SIKU YA IJUMAA NA SIKU YA ARAFAT

 

Katika kitabu chake maarufu kiitwacho Zaadul Ma-aad anasema mwanachuoni Ibnul Qayyim:

Mtu mmoja alimuuliza Sheikhul Islam Ibni Taymiya:

“Siku ipi bora zaidi, siku ya Ijumaa au siku ya Arafat?’

Akajibu:

“Katika Sahih yake Ibni Hibban imepokelewa hadithi ya Abu Hurairah (Radhiya Llahu anhu) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) amesema:

“Halijawahi kutoka jua katika siku bora kuliko siku ya Ijumaa.”

Na kutoka kwake pia kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) amesema:

“Siku bora kupita zote zilizowahi kutokewa na jua ni siku ya Ijumaa”.

Na baadhi ya maulamaa wameifadhilisha siku ya Ijumaa kuliko hata siku ya Arafat wakiiegemea hadithi hii.

Al Kadhi Abu Yaala anayo riwaya aliyoinukuu kutoka kwa Imam Ahmad kuwa usiku wa Ijumaa (Alkhamisi usiku) ni usiku bora kuliko usiku wa Lailatul Qadr”.

(Mwisho wa maneno ya Ibni Taymiya)

 

"Lakini kilicho sahihi," anaendelea kusema Ibnul Qayyim: "ni kuwa siku ya Ijumaa (mchana wake) ni bora kuliko siku zote za wiki, na siku ya Arafat na siku ya Al Nahar (siku inayofuatilia Arafat - Sikukuu mosi) ni siku bora kuliko siku zote za mwaka, na pia usiku wa Lailatul Qad'r na usiku wa Ijumaa (Alkhamisi usiku), na kwa ajili hiyo ikawa siku ya Arafat ikiangukia siku ya Ijumaa inakuwa siku tukufu sana kwa sababu zifuatazo:-

 

Ya kwanza ni kujumuika kwa siku mbili zilizo bora kupita siku zote.

Ya pili ni kuwa katika siku mbili hizo ipo saa ambayo dua ndani yake inakubaliwa, na kauli nyingi zinasema kuwa saa hiyo ni ule wakati wa mwisho baada ya Sala ya alasiri. Na watu wanaokuwepo Arafat siku hiyo wanakuwa wakati huo wa jioni wamesimama wakimuomba Mola wao kwa unyenyekevu.

Ya tatu ni kuwa ule mwaka aliohiji Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam), siku ya Arafat iliangukia siku ya Ijumaa, na kwa ajili hiyo kusimama Arafat siku ya Ijumaa kunakwenda sambamba pia na siku aliyohiji Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam).

Ya nne ni kuwa siku hiyo watu katika kila pembe ya dunia wanakusanyika misikitini kwa ajili ya kusikiliza hotuba na kwa ajili ya kuomba dua na kumnyenyekea Mwenyezi Mungu, na wakati huo huo watu walioko Arafat wanakuwa wamekusanyika huko Arafat kwa ajili hiyo hiyo ya kumnyenyekea na kumuomba Mwenyezi Mungu, na kwa ajili hiyo katika mkusanyiko wa Waislamu misikitini na ule wa Arafat pamoja na dua wanazoomba na unyenyekevu, unapatikana mkusanyiko ambao haupatikani katika siku yoyote ile isipokuwa siku hiyo pekee.

Ya tano ni kuwa siku ya Ijumaa ni Sikukuu kwa Waislamu, na siku ya Arafat ni Sikukuu kwa watu wa Arafat, na hii ndiyo sababu ni makruh kwa waliokuwepo Arafat kufunga siku hiyo.

Na katika Annasai kutoka kwa Abu Hurairah (Radhiya Llahu anhu) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) amekataza kwa watu walioko Arafat kufunga siku hiyo. Ingawaje hadithi hii ina udhaifu ndani yake, kwa sababu mmoja wa wapokezi wa hadithi hii na jina lake ni Mehdi bin Harb ni mtu asiyejulikana, lakini wakati huo huo ipo hadithi ya Ummul Fadhal (Radhiya Llahu anha) katika Bukhari na Muslim inayosema kuwa watu walibishana mbele yake siku ya Arafat wengine wakisema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) amefunga na wengine wakisema kuwa hajafunga, na Ummul Fadhal ((Radhiya Llahu anha) akampelekea Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) chombo chenye maziwa ndani yake na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) aliyekuwa amekaa juu ya ngamia akanywa maziwa hayo.

Ipo khitilafu pia baina ya maulamaa juu ya hikma ya watu kukatazwa kufunga siku ya Arafat. Wapo waliosema kuwa ni kwa ajili ya kuwa na nguvu za kuomba dua siku hiyo, na na wengine akiwemo Sheikhul Islam Ibni Taymiya wakasema kuwa ni kwa sababu siku hiyo ni Sikukuu kwa watu wa Arafat na kwa ajili hiyo haipendezi kwao kufunga. Na ushahidi ni hadithi iliyomo ndani ya vitabu vya Ahli Sunnah kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) alisema:

“Siku ya Arafat na siku ya An Nahar (Sikukuu mosi) na siku za Mina ni Sikukuu zetu Waislamu”.

Anasema Ibni Taymiya:

“Hakika ya siku ya Arafat ni Sikukuu kwa watu wa Arafat peke yao kwa sababu ya mkusanyiko wao, tofauti na watu wa miji mbali mbali, maana wao hukusanyika siku ya Sikukuuu mosi kwa sababu hiyo ndiyo Sikukuu yao”.

Kusudi langu ni kuwa Siku ya Arafat ikiangukia Siku ya Ijumaa, hupatikana Sikukuu mbili kwa pamoja.

Ya sita ni kuwa siku hiyo inawafikiana na siku ambayo Mwenyezi Mungu amewakamilishia waja wake dini yao na kuwatimizia neema Yake juu yao.

Ya saba ni kuwa siku hiyo inafanana na siku tukufu ambayo watu wote watakusanywa mbele ya Mola wao, nayo ni Siku ya Kiama, kwa sababu Kiama kitasimama siku ya Ijumaa.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) amesema:

“Siku bora iliyopata kutokewa na juwa ni siku ya Ijumaa. Ndani yake siku hiyo Adam aliumbwa, ndani yake aliingizwa Peponi na ndani yake siku hiyo alitolewa, na ndani yake siku hiyo itasimamishwa Saa (Kiama), na ndani yake upo wakati ambao haumkuti mja Muislamu akiwa anamuomba Mwenyezi Mungu katika kheri Zake, isipokuwa (lazima) atampa, na kwa ajili hiyo Mwenyezi Mungu akawawekea waja wake siku maalum ambayo ndani yake wanakutana na kuzungumza juu ya kuumbwa kwao na juu ya kurudi kwa Mola wao na juu ya Pepo na Moto, na kwa ajili hiyo Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) alikuwa katika Sala ya asubuhi ya kila Ijumaa akisoma Surat Assajdah na Hal ataa (Suratul Dahar) kutokana na yale yaliyokusanya sura hizo katika yaliyopita na yanayotokea na yale yatakayotokea, na pia katika kuumbwa kwa Adam kwa ajili ya kuukumbusha umma juu ya siku hii na yale yatakayotokea ndani yake, na kwa ajili hii watu wa Arafat nao wanaikumbuka siku hii wakiwa wamesimama mbele ya Mola wao Subhanahu wa Taala.

Ya nane ni kuwa Waislamu wanaiheshimu na wanakuwa watiifu sana mbele ya Mola wao katika usiku wa Ijumaa (Alkhamisi usiku) na mchana wa Ijumaa kuliko wanavyokuwa watiifu katika siku nyingine, hata wale wenye kumuasi sana Mola wao nao pia wanaiheshimu siku hii ya Ijumaa wakiitakidi kuwa mtu akifanya maasi ndani yake basi Mwenyezi Mungu atamtia adabu hapa duniani kwanza.

Na itikadi hii imo nyoyoni mwao kutokana na yale waliyokwishaona kwa waasi wenzao, na hii ni kwa sababu ya utukufu wa siku hii na heshima yake, kwa sababu Mwenyezi Mungu ameichaguwa siku hii miongoni mwa siku zote nyingine, na bila ya shaka siku ya Arafat pia ni siku aliyoichaguwa Mwenyezi Mungu miongoni mwa siku zote nyingine.

Ya tisa ni kuwa siku ya Ijumaa inawafikiana na siku ya kuzidishiwa huko Peponi (Yawmul maziyd), na hiyo ni siku ambayo Mwenyezi Mungu anawakusanya watu wote wa Peponi katika bonde kubwa sana na kuwawekea membari za lulu na membari za dhahabu na membari za zubarjad na membari za yaquti zenye harufu ya miski, kisha watamuona Mola wao Mtukufu, na watakaofanikiwa kumuona haraka zaidi ni wale wenye kupenda kwenda misikitini na wale wanaosimama karibu zaidi na imamu. Kwa ajili hiyo watu wa Peponi watakuwa wakiingoja kwa hamu kubwa sana siku hiyo ya (Yawmul maziyd) siku ya kuzidishiwa kutokana na kukirimiwa na Mola wao siku hiyo, na siku hiyo itakuwa ni siku ya Ijumaa.

Ya kumi ni kuwa katika siku ya Arafat, Mwenyezi Mungu huwakaribia watu wa Arafat wakati wa jioni na kuwasifia mbele ya Malaika Wake kwa kuwaambia:

“Wanachokitaka watu hawa (nitawapa), na nakushuhudishieni kuwa nimekwishawasamehe”.

Na kutokana na kuwakaribia Kwake Mwenyezi Mungu mtukufu, kunapatikana wakati ambao ndani yake dua inakubaliwa, na mtu haombi dua yoyote ya kheri siku hiyo isipokuwa itakubaliwa.

 

Kwa hivyo watu wa Arafat wanajikurubisha kwa Mola wao kwa kuomba dua na kumnyenyekea Mola wao, na kwa ajili hiyo wanapata kukaribiwa kwa aina mbili. Ya kwanza ni kukaribiwa na Mola wao mkaribio mahsusi pamoja na kuwasifia mbele ya Malaika Wake, na kukaribiwa kwa aina ya pili ni kwa kukubaliwa dua zao, na kwa ajili hiyo nyoyo za wenye imani zinaathirika kutokana na haya na kuongezeka nguvu zaidi ya ile nguvu iliyokuwepo pamoja na furaha inayotokana na fadhila hizo zinazotoka kwa Mola wao kwa kukirimiwa huko.

Kwa ajili ya yote hayo ikafadhilishwa Arafat inayoangukia siku ya Ijumaa kuliko inayoangukia siku nyingine isiyokuwa hiyo.

 

Ama zile kauli za baadhi ya watu kuwa siku Arafat ikiangukia siku ya Ijumaa basi hija yake huwa sawa na hija sabini na mbili, kauli hizi si sahihi na hazina msingi wowote, wala hapana kauli yoyote iliyonukuliwa kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) au kutoka kwa Sahaba yeyote (Radhiya Llahu anhu) na wala kutoka kwa wale waliokuja baada yao ‘Attabi iyn’.

 

Wallahu taala aalam

Wassalaam alaykum wa Rahmatullahi wa Barakatuh

Imetafsiriwa na

Ndugu yenu

Muhammad Faraj Salem Al Saiy