabia bin Al Harith - alikuwa na mtoto anayenyonyeshwa katika kabila la Bani Saad,akauliwa na watu wa kabila la Hudhayl - Na riba iliyokuwa ikichukuliwa wakati wa Ujahilia ishabatilika, na riba ya mwanzo ninayoibatilisha ni riba yetu, riba ya Abbas bin Abdul Muttalib, ishabatilika yote, na muogopeni Mwenyezi Mungu katika wake zenu, kwani nyinyi mumewachukuwa kwa dhamana ya Mwenyezi Mungu, na mkahalalishiwa tupu zao kwa neno la Mwenyezi Mungu, na nyinyi mna haki zenu juu yao. Wasiwaingize nyumbani kwenu yeyote msiyempenda (awe mwanamume au mwanamke), na wakifanya hivyo, mnayo haki ya kuwapiga kipigo kisichoumiza. Na haki yao juu yenu ni kuwalisha na kuwavisha kwa wema. Na nimekuwachieni ambayo hamtopotea baada yake ikiwa mtashikamana nayo, kitabu cha Mwenyezi Mungu. Mkiulizwa juu yangu mtasema nini?"

Wakasema:

"Tutashuhudia kuwa umefikisha na umekamilisha na umenasihi".

Akanyanyua kidole cha shahada akawa mara anakielekeza mbinguni mara anakielekeza kwa watu, akasema:

"Mola wangu shuhudia - (mara tatu)".

 

Kisha akaadhini, akakimu na kuswali Swala ya adhuhuri, kisha akakimu tena na kuswali Swala ya alasiri bila kuswali Sunnah baina yao. Kisha akampanda ngamia wake na kuelekea naye moja kwa moja mpaka mahali pa kusimama (katika uwanja wa Arafat), akamuelekeza ngamia wake Al Qaswaa penye majabali na yeye akaelekea kibla.

Akasimama mahali hapo mpaka wakati wa magharibi ulipoingia na umanjano wa juwa kutoweka na juwa kuzama kabisa, ndipo alipoondoka akiwa amempakia Usama nyuma yake.

Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akampanda ngamia wake Al Qaswaa na kuianza safari ya kwenda Muzdalifa. Akawa anazikaza kamba za hatamu za ngamia wake na kumbana nazo ili asiweze kwenda mbio kwa ajili ya zahma ya watu. Akawa anaashiria watu kwa mkono wake wa kulia huku akiwaambia:

"Enyi watu! (nendeni kwa) utulivu (nendeni kwa) utulivu".

Na kila anapolifikia jabali akawa anailegeza kamba ili mnyama wake aweze kupanda kwa wepesi. Akawa anafanya hivyo mpaka alipowasili Muzdalifa, akaswali hapo Swala ya Magharibi na Isha kwa adhana moja na iqama mbili, bila ya kusabih baina ya Swala hizo.

Kisha Mtume wa Mwenyezi Mungu akapumzika mahala hapo mpaka alfajiri ilipoingia, akaswali Alfajiri pale ilipombainikia kuwa wakati wa Swala ya alfajiri ushaingia, kwa adhana na iqama.

Kisha akampanda Al Qaswaa mpaka alipowasili Mashaaril haraam - (jabali lililopo hapo hapo Muzdalifa), akaelekea kibla na kuomba dua huku akikabir na kumtukuza na kumpwekesha Mwenyezi Mungu. Akawa katika hali hiyo mpaka kulipopambazuka.

Kisha akaondoka na kuianza safari ya kuelekea Mina kabla ya jua kupanda akiwa amempakia Al Fadhal bin Abbas aliyekuwa kijana mwenye nywele nzuri, mweupe, na mwenye sura nzuri. Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alipokuwa akiondoka naye, akapita mbele yao ngamia aliyebeba wanawake wawili, na Al Fadhal akawa anawaangalia wanawake hao. Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akauweka mkono wake usoni pa Al Fadhal ili asiweze kuwatizama, lakini Al Fadhal aliugeuza uso wake upande wa pili na kuendelea kuwatizama, na Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akaukamata uso wa Al Fadhal na kuugeuza upande mwingine. Akaendelea na safari yake mpaka alipolifikia bonde la Muhsir akaongeza mwendo kidogo, kisha akapita njia ya kati inayopeleka moja kwa moja mpaka penye Jamarat kubwa (shetani mkubwa), na alipolifikia Jamarat (hilo) lililokuwa karibu na mti akalipiga kwa mawe saba huku akikabir kila anaporusha jiwe.

Kisha akaondoka kuelekea mahali pa kuchinja, akachinja (ngamia) sitini na tatu kwa mkono wake, kisha akampa Aliy achinje waliobaki, kisha akaamrisha nyama ikatwe katwe, ikatiwa ndani ya vyungu vya kupikia, ikapikwa, wakala katika nyama ile na kunywa supu yake.

Kisha Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akampanda ngamia wake na kuelekea penye Al Kaaba, akaswali adhuhuri alipowasili Makka.

Baada ya kuswali akawaendea watu wa kabila la Bani Abdul Muttalib waliokuwa na jukumu la kuwahudumia watu katika kunywa maji ya Zamzam, akawaambia:

"Wanywisheni maji enyi watu wa kabila la Bani Abdul Muttalib, ingekuwa sikuogopeeni watu kukuchukulieni kazi hii ya kunywesha maji, basi ningelikusaidieni".

Wakampa maji (ya Zamzam), akanywa.