HISTORIA FUPI YA AL KAABA

Muhammad Faraj Salem Al Saaiy

 

Anawasili Misri 1

Anarudi kwao. 1

Anawasili Makka. 2

Amchinje mwanawe. 3

Kisima cha Zamzam.. 4

Watu wa Jurhum.. 5

Abadilishe kizingiti 5

Wananyanyua nguzo

Watu wa ndovu

Kuujenga upya

Pesa za halali 13

Kubomolewa na kujengwa

Inajengwa tena. 16

Hitimisho. 16

 

 

Nabii Ibrahim (Alayhis salaam) alizaliwa katika mji unaoitwa Aar uliopo kandokando ya mto wa Furaat (Euphrates) Al Kufa - Iraq.

Inajulikana kuwa Nabii Ibrahim (Alayhis salaam) aliuhama mji huo na kuishi sehemu iliyokuwa ikiitwa Haraan na hatimaye akahamia nchi ya Palastina na huko ndiko alikofanya makao yake ya kuufikisha ujumbe alopewa na Mola wake.

Rudi juu

Nabi Ibrahim (Alayhis salaam) anawasili Misri

Nabii Ibrahim (Alayhis salaam) akifuatana na mkewe alikwenda kutembelea nchi ya Misri, na huko alipokelewa na mfalme wa Misri aliyewaweka ndani ya qasri yake, na usiku ulipoingia mfalme huyo alijaribu kumdhuru Bibi Sarah mke wa Nabii Ibrahim (Alayhis salaam), lakini Mwenyezi Mungu alimkinga bibi huyo na shari hiyo kwa kuufanya mkono wa mfalme upooze kila anapojaribu kumsogelea.

Alipoona dalili za qudra ya Mwenyezi Mungu zikimlinda bibi huyo, mfalme akaacha vitimbi vyake na kuamua kumpa Bibi Sarah zawadi, na zawadi hiyo ni binti yake aitwae Hajarah, na Sarah akaikubali zawadi hiyo na akamuozesha binti huyo mumewe Ibrahim (Alayhis salaam).

 

Anarudi kwao

Ibrahim (Alayhis salaam) akarudi kwao akiwa amefuatana na wake zake wawili, Bibi Sarah na Bibi Hajarah, na kutokana na mke mpya, Mwenyezi Mungu alimruzuku mtoto wa kiume waliyempa jina la Ismail, jambo lililomfanya Bibi Sarah awe na wivu mkubwa juu ya mke mwenzake, na baada ya kuamrishwa na Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala, Nabii Ibrahim akamchukuwa Bibi Hajarah pamoja na mwanawe Ismail aliyekuwa bado mchanga wakati huo, na kufunga nao safari ndefu kutoka Palastina hadi nchi ya Hijazi (Saudia hivi sasa).

Rudi juu

Anawasili Makka

Alipowasili Makkah penye bonde baina ya Safa na Marwa mahali kilipo kisima cha maji ya zamzam hivi sasa, na wakati huo nyumba ya Mwenyezi Mungu (Al Kaaba) ilikuwa ni sehemu iliyonyanyuka tu juu ya ardhi, ikishambuliwa na upepo mkali pamoja na mikondo ya maji ya mvua iliyokuwa ikizikwanguwa pembe nne za nyumba hiyo.

Hapakuwa na mtu anayeishi mahali hapo wala nyumba wala maji isipokuwa mti mmoja alipowaacha mkewe na mwanawe chini yake, akawawekea birika la maji pamoja na chombo alichowatilia tende ndani yake, kisha akageuka na kuianza safari ndefu ya kurudi Palastina.

Mama yake Ismail alipomuona mumewe akirudi na kuwaacha mahali hapo walipopafikia baada ya safari ndefu iliyowachukuwa siku nyingi njiani, mahali pasipo na mji wala kijiji. Hapakuwa na hata dalili ya kuwepo mtu mahali popote karibu na hapo, akamfuata mumewe na kumuuliza:

Unatuachia nani mahali hapa pasipo na mtu yeyote?

Akamuuliza hivyo mara nyingi lakini Nabii Ibrahim (Alayhis salaam) hakumjibu.

Mwisho Mama yake Ismail akamuuliza:

Mwenyezi Mungu ndiye Aliyekuamrisha?

Nabii Ibrahim akamjibu:

Naam, ndiyo.

Kwa imani iliyothibiti, kwa utiifu mkubwa na kwa moyo uliosalimu amri, Bibi Hajarah akamwambia:

Kwa hivyo Hatotupoteza.

Rudi juu

Hapo ndipo Nabii Ibrahim (Alayhis salaam) alipogeuka na kuianza safari ndefu ya kurudi Sham akimuacha nyuma mkewe na mwanawe wa mwanzo na wa pekee wakati ule, na baada ya kutembea muda kidogo mahali ambapo mkewe hakuweza kumuona, Nabi Ibrahim (Alayhis salaam) akageuka nyuma na kuomba dua ifuatayo:

Mola wetu! Hakika mimi nimewaweka (nimewakalisha baadhi ya kizazi changu (mwanangu Ismaili na mama yake Hajarah) katika bonde (hili la Makkah) lisilokuwa na mimea yoyote; katika nyumba yako takatifu (ya Al Kaaba utakayotwambia tuijenge).

Mola wetu! Wajaalie wasimamishe Sala. Na ujaalie nyoyo za watu zieleke kwao (wapende kuja kukaa hapa ili pawe mji) na uwaruzuku matunda ili wapate kushukuru.

Ibrahim 37

 

Anaamrishwa amchinje mwanawe

Nabii Ibrahim alikuwa mara kwa mara akija Makkah kuwazuru mkewe na mwanawe na hapana anayejuwa uhakika wa idadi ya ziara hizo, isipokuwa wanahistoria wameelezea juu ya ziara nne maarufu.

Ya mwanzo ni pale alipooteshwa kumchinja mwanawe wa pekee Ismail (Alayhis salaam) na mwanawe akakubali kutii amri hiyo, na alipomlaza mwanawe kifudifudi ili asiuone uso wake asije akamuonea huruma, na baada ya Ismail (Alayhis salaam) kutoa shahada, na Ibrahim kusalimu amri kwa Mwenyezi Mungu huku akijitayarisha kumchinja mwanawe, Mwenyezi Mungu akamfunulia Nabii Ibrahim (Alayhis salaam) kuwa asimchinje mwanawe na badala yake akamkomboa kwa kondoo.

Kisa hicho kimeelezwa ndani ya kitabu cha Mwenyezi Mungu Aliposema:

. . . .

Basi wote wawili walipojisalimisha (kwa Mwenyezi Mungu), na akamlaza kifudifudi (amchinje).

Pale pale tulimwita; Ewe Ibrahim; Umekwishasadikisha ndoto. (Usimchinje mwanao). Kwa yakini hivi ndivyo tunavyowalipa watendao mema.

Bila shaka (jambo) hili ni jaribio lililo dhahiri, (mtihani ulio dhahiri).

Basi tukamkomboa kwa mnyama wa kuchinjwa mtukufu,

As Saaffaat 103-107

Rudi juu

Mama yake Ismail na kisima cha Zamzam

Bibi Hajarah (Mama yake Ismail) akawa anakula zile tende alizowekewa na mumewe huku akimnyonyesha mwanawe, lakini haukupita muda mrefu maji yakaanza kupunguwa na hatimaye kumalizika, na mwanawe alipoanza kuona kiu, Bibi Hajarah akaanza kuhangaika huku na kule akimtafutia maji.

Akaliendea jabali lililokuwa karibu yake - Jabal Safa na kulipanda, na alipofika kileleni akaanza kutizama huku na kule akitafuta maji au msafara wa watu watakaokuwa na maji, lakini hakuona kitu.

Akateremka na kuanza kutembea taratibu penye bonde lililopo baina ya jabali Safa na jabali Marwa, na alipofika kati kati ya bonde akaanza kukazana huku akiliendea jabali Marwa na kulipanda, na alipofika kileleni akaanza kutizama huku na kule, lakini bila mafanikio yoyote.

Anasema Ibni Abbas (Radhiya Llahu anhu) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wasallam)) amesema:

Hiyo ndiyo Saayi mnayotembea baina ya Safa na Marwa.

 

Bibni Hajarah aliendelea kufanya hivyo mara saba, na alipokuwa akiliendea jabali Marwa akasikia sauti ngeni ikimsemesha. Alinyamaza kimya ili aisikie vizuri huku akitazama mahali alipo mwanawe, akamuona Malaika amesimama mahali kilipo kisima cha Zamzam hivi sasa, huku akichimba kwa ubawa wake mpaka maji yalipofurika, ndipo mamake Ismail alipoyaendea na kuanza kuyachota kwa mikono yake huku akimnywesha mwanawe na kunywa yeye mwenyewe.

Alipokuwa akinywa na kumnywesha mwanawe, Malaika akamwambia:

Usiogope - hutopotea, kwani hapa ndipo ilipo nyumba ya Mwenyezi Mungu itakayojengwa na mtoto huyu na baba yake."

Rudi juu

Watu wa kabila la Jurhum

Hazikupita siku nyingi na mama yake Ismail akajiwa na msafara wa watu wa kabila la Jurhum ambao asili yao ni kutoka Yemen waliokuwa wasafiri waliopiga kambi sehemu ya chini ya mji wa Makkah mbali na hapo, na walikuja baada ya kuwaona ndege wakiruka sehemu aliyopo mama yake Ismail wakasema:

Bila shaka ndege hawa wameona maji, na kwa vile inajulikana kuwa sehemu zile si kawaida kupatikana maji, wakaamua kutuma watumishi wakachunguze sehemu walipoonekana ndege, na walipokiona kisima cha maji ya Zamzam wakarudi kuwajulisha wenzao walioamua kukiendea haraka sana, lakini walipomuona mama yake Ismail na mwanawe wakamuomba wakae naye wakamwambia:

Utaturuhusu tukae pamoja na wewe mahali hapa?

Mama yake Ismail akawaambia:

Nitakuruhusuni, lakini maji haya ni yangu.

Wakasema:

Tumekubali.

Anasema Ibni Abbas (Radhiya Llahu anhu) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wasallam)) amesema:

Jambo hilo lilimfurahisha sana mama yake Ismail, kwani alikuwa mwenye kupenda watu.

 

Mwambie abadilishe kizingiti

Watu wa kabila la Jurhum wakateremka na kuazisha maisha mepya mahali hapo, na Nabii Ismail (Alayhis salaam) akaishi pamoja nao, akajifundisha kwao lugha ya kiarabu, akajifundisha kuwinda, na alipokuwa mkubwa wakamuozesha mmoja katika binti zao.

Baada ya kuishi muda aloishi, mama yake Ismail akafariki dunia na Ismail akaendelea kuishi mahali hapo pamoja na watu wa kabila hilo la Jurhum.

Nabii Ibrahim alikuja kumtembelea mwanawe katika ziara yake ya pili lakini bahati mbaya hajamkuta nyumbani na badala yake alimkuta mkewe, na alipomuuliza mahali alipo Ismail akamwambia:

Ametoka kwenda kututafutia rizki.

Nabi Ibrahim akamuuliza juu ya hali zao na mwanamke akamjibu:

Sisi ni wanadamu na hali zetu ni za dhiki na shida.

Akaendela kumshitakia hali zao, na Nabi Ibrahim alipoondoka kurudi nchi ya Palastina akamwambia:

Akirudi mumeo msalimie kisha mwambie abadilishe kizingiti cha nyumba.

Aliporudi Nabii Ismail (Alayhis salaam) alihisi kuwa jambo fulani limetokea nyumbani kwake, akamuuliza mkewe:

Alikuja mtu hapa?

Mkewe akajibu:

Ndiyo, alikuja mzee mmoja na wasfu wake ni hivi na hivi, akauliza juu yako na mimi nikamwambia ulipo, akaniuliza juu ya hali zetu, nikamwambia kuwa sisi ni wanadamu na kwamba hali zetu ni za dhiki na shida.

Akamuuliza:

Alikuusia jambo lolote?

Akajibu:

Ndiyo, alinambia ukija nikusalimie kisha nikwambie ubadilishe kizingiti cha nyumba.

Akamwambia:

Yule alikuwa baba yangu na ameniamrisha nifarikiane na wewe, kwa hivyo rudi kwa wazee wako.

Rudi juu

Baada ya kumtaliki mkewe wa mwanzo, Nabii Ismail (Alayhis salaam) akaoa mke mwingine, na inasemekana kuwa alikuwa binti wa Mudhaadh bin Amru aliyekuwa Sheikh wa kabila la Jurhum.

Nabii Ibrahim (Alayhis salaam) akaja tena kumtembelea mwanawe katika ziara ya tatu, na safari hii hajamkuta pia, na alipomuuliza mkewe akamwambia:

Amekwenda kutuletea mahitaji yetu. Na Ismail alikuwa mwindaji anayesafiri mara kwa mara sehemu za mbali kwa ajili ya kazi yake hiyo na huchukuwa muda mrefu safarini.

Nabii Ibrahim (Alayhis salaam) akamuuliza:

Vipi hali zenu?

Akajibu:

Tumesitirika alhamdulillah tumo katika kheri kubwa.

Akawa anasema hivyo huku akimshukuru Mwenyezi Mungu.

Nabii Ibrahim akamuuliza:

Mnakula chakula gani?

Akajibu:

Nyama.

Akamuuliza:

Mnakunywa nini?

Akajibu:

Maji.

Akamwambia:

Mola wangu vibariki nyama na maji.

Anasema Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wasallam): Siku hiyo hawakuwa na chochote nyumbani kwao.

Nabii Ibrahim akamwambia:

Akirudi mumeo mpe salamu zangu na umwambie akidhibiti vizuri kizingiti cha nyumba yake.

Aliporudi Ismail akauliza:

Alikuja mtu leo?

Akajibu:

Alikuja mzee mmoja mwenye umbo zuri, akataka kujuwa habari zako, nikamjulisha, akaniuliza juu ya hali zetu nikamwambia kuwa tupo katika kheri.

Akamuuliza:

Alikuusia jambo lolote?

Akamwambia:

Ndiyo, yeye anakupa salamu nyingi na anakwambia ukidhibiti vizuri kizingiti cha nyumba yako.

Akamwambia:

Yule alikuwa baba yangu na ananiamrisha nikamatane na wewe.

Rudi juu

Wananyanyua nguzo za Msikiti

Nabii Ibrahim akaja tena katika ziara yake ya nne, na safari hii Ismail alikuwepo nje ya nyumba yake chini ya mti karibu na kisima cha maji ya zamzam akichonga mshale wake, na alipomuona baba yake akamnyanyukia kwa heshima kubwa, akamwamkia kama mtoto anavyoamuamkia baba yake wakakumbatiana kisha Nabii Ibrahim akasema:

Mwenyezi Mungu amenipa amri.

Ismail akamwambia;

Fanya kama ulivyoamrishwa na Mola wako.

Akamwambia:

Na wewe unisaidie.

Akamwambia:

Nitakusaidia.

Akamwambia:

Mwenyezi Mungu ameniamrisha nijenge nyumba mahali hapa..

Akamuonesha ile sehemu ya ardhi iliyoinuka karibu na kisima cha maji ya zamzam, kisha wote kwa pamoja wakaanza kufanya kazi ya kuzinyanyua nguzo za nyumba na kuijenga Al Kaaba, na Ismail akawa anamsogezea baba yake mawe huku Ibrahim akijenga, mpaka nyumba ilipokamilika. Walikuwa wakijenga huku wakiomba dua ifuatayo:

Ewe Mola Wetu! Tutakabalie (tutakabalie amali yetu hii ya kujenga huu msikiti.

Mwenyezi Mungu Anasema:

Na Ibrahimu alipoinua kuta za nyumba (hii ya Al Kaaba) na Ismaili (pia) (wakaomba wakasema) Ewe Mola Wetu! Tutakabalie (tutakabalie amali yetu hii ya kujenga huu msikiti. Hakika wewe ndiye Mwenye kusikia na Mwenye kujua.

Ibrahim 127

Rudi juu

Na kasema:

Ee, Mola Wetu! Waletee Mtume anayetokana na wao awasomee Aya Zako, na kuwafundisha Kitabu (chako) na hikima (nyingine) na awafundishe kujitakasa (na kila mabaya) hakika Wewe ndiye Mwenye, nguvu na ndiye Mwenye hikima.

Al Baqarah-129

 

Na hii ndiyo tafsiri ya hadithi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wasallam)) alipoulizwa juu ya mwanzo wa amri yake akasema:

Mimi ni dua ya baba yangu Ibrahim na bishara ya ndugu yangu Issa alayhimu ssalaam.

 

Anasema Ibni Abbas (Radhiya Llahu anhu) kuwa baada ya kukamilisha ujenzi wa msikiti wa Al Kaaba, Mwenyezi Mungu akamuamrisha Nabii Ibrahim awatangazie watu waje kuhiji, na Nabii Ibrahim akasema:

Ewe Mola wangu vipi itawafikia sauti yangu.

Akamwambia:

Juu yako ni kutangaza tu, na ni juu Yangu kuifikisha, ndipo Nabii Ibrahim alipopanda juu ya kilele cha mojawapo ya milima ya Makkah na kupaza sauti yake akisema:

Enyi watu mumefaridhishiwa Hija katika nyumba kongwe, na tangazo hilo likamfikia kila kiumbe baina ya mbingu na ardhi.

Hamuoni kuwa watu wanauitikia mwito huo kutoka katika kila pembe ya dunia? Na katika riwaya nyingine; Na wa mwanzo kuuitikia mwito huo walikuwa watu wa Yemen."

Rudi juu

Kisa cha Watu wa ndovu (As habul fiyl)

Abraha Mhabeshi aliyekuwa gavana wa Al Najashi katika nchi ya Yemeni iliyokuwa ikitawaliwa na Ethiopia wakati huo alikuwa akiona wivu kila anapowaona waarabu wakifunga safari ndefu kwenda kuizuru Al Kaaba, na kwa ajili hiyo akaamua kujenga kanisa kubwa kati ya mji wa Sana-a (mji mkuu wa Yemen) kisha akawataka waarabu waache kwenda Makkah na badala yake wakahiji penye kanisa lake.

Habari hizo zilimfikia mmoja katika watu wa kabila la bani Kinanah, aliyeamua kuingia kanisani nyakati za usiku na kulipaka mavi, jambo lililomghadhibisha sana Abraha aliyekusanya jeshi kubwa lenye idadi ya askari wanaozidi elfu sitini pamoja na tembo ishirini na mbili na yeye mwenyewe akiwa juu ya tembo mkubwa sana, na kuelekea nalo Makkah kwa ajili ya kuibomoa Al Kaaba.

Alipokaribia Makkah, penye bonde la Muhsir baina ya Muzdalifa na Mina, tembo mkubwa akapiga magoti na kukataa kuendelea na safari. Ikawa kila wanapomuelekeza kusini au kaskazini anainuka na kutembea, lakini wanapomuelekeza upande wa Makkah anakataa na hupiga magoti.

Wakawa katika hali hiyo mpaka pale Mwenyezi Mungu alipowapelekea ndege makundi kwa makundi, wakawapiga kwa mawe ya udongo unaounguza.

Mwenyezi Mungu Anasema:

. . . .

Je! Huoni jinsi Mola wako Alivyowafanya watu wenye ndovu?

Je! Hakujaalia vitimbi vyao kuharibika.

Na akawapelekea ndege makundi kwa makundi

Wakawapiga kwa mawe ya udongo wa kuchoma.

Akawafanya kama majani yaliyoliwa (yakatapikwa)?

Suratul Fiyl

Rudi juu

Ndege walikuwa wakiwajia kwa wingi makundi kwa makundi, mfano wa vijumba mshale au zuwarde, kila mmoja akiwa amebeba mawe matatu yenye ukubwa kiasi cha dengu, moja mdomoni na mawili ameyabana mguuni, na kila anayepigwa na jiwe mwili wake hukatika vipande vipande na kufa.

Si wote waliopigwa na mawe hayo, walikuwemo wachache walioachwa wakarudi mbio kuelekea makwao huku wakiangukiana. Ama Abraha, Mwenyezi Mungu alimsalitishia maradhi yaliyosababisha makucha yake kukatika na kupukutika huku akirudi alikotoka, na alifariki alipowasili mji wa Sana-a mwili wake ukiwa mfano wa kuku aliyenyonyoka manyoa.

Makureshi, wao walikimbilia sehemu mbali mbali mbondeni na juu ya vilele vya majabali wakihofia maisha yao, na hawakurudi majumbani mwao mpaka baada ya kumalizika yaliyotokea.

Tukio hili lilitokea mwezi wa Muharram kabla ya kuzaliwa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wasallam) kwa siku hamsini au hamsini na tano takriban muwafaka wa mwisho wa mwezi February au mwanzo wa mwezi wa March mwaka 571 baada ya Nabii Issa.

 

Katika tafsiri ya Suratul Fyl anasema Ibni Kathiyr;

Hii ni mojawapo ya neema za Mwenyezi Mungu walizopewa Makureshi baada ya kuwalinda na shari walokuja nayo watu wa ndovu waliokuja wakiwa na azma ya kuibomoa Al Kaaba na kuiondoa ili isiwepo tena. Lakini Mwenyezi Mungu aliwaangamiza na kuwalazimisha waliobaki warudi wakiwa wameshindwa juu ya kuwa walikuwa watu wanaofuata dini ya Manasara na kwa wakati ule wao walikuwa bora kuliko Makureshi waliokuwa wakiabudu Masanamu, lakini haya yalikuwa ni matayarisho ya kuja kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wasallam), kwa sababu kauli nyingi zinasema kuwa katika mwaka ule alizaliwa.

Kama kwamba uhakika wa mambo unasema; Enyi Makureshi hamkupata nusura hii juu ya Mahabeshi kutokana na ubora wenu, bali kwa ajili ya kuilinda nyumba kongwe itakayopata heshima kwa kuzaliwa hivi karibuni kwa Mtume wa Mwenyzi Mungu, Muhammad (Swalla Llahu alayhi wasallam) mwisho wa Manabii."

 

Habari za tukio hili zilienea kila pembe ya ulimwengu wa wakati ule, na kwa vile Wahabeshi walikuwa na uhusiano mzuri na Warumi, Waajemi waliokuwa wakingoja fursa nzuri kama hii wakaingia na kuiteka nchi ya Yemen kwa haraka sana, na dola mbili hizi (Uajemi na Roma) ndizo zilizokuwa dola kubwa za wakati ule, na wakati huo huo tukio hili la kuangamizwa kwa watu wa ndovu liliujulisha ulimwengu juu ya utukufu wa nyumba ile ya Mwenyezi Mungu na kwamba Mwenyezi Mungu ndiye aliyeitukuza na kuiadhimisha, na kwa ajili hiyo atakapotokea yeyote katika watu wake akasema kuwa yeye ni Mtume, basi tukio hilo linampa nguvu mtu huyo.

Kwa hivyo ndani ya tukio hili mna hekima iliyojificha ya Mwenyezi Mungu ya kuwapa ushindi washirikina dhidi ya watu wa imani kwa njia ya kimiujiza.

Rudi juu

Kuijenga upya Al Kaaba

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wasallam) alikuwa na umri wa miaka thelathini na tano wakati Makureshi walipoujenga upya msikiti wa Al Kaaba, kwa sababu miaka mingi ilikwishapita tokea Nabi Ismail alipoujenga na hapakuwa na kilichobaki katika jengo hilo isipokuwa rundu la udongo lenye urefu wa kiasi cha dhiraa sita, bila ya kipaa, jambo lililowarahisishia wezi kuingia ndani na kuiba hazina zinazowekwa humo.

Na kwa vile miaka mingi ilikwishapita tokea kujengwa kwake, kanuni za maumbile zilikwishafanya kazi yake. Kuta zilikuwa na nyufa, na miaka mitano kabla ya kupewa utume (Swalla Llahu alayhi wasallam) yalitokea mafuriko makubwa yaliyosababisha maji kuingia ndani ya msikiti na kubomoa sehemu kubwa za msikiti huo, na kwa ajili ya yote hayo Makureshi wakaamua kuujenga tena msikiti huo.

 

Wakakubaliana kuwa zisiingizwe katika ujenzi wa jengo hilo pesa zozote za haramu. Zisiingizwe pesa za mahari ya mzinzi, wala pesa za riba, wala pesa alizodhulumiwa mtu nk.

Walikuwa wakiogopa kuubomoa msikiti na kuanza kuujenga upya wasije wakadhurika, mpaka alipotangulia Al Walid bin Mughiyrah na kuianza yeye kazi hiyo, na wenzake walipoona kuwa hapana kilichomsibu, ndipo nao wakaingia kazini. Wakawa wanaendelea kuubomoa mpaka walipozifikia nguzo zilizosimamishwa na Nabii Ibrahim (Alayhis salaam), kisha wakaanza kuujenga upya msikiti huo, na kila kabila likapewa sehemu yake ya kujenga, na kila kabila lilikuwa likikusanya mawe yake ya ujenzi, na msimamiaji wa ujenzi alikuwa Mrumi aitwae Baqum.

Kazi ilikwenda vizuri mpaka ulipofika wakati wa kulirudisha jiwe jeusi mahali pake, ndipo mzozo ulipoanza kila kabila likataka kupewa heshima hiyo ya kulirudisha mahali pake.

 

Mgogoro uliendelea muda wa siku nne au tano na mambo yakawa magumu hata watu wakakaribia kutaka kupigana vita, panga mkononi mpaka pale Abu Umayyah bin Mughiyra Al Makhzumiy alipotoa rai kuwa; wa mwanzo kuingia msikitini kupitia mlangoni ndiye atakayeamua baina yao, na wote wakaridhika na rai hiyo.

Mwenyezi Mungu akataka Mtume wake (Swalla Llahu alayhi wasallam)) awe mtu huyo, na walipomuona tu akiingia, wote kwa pamoja wakapiga ukulele wa kuridhika:

"Huyu Muaminifu! Sote tumeridhika naye, huyu Muhammad."

Alipojulishwa juu ya uamuzi huo, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wasallam) (hii ilikuwa kabla ya kupewa utume) alikubali, na kwa utulivu akaomba kiletwe kitambaa, akakitandaza na kuliweka jiwe jeusi juu yake, kisha akawataka viongozi wa makabila yote kila mmoja akamate upande wa kitambaa, kisha wanyanyuwe kwa pamoja. Wakalinyanyua na walipopafikia mahali pa kuliweka, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wasallam)) akalinyanyua yeye kwa mikono yake miwili na kulirudisha mahali pake.

Kwa njia hii Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wasallam) aliweza kulitatua tatizo lililokaribia kuleta umwagaji wa damu mkubwa baina ya Makabila ya Kikureshi, na kila mmoja aliondoka hapo akiwa ameridhika.

Rudi juu

Wanaishiwa na pesa za halali

Makureshi walishindwa kuukamilisha msikiti baada ya kuishiwa na pesa za halali, wakaamua kupunguza kiasi cha dhiraa sita upande wa kaskazini mwa Al Kaaba na hii ni ile sehemu inayojulikana kwa jina la Al Hijr (Hijr Ismail) wakashindwa kuunganisha msikiti pamoja na Hijri Ismail ambayo asili yake ilikuwa imekamatana na msikiti. Wakaunyanyua mlango kiasi cha dhiraa mbili kutoka juu ya ardhi asiweze kuingia isipokuwa wanayemtaka wao tu, na urefu wa jengo ulipotimia kiasi cha dhiraa kumi na tano wakaezeka sakafu juu ya nguzo sita, na baada ya kumalizika kazi hiyo, Al Kaaba ikawa na umbo la mraba lenye urefu wa mita kumi na tano, na upande wa jiwe jeusi pamoja na upande wa pili yake (mkabala wake) pande zote mbili kila moja ilikuwa na urefu wa mita kumi.

Na jiwe jeusi liliwekwa juu kiasi cha urefu wa mita unusu kutoka juu ya ardhi, na upande wa mlango na upande wa mkabala wake ukawa na urefu wa mita kumi kila upande, na mlango ukanyanyuliwa kiasi cha mita mbili kutoka juu ya ardhi, na upande wa nje ya Al Kaaba ikaachwa ikiwa imezungukwa na msingi ulionyanyuka kutoka juu ya ardhi kiasi cha robo mita na upana wa kiasi cha nusu mita.

Na sehemu hii ilikuwa ikiitwa Ash Shadherwan, sehemu ambayo asili yake ilikuwa ndani ya jengo la Al Kaaba, lakini Makureshi iliwabidi waiache sehemu hii bila kuijenga, na kwa ajili hiyo msikiti ukawa na umbo la mraba badala ya umbo lake la asili lililofanana na herufi D iwapo utaunganishwa na Hijr kama ulivyojengwa na Nabi Ibrahim (Alayhis salaam).

Rudi juu

Mara ngapi umebomolewa na kujengwa upya?

Inajulikana kuwa Msikiti wa Al Kaaba umejengwa kwa mara ya mwanzo na Nabi Ibrahim (Alayhis salaam).

Mwenyezi Mungu Anasema:

Na Ibrahimu alipoinua kuta za nyumba (hii ya Al Kaaba) na Ismaili (pia) (wakaomba wakasema) Ewe Mola Wetu! Tutakabalie (tutakabalie amali yetu hii ya kujenga huu msikiti). Hakika wewe ndiye Mwenye kusikia na Mwenye kujua.

Ibrahim 127

 

Imesimuliwa na Imam Muslim katika Sahihi yake na pia ndani ya vitabu vyengine mbali mbali vya elimu ya hadithi na vya sira katika mlango ya 'Kubomolewa na kujengwa upya msikiti wa Al Kaaba' kama ifuatavyo:-

Sehemu kubwa ya msikiti iliungua wakati Al Hajjaj alipoushambulia akitumia 'Manjaniq' (mtambo wa kutupa mawe uliokuwa ukitumika katika vitani vya zamani) akitaka kumuuwa Abdullah bin Al Zubair bin Awaam (Radhiya Llahu anhu) na hii ilikuwa wakati wa utawala wa Yazid bin Muawiyah.

Mwana wa Al Zubair (Radhiya Llahu anhu) aliuacha msikiti kama ulivyo mpaka ulipoingia msimu wa Hija wa mwaka ule na watu wakawa wengi, akawakusanya na kuwahutubia, akasema:

"Enyi watu! Nataka ushauri wenu juu ya Al Kaaba. Niuvunje msikiti wote kisha niujenge upya au nitengeneze tu sehemu zilizoungua?"

Ibni Abbas (Radhiya Llahu anhu) akasema:

"Mimi ninayo rai, naona ni bora usiubomoe, bali utengeneze tu na uiache kama ilivyo nyumba waliosilimu watu juu yake, na mawe waliosilimu watu juu yake, na alitumwa kwa ajili yake nyumba hiyo Mtume (Swalla Llahu alayhi wasallam)."

Mwana wa Al Zubair (Radhiya Llahu anhu) akasema:

"Mmoja wenu ikiungua nyumba yake hatoridhika kuiacha ilivyo (bila shaka atapenda kuijenga upya), vipi basi nyumba ya Mola wenu? Mimi nitaswali Istikhara mara tatu kisha nitaamua."

Na baada ya kukamilisha tatu akaamua kuubomoa, lakini kila mmoja aliogopa kupanda na kuianza kazi hiyo asije akadhurika, mpaka alipopanda mtu mmoja na kunyanyua jiwe, akalitupa chini, na watu walipomuona hajadhurika wakaingia na wao kazini na kuianza kazi ya kuubomoa msikiti mpaka walipozifikia nguzo, kisha mwana wa Al Zubair (Radhiya Llahu anhu) akazinyanyua nguzo na kuujenga upya, na alipomaliza akaishonea Al Kaaba pazia, akaujenga msikiti kama ulivyokuwa wakati wa Nabi Ibrahim (Alayhis salaam) kisha akasema:

"Nilimsikia khale yangu (Bibi Aisha (Radhiya Llahu anha) akisema kuwa amemsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wasallam)) akisema:

"Ingelikuwa watu hawakutoka hivi karibuni tu katika ujahilia na ningelikuwa na pesa za kutosha kuujenga vizuri msikiti, ningeongeza dhiraa tano na kuuganisha na Hijri (Ismail) kisha nikajaalia mlango kwa ajili ya watu kuingia ndani yake na mlango wa kutokea."

Na katika riwaya nyingine:

"Makureshi walipoijenga nyumba walishindwa kuikamilisha kwa sababu waliishiwa na pesa."

Na katika riwaya nyengine kupitia kwa Abdullah bin Abubakar (Radhiya Llahu anhu) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wasallam)) alisema:

"Na ningejenga milango miwili, mmoja mashariki na mmoja magharibi ikawa juu ya ardhi kisha ningeunganisha msikiti na Hijri Ismail."

Akasema Abdullahi bin Zubair (Radhiya Llahu anhu):

"Mimi leo ninazo pesa na siwaogopei watu."

Akaongeza dhiraa tano na akajenga milango miwili, mmoja kwa ajili ya watu kuingia na mwengine wa kutokea.

Rudi juu

Inajengwa tena

Alipouliwa Abdullahi bin Al Zubeir (Radhiya Llahu anhu), Al Hajjaj akamuandikia Abdul Malik bin Marawan aliyekuwa Khalifa wa Waislamu wakati huo na kumjulisha juu ya mabadiliko aliyofanya mwana wa Al Zubair katika msikiti, na Abdul Malik akamjibu:

"Urefu alouongeza mwana wa Al Zubair uache na sehemu aloongeza katika Hijri ibomowe na milango aloiongeza izibe."

Al Hajjaj akafanya kama alivyoambiwa.

 

Hitimisho

Riwaya zinazokubalika zilizopokewa na maulamaa zinasema kuwa msikiti umejengwa mara nne.

Ya kwanza ulipojengwa na Nabi Ibrahim (Alayhis salaam).

Ya pili wakati wa ujahilia kabla ya Uislamu, na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wasallam)) alishiriki katika ujenzi huo na wakati huo alikuwa na umri wa miaka thelathini na tano na katika riwaya nyingine alikuwa na umri wa miaka ishirini na tano.

Ya tatu ulipojengwa na mwana wa Al Zubair (Radhiya Llahu anhu).

Ya nne ulipojengwa tena na Al Hajjaj baada ya kupewa amri na Abdul Malik bin Marawan ya kubomoa zile sehemu zilizoongezwa na mwana wa Al Zubair (Radhiya Llahu anhu).

 

Imepokelewa pia kuwa Harun Al Rashid alitaka ushauri wa kuujenga upya msikiti huo na kuzirudisha zile sehemu zilizojengwa na Abdullah mwana wa Zubair (Radhiya Llahu anhu), lakini Imam Malik akamnasihi kwa kumwambia:

"Kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ewe amiri wa Waisalamu, tafadhali iache nyumba kama ilivyo, na usiifanye ikawa mchezo kwa wafalme, kila mmoja akaja kubomoa na kuujenga upya atakavyo, na mwisho wake haiba ya nyumba itaondoka ndani ya vifua vya watu."

 

Wassalaam alaykum wa Rahmatullahi wa Barakatuh

Ndugu yenu

Muhammad Faraj

 

Rudi juu