HUKUMU ZA MSIKITI

Sameer kutoka Yemen

        Shukurani njema zinamstahikia Mwenyezi Mungu aliyeujaalia Msikiti kuwa ni nyumba tukufu hapa ulimwenguni,na sala na amani zimfikie Mtume wetu Muhammad pamoja na jamaa zake na masahaba zake na kila mwenye kushikamana na misikiti.

         Ninachukuwa fursa hii kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu kujaribu kuelezea hukumu za Msikiti ambazo tunahitajika waislam kuzifahamu ,na hii inatokana kuwa nafasi ya Msikiti kwetu ni kubwa mno tofauti na wanavyofahamu baadhi ya watu kuwa Msikiti ni kama sehemu ya kukusanyika waislam kwa ajili ya kutekeleza ibada ya sala tu.

         Msikiti ni kituo kamili cha kuwakusanya waislam katika kufanikisha mambo yao yote ya kilimwengu na tukiangalia historia ya Uislam tutakuta kuwa Msikiti,  Mtume (S.A.W) ulikuwa ni makutano ya waislam kila penye haja ya kufanya hivyo,bali ilifikia hadi Msikiti kuwa ni sehemu pia ya kupanga na kupangua namna ya kukabiliana na Makafiri wakati wa vita .

          Hivyo kutokana na umuhimu huo tumeonelea ni busara kuziangalia hukumu zinazoambatana na misikiti ili tuweze kufaidika na nyumba hii tukufu ,na tuweze kujiepusha na makatazo kwayo.

Maana ya msikiti

         Maana ya Msikiti kilugha ni kila sehemu inayosujudiwa, ama katika sheria Msikiti ni sehemu yoyote ya ardhi iliyokusudiwa na mwenyewe kwa ajili ya kuwa Msikiti (kusaliwa)pamoja na kuiweka wakfu sehemu hiyo, yaani ili sehemu ya ardhi iitwe Msikiti na kuchukuwa hukumu za Msikiti basi ni lazima mmiliki wa ardhi hiyo atamke kuwa sehemu hiyo ni wakfu kwa ajili ya msikti na lengo ni kuweza kuutumia kila muumini kwa kusali na kuweza kusaliwa sala za Jamaa.

Hii ndio maana ambayo huzungumzwa katika vitabu vyetu, pia kuna hali nyengine ambazo ardhi huwa ni Msikiti lakini.

        Zimekuja hadithi za Mtume zinazotufahamisha kuwa kila sehemu ya ardhi inafaa kuwa Msikiti, imepokelewa na sahaba Jabir (RA) kuwa, amesema Mtume (S.A.W) " Imejaaliwa sehemu ya ardhi ni Msikiti kwangu (na kwa umma wangu), na kuwa ni safi."

        Yaani sehemu yoyote katika ardhi basi inaweza ikawa ni Msikiti bali muislam akiwa safirini na akataka kusali ,basi anaweza akasali popote pale, muhimu pawe ni pasafi kutokana na najisi, ama katika baadhi ya umma zilizotangulia wao walikuwa hawawezi kutekeleza ibada zao isipokuwa wakiwepo katika sehemu maalumu, pia imejaaliwa sehemu yote ya ardhi kuwa ni safi kwa anayetaka kutayammam akiwa amekosa maji ya kutawadha.

        Hadithi hii ina mafunzo mengi ,na moja kati ya hayo ni kuwa Muislam hatakiwi kuacha sala kwa hali yoyote ile, wala hana kisingizio kwa kusema hana maji ya kujitoharisha au hawezi kusali mpaka afike Msikitini ,hata hivyo nafasi ya Msikiti itabakia kuwepo na ni bora kwa anayeweza kufika Msikitini akafanya ibada zake humo kuliko kusali popote tu, na bila ya shaka atakayekuwa na ufahamu huu wa kukataa kwenda Msikitini basi amekwenda kombo wala hajafahamu hasa lengo la Mtume (S.A.W).

Msikiti wa mwanzo kujengwa duniani.

        Msikiti wa mwanzo kujengwa duniani ni Msikiti wa Makka (Al-Qaba) kama alivyosema Mwenyezi Mungu katika Qura-an "Hakika Msikiti wa kwanza kuwekwa kwa watu (duniani ) ni Msikiti wa Makka " (Al-Imran  3: 96)

         Na imepokewa hadithi kutoka kwa sahaba Abi Dharri radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake amesema: "Nilimuuliza Mtume (S.A.W) ni Msikiti gani wa mwanzo uliojengwa duniani ? ,akanijibu ni Msikiti wa Makka, nikamuuliza kisha upi ,akasema kisha ukajengwa Msikiti wa Aksa (uliopo Palestina )…."Hadithi imepokewa na Imam Bukhari na Muslim.

         Kutokana na mapokezi hayo inatubainikia kuwa Msikiti wa Makka (Al-Qaba tukufu) ndio Msikiti wa mwanzo kujengwa duniani, na aliyeujenga Msikiti huo ni Nabii Ibrahim rehema na amani juu yake, kisha ukajengwa Msikiti wa Al-Aqsa  na mjukuu wake Nabii Yaakub bin Is-hak bin Ibrahim, ama Nabii Suleiman yeye hakuujenga kwa maana ya kuasisi  bali yeye aliufanyia matengenezo upya.

Fadhila za kujenga Msikiti

         Kwa kuwa Msikiti ni nyumba ya Mwenyezi Mungu, na kutokana na utukufu wake kwa waumini basi kuna fadhila kubwa kwa mwenye kujenga msikiti. Kuna mapokezi mengi yamepokewa kutoka kwa Mtume S.A.W kuelezea fadhila za mwenye kujenga Msikiti, na muhimu kati ya hadithi hizo ni ile iliyopokewa kutoka kwa sahaba Syd Uthman bin Affan (RA) (khalifa wa Tatu wa Mtume (S.A.W). Imepokewa kuwa wakati Sahaba Uthman alipotaka kuutanua Msikiti wa Mtume (S.A.W) baadhi ya watu walikataa kuungana nae juu ya fikra hii na  kutaka Msikiti wa Mtume uwachwe kama ulivyokuwa, akawajibu kuwa "Nimemsikia Mtume S.A.W akisema mwenye kujenga Msikiti kwa ajili ya Mwenyezi Mungu basi Mwenyezi Mungu atamjengea mtu huyo nyumba peponi ." (Bukhari na Muslim).

        Na imepokewa kutoka kwa sahaba Uthman tena kuwa amemsikia Mtume (S.A.W) akisema "Mwenye kujenga Msikiti, MwenyeziMungu atamjengea mtu huyo nyumba peponi mfano wake ( Msikiti alioujenga )". (Muslim).

        Kutokana na hadithi hizi inatosha kufahamu umuhimu wa kujenga Msikiti kwani kila mmoja wetu anahitaji kuingia peponi ,na kila mmoja anajitahidi kufanya ibada ili aweze kuingia humo ,lakini kwa yule anayejenga Msikiti basi tayari ameshahadiwa kuwa atajengewa nyumba yake peponi ,hivyo ni ishara tosha kuwa mtu huyo ataingia peponi.

        Na wanavyuoni katika kufasiri hadithi hii ya pili pale Mtume (S.A.W) aliposema :atajengewa nyumba mfano wake, maana yake ni kwamba atajengewa nyumba peponi ambayo utukufu wake humo peponi utakuwa ni sawa na utukufu wa Msikiti huku duniani, na kama tulivyotanguliza kusema kuwa Msikiti ni nyumba tukufu duniani kuliko nyumba nyengine yoyote ile na hili halina shaka, na wako waliosema kuwa atajengewa kutokana na thawabu zake za kujenga Msikiti jengo kubwa tukufu la kifakhari humo peponi.

           Pia Mtume (SAW) hakuwahimza watu wajenge misikiti tu, bali yeye ndiye wa mwanzo kuonyesha mfano katika suala hili, na haya tunayapata pale Mtume (S.A.W) alipowasili Madina kwa mara ya kwanza kutoka Makka (Hijra), na alipofika tu jambo la kwanza aliamrisha ujengwe Msikiti, nae akawa ni mmoja kati ya hao wajenzi alikuwa akibeba matofali kama waumini wengine.

          Lakini tunaona kutokana na maneno ya Mtume (S.A.W) kuwa ni lazima kwa anayetaka fadhila hizi basi awe amekusudia kujenga kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ,sio anajenga ili watu waseme, au wamuone ni mtu mwema, na hili suala la kufanya amali njema kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ndio msingi wa kukubaliwa amali zetu ,hivyo kila mmoja ajitahidi anapowafikishwa na Mola wake kufanya jambo jema basi atakase nia yake.

        Pia tunatakiwa tuimarishe misikiti kwa ibada mbali mbali, kwani Mtume S.A.W amesema kuwa "Watu wa aina saba watapata kivuli siku ya kiama siku isiyokuwa na kivuli isipokuwa hicho, na mmoja kati ya hao saba ni mtu ambaye moyo wake umeshikamana na misikiti”, yaani anautukuza Msikiti na kufanya ibada kwa wingi zikiwemo sala, itikafu na mengineyo kama kusoma Qur -an.

        Na amesema Mtume (S.A.W) kutufahamisha utukufu wa Msikiti kuwa "Sehemu iliyobora mbele ya Mwenyezi Mungu ni misikiti ,na sehemu zinazomchukiza Mwenyezi Mungu ni Masoko" (Muslim).

Misikiti iliyobora zaidi

        Baada ya kufahamu nafasi na utukufu wa misikiti hapa duniani na kwamba ni nyumba tukufu kuliko nyumba nyengine ,pia hiyo misikiti imetofautiana kwa utukufu ,kuna mingine inafadhila zaidi ,nayo ni misikiti mitatu , Mtikiti wa Makka kisha Msikiti wa Mtume S.A.W Madina, kisha Msikiti wa Kudsi (iliopo Palestina ).

        Na utukufu huu ni kutokana na hadithi mbali mbali za Mtume (S.A.W) kama alivyosema "Sala moja katika Msikiti wangu (Madina ) ni bora kuliko  Msikiti mwengine kwa mara elfu isipokuwa msikti wa Makka " imepokewa na Imamu Bukhari na Muslim.

       Pia amesema " sala moja katika Msikiti wa Makka ni bora kuliko sala mia moja katika Msikiti wangu ." imepokewa na Imamu Ahmad bin Hanbal na Ibnu Hibbani.

      Na amesema Mtume (SAW) katika hadithi nyengine kuwa "Sala moja katika Msikiti wa Aksa ni bora kuliko sala mia tano katika misikiti mengine " imepokewa na Imam Bazzar.

      Kutokana na mapokezi hayo tunafahamu kuwa Sala moja katika Msikiti wa Makka ni bora kuliko sala laki moja katika Msikiti mwengine ,na sala moja katika Msikiti wa Mtume (S.A.W) ni bora kuliko sala elfu moja katika Msikiti mwengine ,na sala moja katika Msikiti wa Aksa (Baytil Makdid ) ni bora kuliko sala mia tano katika msikti mwengine.

     Ama misikiti isiyokuwa hiyo mitatu basi yote ni sawa katika fadhila za sala ,wala hakuna ulio bora kuliko mwengine kwa dhati ya Msikiti .

Wallahu aalam.