MIEZI MITUKUFU

 

Dunia imekamilika

Mwezi wa Dhul Hijja ni katika miezi iliyotukuzwa na Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala.

Mwenyezi Mungu anasema;

“Hakika idadi ya miezi kwa Mwenyezi Mungu ni miezi kumi na mbili katika hukmu ya Mwenyezi Mungu tangu alipoumba mbingu na ardhi. Katika hiyo iko minne mitukufu (kabisa).

Hiyo ndiyo Dini iliyo sawa. Basi msidhulumu nafsi zenu humo. Na piganeni na washirikina wote kama wao wanavyopigana nanyi nyote. Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu yu pamoja na wachaMungu”.

“Bila ya shaka kuakhirisha (miezi) ni kuzidi katika kukufuru; kwa hayo, hupotezwa walio kufuru. Wanauhalalisha mwaka mmoja na kuharimisha mwaka mwingine, ili wafanye kuwa sawa idadi ya ile (miezi) aliyo itukuza Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo huhalalisha alivyo viharimisha Mwenyezi Mungu. Wamepambiwa ubaya wa vitendo vyao hivi. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu makafiri”.

At Tawba – 36 – 37

Wakiisogeza miezi

Katika kuzifasiri aya hizi, Sheikh Abdulla Saleh Farsy (Mwenyezi Mungu amrehemu) amesema:

“Nabii Ibrahimu na Nabii Ismail waliwafundisha Waarabu kuihishimu sana sana miezi minne hii ; Dhul Qaedah (Mfunguo pili) – Dhul Hijjah (Mfunguo tatu) - Muharram (Mfunguo nne) na Rajab wasifanye jambo lolote baya, khasa kupigana (Vita). Lakini karne nyingi zilipopita waliionea uzito sharti hii ya kutopigana. Basi wakaanza kufanya ujanja wa kuikimbia kimbia. Wakaanza kuisogeza miezi ya mwaka. Badili ya kuwa mwaka mmoja una miezi kumi na mbili wakaifanya miezi kumi na tatu au zaidi ili ikawie kufika ile miezi mine inayokatazwa kupigana ndani yake.

Kwa hivyo kila mwaka wanapokutana Makka siku ya Arafa mmoja katika wakubwa wao (Mkubwa wa makabila ya Kiarabu) huinuka na kutoa habari kuwa mwaka huo mpya ujao waufanye mezi kumi na tatu au kumi na nne, kwa kuihisabu mara mbili baadhi ya ile miezi isiyokatazwa kupiganwa. Kama kusema:

“Ukiandama Mfunguo nne uliotukabili tuwite mwezi mpya; ‘Mfunguo tano wa mwanzo,’ na wa pili wake tuwite; ‘Mfunguo tano wa pili,” badala ya kuuwita Mfunguo sita.

Tena wa tatu ndio wauwite Mfunguo sita, ili miezi minne (iliyoharamishwa kupigana) ikawie kufika.

Ndio Mwenyezi Mungu anawalaumu hapa na kuonyesha kuwa japo wanaitukuza miezi minne katika mwaka, lakini miezi minne la haiwi thuluthi ya mwaka kwani mwaka wanauzidisha miezi mingine kusudi, ili ikawie kufika”

(Mwisho wa maneno ya Sheikh Abdullah Saleh.

 

Kutoka kwa Abibakra Nafiu bin Al Harith (Radhiya Llahu anhu) amesema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) alipowahutubia Waislamu katika Hija yake ya mwisho ‘Hijjatul Wida'a’, alisema:

“Hakika dunia imekamilika kama ilivyokamilika siku ile Mwenyezi Mungu alipoziumba mbingu na ardhi. Mwaka una miezi kumi na mbili. Ndani yake imo (miezi) minne Mitukufu, mitatu imekamatana Dhul Qaeda, Dhul Hijja na Muharram. Na Rajab (upo peke yake) baina ya Jamaad na Shaabani. Huu (mwezi tulio ndani yake) ni mwezi gani?

Tukasema;

Mwenyezi Mungu na Mtume wake ndio wajuao zaidi

Akanyamaza, hata tukadhani kuwa labda ataubadilisha jina.

Kisha akauliza:

Huu si mwezi wa Dhul Hijja?

Tukamjibu: “Ndiyo

Akauliza:

Mji gani huu?

Tukasema: “Mwenyezi Mungu na Mtume wake ndio wajuao zaidi.

Akanyamaza hata tukadhania kuwa labda ataubadilisha jina lake.

Kisha akasema: “Huu si Mji (Mtukufu)?”

Tukamjibu: “Ndiyo.”

Kisha akauliza: “Siku gani hii?”

Tukamjibu: “Mwenyezi Mungu na Mtume wake ndio wajuao zaidi

Si siku ya Al Nahr hii (Siku kuu mosi kubwa)?”

Tukamjibu:

Ndiyo.”

Akasema:

Hakika damu zenu na mali zenu na heshima zenu ni tukufu baina yenu kama ulivyo utukufu wa siku hii yenu katika mji huu wenu katika mwezi huu wenu. Na Mtakuja kuonana na Mola wenu na atakuulizeni juu ya amali zenu, basi msije mkarudi baada yangu (baada ya kufa kwangu) mkawa makafiri mnakatana shingo wenyewe kwa wenyewe. Aliyehudhuria amjulishe asiyehudhuria…

Kisha akasema:

Si nimefikisha?”

Tukasema: “Ndiyo

Akasema:

Mwenyezi Mungu shuhudia

Bukhari na Muslim

Sababu za kutukuzwa

Kalenda ya Kiislam (Al Hijri) ina miezi kumi na miwili sawa na kalenda ya Gregory, isipokuwa majina ya miezi yake inakhitalifiana, na idadi ya siku chache pia inakhitalifiana.

Yafuatavyo ni majina ya miezi ya kalenda ya Kiislamu (Al Hijri):

Miezi mitukufu nimeiandika kwa herufi kubwa:

1.   MUHARRAM (Mfunguo nne)

2.   Safar

3.   Rabiul Awwal (Mfunguo sita)

4.   Rabiul Thani

5.   Jamadul Awwal

6.   Jamadul Thani

7.   RAJAB

8.   Shaaban

9.   Ramadhan

10. Shawwal

11. DHUL QAEDA (Mfunguo pili)

12. DHUL HIJJA (Mfunguo tatu)

 

Maulamaa wanasema kuwa Mwenyezi Mungu ameiteuwa miezi minne hiyo kuwa mitukufu na kukataza watu kupigana vita ndani yake kwa sababu maalum; nayo ni kuwawezesha watu kwenda Makka kufanya Ibada ya Hija na ya Umra kwa amani na kurudi makwao kwa amani.

Ameuteuwa mwezi wa Dhul Qaeda (Mfunguo pili) ulio kabla ya mwezi wa Dhul Hijja (Mfunguo tatu), ili watu waweze kusafiri kutoka makwao kuelekea Makka bila ya kudhuriwa. Na akauchagua mwezi wa Dhul Hijja kwa ajili ya kuifanya ibada hiyo ya Hija kwa amani. Kisha akautukuza mwezi wa Muharram ili watu baada ya kuhiji waweze kurudi makwao kwa amani.

Ama mwezi wa Rajab ulio kati kati ya mwaka, Mwenyezi Mungu ameutukuza kwa ajili ya kuwawezesha watu kwenda Makka kuizuru nyumba, na kwa ajili ya kufanya Umra.

 

Kisha Mwenyezi Mungu akasema:

Hiyo ndiyo Dini iliyo sawa”

Na maana yake ni kuwa huo ndio mwenendo ulio sawa wa kuiheshimu miezi hiyo na kutopigana vita ndani yake kama anavyokutakeni Mola wenu.

Kisha akamalizia kwa kusema:

Basi msidhulumu nafsi zenu humo”.

Na maana yake ni kuwa; msidhulumu nafsi zenu katika miezi hii minne ambayo ni mitukufu, na hasa katika mji mtukufu au kwa kuwafanyia maovu wale waendao kufanya ibada hii tukufu.

Msidhulumu nafsi zenu

Wafasiri wengine wamesema kuwa maana ya kauli ya Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala:

Msidhulumu nafsi zenu”, Ni katika miezi yote kumi na miwili, isipokuwa katika miezi minne hiyo dhambi zake huwa kubwa zaidi.

Imam Shafi na baadhi ya maulamaa wanaona kuwa malipo ya Fidya katika miezi hii ni kubwa zaidi kupita katika miezi mingine kutokana na ukubwa wa dhambi ndani yake.

Ama Ibni Abbas (Radhiya Llahu anhu) akiifasiri aya hii alisema:

Basi msidhulumu nafsi zenu humo,” ni katika miezi yote,  kisha Mwenyezi Mungu akaihusisha miezi minne hiyo, akaitukuza na kulifanya tendo la dhambi katika miezi hiyo kuwa ni kubwa na matendo mema pia ujira wake akaufanya kuwa ni mkubwa”.

Ama Qatada yeye anasema:

“Hakika ya dhulma na dhambi katika miezi mitukufu malipo yake ni makubwa zaidi kupita katika miezi mingine, ingawaje dhulma kwa vyovyote dhambi yake ni kubwa sana. Lakini Mwenyezi Mungu hutukuza na kuteua anavyotaka. Mwenyezi Mungu ameteuwa na kuvitukuza vingi katika viumbe vyake. Ametukuza miongoni mwa Malaika akawajaalia wengine kuwa ni wajumbe, na katika wanadamu pia akawateuwa wengine kuwa Mitume, na katika maneno, ameteuwa utajo wa Mwenyezi Mungu Dhikri, na katika ardhi, akateuwa misikiti kuwa ni mwahali bora, akateua katika miezi mwezi wa Ramadhani pamoja na miezi hiyo Mitukufu kuwa ni bora, na katika siku akaiteuwa siku ya Ijumaa na katika usiku ameuteuwa usiku wa Laylatul Qadr, kwa hivyo tukuzeni yale aliyoyatukuza Mwenyezi Mungu, na hayatukuzi yale aliyoyatukuza Mwenyezi Mungu isipokuwa mwenye kufahamu na mwenye akili”.

Mwenyezi Mungu anasema:

Enyi mlioamini! Msivunje hishima ya alama za (dini ya) Mwenyezi Mungu wala (hishima) ya mwezi uliotukuzwa….”

Al Maidah – 2

Wanakuuliza

Masahaba (Radhiya Llahu anhum) walipigina na makafiri waliokuwa wakiongozwa na Amru bin Al Hadhramiy huko Taif, wakidhani kuwa siku hiyo ilikuwa ni usiku wa mwisho wa mfunguo tisa (tarehe 30 Jamadul thani). Hawakujua kuwa mwezi wa Rajab ambao ni katika miezi mitukufu umekwishashaingia.

Amru bin Al Hadhramiy aliuliwa, na Waislamu wakateka kila kilichokuwemo ndani ya  msafara wa makafiri hao.

Makafiri wakaenda kumsikitikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) na kumlaumu kuwa amevunja heshima ya miezi mitukufu.

Ndipo Mwenyezi Mungu alipowateremshia aya zifuatazo kuwafahamisha kuwa kupigana vita katika miezi hiyo ni dhambi kubwa sana, lakini yale wanayofanya wao katika kuwatesa, kwauwa na kuwazuwia Waislamu wasiilinganie dini ya Mwenyezi Mungu, dhambi yake ni kubwa zaidi.

Mwenyezi Mungu anasema:

Wanakuuliza juu ya kupigana vita katika mwezi mtakatifu. Sema: Kupigana vita wakati huo ni dhambi kubwa. Lakini kuzuilia watu wasende katika Njia ya Mwenyezi Mungu na kumkanusha Yeye, na kuzuilia watu wasende kwenye Msikiti Mtakatifu na kuwatoa watu wake humo, ni makubwa zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. Na fitina ni mbaya zaidi kuliko kuuwa. Wala hawatoacha kupigana nanyi mpaka wakutoeni katika Dini yenu kama wakiweza. Na yeyote katika nyinyi akiacha Dini yake akafa naye ni kafiri, basi hao ndio ambao a'mali zao zimeharibika duniani na Akhera. Na hao ndio watu wa Motoni; humo watadumu.

Al Baqarah – 217

Ibada ndani yake

Kutoka kwa Abu Hurairah (Radhiya Llahu anhu) amesema:

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) aliulizwa;

Swala ipi iliyo bora baada ya zile za fardhi?

Akajibu:

Sala katika usiku wa manane.”

Kisha akaulizwa:

Saumu ipi iliyo bora baada ya funga ya Ramadhani?”

Akajibu:

Mwezi mnaouita Muharram”.

Muslim na Abu Daud.

 

Mtu mmoja kutoka mji uitwao Baahila alimwendea Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam)  na kumuambia:

Ewe Mtume Wa Mwenyezi Mungu, mimi ni yule mtu aliyekujia mwaka uliopita”.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) akamuuliza:

“Nini kilichokufanya ubadilike hivi, kwani ulikuwa na umbile zuri?”

Akasema:

Sikuwa nikila chakula isipokuwa usiku tu tokea siku ile tulipoachana

(na maana yake ni kuwa mwaka mzima alikuwa kila siku akifunga).

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa Sallam) akamuuliza:

Kwa nini umejiadhibisha nafsi yako hivi?

Kisha akamuambia:

Funga Mwezi wa Subira (Ramadhani), kisha funga siku moja kila mwezi”.

Yule mtu akasema:

Niongezee, kwani ninao uwezi wa kufunga zaidi”.

Akamuambia:

Funga siku mbili.”

Akasema: “Niongezee

Akasema:

Funga katika miezi mitukufu uache, funga katika miezi mitukufu uache”,

huku akiashiria vidole vitatu kisha akivikunja. (akimjulisha kuwa ndani ya Miezi mitukufu afunge siku tatu kisha ale siku tatu).

Abu Daud, Ibni Majah na Al Baihaqi.

Anasema Sayid Sabeq mwenye kitabu cha Fiqhi Ssunah:

Funga ya Rajab ina fadhila zaidi kupita miezi mingine si kwa sababu nyingine isipokuwa ni kwa kuwa mwezi huo ni katika ile Miezi mitukufu”.