Hijjah Ya Mwenye Deni

 

Kamati ya kudumu ya Utafiti wa Kielimu na Utoaji Fatwa imetoa fatwa kuhusiana na suala la Hijjah ya mwenye deni kwa kueleza yafuatayo:

Moja ya masharti ya Hijjah ni uwezo, na mtu kuwa na uwezo wa mali wa kuifanya Hijjah. Ikiwa mtu ana deni ambalo anadaiwa na mkopeshaji na mkopeshaji akawa hakubali yule mtu aende Hijjah bila kumlipa pesa zake, basi hatoruhusika kwenda Hijjah hadi alipe deni analodaiwa, kwani mtu huyo atahesabika si mwenye uwezo wa kwenda Hijjah. Lakini endapo mkopeshaji hatomshikilia alipe pesa zake na ima kamruhusu aende Hijjah hali ya kuwa ana deni lake, basi anaweza kwenda na Hijjah yake kwa hali hiyo itakubalika.

[Fataawa al-Lajnah ad-Daaimah 11/46]

 

Na katika Fatwa nyingine, Kamati ya Kudumu ya Fatwa walipoulizwa swali kuhusu Hijjah ya mwenye deni la nyumba ambalo muulizaji alisema anapaswa kulilipa kwa awamu, ilieleza ifuatavyo:

Uwezo wa kutekeleza Hijjah ni moja ya masharti ya kuwa kwake ni waajib. Ikiwa una uwezo wa kulilipa deni hilo kwa awamu ambayo imekutana na wakati wa Hijjah, basi unaweza kwenda baada ya kulilipa deni katika awamu hiyo. Lakini ikiwa huwezi kulipa deni hilo kwa awamu hiyo, basi ahirisha Hijjah hadi utakapopata uwezo kwani Allaah Anasema:

“Na kwa ajili ya Allaah imewajibikia watu wahiji kwenye Nyumba hiyo, kwa yule awezae njia (mwenye uwezo) ya kwendea.” [Aal ‘Imraan 3: 97]

Na at-Tawfiyq ni kutoka kwa Allaah

[Al-Lajnah ad-Daaimah lil Buhuuth al-‘Ilmiyyah wal Iftaa 11/45]

 

Naye Mwanachuoni Shaykh Muhammad bin Swaalih al-‘Uthaymiyn anasema:

Deni linalodaiwa linapaswa kutangulizwa kulipa kuliko Hijjah, kwani wajibu wa kulilipa unawekwa mbele kuliko mtu kwenda kutekeleza Hijjah. Hivyo, anapaswa mtu kulipa kwanza deni kisha ndio kwenda Hijjah. Na ikiwa hatobakiwa na chochote au kitakachobaki hakimtoshelezi gharama za kwenda Hijjah, basi atasubiri hadi Allaah Amjaalie uwezo wa kwend akuitekeleza nguzo hiyo. Lakini likiwa ni deni lenye kuwa na muda mrefu aliopewa mkopeshwa la kulilipa siku za mbele, hivyo, kwa hali hii hata kama mkopeshaji akimruhusu au asimruhusu kwenda Hijjah, hatoruhusika kwenda Hijjah ikiwa hana uhakika au dhamana ya kulilipa kwa ule muda aliopewa/waliokubaliana na mkopeshaji.

Kwa hali hiyo tunasema: Ikiwa mtu anadaiwa deni, na anafahamu kuwa ana uwezo wa kulilipa kwa muda aliopewa (hata ikiwa ni mbeleni baada ya Hijjah), basi Hijjah kwa hali hiyo inakuwa ni wajibu kwake japokuwa ana deni.

[Fataawa Ibn ‘Uthaymiyn, 21/96]