Hii ndiyo itikadi sahihi ya Kiislamu

 

Imeandikwa na Shaykh Muhammad bin Uthaymiyn

Imetafsiriwa na Muhammad Faraj Salem

 

www.mawaidha.info  www.alhidaaya.com

Utangulizi 2

Itikadi yetu. 3

Sifa ya kusema. 6

Kuwepo Kwake Juu

Anayo Arshi 9

Sifa ya kushuka. 10

Sifa ya Irada) 11

Sifa ya Kupenda. 13

Wajihi Wake. 14

Mikono. 14 Yake

Macho. 16

Tanbih. 18

Malaika. 19

Vitabu. 22

Mitume. 25

Dini Yake. 28

Makhalifa waongofu. 29

Siku ya mwisho. 31

Shafaa. 33

Hodhi na Swiraat 33

Pepo na Moto. 34

Masuali ya kaburini 35

Adhabu ya kaburini 35

Qadar 36

Kutaka kwa Mwenyezi Mungu. 37

Baadhi ya faida. 41

Matunda ya kuamini Malaika. 41

Matunda ya kuviamini vitabu. 41

Matunda ya kuamini Mitume. 42

Matunda ya kuiamini Qiyaamah. 42 na Qadar 42

Utangulizi

Shukrani zote ni zake Mola wa uliwengu wote, na mwisho mwema ni wa wamchao Mwenyezi Mungu, na hapana uadui isipokuwa kwa madhalimu.

Nashuhudia kuwa hapana anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Allah Peke yake Asiye na mshirika mwenye Ufalme na haki iliyo wazi. Na nashuhudia kuwa Muhammad (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) ni mjumbe wake na Mtume wake na mwisho wa wajumbe wake na ni kiongozi wa wacha Mungu. Mola wetu mswalie na msalimie Mtume wako huyu pamoja na Masahaba wake na kila atakayemfuata kwa wema na uongofu mpaka Siku ya Qiyaamah.

 

Amma baad,

Hakika Mwenyezi Mungu amemtuma Mtume wake Muhammad (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) awe dalili iliyo wazi juu ya waja wake, na awabainishie yale aliyoteremshiwa katika Kitabu, na awe mfano mwema wa kuigwa na walimwengu wote, na ili watu wapate kuwa na muongozo mwema katika dini yao na dunia yao.

Ametumwa kutufundisha itikadi sahihi pamoja na hekima kwa ajili ya kutengenea hali ya umati wake, na pia kuwaweka juu ya njia safi na sahihi, ili watu wawe juu ya kitanga cheupe, mchana wake sawa na usiku wake, na asiende kinyume na njia hiyo isipokuwa mpotofu.

Wakaifuata njia hiyo Maswahaba wake (Radhiya Llaahu anhum) na wale waliokuja baada yao na waliowafuatilia kwa wema. Wakaisimamisha shariah ya Mwenyezi Mungu na kuyakamata vizuri mafundisho hayo kwa magego yao kwa kuifuata itikadi hii iliyo sahihi, na ibada na mwenendo na tabia. Na sisi Alhamdulillah tunaendelea kuufuata mwenendo wao huo kwa kufuata dalili zilizomo ndani ya Qur-aan na zilizomo ndani ya mafundisho yake (Swalla Llaahu alayhi wa sallam), na tunamuomba Mwenyezi Mungu Atuthibitishe juu ya njia hiyo sisi na ndugu zetu wote wa Kiislamu kwa kauli iliyo thabit katika maisha ya duniani na ya akhera na atumiminie rehma Zake kwani yeye ni Mwenye kutoa kwa wingi.

 

Kutokana na umuhimu wa maudhui haya, na kutokana na tofauti iliyokuja baadaye, baada ya kuingizwa matamanio ya watu ndani ya itikadi hii, nilipenda kuiandika iwe kama ndiyo itikadi yetu. Itikadi ya Ahlus Sunnah wal Jamaah, nayo ni imani ya kuwepo kwa Mwenyezi Mungu na Malaika Wake na vitabu Vyake na Mitume Yake na Siku ya Qiyaamah na Qadar (qudra) kheri yake na shari yake.

Namuomba Mwenyezi Mungu Aijaalie kazi hii iwe halisi kwa ajili yake, Aridhike nayo na iwe funzo kwa waja Wake.

Rudi juu

 

Itikadi Yetu

Itikadi yetu ni kumuamini Mwenyezi Mungu na Malaika Wake na Mitume Yake na Vitabu Vyake na Siku ya Mwisho na kila kinachotokea au kutusibu (Qadar) kheri na shari, vyote vinatoka kwa Mwenyezi Mungu.

Kwa hivyo sisi tunaamini kuwa Yeye Subhaanahu wa Taala ndiye Aliyeumba na ndiye Mfalme Mwenye kukiendesha kila kitu, na ni Yeye peke yake anayestahiki kuabudiwa, na kila kinachoabudiwa kisichokuwa Yeye ni batil.

 

Tunaamini pia kuwa Mwenyezi Mungu Anayo majina mazuri mazuri na sifa nzuri nzuri na njema, sifa za ukamilifu, na tunaamini kuwa Yeye ni mmoja Asiye na mshirika katika kuumba Kwake na katika kuabudiwa Kwake na katika majina Yake mazuri na katika sifa Zake njema.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Mola wa mbingu na ardhi na vilivyo baina yake. Basi muabudu Yeye tu, na udumu katika ibada yake. Je, mnamjua mwenye jina kama lake?"

Maryam 65

 

 

Na tunaamini kuwa Yeye ndiye:

 

"Mwenyezi Mungu - hapana mungu ila Yeye, Aliye hai, Msimamiaji wa mambo yote milele. Hashikwi na usingizi wala kulala. Ni Vyake pekee vyote viliomo mbinguni na duniani. Ni nani huyo awezaye kuombea mbele yake bila ya idhini Yake? Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao; wala wao hawajui chochote katika vilio katika ujuzi Wake, ila kwa atakalo mwenyewe. Enzi yake imetanda mbinguni na duniani; na wala haemewi na kuvilinda hivyo. Na Yeye ndiye Aliye juu, na ndiye Mkuu."

Al-Baqarah 255

 

 

Na tunaamini kuwa:

 

"Yeye ndiye Mwenyezi Mungu, Muumbaji, Mtengenezaji, Mtia sura, Mwenye majina mazuri kabisa. Kila kilioko katika mbingu na ardhi kinamtakasa, naye ni Mwenye kushinda, Mwenye hikima."

Al-Hashr - 24

 

 

Na tunaamini kuwa:

 

.

"Ufalme wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu; Anaumba Apendavyo, Anamtunukia amtakaye watoto wa kike, na Anamtunukia amtakaye watoto wa kiume.

Au huwachanganya wanaume na wanawake, na akamfanya amtakaye tasa. Hakika Yeye ni Mjuzi Mwenye uweza."

Ash-Shuuraa 49-50

 

 

Na tunaamini kuwa:

 

.

"Yeye ndiye Muumba mbingu na ardhi, Amekujaalieni mke na mume katika nafsi zenu, na katika wanyama nao (Akawaumba) dume na jike, Anakuzidishieni namna hii. Hapana kitu kama mfano wake. Naye ni Mwenye kusikia Mwenye kuona.

Yeye ndiye Mwenye funguo za mbingu na ardhi. Humkunjulia riziki Amtakaye, na humpimia Amtakaye. Hakika Yeye ni Mjuzi wa kila kitu."

Ash-Shuuraa 11-12

 

 

Na tunaamini kuwa:

 

"NA HAKUNA mnyama yoyote katika ardhi ila riziki yake iko kwa Mwenyezi Mungu. Naye Anajua makao yake na mapitio yake. Yote yamo katika Kitabu chenye kubainisha."

Huud - 6

 

 

Na tunaamini kuwa:

 

"Na ziko kwake funguo za ghaibu; hakuna azijuaye ila Yeye tu. Na Yeye Anajua kilioko nchi kavu na baharini. Na halidondoki jani ila Analijua. Wala punje katika giza la ardhi, wala kinyevu, wala kikavu ila kimo katika Kitabu kinachobainisha."

Al-Anaam 59

 

 

Na tunaamini kuwa:

 

"Hakika kuijua Saa (ya Qiyaamah) kuko kwa Mwenyezi Mungu. Na Yeye ndiye Anayeiteremsha mvua. Na Anavijua viliomo ndani ya matumbo ya uzazi. Na haijui nafsi yoyote itachuma nini kesho. Wala nafsi yoyote haijui itafia nchi gani. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kujua, Mwenye khabari".

Luqmaan 34

 

Rudi juu

Sifa Ya Kusema

Tunaamini kuwa Mwenyezi Mungu Anasema wakati wowote Anapotaka na kwa njia yoyote Anayotaka.

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Na Mwenyezi Mungu Akamsemeza Muusa."

An-Nisaa 164

 

 

Na Akasema:

 

"Na alipokuja Muusa kwenye miadi yetu, na Mola wake Akamsemeza."

Al-Aaraf 143

 

 

Na Akasema:

"Na Tulimwita upande wa kulia wa mlima na tukamsogeza kunong'ona naye."

Maryam 52

 

 

Na tunaamini kuwa:

 

"Lau kama bahari ndio wino kwa maneno ya Mola wangu, basi bahari ingelimalizika kabla ya kumalizika maneno ya Mola wangu, hata tungeliileta mfano wa hiyo kuongezea."

Al-Kahf 109

 

 

Na tunaamini kuwa:

 

"Na lau kuwa miti yote iliyomo duniani ikawa ni kalamu, na bahari (ikawa wino), na ikaongezewa juu yake bahari nyengine saba, maneno ya Mwenyezi Mungu yasingelikwisha. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima."

Luqmaan 27

 

 

Na tunaamini kuwa maneno Yake ni ya ukamilifu uliokamilika na ya ukweli uliokamilika na yenye uadilifu uliokamilika.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Yametimia maneno ya Mola wako kwa kweli na uadilifu. Hapana awezaye kuyabadilisha maneno Yake. Na Yeye ndiye Mwenye kusikia na Mwenye kujua."

Al-Anaam - 115

 

Na Akasema:

"Na ni nani msema kweli kuliko Mwenyezi Mungu?"

An-Nisaa 87

 

 

Na tunaamini kuwa Qur-aan ni maneno ya Mwenyezi Mungu, aliyeyatamka kwa uhakika kabisa kwa kumfundisha Jibriyl aliyeiteremsha ndani ya kifua cha Mtume wa Mwenyezi Mungu Muhammad (Swalla Llaahu alayhi wa sallam).

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

"Sema: Ameiteremsha hii (Qur-aan) Roho takatifu kutokana na Mola wako kwa haki."

An-Nahl 102

 

 

Na Akasema:

. . . .

"Na bila ya shaka hii ni Uteremsho wa Mola wa walimwengu wote.

Ameuteremsha Roho muaminifu, Juu ya moyo wako, ili uwe katika Waonyaji. Kwa ulimi wa Kiarabu ulio wazi."

Ash-Shuaraa 192 195

Rudi juu

 

Sifa Ya Kuwepo Kwake Juu Al-Uluw

Tunaamini kuwa Mwenyezi Mungu yupo juu kabisa mbali na viumbe vyake kwa dhati Yake na kwa sifa Zake, na hii inatokana na kauli Yake Subhaanahu wa Taala Aliposema:

 

"Na Yeye ndiye Aliye juu, na ndiye Mkuu."

Al-Baqarah 255

 

Na Akasema:

 

"Malaika na roho hupanda kwake katika siku ambayo muda wake ni miaka elfu hamsini."

Al-Maaarij 4

 

Na Akasema:

 

"Je! Mnadhani muko salama kwa (Mwenyezi Mungu) Ambaye Yuko mbinguni ya kuwa Yeye hatokudidimizeni ardhini tahamaki hiyo inataharaki?"

Al-Mulk - 16

 

Na Akasema:

 

"Naye Ndiye Mwenye nguvu juu ya waja Wake."

Al-Anam -18

 

Na imekuja katika Sunnah (Mafundisho ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam):

 

"Mrehemu aliye ardhini Atakurehemu aliye mbinguni."

Abu Yaala na Atw-Twabaraaniy na Al-Haakim

 

Na kuwepo mbinguni hakuna maana kuwa yupo katika mojawapo ya sayari zilizopo juu kama baadhi ya watu wanavyoweza kudhania, bali dunia yetu ukiilinganisha na mbingu ni mfano wa doa dogo sana, bali hata haionekani. Kwani huko juu kuna nyota na sayari zilizoenea hata kama mtu atasafiri kwa kasi ya sauti? (speed of light) basi atachukuwa mamilioni ya miaka na hatoweza kufika mwisho wake, na hata kama ataufikia mwisho wake, basi atakuta kuwa bado ipo anga isiyo na mwisho. Kwa hivyo ni Mwenyezi Mungu Peke Yake ndiye Mwenye kuelewa mfano ya kuwa juu Kwake Subhaanahu wa Taala.

 

Rudi juu

Mwenyezi Mungu Anayo Arshi

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Hakika Mola wenu ni Mwenyezi Mungu, Ambaye Ameziumba mbingu na ardhi kwa siku sita, kisha Akawa juu ya Arshi Yake."

Yuunus 3

Na kuwa juu ya Arshi Yake ni kuwa kunakonasibiana na utukufu wake Subhaanahu wa Taala, hapana anayejua mfano wake isipokuwa Yeye.

 

Na tunaamini kuwa Mwenyezi Mungu Akiwa juu ya Arshi Yake, Yupo pamoja na viumbe Vyake kwa elimu Yake. Anasikia kauli zao na kuona vitendo vyao, huku Akiyaendesha mambo yao. Anamruzuku fakiri na Anampa ufalme Amtakaye na Anamuondolea ufalme amtakaye, Anamnyanyua amtakaye na Anamuangusha amtakaye, na tunaamini kwamba kheri yote imo mikononi Mwake Subhaanahu wa Taala, na kwamba Yeye ni muweza wa kila jambo.

Na Yeyote mwenye uwezo huo, basi bila shaka yupo pamoja na viumbe vyake kikweli huku akiwa juu ya Arshi yake kikweli, na ni Yeye Peke yake ndiye mwenye kuujuwa uhakika wake.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Hapana kitu kama mfano wake. Naye ni Mwenye kusikia Mwenye kuona."

Ash-Shuuraa 11

 

Na Anasema:

 

"Na Malaika watakuwa kandoni mwake (hizo mbingu) na Malaika wa namna nane watachukua Kiti cha enzi cha Mola wako (Arshi) juu yao."

Al-Haaqqah 17

 

 

Sisi hatusema kama wanavyosema wengine kuwa eti Mwenyezi Mungu yupo ardhini pamoja na viumbe Vyake, kwani tunaona kuwa kusema hivyo ni kukufuru au ni upotofu, kwa sababu kumpa Mwenyezi Mungu wasfu usiolingana naye ni kupunguza katika sifa Zake.

 

Rudi juu

Sifa Ya Kushuka

Tunaamini pia yale aliyotujulisha Mtume wake (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) kuwa Mwenyezi Mungu Anashuka katika mbingu za dunia kila usiku katika thuluthi ya mwisho na kusema: "Nani mwenye kuniomba nimkubalie, nani mwenye kuniomba nimpe, nani mwenye kuniomba maghfira nimghufirie."

Alipoulizwa Imaam Ash-Shaafiiy:

'Vipi Mwenyezi Mungu Anashuka?'

Akajibu:

'Kwani vipi Alipanda?'

 

Na tunaamini kuwa Mwenyezi Mungu Atakuja Siku ya Qiyaamah kuwahukumu viumbe vyake.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

.

"Sivyo hivyo! Itakapovunjwa ardhi vipande vipande. Na Akaja Mola wako na Malaika safu safu. Na ikaletwa Jahannamu siku hiyo, siku hiyo mtu atakumbuka! Lakini kukumbuka huko kutamfaa nini?".

Al-Fajr 21 22

 

Rudi juu

Sifa Ya Irada (Atakavyo Mwenyezi Mungu)

Tunaamini kuwa Mwenyezi Mungu Anatenda Atakavyo.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Atendaye Ayatakayo."

Al-Buruuj 16

 

 

Na tunaamini kuwa zipo Irada namna mbili.

Ya kwanza Anatujulisha katika kauli Yake:

 

"Na lau kuwa Mwenyezi Mungu Alipenda wasingelipigana (Lau shaa'a Alaahu). Lakini Mwenyezi Mungu Hutenda Atakavyo."

Al-Baqarah 253

 

Na hapa maana yake ni kutaka, kama ilivyo katika kauli Yake:

 

"Wala nasaha yangu haikufaini kitu nikitaka kukunasihini, ikiwa Mwenyezi Mungu Anataka (Law Yuriydu Allaah) kukuachieni mpotee."

Huud 34

 

 

Na uwezo mwingine ni wa kishariah, na Hamtakii isipokuwa Anayempenda, kama ilivyo katika kauli Yake Subhaanahu wa Taala:

 

"Na Mwenyezi Mungu Anataka (Yuriydu Allaah) kukurejezeni kwenye utiifu wake, na wanaotaka kufuata matamanio wanataka mkengeuke makengeuko makubwa."

(Na maana yake hapa ni kuwa 'Hivi Ndivyo Anavyotaka Mwenyezi Mungu' lakini kakupeni uhuru wa kuchagua wenyewe mnakotaka kwenda.)

An-Nisaa 27

 

 

Na tunaamini kuwa Atakacho Mwenyezi Mungu katika mambo ya kilimwengu na ya kishariah yote ni katika hekima Yake, na hafanyi kitu bila ya kuwa na hekima kubwa ndani yake, na sisi huenda tukaijua hekima hiyo au tusiijuwe kutokana na upungufu wa akili zetu.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Kwani Mwenyezi Mungu si muadilifu kuliko mahakimu wote?"

Atw-Twiyn - 8

 

Na Akasema:

 

"Na nani aliye mwema zaidi katika kuhukumu kuliko Mwenyezi Mungu kwa watu wenye yakini?"

Al-Maaidah - 50

 

Rudi juu

Sifa Ya Kupenda

Na tunaamini kuwa Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Taala Anawapenda wacha Mungu wake wanaompenda.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Sema: Ikiwa nyinyi mnampenda Mwenyezi Mungu basi nifuateni mimi, Mwenyezi Mungu Atakupendeni na Atakufutieni madhambi yenu."

Al-Imraan 31

 

 

Na Akasema:

 

"Basi Mwenyezi Mungu atakuja leta watu anao wapenda nao wanampenda."

Al-Maaidah 54

 

 

Na Akasema:

 

"Hakika Mwenyezi Mungu Anawapenda wanaosubiri."

Al-Imraan 146

 

 

Na tunaamini kuwa Mwenyezi Mungu Huridhika zinapofuatwa shariah Zake na huchukizwa zisipofuatwa.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Mkikufuru basi Mwenyezi Mungu si mwenye haja nanyi, lakini hafurahii kufuru kwa waja wake."

Az-Zumar 7

 

 

Na Akasema:

 

"Lakini Mwenyezi Mungu Kachukia kutoka kwao, na kwa hivyo Akawazuia na ikasemwa: Kaeni pamoja na wanao kaa!"

 

 

Na tunaamini kuwa Mwenyezi Mungu Huridhika na wale wanaoamini na kufanya mema.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Mwenyezi Mungu Yu radhi nao, na wao waradhi naye. Hayo ni kwa anayemwogopa Mola wake."

Al-Bayyinah-6

 

 

Na tunaamini kuwa Mwenyezi Mungu Anamkasirikia kila mwenye kustahiki kukasirikiwa katika makafiri na wasiokuwa makafiri.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Wanaomdhania Mwenyezi Mungu dhana mbaya. Utawafikia mgeuko mbaya, na Mwenyezi Mungu Awakasirikie."

Al-Fat-h 6

 

 

Na Akasema:

 

"Lakini aliyekifungulia kifua chake kukataa - basi hao ghadhabu ya Mwenyezi Mungu ipo juu yao, na wao watapata adhabu kubwa."

An-Nahl 106

Rudi juu

 

Wajihi Wa Mwenyezi Mungu

Na tunaamini kuwa Mwenyezi Mungu Anao wajihi wenye utukufu na ukarimu.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Unabaki Wajihi wa Mola wako wenye utukufu na ukarimu."

Ar-Rahmaan 27

Rudi juu

Mikono

Tunaamini kuwa Mwenyezi Mungu Anayo mikono miwili mitukufu.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Bali mikono yake (miwili - yadaahu) iwazi. Hutoa Apendavyo."

Al-Maaidah 64

 

Na Akasema:

 

"Na wala hawakumhishimu Mwenyezi Mungu kama Anavyostahiki kadiri Yake. Na Siku ya Qiyaamah ardhi yote itakuwa mkononi Mwake, na mbingu zitakunjwa katika mkono Wake wa kuume. Subhaanahu wa Taala Ametakasika na Ametukuka na hayo wanayomshirikisha nayo."

Az-Zumar 67

 

 

(Siku ya RidhwAan Waislamu walipofungamana na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) chini ya mti kwa kumpa mkono wote kwa pamoja, mmoja baada ya mwengine, na Mwenyezi Mungu akateremsha kauli Yake:

 

"Bila Shaka wale wanaofungamana nawe, kwa hakika wanafungamana na Mwenyezi Mungu. Mkono wa Mwenyezi Mungu uko juu ya mikono yao."

Al-Fat-h 10

 

 

Ieleweke kuwa Mwenyezi Mungu Anaposema Anayo mikono au macho, haina maana kuwa mikono Yake ni sawa na mikono yetu, au macho Yake ni sawa na macho yetu - AstaghfiruLlaah. Meza inayo miguu na viti vina miguu, lakini miguu ya viti na ya meza ni tofauti na miguu ya mwanaadamu aloitengeneza meza ile, kwani sifa ya mtengenezaji lazima iwe tofauti na sifa ya kilichotengenezwa, ama sivyo mtengenezaji na kilichotengenezwa watakuwa kitu kimoja. Na Mwenyezi Mungu Ndiye mwenye kupigiwa mifano bora, sifa Zake Subhaanahu wa Taala haziwezi kufananishwa na sifa zetu. Lakini wakati huo huo lazima tukikubali kila Alichojinasibisha nacho Subhaanahu wa Taala.)

Rudi juu

Macho

Na tunaamini kuwa Mwenyezi Mungu Anayo macho mawili kikweli, na hii inatokana na kauli Yake Subhaanahu wa Taala Aliposema kumwambia Nuuh (Alayhis-Salaam):

 

"Na unda jahazi mbele ya macho yetu na kwa mujibu wa ufunuo wetu."

Huud 37

 

Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) amesema:

"Pazia yake ni nuru, na lau kama ataiondoa basi nuru ya wajihi wake ingeunguza kila kilichokifikia."

Na alipokuwa akihadithia juu ya Ad-Dajjaal alisema:

"Dajjaal ana chongo na Mola wenu hana chongo."

 

 

Na tunaamini kuwa macho yetu hayamfikii kumuona Mwenyezi Mungu.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Macho hayamfikilii, bali Yeye anayafikilia macho. Naye ni Mjuzi, Mwenye khabari."

Al-Anaam 103

 

 

Na tunaamini kuwa Waislamu watamuona Mola wao Siku ya Qiyaamah.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

.

"Zipo nyuso siku hiyo zitang'ara. Zinamwangallia Mola wao."

Al-Qiyaamah 22-23

 

 

Na tunaamini kuwa Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Taala hana mfano wake katika ukamilifu wa sifa Zake.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Hapana kitu kama mfano Wake. Naye ni Mwenye kusikia Mwenye kuona."

Ash-Shuuraa 11

 

 

Na tunaamini kuwa Mwenyezi Mungu Hashikwi na usingizi wala halali.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Hashikwi na usingizi wala kulala."

Al-Baqarah 255

 

 

Na tunaamini kuwa Mwenyezi Mungu Hamdhulumu mtu, na hii inatokana na ukamilifu wa uadilifu Wake Subhaanahu wa Taala, na kwamba hapana Asichokijua katika matendo ya waja Wake, na kwamba Hashindiwi na chochote, kwani Anapotaka chochote kiwe hukiambia tu; 'Kuwa' na kikawa.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Hakika amri Yake Anapotaka kitu ni kukiambia tu: Kuwa! Na kikawa."

Yaasiyn 82

 

 

Na tunaamini kuwa Mwenyezi Mungu Haguswi na machofu wala tabu ya aina yoyote ile.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Na bila ya shaka Sisi tumeziumba mbingu na ardhi na vilio baina yao mnamo siku sita; na wala hayakutugusa machofu."

Qaaf 38

 

 

Na tunakiamini kila Alichojithibitishia nafsi Yake, Akasema kuwa Anacho, basi sisi tunaamini kuwa Anacho kwa uhakika, na tunaamini pia kila alichotujulisha Mtume wake (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) juu ya Mola wake, katika Majina Yake mazuri mazuri na Sifa Zake njema.

 

Lakini tunakataa mambo mawili, nayo ni:

 

1.  Kufananisha (kushabihisha). Nako ni kutamka kwa ulimi au kwa moyo kuwa wasfu wa Mwenyezi Mungu unafanana na wasfu wa viumbe Vyake.

2.  Na pia tunakataa kukisia. Nako ni kujisemeza moyoni au kutamka kwa ulimi kuzikisia sifa za Mwenyezi Mungu kuwa labda ni hivi au vile.

 

Na tunakanusha kila Mwenyezi Mungu Alichojikanushia nafsi Yake, au kile alichokikanusha Mtume wake (Swalla Llaahu alayhi wa sallam), na tunakinyamazia kila Alichokinyamazia, na tunaamini kuwa hii ndiyo njia sahihi, kwani kila Alichojikanushia nafsi Yake ni habari kutoka Kwake, na Yeye Subhaanahu wa Taala ndiye mwenye kuijua nafsi Yake na ndiye Msema kweli kupita wote, Mwenye mazungumzo bora kupita wote, waja Wake hawana uwezo wa kujua chochote juu Yake bila Yeye kuwajulisha.

Rudi juu

 

 

Tanbihi:

Kila tulichokitaja katika sifa za Mwenyezi Mungu, iwe kwa urefu au kwa ujumla, katika kuthibitisha au katika kukanusha, yote tumeyanukuu kutoka katika kitabu cha Mwenyezi Mungu (Qur-aan) au mafundisho ya Mtume Wake (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) (Sunnah) iliyo sahihi nayo pia ni itikadi waliyokuwa nayo Maimamu wetu wema waliotangulia.

 

Tunaona kuwa inawajibika kuzifasiri nassw (dalili) zilizomo ndani ya Qur-aan kwa uhakika wake kama Anavyozistahiki Mwenyezi Mungu, na tunajitenga mbali na njia ya wageuzaji wa maana wale waliozigeuza maana na kuzifasiri kwa njia Asiyoitaka Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Taala, na tunajitenga mbali na njia ya wabadilishaji waliobadilisha, mbali na maana iliyokusudiwa, na pia tunajitenga mbali na wazidishaji waliozidisha na kuzifanya sifa zake kuwa ni za kumfananisha.

 

Tuna hakika kuwa yale yaliyomo ndani ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu na ndani ya mafundisho ya Mtume Wake (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) ni haki isiyopingana, na hii inatokana na kauli Yake Subhaanahu wa Taala Aliposema:

 

"Hebu hawaizingatii hii Qur-aan? Na lau kuwa imetoka kwa asiye kuwa Mwenyezi Mungu bila ya shaka wangeli kuta ndani yake khitilafu nyingi."

An-Nisaa 82

 

Na kwa vile kauli zinazopingana huwa zinasutana, na hili ni jambo lisiliowezekana katika habari Anazotupa Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Taala na anazotupa Mtume wake (Swalla Llaahu alayhi wa sallam). Na yeyote anayedai kuwa ndani ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu au ndani ya mafundisho ya Mtume Wake (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) yamo maneno yanayopingana, akasema hayo kwa kukusudia au kwa vile moyo wake umekwenda upande, basi huyo anatakaiwa atubu kwa Mola wake na atoke ndani ya upotofu wake.

 

Na yeyote anayedhani kuwa mna upungufu wowote ndani ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu au ndani ya mafundisho ya Mtume wake (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) au baina yao, basi huyo ima ana upungufu wa elimu au uchache wa fahamu au ana upungufu katika kuzingatia kwake, kwa hivyo aitafute elimu na ajitahidi katika kuzingatia mpaka ukweli utakapombainikia. Na kama haukumbainikia, basi amtafute mwenye elimu kupita yeye na aachane na upotofu wake, na aseme kama wanavyosema wale waliobobea katika elimu:

 

"Tumeamini, zote zimetoka kwa Mola wetu."

Aali-ImraAn 7

 

Na ajue ya kuwa Qur-aan na Sunnah haviwezi kugongana wala kupingana wala hapana hitilafu baina yake.

Rudi juu

 

Malaika

Na tunaamini juu Malaika wa Mwenyezi Mungu kama ulivyokuja wasfu wao ndani ya Qur-aan kwamba wao ni:

 

.

"Bali hao ni watumwa walio tukuzwa. Hawamtangulii kwa neno, nao wanafanya amri Zake."

 

Mwenyezi Mungu Amewaumba ili wamuabudu na kumtii.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

.

"Hawafanyi kiburi wakaacha kumuabudu, wala hawachoki.

Wanamtakasa usiku na mchana, wala hawanyong'onyei."

Al-AnbiyAa 19 20

 

Mwenyezi Mungu Akatujaalia tusiweze kuwaona, na Aliwafanya wengine kati ya waja Wake kuweza kuwaona, kwani Mtume (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) alimuona Jibriyl (Alayhis-Salaam) akiwa katika umbile lake la kweli ana mbawa mia sita, akiwa ameizinga anga yote juu yake.

Jibriyl (Alayhis-Salaam) aliwahi pia kuonekana na Bibi Maryam akiwa katika umbile la binaadamu aliyekamilika, akazungumza naye, na aliwahi pia kumjia Mtume (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) akiwa pamoja na Maswahaba wake (Radhiya Llaahu anhum) akiwa katika umbile la mwanamume asiyejulikana wala hapakuwa na ishara yoyote usoni mwake kama ni mtu aliyetoka safari ndefu, akaliegemeza goti lake juu ya goti la Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) na kuuweka mkono wake juu ya paja la Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam), kisha akazungumza naye huku Mtume (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) akimjibu, na baada ya kuondoka ndipo Mtume (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) akawaambia Maswahaba wake (Radhiya Llaahu anhum) kuwa yule alikuwa Jibriyl (Alayhis-Salaam).

 

Na tunaamini kuwa Malaika wana kazi zao maalum walizopewa na Mola wao. Jibriyl (Alayhis-Salaam)ni mletaji wahyi kwa Mitume. Anawateremshia kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kuwafikishia anaotumwa kuwafikishia katika Mitume yake Subhaanahu wa Taala. Na yupo Mikaaiyl aliyepewa kazi ya kuteremsha mvua na ya mazao anapopewa amri na Mwenyezi Mungu. Na yupo Israafiyl mwenye kazi ya kupuliza parapanda (baragumu) siku ya Qiyaamah. Na yupo Malaika wa kifo aliyepewa kazi ya kutoa roho wakati wa kufa, na yupo Malaika wa majabali, na yupo Malik mlinzi wa mlango wa Motoni, na wapo Malaika wanaowashughulikia watoto wachanga matumboni mwa mama zao, na wengine waliopewa kazi ya kuwahifadhi wanaadamu na wengine wenye kuandika amali zao, na kila mtu ana Malaika wawili.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

.

"Wanapopokea wapokeaji wawili, wanaokaa kuliani na kushotoni

Hatamki neno ila karibu yake yupo mwangalizi tayari (kuandika)."

Qaaf 17 18

 

Na wengine wana kazi za kuwauliza maiti baada ya kufikishwa kaburini, wanajiwa na Malaika wawili na kumuuliza Nani Mola wake, nini dini yake, nani mtume wake?

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Mwenyezi Mungu Huwatia imara wenye kuamini kwa kauli imara katika maisha ya dunia na katika Akhera. Na Mwenyezi Mungu huwaacha kupotea hao wenye kudhulumu. Na Mwenyezi Mungu Hufanya apendavyo."

Ibraahiym 27

 

Na wapo Malaika waliopewa kazi ya kuwashughulikia watu wa Peponi.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

.

"Na Malaika wanawaingilia katika kila mlango. (Wakiwaambia) Assalaamu Alaykum! Amani iwe juu yenu, kwa sababu ya mlivyosubiri! Basi ni mema mno malipo ya Nyumba ya Akhera."

Ar-Raad 23 34

 

Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) alitujulisha kuwa ndani ya 'Baytul Maamuur', iliyopo mbinguni wanaingia na kuswali ndani yake kila siku Malaika elfu sabini wakishamaliza hawaipati fursa ya kurudi humo tena.

 

Rudi juu

Vitabu

Na tunaamini kuwa Mwenyezi Mungu Amewateremshia Mitume Vitabu ili viwe hoja na mwangaza kwa walimwengu kwa ajili ya kuwafundisha hekima na kwa ajili ya kuwatakasa.

 

Na tunaamini kuwa Mwenyezi Mungu Amemteremshia kila Mtume Kitabu.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Kwa hakika tuliwatuma Mitume Wetu kwa dalili waziwazi, na tukateremsha Kitabu pamoja nao na Mizani, ili watu wasimamie uadilifu."

Al-Hadiyd 25

 

Na katika vitabu hivyo tunavyovijua ni:

 

1.  Taurati; Mwenyezi Mungu Alimteremsia Nabii Muusa (Alayhis-Salaam), na hiki ni Kitabu kitukufu kupita vyote vya Bani Israaiyl.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

"Hakika Sisi Tuliteremsha Taurati yenye uongofu na nuru, ambayo kwayo Manabii walionyenyekea Kiislamu, na wacha Mungu, na wanazuoni, waliwahukumu Mayahudi; kwani walikabidhiwa kukihifadhi Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Nao wakawa ni mashahidi juu yake."

Al-Maaidah 44

 

2.  Injili; Mwenyezi Mungu alimteremshia Nabii Iysa (Alayhis-Salaam), na hiki kinakisadikisha Taurati na kukikamilisha.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Na tukampa Injili iliyomo ndani yake uongofu, na nuru na inayosadikisha yaliyokuwa kabla yake katika Taurati, na uongofu na mawaidha kwa wacha Mungu."

Al-Maaidah 46

 

3.  Zaburi; Aliyopewa Nabii Daawuud (Alayhis-Salaam).

 

4.  Sahifa (Suhuf); Walizoteremshiwa Nabii Ibraahiym na Muusa (Alayhimas-Salaam).

 

5.  Qur-aan tukufu; Aliyoteremshiwa Mtume wetu Muhammad (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) mwisho wa ma Nabii.

 

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Ni uongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uongofu na upambanuzi."

Al-Baqarah 185

 

 

Na Akasema:

 

"Kinacho sadikisha yaliyo kuwa kabla yake katika Vitabu na kuyalinda."

Al-Maaidah 48

 

Kwa Kitabu hiki Mwenyezi Mungu Akavifuta vilivyotangulia na Akachukua Yeye mwenyewe jukumu la kukilinda ili kibaki kuwa hoja kwa viumbe wote mpaka siku ya Qiyaamah.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Hakika Sisi ndio Tulioteremsha Ukumbusho huu, na hakika Sisi ndio Tutaoulinda."

Al-Hijr 9

 

Ama Vitabu vilivyotangulia, vilikuwa vikiletwa kwa ajili ya wakati maalum, na ukishamalizika wakati wake vinaletwa vingine kuchukua nafasi yake, na hii ndiyo maana havikuwa na uwezo wa kujilinda kutokana na ubadilishaji.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Miongoni mwa Mayahudi wamo ambao hubadilisha maneno na kuyatoa mahala pake."

An-Nisaa -46

 

Na Akasema:

 

"Basi ole wao wanaoandika kitabu kwa mikono yao, kisha wakasema: Hiki kimetoka kwa Mwenyezi Mungu, ili wachumie kwacho pato dogo. Basi ole wao kwa yale iliyoandika mikono yao, na ole wao kwa yale wanayoyachuma."

Al-Baqarah 79

 

Na Akasema:

 

"Sema: Nani aliyeteremsha Kitabu alichokuja nacho Muusa, chenye nuru na uongofu kwa watu, mlichokifanya kurasa kurasa mkizionyesha, na mengi mkiyaficha."

Al-Anaam 91

 

Na Akasema:

 

.

"Na wapo baadhi yao wanaopindua ndimi zao katika kusoma Kitabu ili mdhanie kuwa hayo yanatoka Kitabuni, na wala hayatoki Kitabuni. Na husema: Haya yametoka kwa Mwenyezi Mungu. Na wala hayatoki kwa Mwenyezi Mungu. Na wanamsingizia Mwenyezi Mungu uongo na wao wanajua.

Haiwezi kuwa mtu aliyepewa na Mwenyezi Mungu Kitabu na hikima na Unabii kisha awaambie watu: Kuweni wa kuniabudu mimi badala ya Mwenyezi Mungu. Bali atawaambia: Kuweni wenye kumuabudu Mola wa viumbe vyote, kwa kuwa nyinyi mnafundisha Kitabu na kwa kuwa mnakisoma."

Aali-Imraan 78 79

 

Na Akasema:

 

"Enyi Watu wa Kitabu! Amekwishakujieni Mtume wetu anayekufichulieni mengi mliyokuwa mkiyaficha katika Kitabu, na anayesamehe mengi. Bila shaka imekujieni kutoka kwa Mwenyezi Mungu nuru na Kitabu kinachobainisha."

Al-Maaidah 15

 

Rudi juu

Mitume

Na tunaamini kuwa Mwenyezi Mungu Amewatuma kwa waja Wake Mitume ili wawe wabashiri na waonyaji.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Mitume hao ni wabashiri na waonyaji, ili watu wasiwe na hoja juu ya Mwenyezi Mungu baada ya kuletewa Mitume. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima."

An-Nisaa 165

 

Na tunaamini kuwa Muhammad ni mbora wa Mitume yote, kisha Ibrahim kisha Musa kisha Nuh kisha Issa mwana wa Maryam, na hawa ndio waliohuswa katika aya ifuatayo.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Na tulipochukua ahadi kwa Manabii na kwako wewe (Muhammad), na Nuuh na Ibraahiym na Iysa mwana wa Mariamu, na tulichukua kwao ahadi ngumu."

Al-Ahzaab 7

 

 

Na tunaamini kuwa shariah ya Muhammad (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) imekusanya fadhila zote walizokuja nazo Mitume iliyotangulia.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Amekuamrisheni Dini ile ile aliyomuusia Nuuh na tuliyokufunulia wewe, na tuliyowausia Ibraahiym na Muusa na Iysa, kwamba shikeni Dini wala msifarikiane kwayo."

Ash-Shuuraa 13

 

 

Na tunaamini kuwa Mitume yote ni watu, viumbe na hawana uwezo wowote wa kuumba au kugawa rizki wala hawajui ghaibu nk.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Wala sikwambiini kuwa nina khazina za Mwenyezi Mungu; wala kuwa mimi najua mambo ya ghaibu; wala sisemi: Mimi ni Malaika."

Huud 31

 

Mwenyezi Mungu Alimuamrisha Muhammad (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) atamke maneno yafuatayo:

 

Sema: Mimi sikwambiini kuwa ninazo khazina za Mwenyezi Mungu. Wala sijui mambo yaliyofichikana. Wala sikwambiini kuwa mimi ni Malaika

Al-Anaam 50

 

Na akaamrishwa pia atamke:

 

"Sema: Siimilikii nafsi yangu manufaa wala madhara, ila apendavyo Mwenyezi Mungu."

Al-Aaraaf 188

 

Na atamke:

 

.

"Sema: Mimi sina mamlaka ya kukudhuruni wala kukuongozeni."

Sema: Hakika hapana yeyote awezaye kunilinda na Mwenyezi Mungu, wala sitapata pa kukimbilia isipokuwa kwake Yeye tu."

Al-Jinn 21-22

 

Na tunaamini kuwa wao ni waja wa Mwenyezi Mungu Aliowakirimu kwa kuwapa ujumbe.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Enyi kizazi tuliyowachukua pamoja na Nuuh! Hakika yeye alikuwa mja mwenye shukrani."

Al-Israa 3

 

Na Akasema:

 

"Ametukuka aliye teremsha Furqaan kwa mja Wake, ili awe mwonyaji kwa walimwengu wote."

Al-Furqaan 1

 

Na juu ya Mitume mingine Akasema:

 

"Wakumbuke waja wetu, Ibraahiym na Is-haaq na Yaa'quub waliokuwa na nguvu na busara."

Swaad 45

 

Na Akasema:

 

"Na Daawuud Tukamtunukia Sulaymaan. Alikuwa mja mwema. Na hakika alikuwa mwingi wa kutubia."

Swaad 30

 

Na juu ya Iysa mwana wa Maryam Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Hakuwa yeye (Iysa) ila ni Mtumwa Tuliyemneemesha na tukamfanya ni mfano kwa Wana wa Israili."

Az-Zukhruf 59

 

 

Tunaamini pia kuwa Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Taala Amekamilisha ujumbe wake kwa kumleta Muhammad (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) kama ni Mtume kwa watu wote.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Sema: Enyi watu! Hakika mimi ni Mtume kwenu nyinyi nyote, niliyetumwa na Mwenyezi Mungu Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi. Hapana mungu ila Yeye Anayehuisha na Anayefisha. Basi muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake asiyejua kusoma na kuandika, ambaye anamuamini Mwenyezi Mungu na maneno Yake. Na mfuateni yeye ili mpate kuongoka."

Al-Aaraf 158

 

Rudi juu

Dini Ya Mwenyezi Mungu

Na tunaamini kuwa dini alokuja nayo ni Islam aliyoridhika nayo Mwenyezi Mungu kwa waja Wake. Na kwamba Mwenyezi Mungu Haikubali dini nyingine isipokuwa hii.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Bila ya shaka Dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu."

Aali-Imraan 19

 

Na Akasema:

 

"Leo Nimekukamilishieni Dini yenu, na Nimekutimizieni neema Yangu, na Nimekupendeleeni UISLAMU uwe ndiyo Dini."

Al-Maaidah 3

 

Na Akasema:

 

"Na anayetafuta dini isiyokuwa Uislamu haitakubaliwa kwake. Naye Akhera atakuwa katika wenye khasara."

Aali-Imraan 85

 

 

Na tunaamini kuwa yeyote atakayedai kuwa ipo dini nyengine inayokubaliwa na Mwenyezi Mungu isiyokuwa Islamu, kama vile dini ya Kiyahudi au ya Kinasara au dini nyengine yoyote, huyo anakuwa amekufuru, na lazima atubu kwa kufru yake hiyo. Akitubu anasamehewa, ama asipotubu huyo anauliwa kama ni Murtaddi, kwa sababu anakuwa ameikadhibisha Qur-aan tukufu.

 

Na tunaamini kuwa hapana tena Mtume baada ya Muhammad (Swalla Llaahu alayhi wa sallam), na yeyote atakayejidai utume baada yake au akamsadiki mwenye kujidai utume anakuwa kafir, kwa sababu anakuwa amemkadhibisha Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na Waislamu wote.

Rudi juu

 

Makhalifa Waongofu

Na tunaamini kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) anao Makhalifa waongofu waliouongoza umma baada ya kufa kwake kwa kueneza elimu na daawah na uongozi, na kwamba mbora wao ni Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhiya Llaahu anhu) akifuatiwa na Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Llaahu anhu) kisha Uthmaan bin Affaan (Radhiya Llaahu anhu), kisha Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Llaahu anhu), na huu ndio mpangilio wao katika kufadhilishwa kwao.

 

Na tunaamini kuwa umma ule ndio umma bora kupita zote, na hii inatokana na kauli yake Mwenyezi Mungu Alipowaambia:

 

"Nyinyi ndio umma bora kuliko umma zote waliodhihirishiwa watu, kwa kuwa mnaamrisha mema na mnakataza maovu, na mnamuamini Mwenyezi Mungu."

Aali-Imran 110

 

 

Na tunaamini kuwa walio bora kupita wote ni Maswahaba (Radhiya Llaahu anhum), kisha waliokuja baada yao, kisha waliokuja baada yao, na kwamba wangali wapo watu wenye kuidhihirisha haki bila kujali lawama za wanaowalaumu, mpaka siku Mwenyezi Mungu atakapoleta amri Yake.

 

Na tunaitakidi kuwa yaliyotokea baina ya Maswahaba (Radhiya Llaahu anhum) katika fitna na mapambano, yanatokana na jitihada zao katika uamuzi. Wapo waliosibu na wapo waliokosea, na kama alivyosema Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam):

 

"Mwenyezi kusibu anapata ujira mara mbili, na mwenye kukosea anapata ujira mara moja."

 

Na kwamba Mwenyezi Mungu Atawasamehe makosa yao, na tunaamini kuwa lazima tuache kuwasema vibaya, na badala yake tuwaseme kwa wema, na tusiwataje isipokuwa kwa kuzitaja sifa wanazozistahiki, na tuziondoe chuki zetu juu yao.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Hawawi sawa miongoni mwenu wenye kutoa kabla ya Ushindi na wakapigana vita. Hao wana daraja kubwa zaidi kuliko wale ambao waliotoa baadae na wakapigana. Na wote hao Mwenyezi Mungu Amewaahidia wema."

Al-Hadiyd 10

 

Na Akasema:

 

"Na waliokuja baada yao (wakawa wanawapenda Waislamu waliotangulia wanawaombea duaa) wanasema: Mola wetu! Tughufirie sisi na ndugu zetu waliotutangulia (kufa) katika Uislamu, wala usijaalie ndani ya nyoyo zetu undani kuwafanyia Waislamu (wenzetu). Mola wetu! Hakika Wewe ni Mpole na Mwenye kurehemu."

Al-Hashr 10

 

Rudi juu

Siku Ya Mwisho

Tunaamini kuwa Siku ya Mwisho ndiyo Siku ya Qiyaamah, ambapo hapana tena siku nyingine baada yake, na siku hiyo Mwenyezi Mungu Atawafufua waja wake kwa ajili ya kuwaingiza katika nyumba ya neema 'Peponi', au katika nyumba ya adhabu iumizayo 'Motoni'.

 

Tunaamini kuwa watu watafufuliwa baada ya baragumu kupigwa, kama Mwenyezi Mungu Alivyosema:

 

"Na litapulizwa barugumu, wazimie waliomo mbinguni na waliomo katika ardhi, isipokuwa Aliyemtaka Mwenyezi Mungu. Kisha litapulizwa mara nyengine. Hapo watainuka wawe wanangojea."

Az-Zumar 68

 

 

Kisha watu watasimamishwa mbele ya Mwenyezi Mungu wakiwa kama siku waliyozaliwa bila viatu wala nguo (kama ilivyoelezwa katika Swahiyh Al-Bukhaariy na Muslim Imepokelewa kuwa Bibi Aaishah (Radhiya Llaahu anha) alimuuliza Mtume (Swalla Llaahu alayhi wa sallam):

"Watu watafufuliwa wakiwa uchi kila mmoja anamtizama mwenzake?" Mtume (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) akamwambia: "Ewe Aisha! mambo siku hiyo yatakuwa magumu kuliko hivyo."

Watu hawatakuwa na wakati wa kutizamana - mambo yatakuwa magumu sana - Ya rabbi sallim.)

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Siku tutakapozikunja mbingu kama mkunjo wa karatasi za vitabu. Kama tulivyoanza umbo la mwanzo tutalirudisha tena. Ni ahadi iliyo juu yetu. Hakika Sisi ni watendao."

Al-Anbiyaa 104

 

 

Na tunaamini kuwa watu watapewa madaftari yao kwa mkono wa kulia au nyuma ya migongo yao au kushotoni mwao.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

. . . . .

"Ama atakayepewa daftari lake kwa mkono wa kulia. Basi huyo atahisabiwa hisabu nyepesi. Na arudi kwa ahali zake na furaha.

Na ama atakayepewa daftari lake kwa nyuma ya mgongo wake. Basi huyo ataomba kuteketea. Na ataingia Motoni."

Al-Inshiqaaq 7 12

 

Na Akasema:

 

.

"Na kila mtu tumemfungia amali yake shingoni mwake. Na Siku ya Qiyaamah tutamtolea kitabu atakachokikuta kiwazi kimekunjuliwa.

Ataambiwa: Soma kitabu chako! Nafsi yako inakutosha leo kukuhisabu."

Al-Israa- 13 14

 

 

Na tunaamini kuwa mezani zitawekwa Siku ya Qiyaamah na kwamba hapana atakayedhulumiwa.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

.

"Basi anayetenda chembe ya wema, atauona! Na anayetenda chembe ya uovu atauona!."

Zilzaal 7 8

 

Na Akasema:

 

. .

"Ama wale ambao mizani zao zitakuwa nzito, hao ndio wenye kufanikiwa. Na wale ambao mizani zao zitakuwa nyepesi, hao ndio walio zitia khasarani nafsi zao, na katika Jahannamu watadumu. Moto utababua nyuso zao, nao watakuwa na nyuso zilizokunjana."

Al-Muuminuun 102-104

Rudi juu

Shafaah

Na tunaamini kuwa ipo Shafaah (msamaha) kubwa ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) atakapowaombea umma wake baada ya kupewa idhini hiyo na Mola wake Subhaanahu wa Taala, na baada ya watu kuona dhiki na kuanza kuwaendea Manabii Nuuh kisha Ibraahiym kisha Muusa kisha Iysa (Alayhimus-Salaam) mpaka watakapoishia kwake Muhammad (Swalla Llaahu alayhi wa sallam).

 

Na tunaamini pia kuwa wale watakaoingia Motoni katika Waislamu (tu) nao pia wataombewa Shafaah watolewe humo, na Shafaah hii ni kwa ajili ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) na Mitume mingine na watu wema na Malaika, na tunaamini kwamba Mwenyezi Mungu Atawatoa Motoni pia makundi kwa makundi ya Waislamu kwa fadhila Zake tu na rehma Yake, bila hata kuombewa Shafaah.

 

 

Hodhi na Swiraat

Na tunaamini kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) ana hodhi lake, na maji yake ni meupe kuliko maziwa na matamu kuliko asali, na yenye harufu nzuri kuliko hal miski. Urefu wake hodhi hilo ni mwendo wa mwezi mzima, na upana wake mwendo wa mwezi mzima.na vyombo vyake vinang'aa kama nyota za mbinguni.

 

Waislamu watakunywa humo, na atakayekunywa hatopata kiu tena.

 

Tuaamini kuwa ipo 'Swiraat' itakayowekwa juu ya Jahannam, na watu watapita juu yake, na kasi zao zitakuwa kiasi cha amali zao. Wapo watakaopita kama umeme, na wengine kama upepo, na wengine kama ndege, na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) atakuwa juu yake huku akisema: "Ya rabbi Sallim sallim" (Mwenyezi Mungu Salimisha Salimisha)

 

 

Na tunaamini kila kilichokuja katika mafundisho ya Mtume (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) kuhusu Siku hiyo pamoja na vitisho vyake - Tunamuomba Mwenyezi Mungu Atusaidie.

 

Rudi juu

Pepo Na Moto

Na tunaamini juu ya Pepo na Moto, na kwamba Pepo ni nyumba ya neema Aliyowaandalia Mwenyezi Mungu waja wake wema wamchao. Ndani yake mna yale ambayo macho hayajapata kuyaona, wala masikio kuyasikia wala halijapata kumpitikia mtu yeyote nafsini mwake.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Nafsi yoyote haijui waliyofichiwa katika hayo yanayofurahisha macho - ni malipo ya yale waliyo kuwa wakiyatenda."

As-Sajdah 17

 

 

Na Moto ni nyumba ya adhabu Aliyoitayarisha Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Taala kwa ajili ya makafiri madhalimu. Ndani yake mna kila aina ya adhabu ambazo hazijapata kumpitikia mtu yeyote nafsini mwake.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Na wakiomba msaada watasaidiwa kwa kupewa maji kama mafuta yaliyotibuka. Yatayowababua nyuso zao. Kinywaji hicho ni kiovu mno!"

Al-Kahf 29

 

Na Akasema:

 

. .

"Hakika Mwenyezi Mungu Amewalaani makafiri na Amewaandalia Moto unaowaka kwa nguvu. Watadumu humo milele. Hawampati mlinzi wala wa kuwanusuru. Siku ambayo nyuso zao zitapinduliwa pinduliwa katika Moto. Watasema: Laiti tungelimtii Mwenyezi Mungu, na tungelimtii Mtume!"

Al-Ahzaab 64 66

 

 

 

Maswali Ya Kaburini

Na tunaamini juu ya mtihani wa kaburini, wakati mtu atakapoulizwa nani Mola wake na ipi dini yake na yupi Mtume wake.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Mwenyezi Mungu Huwatia imara wenye kuamini kwa kauli imara katika maisha ya dunia na katika Akhera."

Ibraahiym 27

 

 

Na tunaamini juu ya neema za kaburini.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Wale ambao Malaika huwafisha katika hali njema, wanawaambia: Amani iwe juu yenu! Ingieni Peponi kwa sababu ya yale mliyokuwa mkiyatenda."

An-Nahl 32

 

 

 

Adhabu Ya Kaburini

Na tunaamini juu ya adhabu ya kaburini kwa madhalimu na makafiri.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Na lau ungeliwaona madhaalimu wanavyokuwa katika mahangaiko ya mauti, na Malaika wamewanyooshea mikono wakiwambia: Zitoeni roho zenu! Leo mtalipwa adhabu ya fedheha kwa sababu ya mliyokuwa mkiyasema juu ya Mwenyezi Mungu yasiyo ya haki, na mlivyokuwa mkizifanyia kiburi Ishara Zake."

Al-Anaam 93

 

Katika mlango huu zipo Hadiyth nyingi zilizo sahihi, na kila Muislamu anatakiwa aamini yote yaliyomo ndani ya Qur-aan na ndani ya Sunnah (Mafundisho ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) yanayohusu mambo ya ghaibu na wala asiyakatae kwa sababu hayalingani na mambo yanayotendeka duniani, kwani ya Akhera hayakisiwi na haya ya duniani kutokana na hitilafu kubwa sana iliyopo baina ya mawili hayo WaLlaahu l Mustaaan.

 

Rudi juu

Qadar

Tunaamini juu ya Qadar (kudra majaliwa - yale yaliyokwisha andikwa) kheri yake na shari yake kuwa yote yamekwisha andikwa na yote yanatokana na Mwenyezi Mungu na kwamba kisha waqadiria waja wake kwa elimu yake iliyokienea kila kitu.

Na Qadar imegawika sehemu nne.

 

1.  Ujuzi: Tunaamini kuwa Mwenyezi Mungu ni Ujuzi wa kila kitu, Anajua kilichotokea na kitakachotokea na namna inavyotokea, na hii inatokana na elimu yake isiyo na mwanzo wala mwisho ilichokienea kila kitu. Hakitokei kipya ikawa Mwenyezi Mungu Hakuwa na elimu nacho, na tunaamini kuwa Mwenyezi Mungu hasahau.

 

2.  Maandishi: Tunaamini kuwa Mwenyezi Mungu Ameandika katika ubao wa Lawh al-Mahfuudh yote yaliyotokea na yatakayotokea mpaka siku ya Qiyaamah.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Je! Hujui kwamba Mwenyezi Mungu Anayajua yaliyomo mbinguni na katika ardhi? Hakika hayo yamo Kitabuni. Hakika (kuyadhibiti) hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi."

Al-Hajj 70

 

3.  Kutaka: Tunaamini kuwa Mwenyezi Mungu Ametaka kiwepo kila kilicho mbinguni na ardhini, kwani hakiwezi kuwepo kitu chochote bila Yeye kutaka kiwepo. Anachokitaka kinakuwa na Asichokitaka hakiwi.

 

4.  Kuumba: Tunaamini kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Aliyeumba kila kitu.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wa kila kitu, na Yeye ndiye Mlinzi juu ya kila kitu. Yeye Anazo funguo za mbingu na ardhi."

Az-Zumar 63

 

Rudi juu

Kutaka kwa Mwenyezi Mungu

Na sehemu hii ya tatu imekusanya kutaka kwa Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Taala na kutaka kwa viumbe Vyake, kwa sababu Mwenyezi Mungu Anakijuwa kila kinachotendwa na waja Wake, na kwamba Yeye mwenyewe Ametaka kiwepo, ama sivyo kisingewezekana kutendeka.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

.

"Kwa yule miongoni mwenu anayetaka kwenda sawa. Wala nyinyi hamtataka isipokuwa Atake Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu wote."

At-Takwiyr 28 29

 

Na Akasema:

 

"Na lau kuwa Mwenyezi Mungu Alipenda wasingelipigana. Lakini Mwenyezi Mungu Hutenda atakavyo."

Al Baqarah 253

 

Na Akasema:

 

"Na lau kuwa Mwenyezi Mungu Angelipenda wasingefanya hayo. Basi waache na hayo wanayoyazua."

Al-Anaam 112

 

Lakini juu ya yote hayo, tunaamini pia kuwa Mwenyezi Mungu Amempa mwanaadamu uhuru wa kuamua na Akampa uwezo wa kutenda. Na ufuatao ni ushahidi kuwa mwanaadamu amepewa uwezo huo.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Basi ziendeeni konde zenu mpendavyo.'

Al-Baqarah 223

 

Na Akasema:

"Na ingelikuwa kweli walitaka kutoka bila ya shaka wangelijiandalia maandalio."

At-Tawbah 46

 

Kwa hivyo Mwenyezi Mungu Amempa mwanaadamu uwezo wa kutaka, kuamua na wa kwenda atakapo na kujiandalia atakavyo.

 

Pili, kule kuamrishwa kufanya mema na kukatazwa kufanya mabaya ni dalili kuwa mwanaadamu anao uwezo wa kufanya atakalo, maana kama asingekuwa na uwezo huo kule kukatazwa na kuamrishwa kusingekuwa na maana yoyote.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Mwenyezi Mungu Haikalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri iwezavyo."

Al-Baqarah - 286

 

Tatu, Mwenyezi Mungu Anamsifia Atendaye mema kwa wema wake, na Anamlaumu atendaye ovu kwa ovu lake. Mwanaadamu asingekuwa na uwezo wa kutenda atakalo basi pasingekuwa na haja ya kumsifia mwema wala kumlaumu muovu kwa sababu huko ni kumpa mtu sifa asiyoistahiki.

 

Nne, Mwenyezi Mungu Ameleta Mitume.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Mitume hao ni wabashiri na waonyaji, ili watu wasiwe na hoja juu ya Mwenyezi Mungu baada ya kuletewa Mitume."

An-Nisaa 165

 

Yangelikuwa matendo ya watu hayafanyiki kwa uwezo wao na uchaguzi wao, hoja yao isingebatilika kwa kuletewa Mitume.

 

Tano, kila mtu anapotenda jambo huhisi kuwa ametenda au ameacha kutenda. Utamuona anaposimama, anapokaa, anapoingia, anapotoka, anaposafiri, anapolala. Anapotenda lolote katika haya hufanya kama anavyotaka na wala hahisi kama yupo yeyote anayemlazimisha kufanya hayo, bali anaiona tofauti iliyopo anapofanya jambo kwa hiari yake mwenywe na anapolazimishwa, na hata shariah inatofautisha pale mtu anapofanya jambo kwa hiari yake na anapolazimishwa wakati Mwenyezi Mungu Hamuhesabii kuwa ametenda kosa mtu anayefanya jambo kwa kulazimishwa.

Wakati huo huo anayefanya maasi kwa hiari yake huyo anahesabiwa kama ni mkosa, kwa sababu amechagua kufanya hayo kwa hiari yake mwenyewe bila kuelewa kuwa Mwenyezi Mungu Keshamuandikia. Kwa hivyo hapana anayejua nini alichoandikiwa ila baada ya kutenda.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Na haijui nafsi yoyote itachuma nini kesho."

Luqmaan 34

 

Na Akasema:

 

"Watasema walioshirikisha: Lau kuwa Mwenyezi Mungu Angetaka tusingelishiriki sisi, wala baba zetu; wala tusingeliharimisha kitu chochote. Vivi hivi walikanusha waliokuwa kabla yao mpaka walipoonja adhabu yetu. Sema: Je, nyinyi mnayo ilimu mtutolee? Nyinyi hamfuati ila dhana. Wala hamsemi ila uongo tu."

Al-Anaam 148

 

Kwa hivyo tunamuambia mwenye kufanya maasi; 'Kwa nini usitende mema huku ukitegemea kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Alokuandikia uyatende? Kwa sababu hapana tofauti kwako baina ya mema na maovu kwa vile hujui nini ulichoandikiwa kabla ya kukitenda.'

 

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) alipowaambia Maswahaba (Radhiya Llaahu anhum);

"Kila mmoja keshaandikiwa makao yake ya Peponi na ya Motoni." Maswahaba (Radhiya Llaahu anhum) wakamuuliza: "Si bora tuache kufanya amali na tuyategemee tuliyokwishaandikiwa?" Mtume (Swalla Llaahu alayhi wa sallam) akawaambia: "Hapana! Bali fanyeni, kwani kila mtu amewepesishiwa yale ambayo kwa ajili yake ameumbiwa."

Na tunamuuliza mwenye kutenda maasi: 'Kwa mfano wewe unasafiri kwa gari kuelekea Makkah, ukakuta mbele yako njia mbili, mtu mkweli akakuambia kuwa ukipita njia ya mwanzo utakutana na vitisho vingi na utapambana na tabu, ama njia ya pili ni nyepesi na haina matatizo yoyote. Bila shaka utapita njia ya pili, na haiwezekani ukapita ya mwanzo ukasema; 'Nishaandikiwa', na kama utafanya hivyo, watu watakuona mwendawazimu.

 

Mfano mwengine; Ukifanikiwa kupata kazi mbili, mojawapo ina mshahara mkubwa sana na nyengine mshahara mdogo, ukaambiwa uchague, bila shaka utachagua ile yenye mshahara mkubwa. Basi vipi unajichagulia nafsi yako katika amali za Akhera zile zilizo duni kisha unasema kuwa 'Hivi ndivyo nilivyokadiriwa (nishaandikiwa)?

 

Unapoumwa kwa mfano, utawatafuta madaktari bora na utakubali kustahamili kupigwa sindano zenye kuuma au kufanyiwa operesheni na kustahamili kunywa dawa chungu, unafanya yote hayo ili upate kupona. Kwa nini basi huachi kujitibia na kusema; 'Nishaandikiwa?'

Rudi juu

Baadhi Ya Faida

Itikadi hii tukufu yenye mizizi mitukufu ina matunda mengi yenye faida nyingi ndani yake, na zifuatazo ni baadhi tu ya faida hizo:

 

Imani ya kumuamini Mwenyezi Mungu na majina Yake na sifa Zake vinaongeza mapenzi yetu kwa Mwenyezi Mungu na kumtukuza. Mambo ambayo kupatikana kwake kunasababisha kuzidisha hima ya kuisimamia dini na kujiepusha na makatazo ya Mwenyezi Mungu na kufuata maamrisho Yake Subhaanahu wa Taala kwa ajili ya kupata furaha ya duniani na ya Akhera.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Mwenye kutenda mema, mwanamume au mwanamke, naye akawa ni Muumini, tutamhuisha maisha mema; na tutawapa ujira wao kwa bora ya waliyo kuwa wakiyatenda."

An-Nahl 97

Rudi juu

Matunda Ya Kuamini Malaika

Kwanza; Tunapata kujua utukufu wa Aliyewaumba Subhaanahu wa Taala na kuzijua nguvu Zake na Ufalme wake.

 

Pili; Kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwalinda waja Wake, kwani Malaika hawa wamo miongoni mwao wenye kazi ya kuwalinda Waislamu na kuandika amali zao n.k.

 

Tatu; Kuwapenda Malaika kwa kumuabudu kwao Mwenyezi Mungu kwa ukamilifu, na kwa kuwaombea kwao maghfira Waislamu.

Rudi juu

 

Matunda Ya Kuviamini Vitabu

Kwanza; Tanapata kuielewa rehma ya Mwenyezi Mungu juu ya waja Wake, kwa vile Amewateremshia Kitabu kila umati kwa ajili ya kuwaongoza.

 

Pili; Tunaiona hekima ya Mwenyezi Mungu Aliyeweka ndani ya Vitabu hivi shariah zenye kunasibiana na kila umati, na akakifanya Kitabu cha mwisho kuwa Qur-aan tukufu ili kiwe kwa umati wote uliobaki katika zama zote na wakati wote mpaka Siku ya Qiyaamah.

 

Tatu; Tunapata kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema Yake hiyo.

 

Rudi juu

Matunda Ya Kuamini Mitume

Kwanza; Tunaijua rehma ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake Aliyewapelekea Mitume kwa ajili ya kuwaongoza.

 

Pili; Tunapata kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema Yake hiyo.

 

Tatu; Kuwapenda Mitume na kuwaheshimu na kuwapa sifa wanazozistahiki, kwani wao ni Mitume wa Mwenyezi Mungu waliochaguliwa miongoni mwa watu wote, wakamuabudu Mwenyezi Mungu kama Anavyostahiki kuabudiwa, wakaifanya kazi ya kuwalingania watu huku wakisubiri na kustahamili udhia.

Rudi juu

Matunda Ya Kuiamini Siku Ya Qiyaamah

Kwanza; Kumtii Mwenyezi Mungu kwa kutegemea kupata thawabu zitakazokufaa Siku ya Qiyaamah, na kuepukana na kufanya madhambi kwa kuihofia adhabu ya Siku hiyo.

 

Pili; Kumliwaza Muislamu kwa yale anayoyakosa katika neema za hapa duniani na anasa zake, akitegemea neema na anasa za Siku ya Akhera.

Rudi juu

Matunda Ya Kuamini Qadar

Kwanza; Kumtegemea Mwenyezi Mungu katika kila jambo, kwa vile vyote ni kwa uwezo Wake Mwenyezi Mungu.

 

Pili; Starehe ya nafsi na utulivu wa moyo, maana mtu anapotambua kuwa hapana kinachoweza kutokea bila Mwenyezi Mungu kutaka, moyo hutulia na nafsi huingiwa na matumaini akaridhika na kile alichomuandikia Mola wake. Na hapana mtu anayeishi maisha mazuri na mwenye nafsi iliyotulia kupita yule mwenye kuamini juu ya Qadar.

 

Tatu; Kuondoa majisifu pale mtu anapofanikiwa kupata analolitaka, kwani kupata chochote ni neema itokayo kwa Mwenyezi Mungu na kwa kuwa keshaandikiwa (keshajaaliwa) mtu huyo kuyapata mafaniko yale au kheri ile, kwa hivyo mtu huyo anatakiwa amshukuru Mwenyezi Mungu badala ya kujisifu.

 

Nne; Kuondosha hofu na uoga pale mtu anapokikosa anachokitaka au anapopata msiba kwani yote hayo yanatokana na Mwenyezi Mungu.

 

Mwenyezi Mungu Anasema:

 

"Hautokei msiba katika ardhi wala katika nafsi zenu ila umekwishaandikwa katika Kitabu kabla hatujauumba. Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi."

Al-Hadiyd 22

 

Tunamuomba Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Taala Atuthibitishe katika itikadi hii na Atuonjeshe matunda yake na atuongezee katika fadhila Zake na asizipoteze nyoyo zetu baada ya kuziongoza, na atumiminie rehma kutoka Kwake kwani Yeye ndiye Mpaji.

 

WalhamduliLlaahi Rabbil aalamin Mola wetu mswalie na msalimie Mtume wako Muhammad pamoja na Maswahaba wake na Aali zake wema, na kila atakayemfuata kwa wema na uongofu mpaka Siku ya Qiyaamah.