MANENO YA HEKIMA: UKARIMU

 

Na Hassan Hemed Abdallah.

Amesema Allah (S.W):

     “Mfano wa wale wanaotoa mali zao katika njia ya Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa punje moja iliyotoa mashuke saba, ikiwa katika shuke pana punje mia. Na Mwenyezi Mungu huzidisha amtakaye, (zaidi kuliko hivi) na Mwenyezi Mungu ni mwenye wasaa mkubwa na mwenye kujua.

       Wale wanaotoa mali zao kwa njia ya Mwenyezi Mungu, kisha hawafuatishi waliyoyatoa-masimbulizi wala udhia, wao wana ujira wao kwa Mola wao, wala haitakuwa hofu juu yao wala hawatahuzunika”. (Al baqarah 2:261, 262)

“Na wanakuuliza watoe nini? Sema “Vilivyokuzidieni”. (Albaqarah 2:219)

      “Wanakuuliza watoe nini? Sema” “Mali yoyote matakayotoa (toeni) muwape wazazi, akraba, mayatima, masikini na wasafiri (walioharibikiwa na waliokuwa kama hawa). Na wema wowote mnaoufanya Mwenyezi Mungu anajua”. (Al baqarah 2: 215)

     “Enyi mlioamini! toeni katika vile tulivyokupeni kabla haijafika siku amabayo hapatakuwa kujikomboa wala urafiki (wa kusaidiana) wala uombezi. Na waliokufuru ndio waliojidhulumu (kweli kweli)”. (Al baqarah 2:254)

      “Enyi mlioamini! toeni katika vile vizuri mlivyochuma, na katika vile tulivyokutoleeni katika ardhi. Wala msikusudie kutoa vilivyo vibaya, hali nyinyi wenyewe msingevipokea isipokua kwa kutoviangalia (basi Mungu atapokea kibaya?) basi jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni mkwasi na asifiwaye”. (Al baqarah 2:267)

        “Wale watowao mali zao usiku na mchana, kwa siri na dhahiri, wana ujira wao kwa Mola wao, wala haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika”. (Al baqarah 2:274)

        “Ambao huamini yasiyoonekana (maadam yamesemwa na Mwenyezi Mungu na Mtume wake na husimamisha sala na hutoa katika yale tuliyowapa”. (Al baqarah 2:3)

        “Maamkiano yao siku ya kukutana naye yatakuwa (ya salama) na amani, na amewaandalia malipo matukufu”. (Al Ahzab 33:44)

       Na miongoni mwenu atakayemtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake na kutenda mema. Tutampa malipo yake mara mbili na kuwaandalia riziki yenye hishima”.  (Al Ahzab 33:31)

       “Muamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na toeni katika yale aliyokupeni. Basi wale walioamini miongoni mwenu na wakatoa, wana malipo makubwa”. (Al-Hadyad 57:7)

      “Na huwalisha chakula masikini na mayatima na wafungwa, na hali ya kuwa wenyewe wanakipenda (chakula hicho)” (Ad-dahr 76:8)

“Soma na Mola wako ni karimu sana” (Alaq 96:3)

Amesema Mtume Muhammad (S.A.W): “Ogopeni moto japo kwa kutoa sadaka upande wa tende”.

      “Hakuna hata siku moja ambayo waja watapambazukiwa ila malaika wawili huteremka. Basi husema mmoja wao: “Ewe Mola! mpe mwenye kutoa badala yake”, na husema mwengine: “Ewe Mola! mpe mwenye kufutika asiyetoa hilaki (ya mali yake).”

      “Toa ewe mwanadamu! utapewa”, sadaka haipunguzi kitu katika mali.

Mtu mmoja alimuuliza Mtume (S.A.W): “Ni upi uislam uliokua boraakasema Mtume (S.A.W), "kulisha chakula, na kutoa salamu kwa unaemjua na usiemjua."

      “Mkarimu yuko karibu na Allah, yuko karibu na pepo, yuko karibu na watu”.

      “Mwenye kumuamini Allah na siku ya mwisho basi amkirimu mgeni wake”.

Amesema Imam Ally bin Abi Talib:

“Miongoni mwa amali bora zaidi kwa mkarimu ni kughafilika na anayo yajua”.

Amesema Abul-Fathi Al-bustiy:

        “Atakaekuwa mkarimu kwa ajili ya mali, watu wote wataelekea kwake. Na mali kwa mwanadamu ni fitina kubwa”.

Imesemwa:

        “Hakua mkarimu anaetoa baada ya kuombwa, lakini mkarimu ni yule anaetoa bila ya kuomba”.

“Ninaona watu marafiki wa ukarimu, wala sijaona bakhili katika ulimwengu kwa rafiki”.

Amesema Bibi Fatma (R.A)

“Aliye karibu mno miongoni mwenu na Allah ni aliye karimu mno kwenu”.

Amesema Imam Hassan bin Ally bin Abi Talib:

        “Atakae kuwa mkarimu atapata utukufu, na atakae kuwa bakhili atadharauliwa na kwa hakika aliye mkarimu mno kwa watu ni yule anaetoa na kumpa asiyetarajia kitu kwake na hakika mkombozi mkubwa kwa watu ni yule anayekomboa kutokana na kudra”.

Amesema Jabran Khalily:

          “Hakuwa mkarimu kwa kunipa mimi wakati haja yangu ni kubwa kuliko yako, bali mkarimu ni kunipa mimi hali yakuwa haja yako ni kubwa zaidi kuliko yangu”.

Amesema Goethe

“Nipe na usitaje na kuzungumza ulichonipa”.

Amesema:

“Mchirizi wa maji wenye kumwangilia ni bora kuliko mto usiomwagilia”.

        “Atakaetoa kwa ajili ya mali aliyokuwa nayo atapata utukufu na atakaetoa kwa ajili ya kupata utukufu atadhalilika”.

        “Aliyemkarimu mno miongoni mwa watu ni yule anaetoa kutokana na kichache alichonacho na akauhifadhi uso wa muombaji na kudhalilika”.

Maneno ya hekima ya Waarabu:

Jiepushe na uvamizi wa mkarimu anapohisi njaa, mnyonge anaposhiba.

Methali za Waaabu:

   Mkarimu anapotoa ahadi hutekeleza.

   Ukarimu hutokana na kuwepo.

Methali za Waswahili:

   Mwaka ni majira, leo mvua kesho jua.

   Kutoa ni moyo na wala sio utajiri