MJUWE SAHABA THUMAMA BIN UTHAAL AL-HANAFIY.

na Suleyman Mohd Said.

 

  • Alisilimu baada ya kuachwa huru.
  • Aliuangusha uchumi wa makafiri wa Makka.
  • Ni sahaba wa mwanzo kuleta Talbiya mbele ya makafiri wa Makka
  • Aunusuru uislam baada ya kufariki Mtume SAW

 

Katika mwaka wa sita tokea kuhamia Madina, Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) aliamua  kueneza ulinganio wa kiislam kwa watu wasiokuwa waarabu wa Makka  na akandika barua nane kwenda kwa wafalme wa kiarabu na wafalme wasio waarabu  na alikuwa miongoni mwa aliowaandikia barua ni Thumaamah bin Uthaal Al-Hanafiy huyo alikuwa kiongozi wa kiarabu na bwana miongoni mwa mabwana wa kabila la Hanafiy na mfalme Al- Yamaamah ambaye amri yake haipingwi. Na alipata barua ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) hali ya kuwa mwenye kudharau, kisha akajitakasa yeye na makosa yake na akaziba masikio yake kusikiliza ulinganio wa haki na wa kheri  akapandwa na shetani na shetani akampoteza kutaka kumuua Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) na akapata fursa ya kumuua Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) lakini akashindwa na Mwenyezi Mung u akamuokoa Mtume wake kutokana na shari hiyo.

 

Lakini Thumaamah alishindwa kumuuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) na badala yake kuwaua masahaba wengi katika uuwaji mbaya na wenye kutisha  na haikupita muda mkubwa akaamua kwenda kufanya ibada ya umra na alipofika njiani karibu na Madina akatekwa na waislam na wakamchukua Madina pamoja na watu wake na wakafungwa katika nguzo za msikiti wa Madina ili kumsuburi Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) atoe hukmu juu ya mateka hao, na pale alipoingia Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW)msikitini akamuona Thumaamah amefungwa katika nguzo na akasema Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) kuwaambia masahaba zake “jee munamjua nani muliyemteka?” Wakajibu  “hatujui ewe mjumbe wa Allah”  na akasema Mtume huyo ni Thumaamah bin Uthaal Al-Hanafiy mfanyieni wema wala musimtese  kisha akarejea Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) kwa watu wake akawaambia kusanyeni mlicho nacho miongoni mwa vyakula na mpelekeeni Thumaamah, kisha akaamrisha ngamia wake akamwe maziwa asubuhi na jioni ili apelekewe na yakatekelezwa yote hayo kabla Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) hajaonana naye na akazungumza naye, baada ya hapo Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) akonana naye kwa ajili ya kumlingania katika uislam na akamuuliza “una nini ewe Thumaamah?” Akasema “mimi ni mzima kabisa ewe Muhammad……pindi ukiniuwa basi unauwa binaadamu …….. na pindi utanineemesha basi unamneemesha mwenye kushukuru…….. na ukiwa unataka mali basi sema nitakupa kila unachotaka”. 

 

Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) akaondoka akamuacha siku mbili, kisha akaonana naye tena mara ya pili akamwambia “una nini ewe Thumaamah?”,  Akajibu “sina chochote isipikuwa kama nilivyokuambia kabla”.

 Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) akamuacha na akamjia siku nyengine na akamuuliza suala lile lile la mwanzo nae akajibu jibu lake lile lile, Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) akawaelekea masahaba kisha akawaambia kuwa wamuachie huru bwana huyu nao wakatii amri.

 

 Bwana Thumama baada ya kufunguliwa akaondoka hadi akafikia karibu na mwisho wakutoka katika mji wa Madina karibu na sehemu inayoitwa Bakii, akakuta maji akakoga kisha akarudi Madina mpaka akafika  katika msikiti wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) na akasilimu mbele ya masahaba kisha akaelekea kwa Mtume na akamuambia “Ewe mjumbe wa Allah hakika nilikuwa nikikuchukia kabla ya kusilimu kwangu kuliko watu wote duniani, lakini baada ya kusilimu hakuna mtu ninayempenda katika ulimwengu huu zaidi yako  ewe! Mtume nimewauwa waisilamu wengi kabla kusilimu kwangu kwa hivyo nini nifanye ili niweze kusamehewa madhambi yangu?”.  Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW)akamjibu “ hakika Uislam unafuta yale madhambi yote yaliyotangulia.” Kisha akasema sahaba huyu kumuambia Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW)kuwa “h akika nitawauwa makafiri kuliko nilivyowauwa waislam na nitajifungamanisha na upanga wangu huu pamoja na watu wangu katika kukuokoa wewe pamoja na dini ya kiislam”, kisha akamuomba Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW)amruhusu aende Makka akatimize ibada ya Umrah ambayo aliikusudia kuifanya lakini kwa namna walivyoizowea Makafiri na Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW)akamruhusu na akamwambia nenda lakini iwe kwa namna alivyoataka Allah na Mtume wake na hapo ikabidi afundishwe namna ya kufanya Umra ndipo akaelekea Makka.

          

Thumama alipofika Makka akazisoma Talbiya (ni takbira zinazosomwa kwa mwenye kufanya ibada hii na Hijja baada ya kuhirimia na inasuniwa kuzileta kwa sauti ) huku anaingia katika mji wa Makka nae ni muislam wa kwanza kudhihirisha talbiya katika mji wa Makka. Makafiri waliposikia talbiya zile wakataharuki na kuchanganyikiwa na huku wakijiandaa kwa mapambano kwa kuchukuwa panga zao wakidhani kuwa washaingiliwa na waislam huku wakiifuata sehemu itokapo sauti na walipomjuwa kuwa ni bwana Thumama ndie anaeleta talbiya zile wakanywea kwa kumuona mtu mkubwa kama huyu kuweza kusilimu.

 

Mmoja kati ya vijana wa Kikureshi alitaka kumrushia mshale ili amuuwe lakini vigogo wa Kikureshi wakamkanya na kumtahadharisha kuwa si mtu wa kufanyiwa uadui, bwana Thumama aliendelea kuleta talbiya zake huku anawapitia Makafiri kwa ufakhari na akawaambia, “Enyi makafiri ikiwa mtanidhuru basi nitakukatieni kukuleteeni chakula na mtakufa kwa njaa”. Hapo tena Makureshi wakamuuliza “una nini ewe Thumama? Umeiwacha dini yako na kuwatukana mababu zako?” Akawajibu “hakika mimi sijawatukana mababu zangu bali nimeifuata dini iliyo bora kuliko dini zote”  kisha akawaambia “ Naapa kwa jina la Mola Mtukufu hakika nitakaporudi Yamama haitokufikieni hata chembe moja ya chakula mpaka muifuate dini ya Muhammad”.

 

Baada ya hapo akafanya Umra yake kisha akaondoka kurudi kwao na alipofika tu kwa watu wake akawazuia kutuma chakula kwa watu wa Makka na kutokana na hali hiyo watu wa Makka wakafikwa na hali mbaya ya uhaba wachakula hadi kuhatarisha maisha yao na vitu vikapanda bei jambo ambalo likawapelekea wamuandikie Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW)na kumuomba awaombee kwa bwana Thumama alete chakula Makka wakaandika barua kuelekea Madina yakiwemo maneno haya: “ Ewe Muhammad hakika ahadi yetu kwako kuwatembelea jamaa na hakika umekata mawasiliano kwetu na kuwaua watoto wetu na baba zetu kwa upanga na sasa unawauwa watoto wetu kwa njaa na hakika Thumama bin Uthaal ametukatia sisi chakula na ametudhuru, hivyo ukiona barua hii muandikie au muambie  atuletee yale aliyoyazuia ambayo tunatahitaji basi fanya hivyo”. 

 

Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW)alipoipata barua hii hapo hapo akamuandikia barua bwana Thumama ili awapelekee chakula ndipo bwana Thumama akawaruhusu watu wake kupeleka  chakula na shida ikaondoka  haya yote yalikuwa ni kutokana na imani yake juu ya dini hii na matendo yake ameyafungamanisha na matakwa ya Bwana Mtume SAW.

              

Kutokana na haya yaliyotokezea nayo ya kusilimu Bwana huyu kwa khiyari yake baada ya kuachwa huru na Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) kuwafungulia mlango wa kupelekewa chakula Makafiri wa Makka tunafahamu namna ya uislam ulivyokuwa ukilinganiwa  wala haikuwa upanga ndio sababu ya kusilimu watu kama inavyodaiwa na maadui wa dini hii, bali ilikuwa ni tabia njema za Mtume wetu Muhammad SAW na ulinganiaji wa khiyari ndio uliosababisha watu wengi kuukubali Uislam kwa imani thabiti na hata sahaba huyu alipoulizwa kwa nini ukasilimu baada ya kuachiwa huru tu? “Akasema kuwa hakika mani iliniingia tokea nilipofungwa lakini lau ningesilimu ingesemwa kuwa nimesilimu ili niwachwe huru ndipo nilipokuwa huru nikasilimu kwa khiyari yangu”. Kwa kweli aliyoyaona bwana huyu wakati alipofungwa kiasi asilimu kwani Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW)kama tulivyoona aliamrisha afanyiwe wema na kupelekewa chakula kila wakati wa kula hakikuwa chakula cha kutupwa kama wanavyofanyiwa wafungwa wengi duniani ,  bali kilikuwa ni chakula cha minal ali haya ni kufahamisha kuwa uislam si dini ya uadui na mateso bali ni dini ya upendo na rehema.

 

Thumama alikuwa ni miongoni kwa waliosimama kidete kuinusuru dini hii ya kiislam baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) kuondoka ulimwenguni,  kwani walijitokeza baadhi ya waislam kurudi katika dini zao za zamani kwa kudhani kuwa dini hii ni dini ya Muhammad akifa na dini imekufa na wamesahau kuwa dini hii ni ya mwenyewe Allah aliyetuumba na hakuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) isipokuwa ni mjumbe tu kwa watu wote .

 

Tena alipotaka Musaylamatil Kadhab kuwatowa watu wa kabila la Hanafi katika Uislam kwa kuwshawishi na kudai kuwa Utume umebaki kwake akasimama sahaba huyu bwana Thumama na kuwalingania watu wake wa kabila la Hanafi na kuwatahadharisha kuiwacha dini yao ya kiislam na akawaambia “hakika Muhammad ni Mtume wa mwisho hakuna Mtume baada yake  kisha akawasomea aya hizi za suratul Ghafir zenye maana yafuatayo:

“Ha mim, Uteremsho wa kitabu umetoka kwa Allah mwenye nguvu mwenye kujuwa, Anaesamehe dhambi na kupokea toba mkali wa kuadhibu mwenye ukarimu hakuna Mungu illa yeye na marejeo ni kwake.”

Baada ya hapo watu hao wakamuunga mkono na wakawa ni miongoni mwa waislam wanaolingania watu wasije wakatoka katika dini hii na wakaungana na Khalifa Abubakar bin Siddiq katika kuwapiga vita wale waliyortadi .

Mola ampe bwana Thumama bin Uthaal kheri na amkirimu pepo yake ambayo ameahidi kwa wenye kumtii. “AMIN”.