SUALI;

Nini hikma ya kuwaweka ushahidi wanawake wawili mbele ya mwanamume mmoja?

JAWABU;

AYA YA DENI

Aya ndefu kupita zote katika Qurani ni aya hii inayojulikana kwa jina la 'Aya ya

Deni' ambayo ndani yake imo kauli yake Subhanahu wa Taala isemayo;

".Na mshuhudishe mashahidi wawili katika watu wenu wanaume (Waislamu). Lakini ikiwa hakuna wanaume wawili, basi mwanamume mmoja na wanawake wawili (watatosha); katika wale mnaowakubali kuwa mashahidi. Ili kama mmoja wao (katika wale wanawake) akipotea, mmoja wao amkumbushe mwingine…."

Al Baqarah - 282

Maulamaa wengi wamejitahidi kuelezea sababu zao, wakijaribu kutafuta hekima ya kuwekwa mashahidi wanawake wawe wawili mbele ya mwanamume mmoja.

Wengine wameona kuwa sababu yake ni udhaifu wa wanawake katika kukumbuka, na ndiyo maana Mwenyezi Mungu akakamilisha kwa kutoa sababu ya uamuzi Wake akasema;

"Ili kama mmoja wao (katika wale wanawake) akipotea, mmoja wao amkumbushe mwingine…"

Wengine wakasema kuwa; Sababu yake ni kuwa wakati ule na katika jamii ile, kwa wanawake lilikuwa ni jambo geni kuingilia mambo kama haya yanayohusu biashara na hesabu na madeni, mambo yanayowahusu wanaume tu, na ndiyo maana Mwenyezi Mungu katika aya hiyo hiyo akasema;

"Wala asitiwe taabuni mwandishi wala shahidi"

Na wengine wakasema kuwa kwa sababu kimaumbile mwanamke ni mtu wa huruma sana na huitumia huruma hiyo zaidi kuliko anvyoitumia akili yake nk.

Lakini Sheikh Abdul Majeed Al Zindani anayejulikana sana kwa umahiri wake katika uwanja wa Miujiza ya Sayansi katika Qurani, alipokuja Abu Dhabi mara ya mwisho katika mojawapo ya mihadhara yake alituelezea juu ya uhakika mwingine mpya wa kisayansi unaohusiana na jambo hili. Uhakika huu alisema kuwa umegunduliwa hivi karibuni tu katika moja wapo ya vyuo vikuu vya huko Marekani (jina nimelisahau).

Sheikh alisema;

"Wataalamu wameguduwa kuwa bongo zetu zimegawiwa katika mafungu mengi yenye viungo vingi sana, na kila kiungo kina kazi yake maalum inayofanywa na viungo vyake mbali mbali. Kwa mfano, pana fungu linayofanya kazi ya kukumbuka tu, na ndani yake mna viungo vilivyogawiwa katika sehemu mbali mbali za kukumbuka. Vimo viungo vinavyofanya kazi ya kukumbuka ajali ziilizotokea hapo zamani na vingine vinakumbuka vichekesho tu nk.

Na pia vipo viungo vinavyofanya kazi ya kulia tu, na vingine kucheka na vingine kusema nk.

Ubongo wetu ni mfano wa kompyuta iliyojaa mafaili ya kila namna yaliyopangika kwa mpangilio wa kiajabu", amesema Sheikh Al Zindani.

Sheikh akaendelea kusema;

"Walifanya uchunguzi kwa njia ya kumpoteza mtu fahamu, kisha wakachukua fimbo za elctroni (electron rod) na baada ya kukibana kichwa kwa vibanio vya kitaalamu vilivyounganishwa na sehemu mbali mbali za ubongo zinazowezesha kufikisha yale yanayotokea ndani ya ubongo kupitia katika vibanio hivyo, na kuyawasilisha matokeo hayo na kompyuta kwa njia ya fimbo hiyo ya electroni. Wakawa wanaichukuwa fimbo hiyo na kuigusisha na sehemu hizo, na kila wanapogusa sehemu tofauti wanamuona yule mtu akifanya kitendo tofauti na kingine.

Kwa mfano; Wakimgusisha nacho sehemu moja yule mtu huanza kuzungumza juu ya ajali za zamani zilizomtokea, na wanapozigusisha na sehemu nyingine mtu huyo hucheka au hulia au hufanya jambo linalohusiana na sehemu ile iliyoguswa nk.

Ndipo walipogunduwa kuwa ndani ya bongo zetu mna mafaili kwa mamilioni zilizopangwa, na kila faili ina kazi yake maalum. Zipo sehemu zinazoshughulika na kuguswa, nyingine zinafanya kazi ya kusikia, nyingine kuona nk.

Wakamchukuwa mwanamke na mwanamume na kuanza kuwafanyia uchunguzi". Akaendelea kusema Sheikh Al Zindani, "Wakagunduwa kuwa kwa mwanamume na mwanamke, wote kila mmoja wao anavyo viungo viwili, kimoja kinafanya kazi ya kufikiri na kingine kazi ya kusema, na viungo hivyo vipo sehemu ya kulia ya bongo zao.

Baada ya kuvifanyia uchunguzi zaidi viungo viwili hivyo, wakagunduwa mambo ya ajabu. Waligunduwa kuwa mwanamume anaposema viungo viwili hivyo, kila kimoja kinafanya kazi yake sawa sawa. Ama mwanamke wamegunduwa kinyume na hivyo. Wameona kuwa mwanamke anaposema, basi viungo viwili hivyo vinaingiliana kazi zao. Yaani anaposema, basi kile kiungo cha kufikiri kinaacha kazi yake ya asili ambayo ni kufikiri na kujiunga na kiungo kinachofanya kazi ya kusema.

Na hivyo hivyo anapofikiri, kile kiungo cha kusema kinaiacha kazi yake ya asili ya kusema na kukisaidia kiungo cha kufikiri.

Ama mwanamume wameona kuwa yeye anapofikiri basi kiungo cha kufikiri kinafanya kazi yake bila ya kuingiliana na kiungo cha kusema na hivyo hivyo anaposema kile kiungo cha kusema kinafanya kazi yake sawa sawa bila ya kuingiliana na cha kufikiri.

Na hii huenda ikawa ndiyo sababu mwanamke anaposema, basi Mashaallah hawezekani na kwa kufikiri pia hawezekani maana wao hukumbuka hata yale mambo madogo kabisa ambayo kwa mwanamume ni vigumu kwake kukumbuka, kama vile rangi ya nguo au rangi ya vifungo au hata maneno ambayo kwa wanaume si rahishi kuweza kukumbuka.

Sasa tatizo linakuja panapotakiwa kutolewa ushahidi", anasema Sheikh Al Zindani.

"Kwa sababu katika ushahidi, mtu anatakiwa wakati mmoja awe anasema na awe anafikiri. Kwa mwanamke inakuwa tabu kwake kufanya hivyo kwa sababu ya kuingiliana kwa vile viungo vya kufikiri na kusema, ndiyo maana utawaona mara nyingi wanasema maneno mengi lakini bila kufikiri vizuri, na kwa ajili hivyo akahitajia mwenzake wa kukaa karibu yake na kufanya kazi ya kumkumbusha kumbusha kila anaposahau.

Shahidi wa pili wa kike hana kazi nyingine isipokuwa kumkumbusha tu mwenzake pale anaposahau. Ndiyo maana Mwenyezi Mungu akasema;

"Ili kama mmoja wao (katika wale wanawake) akipotea, mmoja wao amkumbushe mwingine…."

Al Baqarah - 282

Wallahu taala aalam

MUHAMMAD FARAJ SALEM AL SAIY