WAKATI MGUMU KATIKA HISTORIA YA KIISLAMU

 KIMEANDIKWA NA OTHMAN AL KHAMIS

KIMEFASIRIWA NA MOHAMMAD FARAJ

NAMNA YA KUIS0MA HISTORIA

Tunapoisoma historia ya kiislamu, lazima tuisome kama vile tunavyosoma vitabu vya hadithi za Mtume (SAW), kwa sababu tunaposoma hadithi za Mtume (SAW) huwa tunatafuta ukweli iwapo hadithi hizo ni sahihi au si sahihi.

Na hatuwezi kutambua ikiwa hadithi ni sahihi au si sahihi bila ya kuwajuwa wapokezi wa hadithi hiyo (narrators) pamoja na matni (maneno) yake, na hii ni kwa sababu katika elimu ya hadithi maulamaa wamechukuwa juhudi kubwa ya kuchunguza habari za wapokezi wake na wakaweza kuwajuwa yupi muongo na yupi mkweli miongoni mwao, yupi mwenye kusahau na yupi anayependa kuongeza maneno yake (kutia chumvi), kisha wakazichunguza hadithi na kuzidurusu na hatimaye wakaweza kupambanua baina ya hadithi sahihi na dhaifu pamoja na zile za uongo zilizopachikwa tu. Na kwa ajili hiyo wakaweza kuzisafisha hadithi za Mtume (SAW) kwa kuzibainisha zile za uongo zilizochomekwa na zile zilizo dhaifu.

Lakini tunaposoma vitabu vya historia (tarikh), si rahisi mtu kuweza kutambua yote hayo, na hii ni kwa sababu utakuta ndani yake maelezo mengi yaliyoandikwa bila kutajwa majina ya wapokezi (narrators), tofauti na ilivyo katika vitabu vya elimu ya hadithi. Na mara nyingi maelezo hayo yanaambatanishwa na majina ya wapokezi yasiyokuwemo na yasiyojulikana katika vitabu vya elimu ya wapokezi wa hadithi. Kwa ajili hiyo si rahisi kujuwa iwapo wapokezi hao walikuwepo kweli, na kama walikuwepo kweli si rahisi pia kujuwa juu  ya mwenendo wao kama walikuwa wakweli waaminifu au waongo wenye kupenda kuandika kila wanachosikia nk. Na kwa ajili hiyo ni vigumu sana mtu kuweza kutoa uamuzi juu ya maelezo hayo iwapo ya kweli au ya uongo.

Kwa hivyo katika kuisoma historia mambo ni magumu zaidi kuliko ilivyo katika kusoma vitabu vya elimu ya hadithi, lakini hii isitufanye kuyarahisisha mambo, bali ni wajibu wetu kuutafuta ukweli na kujuwa wapi tuitafute historia yetu.

Mtu anaweza kusema;

“Ikiwa tutavichambua vitabu vya historia na kuzitoa hadithi zisizo sahihi, basi maelezo mengi juu ya historia yetu yatapotea na kubaki machache tu”.

Lakini sisi tunamjibu kwa kumwambia kuwa; la, hayatopotea maelezo mengi, kwani yapo mengi katika maelezo ya historia yaliyoandikwa kwa isnadi zake, na hayo yamo katika vitabu vya historia mfano wa kitabu cha At Tabari na pia yamo ndani ya vitabu vya hadithi kama vile Bukhari na Musnad ya Imam Ahmed na Sunan Attirmidhiy au vitabu vilivyoandikwa na Ibni Abi Shaibah au katika vitabu vya tafsiri vinavyoandikwa ndani yake isnadi za kila riwaya kama vile tafsiri ya Ibni Jariyr na tafsiri ya Ibni Kathiyr na mara nyingine katika vitabu vinavyoandikwa juu ya matukio maalum kama vile vita vilivyotokea baada ya kufa kwa Mtume (SAW) n.k.

Na kama utashindwa kuupata ukweli, basi uamuzi utabaki pale  pale kuwa imani yetu ni kuwa haitupasi kuwatuhumu Masahaba (RA) kwani Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala amewasifia na kuwatakasa. Kwa ajili hiyo tukikutana na maelezo yoyote yale yanayowatuhumu Masahaba (RA) kwanza kabisa tunatizama isnadi ya wapokezi wa maelezo hayo (narrators), na kama isnadi ni sahihi, basi kabla ya kuwatuhumu tutizame kwanza tafsiri ya riwaya hizo na zinaleta maana gani? Ama ikiwa isnadi yake ni dhaifu, basi Alhamdulillah, na kama riwaya hiyo haina isnadi yoyote, basi tunarudi katika asili yetu nayo ni imani yetu kuwa Masahaba (RA) ni watu waadilifu kama tutakavyoona kila tukiendelea mbele namna gani Mwenyezi Mungu amewatakasa watu hawa.

Kwa hivyo tunapoisoma historia hatuna budi kuisoma kwa kuichambua vizuri kama tunavyofanya wakati tunaposoma vitabu vya elimu ya hadithi na hasa katika historia ya Masahaba wa Mtume (SAW).

 

TUSOME VITABU VILIVYOANDIKWA NA NANI?

Wengi siku hizi wanapendelea kusoma vitabu vya historia  vilivyotungwa katika zama hizi zetu, vitabu ambavyo waandishi wake wanajishughulisha na upambaji wa maelezo au kusimulia habari zinazopotosha ukweli au yote mawili mfano wa vitabu vya Abbas Al Aqaad aliyeandika juu ya Ustadi ‘Abqariyaat’, au vitabu vilivyoandikwa na Khalid Muhammed Khalid ‘Khulafaa rasuul’ na ‘Rijaal haula rasuul’ au vya Taaha Husein ‘Mawqifat al Jamal’ au vya Georgie Zeidan ‘Tarikh tamadunil Islam’ au vingine vya mfano huo. Watungaji hawa wanapoandika juu ya historia hujishughulisha na uandishi na upambaji wa visa vilivyomo ndani yake bila kujali kama visa hivyo ni sahih au si sahihi, muhimu kwao ni kukuandikia kisa kizuri kinachovutia.

Kwa hivyo suali linarudi pale pale. ‘Nisome vitabu vilivyoandikwa na mwandishi gani?’

Ikiwa unao uwezo wa kuwachambua wapokezi (narrators) na na kuwajuwa wakweli na waongo miongoni mwao, basi soma kitabu cha Imam At Tabari, kwani yeye ni bingwa miongoni mwa waandishi wa tarikh (historia), ama ikiwa huna uwezo wa kuwachambua wapokezi, basi soma kitabu cha Al Bidaya wal Nihaya kilichoandikwa na Ibni Kathir au kitabu cha Tarikh al Islam kilichoandikwa na Imam Al Dhahabi au kitabu kilichoandikwa na Abubakar bin al Arabi kiitwacho ‘Al Awasim minal Qawasim’, na hiki ni miongoni mwa vitabu vizuri sana vilivyoandika juu ya wakati huu mgumu.

 TUJITAHADHARISHE NA NINI?

Tunaposoma vitabu vya historia lazima tujitahadharishe tusije tukachukuliwa na rai ya mtungaji, kwani inatupasa tuwe waadilifu huku tukisoma, na hatuna budi kuziangalia riwaya zenyewe na si kuangalia rai ya muandishi, na hatuna budi pia kuwa na mambo mawii akili mwetu huku tukisoma vitabu vinavozungumza juu ya historia ya Masahaba wa Mtume (SAW);

La kwanza; ni kuwa na itikadi kuwa Masahaba wa Mtume (SAW) ni viumbe bora kupita wote baada ya Mitume wa Mwenyezi Mungu (SWA) na hii ni kwa sababu Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala amewasifia na Mtume (SAW) pia amewasifia na akatuabainishia katika hadithi nyingi kuwa kuwa umma ule ulikuwa ni umma bora kupita zote baada ya Mitume(SWA).

Jambo la pili; inatupasa tuelewe kuwa Mashaba wa Mtume (SAW) hawakukingwa na kufanya makosa (si Maasumin), ndiyo sisi tunaitakidi kuwa hawawezi kufanya makosa katika jambo lolote walokubaliana nalo wote kwa pamoja (Ijamai), na hii ni kwa sababu Mtume (SAW) alikwishatuambia kuwa umma huu hauwezi kukubaliana wote kwa pamoja katika jambo la upotofu (upotevu), lakini unapowachukulia kama watu binafsi, wao hawakukingwa na kufanya makosa, kwani walokingwa ni Mitume wa Mwenyezi Mungu peke yao, ama wengine wasiokuwa wao sisi hatuamini kuwa yupo yeyote aliyekingwa na kufanya makosa (asiyefanya makosa).

Kwa hivyo hatuna budi kuamini kuwa Masahaba ni umma bora kupita umma zote na hatuna budi kuamini kuwa wao wanaweza kufanya makosa.

Kwa hivyo itakapokujia riwaya (maelezo) ambayo ndani yake mna lawama juu ya Sahaba basi usikimbilie kuikataa na pia usiikubali moja kwa moja mpaka kwanza uitizame vizuri. Utakapoona kuwa isnadi ya riwaya hiyo ni sahihi basi ujuwe kuwa hii ni katika yale mambo ambayo hawakukingwa nayo, ama ikiwa isnadi ya riwaya hiyo ni dhaifu, basi unarudi katika itikadi yetu ya asili nayo ni kuwa Masahaba ni watu wema.

Ama sifa ambazo Mwenyezi Mungu amewasifia Masahaba (RA) ni katika aya ifuatayo;

“Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na walio pamoja naye ni wenye nyoyo thabiti mbele ya makafiri na wenye kuhurumiana wao kwa wao. Utawaona wakiinama kwa kurukuu na kusujudu (pamoja), wakitafuta fadhila za  Mwenyezi Mungu na radhi (Yake). Alama zao zi katika nyuso zao kwa taathira (athari) ya kusujudu. Huu ndio mfano wao katika Taurati. Na mfano wao katika Injili (umetajwa hivi). Kuwa (wao) ni kama mmea uliotoa matawi yake; kisha (matawi hayo) yakautia nguvu, ukawa mnene ukasimama sawasawa juu ya kigogo chake, ukawafurahisha walioupanda ili awakasirishe makafiri kwa ajili yao. Mwenyezi Mungu amewaahidi walioamini na kutenda mema katika wao msamaha na ujira mkubwa.”

Al Fat-h- 29

Katika aya hii Mwenyezi Mungu amewasifia Masahaba wa Mtume (SA) wote kwa pamoja. Kwa hivyo asili ya itikadi yetu ni kuwasifia, na imepokelewa hadithi sahihi ya Mtume (SAW) isemayo;

“Msiwatukane Masahaba wangu, lau kama mmoja wenu atatoa dhahabu ukubwa wake mfano wa jabali la Uhud, basi haitofikia gao lao wala hata nusu yake”

Bukhari na Muslim

Hizi pia ni sifa ambazo Mtume (SAW) amewasifia Masahaba wake (RA), na tutaelezea kwa ufafanuzi zaidi tutakapoufikia mlango nilioutenga katika kitabu hiki niloupa jina la ‘Uadilifu wa Masahaba’.

Kitabu muhimu kupita vyota katika elimu ya tarekh ni kile kilichoandikwa na Imam At Tabari na wengi wananukuu kutoka katika kitabu hicho. Ahli Sunnah wananukuu kutoka katika kitabu cha ‘Tarikh At Tabari’, na Ahlul Bida’a (wanofuata madhehebu a ki Shia) pia wananukuu kutoka katika kitabu cha Tarikh At Tabari.

Ahli Sunnah wanatoa hoja zao katika kitabu cha tarikh At Tabari na Ahlul Bida’a wanatoa hoja zao kutoka katika kitabu cha Tarikh At Tabari.

 

KWA NINI KITABU CHA TARIKH AT TABARI KINAPENDEKEZWA KULIKO VINGINE?

Kwa sababu nyingi zikiwemo zifuatazo;

1.     Kitabu cha At Tabari kimeandikwa wakati ulio karibu zaidi na matukio yenyewe.

2.     Imam At Tabari anahadithia pamoja na isnadi (majina ya wapokezi wa hadithi hizo).

3.     Utukufu wa Imam At Tabari pamoja na haiba na heshima yake kutokana na daraja yake ya elimu.

4.     Vitabu vingi vya historia vinanukuu kutoka kwake.

 

Kwa ajili hiyo na sisi tunapotaka kuisoma historia inatubidi tukiendee kitabu hicho cha At Tabari moja kwa moja. Lakini kama nilivyosema ni kuwa Ahlis Sunnah wananukuu kutoka kitabu hicho kiitwacho ‘Tarikh At Tabari’, na Ahlul Bida-a nao pia wananukuu kutoka katika kitabu hicho cha Tarikh At Tabari. Sasa vipi tutaweza kusawazisha baina ya hii na ile?

Tulikwishaelezea hapo mwanzo kuwa uzuri wa kitabu hiki cha Tarikh At Tabari ni kwamba hakiandiki juu ya hadithi isipokuwa lazima kitataja majina ya wapokezi wa hadithi hiyo (isnadi). Ahlus Sunnah wao wanachukuwa hadithi zilizo na isnadi sahihi katika kitabu hicho lakini Ahlul Bida-a wao wanachukuwa zilizo sahihi na zisizo sahihi, muhimu zikubalieni na matamanio ya nafsi zao.

 

TARATIBU ALIZOTUMIA IMAM AT TABARI KATIKA KUANDIKA KITABU CHAKE CHA TARIKH

Imam At Tabari Mwenyezi Mungu amrehemu ametupumzisha sana katika jambo hili kutokana na utangulizi wa kitabu chake hicho, yareti wale wanaokisoma kitabu hiki cha Tarikh wangesoma utangulizi huo.

Anasema Imam At Tabari katika utangulizi wake;

“Ajue msomaji wa kitabu chetu hiki kuwa yote niliyoyaelezea humu yanatokana na maelezo niliyoyapokea kutoka kwa wasimulizi wa habari na nimejiwekea masharti ya kuandika isnadi (mlolongo wa majina ya wapokezi) ya yote yale walionihadithia.

Iwapo ndani ya kitabu changu hiki zimo habari zozote nilizozisimulia juu ya waliotangulia zisizompendeza msomaji au zitakazomuudhi msikilizaji, na habari hizo zikawa siyo sahihi, basi atambuwe msomaji au msikilizaji huyo kuwa habari hizo hazikutokana na sisi, isipokuwa sisi tumezifikisha vile vile kama tulivyofikishiwa”.

Nadhani Imam At Tabari kwa utangulizi wake huu amekutupia mzigo wewe msomaji, kama kwamba anakwambia;

“Ukikuta ndani ya kitabu changu hiki habari zisizokufurahisha au zisizokubalika, basi tizama kutoka kwa nani tumezipokea habari hizo. Na kama nilivyoahidi kuwa nitaandika majina ya wale walionipa habari hizo, kwa hivyo ukiona kuwa wale niliopokea kutoka kwao habari hizo ni watu wa kuaminika, basi zikubali, la kama si wa kuaminika basi usizikubali”.

Utaratibu huu ndio uliofuatwa na wengi kati ya waandishi wa vitabu vya elimu ya hadithi. Iwapo mtu atarudia na kusoma vitabu vya hadithi, ukivitowa vitabu vya Bukhari na Muslim, kwa sababu waandishi wa vitabu hivyo viwili wameahidi kuandika hadithi zilizo sahihi tu ndani yake. Lakini vitabu vingine kama vile Attirmidhy au Abu Daud au Addaraqutniy au Addarimiy au Musnad ya Imam Ahmed au kitabu chochote kingine katika vitabu vya elimu ya hadithi, utaona kuwa waandishi wake wanakutajia mlolongo wa majina ya wapokezi wa hadithi hizo (isnadi) kwa sababu wao hawakutoa ahadi ya kuandika hadithi zilizo sahihi peke yake, na kwa ajili hiyo wakawa wanakuandikia isnadi na unachotakiwa wewe ni kuziangalia isnadi hizo. Ikiwa wapokezi ni watu wanoaminika utazikubali, ama ikiwa si watu wa kuaminika, basi usizikubali.

Kutokana na utangulizi wake, At Tabari hakutoa ahadi ya kuandika yale yaliyo sahihi peke yake, isipokuwa ametoa ahadi ya kuandika majina ya wale ambao kutoka kwao amepokea maelezo hayo.

Ikiwa mambo yenyewe ni kama hivyo, basi Imam At Tabari hakutoa ahadi (ya kuandika hadithi zile sahihi tu). Na katika kitabu chake, Attabari amenukuu habari nyingi kutoka kwa mtu mmoja aitwae Luut bin Yahya, maarufu kwa jina la ‘Abu Makhnaf’.

Imam At Tabari amenukuu kutoka kwa Luut bin Yahya huyu, riwaya mia tano na themanini na saba. Na riwaya hizi zinaelezea kuanzia wakati alipofariki Mtume (SAW) na kumalizikia wakati wa ukhalifa wa Yazid bin Muawiya, na huu ndio wakati nitakaozungumza juu yake katika kitabu chetu hiki, zikiwemo habari za Saqifat Bani Saaidah, kisha cha Shuura, sababu zilizowafanya Khawarij wachukuwe msimamo dhidi ya Othman (RA) na hatimae kuuliwa kwake, ukhalifa wa Ali (RA), vita vya ‘Al Jamal’, vita vya ‘Siffin’, kuhukumu, (Tahkiym), vita vya Naharawan, ukhalifa wa Muawiya (RA), kuuliwa kwa Al Hussein (RA). Katika yote haya utazikuta riwaya zilizosimuliwa na Abi Makhnaf, riwaya ambazo Ahlul Bida-a ndiyo wanaozitegemea sana na kuzishikilia.

Na si Abu Makhnaf peke yake mwenye riwaya za uongo, isipokuwa tu, Abu Makhnaf ni mashuhuri kupita wenzake, lakini wapo wengine waongo kama yeye kama vile Al Waaqidiy ambaye katika elimu ya hadithi anajulikana kuwa ni muongo ambaye hadithi zake hazikubaliwi, juu ya kuwa yeye ni mjuzi wa riwaya nyingi na mtaalamu wa historia, isipokuwa si mtu mwaminifu wa kufikisha habari.

Wa tatu ni Seif bin Omar At Tamimi ambaye pia ni mtaalamu wa historia maarufu, isipokuwa naye pia si muaminifu wa kufikisha habari na anajulikana kuwa ni mtu muongo na hadithi zake hazikubaliwi.

Yupo mwingine pia aitwae Al Kiliy ambaye ni muongo mashuhuri, na kwa ajili hiyo mtu inampasa achunge asije akazikubali riwaya zilizosimuliwa na watu wa aina hii.

Turudi kwa Abu Makhnaf na tutazame maulamaa wamesea nini juu yake.

Ibni Maiyn ambaye ni mwanachuoni maarufu wa elimu ya wapokezi wa hadithi amesema;

“Abu Makhnaf si mwenye kuaminika”.

Na Abu Hatim amesema;

“Abu Makhnaf hazikubaliwi riwaya zake”.

Na Imam Ad Daraqutny amesema;

“Abu Makhnaf ni dhaifu”.

Imam Adhahabi amesema;

“Mwingi wa habari na mtungaji wa maneno asiyeaminika”.

Na wewe unapokifungua kitabu cha Tarikh ya At Tabari na ukakumbana na riwaya inayowalaumu Masahaba wa Mtume(SAW), kisha ukaona kuwa At Tabari amezinukuu habari hizi kutoka kwa Abu Makhnaf, basi ni juu yako kuziweka upande habari hizo. Kwa nini? Kwa sababu ni riwaya iliyosimuliwa na Abi Makhnaf.

Na Abu Makhnaf huyu amekusanya riwaya nyingi zenye mambo ya Bida-a ndani yake na za uongo.

 

NJIA ZINAZOTUMIWA NA WALETAO HABARI KATIKA KUIPAKA MATOPE HISTORIA

1- Uzushi na maneno ya uongo.

Wanatunga kisa fulani, mfano wa kisa walichokitunga juu ya Bibi Aisha (RA) kwamba eti alisujudu kwa ajili ya kumshukuru Mwenyezi Mungu aliposikia habari za kifo cha Ali (RA). Bila shaka hiki ni kisa cha uongo.

 

 2- Kuongeza maneno au kupunguza kwa nia ya kuleta sura mbaya.

 Huenda kisa cheyewe kikawa ni sahihi, kwa mfano kisa cha tukio la Saqifat bani Saad. Kisa hiki kilitokea kweli mara baada ya kufariki kwa Mtume (SAW) walipokutana Abubakar na Omar na Abu Ubayda upande mmoja, na upande wa pili alikuwa Al Khabab bin Mundhir na Saad bin Obada na wengineo katika watu wa Madina (RAnhum). Waandishi hao wakaongeza maneno yao kama nitakayokuja kuelezea kila tukiendelea mbele. Wameongeza kwa nia ya kuharibu sifa za Masahaba wa Mtume (SAW).

 

3- Kufasiri visivyo sahihi hadithi za Mtume (SAW).

Nako ni kuyafasiri maneno ya Mtume (SAW) kama wanavyotaka wao ili yakubaliane na matamanio yao na itikadi zao.

 

4 -Kudhihirisha lugha mbaya au makosa.

Kisa kinakuwa cha kweli, lakini wao wanakielezea huku wakitilia mkazo pale

Sahaba (RA) alipofanya makosa kwa nia ya kuyabainisha makosa hayo huku wakiyaficha mema yao bila kuyabainisha.

 

5- Kutunga mashairi kwa ajili ya kuyapa nguvu matukio ya kihistoria.

Wanatunga mashairi kisha wanayanasibisha na Amiri wa Waislamu Ali bin Abi Talib (RA) au wanayanasibisha na Mama wa Waislamu Bibi Aisha (RA), au wanayanasibisha na Al Zubeir bin Awaam au Talha (RAnhuma) kwa ajili ya kumtuhumu mmojawapo katika ya Masahaba, kama walivyotunga shairi la kumkashifu Bibi Aisha (RA) kisha wakalinasibisha na Ibni Abbas (RA).

 

4-                 6- Kutunga barua za uongo

Kama tutakavyoona Inshaallah katika kisa cha kuuliwa kwa Othman (RA), jinsi barua za uongo zilivyoandikwa, kisha akasingiziwa Othman (RA) kuwa yeye ndiye aliyeziandika, na namna gani zilivyoandikwa barua za uongo na kunasibishwa na Bibi Aisha (RA) na nyingine zikaandikwa na kusingiziwa Ali (RA) kuwa ndiye aliyeziandika na Talha na Al Zubeir (RA), haya ukiacha kuhesabu barua na vitabu kama kitabu kiitwacho Nahjul Balagha kilichoandikwa na kunasibishwa na Ali bin Abi Talib (RA) pamoja na kitabu kiitwacho Al Imamah walichokinasibisha na Imam Ibni Qutaybah.

 

JUHUDI ZA MASHIA KATIKA KUINGIZA UONGO NA KUIPA SURA MBAYA HISTORIA YA KIISLAMU

Walio mashuhuri kupita wote katika historia kwa uzushi na kwa uongo ni Mashia, na hii ndiyo maana maulamaa wanawapigia mifano kwa kusema;

“Muongo kuliko Rafidhiy (Shia)”, na hii inatokana na wingi wa kusema uongo kwao”.

Anasema Al A-amash;

“Niliwahi kuishi na watu waliokuwa wakijulikana kwa jina la ‘waongo’.

Anasema Shureih Al Kadhi;

“Naipokea elimu kutoka kwa yeyote nitakayeonana naye isipokuwa Mashia, kwa sababu wao wanatunga hadithi za uongo kisha wanaigeuza hadithi hiyo kuwa dini yao”.

Anasema Imam Shafi;

“Sijapata kuona wenye kusema uongo kuliko Mashia”.

Kusudi langu ni kuwa ingawaje makundi mengine pia yanasema uongo lakini hawa ni mashuhuri sana kuliko wengine katika kueneza habari zisizo za kweli na kutunga hadithi za uongo.

 

TARATIBU ZA KUHAKIKISHA UKWELI WA HADITHI KWA AHLUS SUNNAH – WAKATI GANI ZILIANZA?

Zilianza baada ya kutokea vita vya wenyewe kwa wenyewe (fitan).

Muhammed bin Siriyn (RA) ambaye ni miongoni mwa maulamaa wakubwa wa Taabi iyn amesema;

“Watu hawakuwa wakiuliza juu ya isnadi za hadithi walizokuwa wakizisikia, mpaka pale ilipotokea ‘fitna’ (vita vya wenyewe kwa wenyewe), wakaanza kusema; ‘Tutajieni majina ya wale mlopokea hadithi hizi kutoka kwao’, Ikawa watu wanaangalia majina ya wapokezi wa hadithi zinazosimuliwa na watu wa Ahlis Sunnah na kuzikubali riwaya zao, na wanapoangalia majina ya wapokezi wa Ahul Bida-a, wanazikataa riwaya zao”.

(Haya yamo katika utangulizi wa kitabu cha Sahih Muslim).

Na hii ni kwa sababu watu wanapokea riwaya kutoka kwa wanoaminika, na Ibni Siyrin ni mmojawapo wa wakubwa wa maulamaa wa At Tabi iyn aliyewahi kuishi na baadhi ya Masahaba na akaishi pamoja na maulamaa wakubwa wa Taabi iyn na wadogo wao, na kwa sababu fitna zilizotokea ndiyo maana kukatokea makundi ya Shia na Khawarij na Qadiriyah.

 

 

 

KUJA KWA MTUME MUHAMMAD (SAW)

 

Siku ya Jumatatu tarehe 12 mwezi wa Rabiul awwal (ipo khitilafu juu ya siku aliyozaliwa Mtume (SAW)), Mwenyezi Mungu aliwatunukia walimwengu wote zawadi kubwa sana kwa kuzaliwa kwa bwana wa viumbe vyote na kiongozi wao Muhammad bin Abdullah bin Abdul Muttalib Al Hashimy kutoka katika kabila la ki Qureshi.

Alizaliwa akiwa yatima hana baba na alipotimia miaka sita mama yake akafariki na akachukuliwa na babu yake Abdul Muttalib, na miaka miwili baadaye babu yake akafariki na akachukuliwa na ammi yake Abu Talib.

Alipotimia miaka arubaini Mwenyezi Mungu alimpa utume ili awe mwenye kuleta bishara njema na mwenye kuonya, akausimamia ujumbe wake kama unavyostahiki kusimamiwa na akafikishi yale Mwenyezi Mungu alomuamrisha ayafikishe kwa ajili ya kuwatowa watu katika giza na kuwaingiza katika nuru. Wakubwa wa kabila lake wakamfanyia uadui na wakawatendea wafuasi wake kila aina ya udhia, wakamfuata makundi ya watu walioiuza dunia yao kwa ajili ya akhera, wakapigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali zao na kwa nafsi zao, wakainusuru (dini ya) Mwenyezi Mungu na Mtume wake.

Mwenyezi Mungu anasema;

“(Basi) wapewe (mali hayo) mafakiri wa Kimuhajiri ambao walifukuzwa katika nyumba zao na mali zao; (wakakhiari kuwacha hayo) kwa jili ya (kutafuta) fadhila za Mwenyezi Mungu na radhi (yake) na kuinusuru (dini ya) Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Basi hao ndio Waislamu wa kweli”.

Al Hashr - 8

Akaendelea Mtume (SAW) kuwalingania watu muda wa miaka kumi na tatu mpaka Mwenyezi Mungu alipomuamrisha kuhamia Madina, mji ambao Mwenyezi Mungu ameutia nuru kwa kumjaalia Mtume wake kuhamia huko. Wakahamia huko pia Masahaba wake (RA) na kuacha mali zao na watoto wao nyuma yao, yote hayo kwa ajili ya kutaka radhi za Mwenyezi Mungu.

Alipowasili Madina akapokewa vizuri na watu wa mji huo, waliomnusuru na kumsaidia. Wakawasaidia wale waliohama pamoja naye, wakagawana nao mali zao na nyumba zao na hata wake zao, kwani watu wa Madina wenye wake wawili au zaidi walikuwa wakiwaambia watu wa Makka;

“Chagua mmoja kati ya wake zangu yule unayemtaka ili nimtaliki kisha nikuozeshe wewe”.

Mwenyezi Mungu anasema;

“Na wale waliofanya maskani yao hapa (yaani Madina) na wakautakasa Uislamu (wao barabara) kabla ya kuja hao (Muhajir huko Madina) na wakawapenda hao waliohamia kwao, wala hawapati (hawaoni) dhiki nyoyoni mwao kwa hayo waliyopewa (hao Muhajiri), na wanawapendelea kuliko nafsi zao ingawa wenyewe wana hali ndogo. Na waepushwao na ubakhili wa nafsi zao hao ndio wenye kufaulu kweli kweli”.

Al Hashr –9

Mtume (SAW) akaendelea na daawa yake nje ya mji wa Madina na hatimaye bara ya Arabu yote mpaka ilipofika siku ile tukufu ambayo Mwenyezi Mungu alimfungulia Mtume wake (SAW) mji mtukufu wa Makka (alipouteka mji wa Makka) na watu wake wakaingia katika dini ya Kiislamu na baada ya hapo bara ya Arabu yote ikawa chini ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW).

Baada ya kuwalingania watu pamoja na kupigana jihadi muda upatao miaka ishirini na mitatu, ikamfikia qudra ya lazima kwa kila mtu inayosadikishwa na kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo;

“Na hakuwa Muhammad ila ni Mtume tu. Wamepita kabla yake Mitume (wengi kabisa),. Basi akifa au akiuawa ndiyo mtarudi nyuma (kwa visigino vyenu muwe makafiri kama zamani?) Na atakayerudi nyuma kwa visigino vyake hatamdhuru Mwenyezi Mungu chochote . Na Mwenyezi Mungu atawalipa wanaomshukuru”.

Aali Imran – 144

 

Dunia ilikuwa kama kwamba imeingia giza totoro kutokana na tukio hili. Na kwa nini isiwe hivyo wakati Mtume (SAW) alisema;

“Atakayekutwa kati yenu na msiba, basi akumbuke msiba wake kwangu (wa kifo changu), kwani huo ndio msiba mkubwa zaidi”.

Attabaqaat al kubra na imesahihishwa na Sheikh Al Albani.

Haukupata kutokea msiba mkubwa wakati wowote ule tokea iumbwe dunia kuliko msiba wa kifo cha Mtume (SAW). Na huyu Bibi Fatima (RA) binti wa Mtume (SAW) wakati baba yake alipokuwa akijiwa na sakrati l mauti alikuwa akisema;

“Babayangu! ameitikia mwito wa Mola wake, baba yangu! Pepo ya Firdausi makazi yake, baba yangu! kwa Jibril tunafikisha pole yake”.

Ana bin Malik (RA) naye alisema;

“Siku ile Mtume (SAW) alipoingia mji wa Madina, kila kitu kilikuwa kikitowa mwangaza, ama siku ile aliyofariki kila kitu kiliingia giza, na tulipokuwa tukipangusa mikono yetu michanga baada ya kumzika tulihisi nyoyo zetu zimenyongeka (kwa sababu wahyi umeshakatika na hautoshuka tena baada yake (SAW)”.

Ibni Majah katika ‘kitabu l janaiz – mlango wa ‘wafaatun Nabiy (SAW).

Baada ya kifo cha Mtume (SAW), Abubakar alimwambia Omar (Ranhum);

“Twende tukamtembelee Ummu Ayman”.

Walipowasili kwake, Ummu Ayman alilia sana, wakamuuliza;

“Kwa nini unalia hivyo wakati atakayopata Mtume (SAW) kwa Mola wake ni bora zaidi?”

Akajibu;

“Wallahi ninalia si kwa sababu sielewi kuwa yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu ni bora zaidi kwa Mtume wake, isipokuwa kinachoniliza ni kukatika kwa wahyi kutoka mbinguni”.

Maneno hayo yaliwaliza sana Abubakar na Omar (RA)

Muslim

Na hivi ndivyo nafsi hii njema ilivyohamia kwa Mola wake.

 

UKHALIFA WA ABUBAKAR AL SIDDIQUE (RA)

Mara baada ya kutangazwa kufariki kwa Mtume (SAW), Abubakar alikwenda moja kwa moja mpaka mahali alipolazwa, akaufunua uso wake na kumbusu juu ya kipaji cha uso wake baina ya macho yake, kisha akasema;

“(Nakufidia) Kwa baba yangu na mama yangu, unapendeza ukiwa hai au umekufa”.

Kisha akaufunika uso wa Mtume (SAW), akanyanyuka na kupanda juu ya membari na kusema;

“Kama yupo aliyekuwa akimuabudu Muhammad, basi Muhammad kesha kufa, ama kama mlikuwa mkimuabudu Mwenyezi Mungu, basi Mwenyezi Mungu yuhai na hafi. (kisha akaisoma kauli ya Mwenyezi Mungu ifuatayo;)

“Na hakuwa Muhammad ila ni Mtume tu. Wamepita kabla yake Mitume (wengi kabisa). Akifa au akiuawa ndiyo mtarudi nyuma (kwa visigino vyenu), muwe makafiri kama zamani? Na atakayerudi nyuma kwa visigino vyake hatamdhuru Mwenyezi Mungu cho chote. Na Mwenyezi Mungu atawalipa wanaomshukuru”.

Aali Imran – 144

Watu wakawa wanalia na wengine wakawa wanatembea mitaani huku wakiikariri aya hiyo. Anasema Anas (RA);

“Ilikuwa kama kwamba hatujapata kuisikia aya hiyo isipokuwa wakati ule (kama kwamba tunaisikia kwa mara ya mwanzo)”.

Bukhari – kitabu cha Fadhila za Masahaba.

Juu ya kuwa Qurani ilikwisha kamilika kabla ya kufa kwa Mtume (SAW) na kabla ya kufariki kwake, lakini aya hii ilikuwa kama ni mpya kwao, kama kwamba hawakupata kuisikia kabla ya siku hiyo kutokana na mshituko waloupata kwa kifo cha Mtume (SAW).

Al Abbas bin Abdul Muttalib na Ali bin Abi Talib na Al Zubeir bin Al Awaam (RA) ndio waliofanya kazi ya kumuosha na kumkafini Mtume (SAW) na kumshughulikia mpaka aliposaliwa, na hii ni kwa sababu Al Abbas (RA) ni Ami yake Mtume (SAW) na Ali (RA) ni mtoto wa ammi yake Mtume (SAW) na Al Zubair (RA) ni mtoto wa shangazi lake Mtume (SAW) na kwa ajili hiyo wao ndio waliostahiki zaidi kujishughulisha na hayo.

 

SAQIFAT BANI SAIDAH

Wakati Al Abbas na Ali na Al Zubair (RA) walipokuwa wakijishughulisha na kumtayarisha Mtume (SAW), baadhi ya watu wa Madina walikutana mahali panapoitwa Saqifat Bani Saidah, na nitakielezea kisa hiki kwanza kama kilivyoelezwa katika kitabu cha Tarikh cha Imam At Tabari namna kilivyoelezwa na Abi Makhnaf ‘muongo’, kisha nitakielezea kama kilivyoelezwa na Imam Bukhari, kisha pima wewe mwenyewe baina ya riwaya mbili hizi ili uweze kuujuwa uongo ulio ongezwa na Abu Makhnaf.

Huenda mengi katika uongo huo uliozidishwa ukawa katika wakati wetu huu ni jambo lililokwisha kubalika miongoni mwa watu, na haya tutakuja kuyaona pale tutakapozungumza juu ya tukio la Shuura.

Anasema Imam At Tabari (Mwenyezi Mungu amrehemu):

Ametuhadithia Hisham bin Muhammad kutoka kwa Abi Makhnaf, (kuwa) amesema: Nimehadithiwa na Abdullahi bin Abdul Rahman bin Abi Amru bin Abi Amrah Al Ansari kuwa Mtume alipofariki, watu wa Madina walikusanyika (mahali panapoitwa) Saqifat bani Saidah wakasema;

“Baada ya Muhammad tumchaguwe Saad bin Ubada awe kiongozi wetu”.

Mmoja wao akainuka na kusema;

“Kwa panga zenu waarabu wote wamekufuateni, na Mtume (SAW) amefariki akiwa ameridhika nanyi na akiwa amefurahika nanyi (kwa hivyo) musiiache fursa hii wakaja kuichukuwa watu wengine”.

Wote wakajibu;

“Rai yako ni sawa”.

Mmojawao akasema;

“Wakikataa wahajiri wa Kikureshi tutawaambia amiri mmoja atoke kwao na amiri mmoja atoke kwetu”.

Akasema Saad bin Obada;

“Huu ni udhaifu wa mwanzo”.

Kisha zikamfikia habari Omar bin Khattab kuwa baadhi ya watu wa Madina wamekusanyika Saqifat bani Saidah wakisema: ‘Amri mmoja kutoka kwetu na amiri mmoja kutoka kwenu’. Alipewa habari hizo na mmojawapo katika watu wa Madina. Akenda moja kwa moja mpaka kwa Abubakar na kumueleza juu ya jambo hilo, akamwambia:

“Ndugu zetu katika watu wa Madina ‘Al Ansar’, wamekusanyika na wanasema hivi na vile, tuwaendee huko haraka sana”.

Omar na Abubakar walipokuwa wakiondoka wakakutana na Abu Ubaidah wakamwambia:

“Twende pamoja”.

Wakaondoka watatu hao na kuelekea mahali walipojikusanya watu wa Madina. Anasema Omar;

“Nilikuwa nimekweshajitayarishia maneno ya kusema, na nilipokuwa nikijitayarisha kusema, Abubakar akaniashiria kuwa ninyamaze na akaanza Abubakar kusema;

“Alhamdulillah”, kisha akampwekesha Mwenyezi Mungu, kisha akasema;

“Hakika Mwenyezi Mungu amemleta Muhammad…..”

Kisha akaitaja khutba ndefu iliyotolewa na Abubakar na kwamba alisema ndani ya khutba hiyo kuwa watu wa Makka ‘Muhajirin’ ndio wanaostahiki kuwa Makhalifa.

Akasema Al Habaab bin Mundhir;

“Enyi watu wa Madina! Mumiliki wenyewe amri yenu, kwani watu wako chini ya kivuli chenu na hawezi yeyote kujaribu kwenda kinyume nanyi na watu hawatofuata isipokuwa rai yenu, nyinyi ndio wenye nguvu na wenye mali na wenye idadi kubwa ya watu na wenye ulinzi, na kama wakikataa kukufuateni basi watoweni nje ya mji (wenu) huu. Waongozeni nyinyi katika mambo haya, kwani nyinyi wallahi ndiwo wenye haki kuliko wao, kwa sababu kwa panga zenu wameingina katika dini hii walioingia wale wasiokuwa na dini. Mimi ndiye mwenye kuistahikia zaidi na mwenye uwezo mkubwa zaidi wa kulibeba jukumu hili kuliko wengine”

Omar na Abu Ubaidah wakamwambia Abubakar;

“Tandaza mkono wako tufungamane nawe”, walipokuwa wanataka kufungamana naye, akawatangulia Bashir bin Saad (mtu wa Madina) na akawa yeye mtu wa mwanzo kufungamana naye, na hivi ndivyo watu walivyofungamana na Abubakar.

Anasema (Abu Makhnaf);

“Akainuka Usayd bin Hudhair aliyekuwa miongoni mwa viongozi wa kabila la Aus waliokuja kufungamana na Mtume (SAW)  katika ‘Fungamanao la Aqaba la pili’ kabla ya Mtume (SAW) kuhamia Madina, akasema;

“Wallahi ikiwa uongozi juu yenu watauchukuwa watu wa kabila la Khazraj mara moja tu, basi haitoondoka tena fadhila yao hiyo juu yenu”.

(Abu Makhnaf anamaanisha hapa kuwa Usayd alimuonea husda Saad bin Obada anayetokana na kabila la Khazraj kwa kuteuliwa na watu wa Madina kuwa kiongozi wa Waislamu”.

(Aus na Khazraj ni makabila mawili makubwa ya watu wa Madina)

Saad akasema;

“Wallahi kama ningelikuwa na nguvu za kujinyanyua, basi ungelisikia kutoka kwangu mngurumo utakaokujeruhi wewe na sahibu zako, kisha wallahi ningelikufukuzia kwa kaumu ambayo wewe ulikuwa ukiwafuata tu na wala hawakufuati, niondoweni mahali hapa”.

Wakamnyanyua na kumuingiza nyumbani kwake, akaachwa kwa muda wa siku nyingi (RA) kisha akasema;

“Ama wallahi mpaka nikuvurumishieni mishale niliyoibeba ndani ya mfuko wake, na niipake rangi (damu) meno yake (mishale hiyo), kisha nikupigeni kwa upanga wangu kisha nikupigeni vita mimi na watu wa nyumba yangu pamoja na watakaonitii katika watu wa kabila langu”.

Anasema (Abu Makhnaf):

“Saad akawa hasali sala yao wala hasali Ijumaa pamoja nao, anahiji lakini hafuatani nao, akaendelea katika hali hiyo mpaka alipofariki Abubakar (RA)”.

 

Hii ni riwaya kama ilivyoelezewa na Abu Makhnaf juu ya tukio la Saqifat Bani Saidah, na sasa someni riwaya iliyosimuliwa na Imam Bukhari juu ya kisa hiki, kisha linganisheni.

Anasema Imam Bukhari;

“Nimehadithiwa na Ismail bin Abdullah, nimehadithiwa na Suleiman bin Bilal kutoka kwa Hisham bin Uruwah amesema: Amenambia Uruwah bin Al Zubeir kuwa Aisha mke wa Mtume (SAW) amesema;

“Hakika alipofariki Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) watu wa Madina walijumuika kwa Saad bin Ubada mahali panapoitwa Saqifat bani Saidah, wakasema;

“Amiri mmoja atoke kwetu na amiri mmoja atoke kwenu”.

Abubakar na Omar na Abu Ubaidah wakawaendea, na Omar alipotaka kuhutubia akanyamazishwa na Abubakar, na Omar alikuwa akisema;

“Wallahi kwa kufanya vile sikuwa na nia nyingine isipokuwa nilitaka kusema maneno yaliyonipendeza niliyokwishayatarisha na nikaogopa Abubakar asije akashindwa kuifikisha fikra hiyo, lakini Abubakar akaweza kuifikisha vizuri kupita mtu yeyote, na akasema katika maneno yake;

“Ma Amiri watoke kwetu na Ma Waziri watoke kwenu”.

Akasema Khubab bin Mundhir:

“Wallahi hatukubali. Kwetu atoke Amiri na kwenu atoke Amiri”.

Abubakar akasema;

“Sivyo hivyo, sisi ni Ma Amri na nyinyi ni Ma Waziri, wao (Makureshi) ndio waarabu wa kati kwa kati kupita wote na watukufu kupita wote, Fungamaneni na Omar au Abu Ubaydah”.

Omar akasema;

“Bali tutafungamana na wewe, kwani wewe ndiye bwana wetu na mbora wetu na unayependwa zaidi na Mtume wa Mwenyezi Mungu kuliko sisi. Kisha Omar akauchukuwa mkono wake na akafungamana naye, na watu wote wakafungamana naye”.

Sahihul Bukhari katika mlango wa Fadhail al Sahaba

 

Hii ni riwaya ya Imam Bukhari, kama unavyoiona kuwa ni fupi na ndogo na huu ndio uhakika wa mambo yalivyokuwa katika Saqifat bani Saidah. Ama yale aliyozidisha Abu Makhnaf kama mlivyosikia kwamba eti Saad bin Obada alisema;

“Nitapigana vita na nyinyi…” na kwamba eti hakuwa akihiji wala kusali pamoja nao wala hakuwa akisali Ijumaa pamoja nao wala hakuwa akifuatana nao, na kwamba Al Khabaab bin Mundhir alimjibu Abubakar, pamoja na nyongeza nyingine (yoote hayo ni uongo mtupu), kwani tukio la Saqifa halikuchukuwa zaidia ya nusu saa, na tazameni namna gani walivyokifanya kisa hicho kuwa kikubwa kuliko kinavyostahiki.

Ama kuhusu Saad bin Obada, imepokelewa hadithi katika Musnad ya Imam Ahmed kutoka kwa Humaid bin Abdur Rahman kuwa amesema;

“Alizungumza Abubakar na wala hajaacha sifa zozote katika zile walizoteremshiwa watu wa Madina ndani ya Qurani  au zile alozitaja Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) asizitaje (Amezitaja sifa zote za watu wa Madina). Akasema;

“Mnakumbuka kuwa Mtume (SAW) amesema; “Na lau kama watu wote watafuata njia zao katika mabonde na mitaa, na watu wa Madina watafuata njia nyingine, basi mimi ningefuata njia watakayopita watu Madina”.

Kisha baada ya hayo Abubakar akamwambia Saad bin Obada;

“Na wewe unakumbuka ewe Saad kuwa Mtume (SAW) (siku moja) ulipokuwa umekaa alikwambia: “Makureshi ndio watakao ongoza amri hii, na watu wema wanawafuata wema wao na waovu wanawafuata waovu wao”.

Baada ya kusikia maneno hayo Saad akasema;

“Umesema kweli! Sisi ni Ma Waziri na nyinyi Ma Amiri”.

Riwaya hii imesimuliwa na Ahmed katika Musnad yake kwa isnadi sahihi iliyonyanyuliwa (mursal) na Humaid bin Abdul Rahman bin Auf (RA), na ingawaje riwaya hii imenyanyuliwa, lakini ina nguvu zaidi kuliko riwaya za muongo yule – Abu Makhnaf.

 

 

ABUBAKAR AL SIDDIQUE (RA)

 

Jina lake ni Abdillahi bin Othman bin Amer bin Amru bin Kaab bin Saad bin Tiym bin Murrah bin Kaab bin Luayyi bin Ghalib bin Fihr, na Fihri huyu ndiye Quraish.

Amesema Ali bin Abi Talib (RA);

“Mwenyezi Mungu ameteremsha jina la Abubakar (la) Al Siddique kutoka mbinguni”.

Attabarari hadithi nambari 1/55 na ameitaja hadithi hii pia Al Hafidh Ibni Hajar katika Al Fatah 7/11.

 

KUSILIMU KWAKE

Kutoka kwa Abid Dardaa (RA) amesema;

“Nilikuwa nimekaa kwa Mtume (SAW) akatokea Abubakar akiwa ameshika (na kuinyanyua) ncha ya nguo yake hata goti lake likawa linaonekana, akasema Mtume (SAW);

“Ama sahibu yenu (anaonesha) kesha kasirishwa”.

Abubakar akatoa salamu kisha akasema;

“Ilikuwa baina yangu na Omar jambo, nilimfanyia haraka, kisha nikajuta, nikamuomba anisamehe akakataa, nikakujia wewe”.

Mtume (SAW) akasema;

“Mwenyezi Mungu akughufirie ewe Abubakar (akasema hivyo mara tatu)”.

Kisha Omar naye akajuta, akenda mpaka nyumbani kwa Abubakar na kuuliza;

“Abubakar yupo?”

Wakasema;

“Hayupo”.

Akenda kwa Mtume (SAW) na uso wa Mtume (SAW) ukawa umebadilika rangi kwa ghadhabu, mpaka Abubakar akamuonea huruma Omar, akapiga magoti mbele ya Mtume (SAW) na kusema;

“Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, wallahi mimi ndiye niliyemkosea (mara mbili)”.

Mtume (SAW) akasema;

“Mwenyezi Mungu alinituma kwenu (na nyote) mkanambia muongo, (isipokuwa) Abubakar alisema; ‘nakusadiki’, akaniliwaza kwa kwa hali na mali, sasa nyinyi mtamuacha sahibu yangu (akasema hiyvo mara mbili)”.

Tokea siku hiyo Abubakar hakukasirishwa tena na mtu.

Bukhari mlango wa Fadhila za Masahaba

Na kutoka kwa Amaar bin Yasir (RA) amesema;

“Nilimuona Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) akiwa hakufuatana na zaidi ya watu watano na wanawake wawili na Abubakar”.

Bukhari

KUHAJIRI KWAKE

Kutoka kwa Abubakar (RA) amesema;

“Nilikuwa na Mtume (SAW) pangoni, nikanyanyua kichwa changu, nikajikuta nipo karibu na miguu ya watu (makafiri). Nikasema; “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu mmoja wao akitupa jicho lake chini atatuona”.

Mtume (SAW) akasema;

“Nyamaza ewe Abubakar, (sisi) wawili na Allah wa tatu wao”.

Bukhari kitabu cha sifa za watu wa Madina, mlango wa Hijra ya Mtume (SAW) na Sahaba zake. Hadithi nambari 3922.

Muslim kitabu cha wa sifa za Masahaba hadithi nambari 1.

 

FADHILA ZAKE

Kutoka kwa Abu Huraira (RA) amesema;

“Nilimsikia Mtume (SAW) akisema;

Atakayetoa viwili  vya aina moja katika njia ya Mwenyezi Mungu (mfano ngamia wawili au mbuzi wawili au dirham mbili n.k.), ataitwa kwenye milango ya Peponi huku akiambiwa; “Ewe mja wa Mwenyezi Mungu, hii ni kheri (yaani njoo uingie Peponi kupitia mlango huu). Aliyekuwa katika watu wenye kusali (kwa wingi) ataitwa kupitia mlango wa Sala, na aliyekuwa katika watu wa Jihadi ataitwa kupitia mlango wa Jihadi, na aliyekuwa mtoaji wa Sadaka (mwingi wa kutoa Sadaka) ataitwa kupitia mlango wa Sadaka na aliyekuwa katika watu wa saumu (mwingi wa kufunga) ataitwa kupitia mlango wa saumu au mlango wa Al Rayan”.

Abubakar akasema;

“(Nimefahamu kuwa) Si lazima mtu aitiwe kupitia milango yote hiyo (muhimu aingie Peponi tu).

Kisha Abubakar akauliza;

“Yupo atakayeitwa kupitia milango yote hiyo ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?”

Mtume (SAW) akasema;

“Naam – yupo na nataraji utakuwa miongoni mwao ewe Abubakar”.

Bukhari kitabu cha ‘Fadhila za Masahaba’, hadithi nambari 3666

 

Kutoka kwa Anas bin Malik (RA) amesema;

“Aliupanda Mtume (SAW) na Abubakar na Othman (mlima Uhud), ukatikisika mlima, Mtume (SAW) akasema;

“Tulia (ewe) Uhud, kwa sababu juu yako yupo Mtume na Al Siddique na mashahidi wawili (watakaokufa shahid)”.

Bukhari kitabu cha ‘Fadhila za Masahaba’ hadithi nambari 3675

 

Kutoka kwa Amru bin Al Aas (RA) amesema;

“Nilimuuliza Mtume (SAW): mtu gani unayempenda zaidi kupita wote?”

Akanambia;

“Aisha”.

Nikamuuliza tena:

“Yupi katika mwanamume (unayempenda zaidi)?”

Akanambia:

“Baba yake”.

Nikamuuliza:

“Kisha nani?”

Akanambia:

“Omar bin Khattab”.

Bukhari katika kitabu cha Fadhila za Masahaba hadithi nambari 3662

Muslim mlango wa Fadhila za Masahaba hadithi nambari 8

Kisha Mtume (SAW) akasema;

"Katika watu walonisaidia sana kwa hali na mali ni Abubakar, ingelikuwa naweza kumchagua Khalil (rafiki), basi angekuwa Abubakar, lakini ni ndugu katika Uislamu na kupendana. Milango yote iliyoelekea msikitini ifungwe isipokuwa mlango wa Abubakar".

Bukhari kitabu cha Fadhila za Masahaba hadithi nambari 3654

 

KUWA KWAKE PAMOJA NA MTUME (SAW)

Kutoka kwa Abdullah bin Amru (RA) alipoulizwa juu ya jambo gani ovu kupita yote alowahi kutendewa Mtume (SAW) na washirikina, akasema;

“Nilimuona Uqba bin Abi Muit akimuendea Mtume (SAW) wakati akiwa anasali, akamzungushia nguo yake shingoni pake na kumkaba nayo rohoni pake kwa nguvu sana, akatokea Abubakar na kumsukumilia mbali na Mtume(SAW) kisha akasema;

Oh! Mtamuua mtu kwa sababu anasema Mola wangu ni Mwenyezi Mungu? Na kwa yakini yeye amekujieni kwa dalili waziwazi zitokazo kwa Mola wenu”

Bukhari kitabu cha Fadhila za Masahaba hadithi nambari 3678

 

DALILI ZA KUPEWA UKHALIFA KUTOKA KWA MTUME (SAW)

Kutoka kwa Aisha (RA) amesema;

“Mtume (SAW) alipokuwa akiumwa alinambia;

“Muamrishe Abubakar asalishe watu”.

Bukhari katika kitabu cha ‘Adhani’ mlango wa ‘Ahlul ilm wal fadhal ahaqu bil Imamah’, hadithi nambari 678

 

Kutoka kwa Jaafar bin Mutiim amesema:

“Alikuja mwanamke mmoja kwa Mtume (SAW) na Mtume (SAW) akamuarisha arudi siku nyingine, akauliza:

“Nisipokukuta (nifanyeje)?” (kama kwamba anamuuliza ‘ukifa nimuendee nani?”

Mtume (SAW) akamwambia:

“Usiponikuta mwendee Abubakar”.

Bukhari kitabu cha Fadhila za Masahaba hadithi nambari 3659

Muslim kitabu cha Fadhila za Masahaba hadithi nambari 10

 

Kutoka kwa Aisha (RA) amesema:

“Alinambia Mtume (SAW) alipokuwa akiumwa: “Niitie Abubakar na ndugu yako ili nimwandikie maneno kwani mimi naogopa asije akatamani mwenye kutamani kisha akasema: “Mimi ndiye ninayestahiki zaidi na Mwenyezi Mungu hamkubali mwengine na Waislamu hawamkubali mwengine isipokuwa Abubakar”.

Muslim kitabu cha Fadhila za Masahaba hadithi nambari 11

Bukhari kitabu cha ‘Kuumwa’ mlango wa ‘Anachoruhusiwa mgonjwa kusema anapoumwa hadithi nambari 5666

 

MAMBO MUHIMU YALIYOTOKEA WAKATI WA UKHALIFA WA ABUBAKAR (RA)

1- JESHI LA OSAMA

Mtume (SAW) alikuwa keshatayarisha jeshi chini ya ongozi wa Osama (RA) litakalokwenda kupigana vita nchi ya Sham, na Mtume (SAW) alifariki dunia kabla ya jeshi hilo kuondoka Madina, na jambo la mwanzo alofanya Abubakar (RA) ni kulipeleka jeshi hilo la Osama.

Na katika kulipeleka jeshi hilo la Osama, ilikuwa pigo kubwa kwa wanafiki waliortadi waliodhania kuwa baada ya kufa kwa Mtume (SAW) Uislamu utadhoofika na kutoweka, na katika kulipeleka jeshi hilo pia kulinyanyua nguvu za irada ya Waislamu.

2- VITA VYA WALORTADI

Walortadi ni wale waliotoka katika Uislamu baada ya kufa kwa Mtume (SAW) na wengi wao ni wafuasi wa Musailima l Kadhab (Mtume wa uongo) na Taliha al Aswad na Sajaaj, na vilipiganwa vita vikali sana na vilivokuwa vikali zaidi ni vita vilivyojulikana kwa jina la ‘Mapambano ya bustanini’ (Maarakatul hadiqah) dhidi ya Musailimah l Kadhab katika mji wa Yamama na Waislamu wakashinda

ushindi mkubwa kabisa.

3- VITA DHIDI YA WALOKATAA KUTOA ZAKA

Waliokataa kutoa Zaka ni wale walikuwa wakidhania kuwa zile pesa za Zaka walizokuwa wakimpa Mtume (SAW) kuwa ni kodi na kwamba baada ya kufa kwa Mtume (SAW) hapana haja tena ya kuilipa kodi hiyo.

Imetolewa na Bukhari kutoka kwa Abu Hurairah (RA) kuwa amesema:

“Alipofariki Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) na Abubakar akawa khalifa walikufuru waliokufuru katika waarabu na Omar (RA) akasema (kumwambia Abubakar): Vipi tutapigana vita na watu wanaoitamka shahada ya laa ilaaha illa Llah wakati Mtume (SAW) alisema: ‘Nimeamrishwa nipambane na watu mpaka watamke Laa ilaaha illa Llah, na atakayeitamka itahifadhika kwangu mali yake na nafsi yake na hesabu yake iko kwa Mwenyezi Mungu?

Abubakar(RA) akasema;

"Wallahi nitapambana na kila anayefarikisha baina ya Sala na Zaka kwa sababu Zaka ni katika haki ya mali. Wallahi kama watakataa kunipa mbuzi mdogo waliyekuwa wakimpa Mtume (SAW) ningepigana nao kwa kukataa kwao huko”.

Sahih Bukhari kitabu cha Zaka mlango wa ‘Kuwajibika kwa Zaka’ hadithi nambari 1399

 

KUTEKWA KWA MIJI YA UAJEMI (IRAN)

Abubakar alipeleka majeshi yake katika nchi ya Uajemi (Iran) yakiongozwa na Al Muthanna bin Al Haritha, kisha akampeleka Khalid bin Walid na akamfuatilia na Al Qaa qaa bin Amru Al Tamimi.

 

KUTEKWA KWA MIJI YA SHAM

Abubakar alimchaguwa Khalid bin Said bin Al Aas kuwa mkuu wa majeshi yake aliyoyapeleka katika nchi ya Sham, akapambana na majeshi ya Warumi na alipotaka msaada kutoka kwa Abubakar, akampeleka Al Walid bin Utbah na Ikrimah bin Abu Jahal na Amru bin Al Aas na Abu Ubayda Amir bin Al Jarah na yeye ndiye aliyechukuwa uongozi wa majeshi baadaye.

Yakasonga mbele majeshi ya Waislamu mpaka yakaweza kuuteka mji wa Yarmuk, kisha Abubakar akampeleka huko Khalid bin Walid na Mwenyezi Mungu akawapa ushindi.

 ITAENDELEA INSHAALLAH