MAKABURI MSIKITINI
Muhammad
Faraj Salem Al Saiy
Kuna
baadhi ya kauli zilizotolewa na baadhi ya watu kuwa Haajar na baadhi ya Mitume
(‘Alayhimus Salaam) wamezikwa ndani ya Msikiti wa Makkah, na kwamba maneno hayo
yameandikwa katika vitabu vya historia.
Bila
shaka yoyote mwenye hoja hii anaelewa wazi kabisa kuwa waandishi wa historia
hawajiwekea shuruti za usahihi wa hadithi zao, pamoja na kufanya tahakiki juu
ya mlolongo wa wapokezi wa hadithi hizo (narrators), kwani wao hukusanya tu
habari na kuziandika. Ama vitabu vilivyo sahihi na vinavyojiwekea shuruti za
kuandika hadithi sahihi hapana hata kimoja kilichoandika juu ya jambo hilo.
Katika
kitabu cha Al-Jaami’ as-Swaghiyr mwandishi wake Al-Manaar anasema;
"Hakuna
hata moja katika makaburi ya Mitume yaliyo na uhakika kuwa wamezikwa hapo
isipokuwa kaburi la Mtume Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) peke yake,
ama kaburi la Nabii Muusa na Ibraahiym (‘Alayhimas Salaam) ni dhanna tu, na
wala hapana uhakika juu yake".
Kwa
hivyo kauli hizo haziwezi kuchukuliwa kuwa ni hoja, hasa katika mambo
yanayohusu itikadi za dini.
Ama
kuhusu kauli kuwa katika kisa cha Asw-haabul Kahf, baada ya kufa kwa watu hao,
palisemwa kuwa; ‘Watawajengea Msikiti’, hiyo pia si hoja, kwa sababu katika Aayah
hiyo hiyo imeandikwa kuwa; wenzao walisema;
"Jengeni jengo juu yao (wasipate kupita watu kuja kuwachungulia) Mola
wao Anawajua vyema (Basi inatosha)"
Wakasema
wale walioshinda;
"Bila shaka sisi tutajenga Msikiti juu yao" (yaani katika
pango)"
Ukichunguza
utaona kuwa waliotaka wajengewe jengo, ndio waliotoa hoja ya UchaMungu kuliko
hao walioshinda, na Mwenyezi Mungu hakueleza lolote katika hali zote mbili, na
maneno haya ndiyo yanayokubaliwa na maulamaa wengi, wa zamani na wa sasa,
akiwemo mwanachuoni wetu wa Afrika Mashariki Shaykh Abdullah Saleh Farsi
(Mwenyezi Mungu Amrehemu).
Isitoshe,
hata ikiwa tutakubali kwa ajili ya mjadala tu, basi kauli hii haileti maana
yoyote ya kututaka sisi tufuate maneno yao, kwani Mwenyezi Mungu Ametuletea
Mtume wetu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na akatufundisha yale anayotaka
kutoka kwetu, na miongoni mwa aliyotufundisha ni kauli yake (Subhaanahu wa Ta’ala)
katika hiyo Suratul Maidah, Sura ambayo ni ya mwisho kuteremshwa, kauli
isemayo;
“Likullin ja-alna minkum shir-ataw-wa
minhaaja”
"Na kila (Umma) katika nyinyi (binadamu) Tumeujaalia shari’ah yake
na njia yake".
Al-Maaidah:
48
Kwa
hivyo wao walikuwa na shari’ah zao na njia zao, na sisi tuna shari’ah zetu na
njia zetu. Kama vile wao walivyokuwa wakiruhusiwa kumsujudia kiumbe mwenzao
(Soma Surat Yuusuf) na waliharamishiwa kula baadhi ya nyama na shahamu, wakati
sisi tumeruhusiwa kula vyakula hivyo na tumeharamishiwa kumsujudia yeyote
mwengine asiyekuwa Mwenyezi Mungu.
Na
kwa vile Sura hii ya Al-Maaidah inajulikana kuwa ni Surah ya mwisho kuteremshwa
na kwa ajili hiyo kila kilichoandikwa ndani yake kinahesabiwa kuwa ni hukmu ya
mwisho kabisa.
Tukirudia
katika maudhui yetu ya Kaburi la Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam),
nilikwishanukuu hapo mwanzo kauli mbali mbali za Maulamaa zinazotofautisha hali
baina ya kaburi la Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na yale wanayozikwa
watu ndani ya Misikiti au kujengewa juu yake Misikiti.
Ndugu
zangu Waislam, hadithi sahihi ziko nyingi sana na zinaeleza kwa uwazi kabisa
kuhusu maudhui yetu haya;
Kutoka
kwa bibi ‘Aaishah (Radhiya Llaahu ‘anha) kuwa Ummu Habiybah na Ummu Salamah (Radhiya
Llaahu ‘anha) walimhadithia juu ya kanisa waliloliona walipokuwa katika nchi ya
uhabeshi, ndani yake mna picha nyingi, na bibi ‘Aaishah (Radhiya Llaahu ‘anha)
akamhadithia Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), na Mtume (Swalla Llaahu
‘alayhi wa sallam) akamwambia;
“Watu wale anapokuwa nao mtu mwema baina yao, basi anapokufa mtu huyo
wanajenga juu ya kaburi lake msikiti (mahala pa ibada), asha wanachora juu yake
picha hizo, hao ni watu wabaya kabisa kwa Mwenyezi Mungu”.
Al-Bukhaariy
na Muslim
Hadithi
nyingine;
Mtume
(Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema;
“Ghadhabu ya Mwenyezi Mungu imekuwa kali sana juu ya watu wanaoyageuza
makaburi ya Mitume yao na watu wema wao kuwa misikiti”.
Al-Bukhaariy
na Muslim
Na
akasema;
"Mola wangu usilijaalie kaburi langu likawa sanamu
linaloabudiwa".
Muslim
Na
akasema;
"Msiswali kuyaelekea makaburi wala msikae juu yake.”
Muslim
Na
akasema
"Mwenyezi Mungu Amewalaani Mayahudi na Manaswara wamegeuza makaburi
ya Mitume yao kuwa Misikiti".
Imepokelewa
na Maimamu wa Sunnah wote
Imesimuliwa
na Abdul Razak katika Musanaf yake kuwa;
"KAULI
YA MWISHO KABISA ALIYOITAMKA MTUME (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kabla ya
kuirudisha roho yake iliyotwaharika kwa Mola wake aliyeiumba, alisema;
"Mwenyezi Mungu Awaangamize Mayahudi na Manaswara, wameyageuza
makaburi ya Mitume yao kuwa mahali pa ibada, pasibaki na dini mbili katika bara
ya Arabuni".
Hadithi
hii pia imo katika Muwatwaa ya Imaam Malik
Kutokana
na hadithi zote hizi, ndiyo maana Maulamaa wetu wakatuambia kuwa ni haramu kuswali
ndani ya Misikiti iliyo na makaburi ndani yake, yote haya kwa ajili ya kuogopa
laana za Mwenyezi Mungu zisije zikatusibu kama zilivyowasibu Mayahudi na Manaswara
kwa ajili ya kuyageuza makaburi ya Mitume yao kuwa ni mahali pa ibada.
Hadithi
za aina hii zilizo sahihi ziko nyingi sana, na tukiendelea kuzitaja tunaweza
kujaza kurasa nyingi, isipokuwa ningependa kuongezea jambo moja, nalo ni kuwa,
Imam An-Nawawiy amezielezea hadithi hizi katika kitabu cha Adhkaar katika
mlango wa kutujulisha juu ya watu wanaostahiki kulaaniwa, akawataja hawa
wanaotenda mambo haya kuwa ni miongoni mwa watu hao wanaostahiki kulaaniwa.
Kwa
hivyo ni bora mtu ayakimbie mambo kama haya yenye kutatanisha na yanyomuingiza
mtu katika kundi la wanaostahiki kulaaniwa na badala yake kufuata yale yaliyo
dahiri na sahihi, yale yanayomkaribisha mja na radhi za Mola wake
Watu
hawa, wanasema Maulamaa kuwa wanayajengea makaburi hayo kwa niyah njema ya
kutaka kuwaigiza katika juhudi zao za kufanya ibada, lakini baada ya kupita
miaka mingi wakaja vizazi wasiotambua kusudi la kujengewa, Shaytwaan ataanza
kuwatia wasiwasi wake na kuwaambia kuwa wazee wao na babu zao walikuwa
wakiwaabudu, kisha na wao wakawaabudu. Na hii ndiyo sababu Mtume (Swalla Llaahu
‘alayhi wa sallam) akatukataza kufanya hivyo ili kuufunga mlango wa fitina
tokea mwanzo wake"
Mwenyezi
Mungu Anasema;
“Wamewafanya wanavyuoni wao na watawa wao kuwa ni miungu badala ya
Mwenyezi Mungu, na (wamemfanya) Masihi mwana wa Maryamu (pia Mungu), hali
hawakuamrishwa isipokuwa kumuabudu Mungu mmoja, hakuna anayestahiki kuabudiwa
ila Yeye. Ametakasika na yale wanayomshirikisha nayo”.
At-Tawbah:
31
Imepokelewa
kutoka kwa Imaam Ahmad na At-Tirmidhiy kuwa Uday bin Haatim At-Taaiy (Radhiya
Llaahu ‘anhu) aliyekuwa mkubwa wa kabila la At-Taaiy, kwamba aliposikia juu ya
kuja kwa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na dini ya Kiislam,
alikimbilia nchi ya Shaam, na hii ni kwa sababu kabila lake liliingia katika
dini ya Manaswara tokea wakati wa Jahilia (kabla ya kuja kwa Mtume (Swalla
Llaahu ‘alayhi wa sallam).
Katika
mapambano baina ya watu wake Uday bin Haatim At-Taaiy, na majeshi ya Waislam, dada yake
aitwae Savanah alikuwa miongoni mwa mateka waliotekwa na Waislam.
Mtume
(Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alipojua kuwa Savanah ni binti wa Haatim At-Taaiy aliyekuwa
akijulikana sana
na akipigiwa mifano kwa ukarimu wake, akamuacha huru. Aliporudi kwa kaka yake ambaye ni mkuu
wa kabila hilo kubwa, alimshikilia sana aingie katika dini ya Kiislam.
Wakatoka
pamoja kwenda Madiynah ili Uday amuone Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).
Alipokuwa amekaa chumbani kwa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na
msalaba wake alouvaa shingoni pake ukiwa unaning’inia kifuani pake,
ikateremshwa Aaayah hiyo hapo juu;
“Ittakhadhuw ahbaarahum wa ruhbaanahum arbaabam-min
duuni Llaahi…”
“Wamewafanya wanavyuoni wao na watawa wao kuwa ni miungu badala ya
Mwenyezi Mungu…”
Uday
akasema kumwambia Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam);
“Lakini hatukuwa tukiwaabudu ewe
Mtume wa Mwenyezi Mungu”.
Uday
masikini alikuwa akdhania kuwa ‘Ibada’ ni kumsujudia mtu au kumswalia.
Lakini Mtume (Swalla Llaahu
‘alayhi wa sallam) akamsahihisha na kumfundisha nini hasa maana ya ibada, akamuuliza;
“Si (hawa wanavyuoni wao na watawa wao) walikuwa wakiharamisha yale
aliyohalalisha Mwenyezi Mungu na wakihalalisha yale aliyoharamisha Mwenyezi
Mungu na wao wanawafuata?”
Akasema;
“Ndiyo walikuwa wakifanya hivyo”.
Mtume(Swalla
Llaahu ‘alayhi wa sallam) akasema;
“Basi huko ndiko kuwaabudu”.
Hapa
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) anatufundisha kuwa kuabudu, si lazima
kuwe kwa kusujudu au kuswali tu, bali hata kumfuata mwenye kuhalalisha haramu
na kuharamisha halali pia hiyo ni ibada.
Kisha Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi
wa sallam) akamwambia Uday (Radhiya Llaahu ‘anhu);
“Ewe Uday! Unasemaje, kwani unadhurika kitu wewe
panaposemwa ‘Allaahu Akbar? Kwani unakijua chochote
kingine kilichokuwa kikubwa kuliko Allaah?
Kwani
unadhurika wewe
panaposemwa ‘Laa
ilaaha illa Allaah’. Kwani unamjua mungu mwengine asiyekuwa Allaah?”
Kisha
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akamuita katika Uislam na Uday (Radhiya
Llaahu ‘anhu) akaitikia wito wake na akaitoa shahada ya haki.
Katika
mafundisho ya Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), tutaona anatukataza
kuyaabudu makaburi ya watu wema (wacha Mungu – au kama wanavyoitwa sasa
Mawalii).
Mtume
(Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema;
“Ghadhabu ya Mwenyeizi Mungu imezidi kwa
wale wanaogeuza makaburi ya Mitume yao na wacha Mungu wao kuwa mahala pa ibada,
Mola wangu usijaalie kaburi langu likawa mahali pa ibada”.
Muslim
Na
katika riwaya nyingine;
“Uslijaalie kaburi langu likawa
sanamu linaloabudiwa”.
Juu
ya kuwa imeshapita karne nyingi tokea alipofariki Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi
wa sallam), inasikitisha kuona kuwa mpaka leo katika nchi nyingi za Waislam bado wapo watu
wanaojishughulisha na ibada hizo za makaburi.
Ama
kuhusu kaburi la Mtume, hali yake inakhitililafiana kabisa na maudhui haya, kwa
sababu kwanza Msikiti huo haukujengwa juu ya kaburi hilo, wala Mtume (Swalla
Llaahu ‘alayhi wa sallam) hakuzikwa ndani ya Msikiti, isipokuwa katika upanuzi
wa Msikiti wakati wa utawala wa Banu Umayyah, kwa vile Mtume (Swalla Llaahu
‘alayhi wa sallam) alizikwa ndani ya nyumba yake iliyoambatana na Msikiti, ikabidi
kaburi hilo liwe ndani yake, na Maulamaa wakafanya kila njia na kuweza
kuuzungushia ukuta na kuutenga mbali na watu wanaoswali.
Hili
ndilo waliloweza, pamoja na kujenga viti vya saruji mahali ambapo watu
wangesimama kwa ajili ya kuswali, na kwa ajili hiyo haiwezekani mtu kusimama na
kuswali hapo, na wanaweza kukaa tu na kumswalia Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa
sallam) pamoja na kumuombea du’aa.