Nyoyo hukutana angani;. 1

Madhambi yanapozidi moyo hupigwa mhuri;. 2

Mchungeni Mola wenu;. 4

Athari ya Maasi;. 5

Mitihani;. 6

Maymun bin Maharan;. 8

Adhabu za nyoyo;. 10

Kuutakasa Moyo;. 12

Kuishi ndani ya siku yako. 14

Siha ni Ufalme. 16

Dhiki ya Nafsi 18

 

MOYO SAFI

Nyoyo hukutana angani;

Impokelewa kuwa siku moja Omar bin Khattab (RA) alimuuliza Ali bin Abu Talib (RA);

"Ewe Abal Hassan (baba yake Hassan), huenda ikawa umeona na kusikia yale ambayo mimi sikuona wala kusikia, kama vile huenda ikawa nimeona na kusikia yale ambayo wewe hukuona wala kusikia. Nina masuali nataka kukuuliza kama unayo elimu juu yake."

Ali (RA) akamwambia;

"Uliza"

Omar (RA) akasema;

"Mtu anampenda mwenzake juu ya kuwa hajaona kheri yoyote kutoka kwake, na mwengine anamchukia mwenzake (bure bure tu) juu ya kuwa hajaona ubaya wowote kutoka kwake."

Ali (RA) akasema;

"Ndiyo, nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) akisema; "Hakika nyoyo ni askari waliotayarishwa. Zinakutana (nyoyo) angani, kisha zile zinazochunukiana zinapendana, na zile zinazokhitalifiana zinachukiana."

Omar (RA) akasema;

"Moja hiyo. Ama suali la pili; Mtu huwa anahadithia jambo kisha ghafla anasahau, kisha mara baada ya kusahau anakumbuka tena."

Ali (RA) akasema;

"Ndiyo, nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) akisema;

'Kila moyo hupitiwa na kiwingu kama kiwingu cha mwezi. Utauona mwezi ukiangaza, kisha ghafla unapitiwa na kiwingu na kuufunika, na mara kinapoondoka kiwingu hicho mwezi unaangaza tena "

Sahih Al Jamea.

Ndugu yangu Muislamu, usiuendekeze moyo wako ukapenda na kuchukia kwa matamanio ya nafsi, ukaipenda dunia na kuichukia akhera, au ukaipenda batil na kuichukia haki bure bure tu, eti kwa sababu moyo wako haujampenda yule aliyekujulisha haki hiyo. Ukiendelea kuiendekeza nafsi yako basi hutoweza kuiona haki wala kuifuata. Ukitaka kufanikiwa, nenda kinyume na nafsi yako na umtii Mola wako, kwani nafsi siku zote inaamrisha maovu, na kumbuka kuwa jihadi ya nafsi ni kubwa kupita jihadi ya mwili.

Anasema Abdul Qader al Jaylani (Mwenyezi Mungu amrehemu);

"Ukishindwa kuimiliki nafsi yako usitegemee kupata mafanikio kutoka kwa Mola wako, kwani Mwenyezi Mungu yuko pamoja na mwenye kumtii na mwenye kujipendekeza Kwake. Utakuwaje karibu na Mfalme wakati nafsi yako si safi na haikutahirika kutokana na najsi. Jipunguzie tamaa ya kuwa utaishi milele, kisha iwaidhi nafsi yako kwa mafundisho ya Mtume wako (SAW).

Wewe ndiye mwenye kustahiki zaidi kuionea huruma nafsi yako. Sasa ikiwa wewe mwenyewe huionei huruma unategemea nani atakuhurumia? Jitahidi katika kuipunguzia matumaini, na daima ikumbushe juu ya kifo na katika kumchunga Mwenyezi Mungu. Iambie;

'Faida uliyoichuma ni yako na hasara uliyoichuma ni juu yako'.

Hapana atakayekupa katika thawabu zake, huna budi kuzifanyia kazi wewe mwenyewe, (na kumbuka kuwa siku hiyo hatofuzu isipokuwa atakayekuja kwa Mola wake na Moyo Safi.)"

Janatu naimu          fil Jinani

Jini na Insi             wanaitamani

Jumla ya watu        Hawaioni

Ila kwa amali          Kutaqadama

Thamani ya Pepo   Ukiitaka

Thiqi moyo wako  kutozunguka

Thubutisha taa       Yake Rabuka

Ili akujazi               Majaza mema

(Shairi nimenukuu kutoka katika tafsiri ya Sheikh Abdullah Saleh Al Farsy – Mwenyezi Mungu amrehemu)

Madhambi yanapozidi moyo hupigwa mhuri;

Kuyadharau madhambi ni moja katika sababu kubwa ya kudhoofika kwa moyo, nayo hurimbikika juu ya mtu mpaka yakamuangamiza.

Imepokelewa kutoka kwa watu wema kuwa;

"Mcha Mungu anapotenda dhambi ndogo huiona kama jabali juu ya kichwa chake, ama mtu asi huiona dhambi kubwa kama nzi anayemkera puani akamfukuza kwa mkono wake."

Katika hadithi iliyosimulia na Al Bayhaqiy anasema Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW);

"Hakika nyoyo zinaingia kutu kama chuma kinavyoingia kutu."

Wakamuuliza; "Vipi unasafika ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?"

Akasema;

"Kusoma sana qurani na kumtaja sana Mwenyezi Mungu."

Na katika hadithi nyingine Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) amesema;

"Hakika Muislamu anapotenda dhambi linaingia ndani ya moyo wake doa jeusi, na anapotubu na kuomba maghfira doa hilo hufutika, na anapofanya tena madhambi, madoa nayo yanaongezeka mpaka rangi ya moyo inageuka kuwa nyeusi, na hiyo ndiyo 'Raana' aliyoitaja Mwenyezi Mungu aliposema:

"Sivyo hivyo! Bali yametia kutu (Raana) juu ya nyoyo zao (kwa maovu) waliyokuwa wakiyachuma".

Na mwenye kufanya maasi makubwa au mwenye kuyadharau madogo si kama anapata dhambi tu, bali anaudhuru moyo wake na anaingia katika laana ya Mwenyezi Mungu na ya Mtume wake (SAW), na hii ni kwa sababu Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala amewalani wengi katika wafanyao maasi.

Katika qurani tukufu Mwenyezi Mungu amemlani kila mwenye kueneza ufisadi juu ya ardhi na mwenye kuwakata ndugu wa nasaba, na kila mwenye kumuudhi Mwenyezi Mungu na mwenye kumuudhi Mtume wake (SAW), na akamlani kila mwenye kuuficha ukweli na kuuficha uongofu ulioteremshwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na akawalani wanaowasingizia uongo wanawake wema, na akamlani kila mwenye kuufanya mwenendo wa kikafiri kuwa bora kuliko mwenendo wa Kiislamu nk.

Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) pia amewalani wengi katika wafanyao maasi; Amemlani mchongaji nyusi na mwenye kuchongwa, amemlani mwenye kuunganisha nywele zake na nywele za bandia, amemlani mwenye kuunguza ngozi yake kwa kufanya 'tatoo', amemlani anayekula riba na mwenye kulisha riba pamoja na mashahidi wake, amemlani mwizi, amemlani mwenye kula rushwa na mwenye kutoa, amemlani mlevi na mtiaji pombe na mkamuaji na mchujaji na muuzaji na mnunuaji na mwenye kula thamani yake na mbebaji na anayepelekewa.

Amemlani mpigaji ramli na amewalani makhanithi wanaume na wanawake wanaoingiliana wenyewe kwa wenyewe, na amemlani mwenye kuchinja mnyama kwa ajili ya mwingine asiyekuwa Mwenyezi Mungu, na amemlani mwenye kueneza ufisadi na ujambazi na amemlani mwenye kumficha jambazi, na amemlani kila mwenye kuchonga masanamu, na amemlani mwenye kutenda kitendo cha qaumu Lut, na amemlani mwenye kumtukana baba yake na mama yake, na amemlani mwenye kumuingilia mnyama, na amemlani mwenye kumfisidi mwanamke akamfanya amchukie mumewe, na amemlani mwenye kumuingilia mkewe kwa nyuma, na akatujulisha kuwa mwanamke anayekataa kulala na mumewe kuwa analaaniwa na Malaika mpaka asubuhi inapoingia, na amemlani mwenye kujinasibisha na ubini usiokuwa wa baba yake, na akatujulisha kuwa atakayemuelekezea ndugu yake Muislamu silaha au upande wa ukali wa kisu au wa upanga au chuma analaaniwa na Malaika, na amemlani kila mwenye kumtukana Sahaba wake.

Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) amemlani pia mwanamume mwenye kuvaa nguo za kike na mwanamke mwenye kuvaa nguo za kiume, na akawalani wengi wengine.

Inatosha laana ya Mwenyezi Mungu na ya Mtume wake (SAW) kumfanya mtu ayakimbie maasi, lakini juu ya laani hiyo mwenye kufanya maasi hayo anapata pia madhambi pamoja na ghadhabu za Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala na moyo wake unasibiwa na maradhi ambapo hatoweza tena kuiona raha mpaka atakapotubu na kurudi kwa Mola wake.

Usitizame udogo wa maasi bali mtizame Nani unayemuasi - Subhanahu wa Taala na umtukuze ili kila anapoangalia ndani ya moyo wako asione isipokuwa Moyo Safi.

Mchungeni Mola wenu;

Anasema Abdul Qader al Jaylani (Mwenyezi Mungu amrehemu);

"Mmoja wenu akiwa mgonjwa akafahamishwa na mganga dawa ya kumponyesha, hatoona raha mpaka aipate dawa hiyo. Kwa hivyo mchungeni Mola wenu Azza wa Jallah mnapokuwa peke yenu na mnapokuwa mbele za watu. Uwe kama Yupo mbele yako unamuona, kwani hata kama wewe humuoni Yeye anakuona.

Mwenye kumkumbuka Mwenyezi Mungu moyoni mwake huyo ndiye mwenye kumkumbuka kweli, ama asiyemkumbuka moyoni mwake, huyo hamkumbuki kweli. Ulimi ni mwana wa moyo na unaufuta. Jishughulishe na kusikiliza mawaidha, kwa sababu moyo ulio mbali na mawaidha unapofoka. Kutubu kweli ni kumtukuza Mwenyezi Mungu katika amri zote. Na kwa ajili hii wamesema baadhi yao - Mwenyezi Mungu awarehemu; "Kheri yote imo ndani ya maneno mawili; Kutukuza amri za Mwenyezi Mungu na kuwahurumia waja Wake. Kwa hivyo yeyote asiyezitukuza amri za Mwenyezi Mungu wala asiwaonee huruma waja wake, huyo yuko mbali kabisa na Mwenyezi Mungu.

Enyi washirikina, enyi mnaoabudu masanamu yaliyokuzungukeni, na wenye kuabudu vyeo vyenu na mishahara yenu na wakubwa wenu na wafalme wenu. Hamumuoni Mwenyezi Mungu? Kila mwenye kuona kuwa yupo asiyekuwa Mwenyezi Mungu mwenye uwezo wa kumnufaisha au kumdhuru, huyo yupo mbali na Mwenyezi Mungu na huyo hamuabudu Mwenyezi Mungu. Huyo anamuabudu yule anayemdhania kuwa anaweza kumnufaisha, leo mtu huyo yumo ndani ya ghadhabu za Mwenyezi Mungu na kesho atakuwa ndani ya moto wa Jahannam. Hatosalimika na moto huo isipokuwa mcha Mungu, mwenye kumpwekesha, aliyetubu akaja na Moyo Safi".

(Mwisho wa maneno ya Al Jaylani)

Athari ya Maasi;

Anasema Muadh Al Razi;

"Nashangazwa ninapomuon Muislamu anapoomba dua akasema; 'Mola wangu usinijaalie nikawa  kichekesho mbele ya adui zako', kisha wakati  huo huo anamuasi na kujifanya kuwa kichekesho mbele yao siku ya Kiama."

Amesema Dha Nnun;

"Mwenye kufanya khiana kwa siri, Mwenyezi Mungu atamfedhehesha mbele za watu."

Bila shaka athari ya madhambi ni kubwa sana. Kwani ni kipi kilichomtoa baba yetu Adam (AS) kutoka katika raha za Peponi akaingizwa katika maisha ya tabu ya hapa duniani, na kipi kilichosababisha Ibilisi kutolewa katika rehma ya Mwenyezi Mungu na kuingizwa katika laana yake, na kipi kilichosababisha kuangamizwa kwa watu wa Nabi Nuh (AS) wakamiminiwa mvua iliyoizamisha dunia yote ya wakati wao, na kipi kilichosababishwa kupelekewa watu wa Thamud ukelele uliozikata nyoyo zao wakaangamia, na kipi kilichosababisha kuangamizwa kwa watu wa Nabi Lut (AS) na kugeuzwa ardhi yao juu chini, na Haaman na Qarun na Qaumu Saleh (AS) na wengi waliotangulia?.

Mwenyezi Mungu anasema;

"Atawaletea mpaka siku ya Kiama watu ambao watawaadhibu kwa adhabu mbaya."

Al Aaraf – 167

Na maasi nayo yana athari mbaya ndani ya nyoyo na ndani ya mwili, na mojawapo ya athari zake ni kuikosa elimu. Kwa sababu elimu ni nuru, na maasi yanaizima nuru hiyo

Kutoka kwa Abu Huraira (RA) amesema kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) amesema;

"Kwa yakini Moyo unachakaa katika kifua cha mmoja wenu kama nguo inavyochakaa".

Imam Ahmed na Attirmidhy

Imepokelewa kuwa mara ya mwanzo Imam Shafi alipokwenda kutafuta elimu kwa Imam Malik (Mwenyezi Mungu awarehemu), na wakati huo alikuwa kijana mdogo, na alipomuona namna alivyoweza kukihifadhi kitabu cha Muwata'a katika siku chache tu, na alipoiona nuru ya ucha Mungu usoni pake, Imam Malik alimwambia Imam Shafi;

"Mimi naona kuwa Mwenyezi Mungu ameingiza moyoni mwako nuru, kwa hivyo usiizime kwa kiza cha maasi."

Imam Shafi alitunga shairi maarufu sana katika maudhui haya aliposema;

Na maana yake ni;

'NilimshitakiaWaqii (mwalimu wake), kupungua uwezo wangu wa kuhifadhi, naye akaninasihi niache maasi, akanambia kwamba elimu ni nuru, na nuru ya Mwenyezi Mungu hatunukiwi mtu asi'.

Haya yanasemekana yalimkuta Imam Shafi alipokuwa sokoni akaona kwa bahati mbaya tu kisigino cha mwanamke. Vipi basi hali zetu sisi wakati huu kutokana na tunayoyaona kila siku masokoni na mabarabarani na kwengineko.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu atuepushe na ghadhabu zake na atufanye tuchukizwe kuangalia na hata kuyasogelea maasi, na atutahirishe nyoyo zetu ziwe mbali na unafiki na aingize nyoyoni mwetu nuru yake na azijaalie nyoyo zetu ziwe Nyoyo Safi -  Amin.

Mitihani;

Ukitaka kuujuwa unadhifu wa dhahabu basi ipambanishwe na moto. Ikibadilika rangi utajuwa kuwa hiyo si safi, ama ikiweza kusimama imara, basi hiyo ndiyo dhahabu kweli.

Mwenyezi Mungu anasema;

"Je, Watu wanadhani wataachwa (wasitiwe katika misukosuko) kwa kuwa wanasema ;"Tumeamini", basi ndio wasijaribiwe?

Hapana; bila shaka tuliwatia katika tabu wale waliokuwa kabla yao, na kwa yakini Mwenyezi Mungu atawatambulisha wale walio wa kweli na atawatambulisha (wale walio) waongo."

Al Ankabuut – 3

Hapa Mwenyezi Mungu anauliza kwa maana ya kukanusha kuwa walioamini kikweli wasidhani kuwa wataachwa vivi hivi tu, bali atawaingiza katika mitihani kama alivyowaingiza waliotangulia kabla yao, wakathibiti mbele ya mitihani hiyo, juu ya kuwa Mwenyezi Mungu anamjuwa nani mwenye kuamini kweli na nani asiyeamini, kwani Mwenyezi Mungu anajuwa kila kinachotokea na kitakachotokea na kile kisichotokea, na kile ambacho hakijatokea lau kama kingetokea vipi kingekuwa.

Mwenyezi Mungu alimuingiza katika mtihani kipenzi chake (Khalil wake) Ibrahim (AS) akamtaka amchinje mwanawe, na kipenzi chake huyo akatii pale alipooteshwa kumchinja mwanawe wa pekee Ismail (AS) na mwanawe akakubali kutii amri alopewa baba yake ndani ya ndoto yake hiyo (na ndoto za Mitume ni wahyi), na alipomlaza mwanawe kifudifudi ili asiuone uso wake akamuonea huruma, na baada ya Ismail kutoa shahada na Ibrahim kusalimu amri kwa Mwenyezi Mungu huku akijitayarisha kumchinja mwanawe, Mwenyezi Mungu akamfunulia Nabii Ibrahim (AS) kuwa asimchinje mwanawe na badala yake akamkomboa kwa kondoo.

Kisa hicho kimeelezwa ndani ya kitabu cha Mwenyezi Mungu aliposema;

“Basi wote wawili walipojisalimisha (kwa Mwenyezi Mungu), na akamlaza kifudifudi (amchinje).

Pale pale tulimwita; “Ewe Ibrahim; Umekwishasadikisha ndoto. (Usimchinje mwanao).” Kwa yakini hivi ndivyo tunavyowalipa watendao mema.

Bila shaka (jambo) hili ni jaribio lililo dhahiri, (mtihani ulio dhahiri).

Basi tukamkomboa kwa mnyama wa kuchinjwa mtukufu.”

As Saaffaat – 103-107

Na imepokelewa katika hadithi kuwa wenye kuingizwa katika mitihani mikubwa zaidi ni Mitume kisha watu wema, kisha wanaowafuatilia na wanaowafuatilia, kila mtu kiasi cha imani yake.

Na imepokelewa pia kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) alikuwa akipenda kuomba dua ifuatayo;

"Ya muthabbita l qulub thabbit qalbiy alaa diynika."

(Ewe Mwenye kuzithibitisha nyoyo, uthibitishe moyo wangu katika dini yako.)

Wakamuuliza;

"Unaogopa ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?"

Akasema;

"Kipi kitakachonipa dhamana wakati nyoyo zipo baina ya vidole viwili vya Mwenyezi Mungu anazigeuza apendavyo."

Attirmidhiy na Al Hakim

Na Mwenyezi Mungu anasema;

"Enyi mlioamini! Muitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume wake anapokuiteni katika yale yatakayokupeni uhai mzuri (wa duniani na Akhera) Na jueni ya kuwa Mwenyezi Mungu huingia kati ya mtu na moyo wake, na jueni ya kuwa kwake Yeye mtakusanywa."

Al Anfal – 24

Katika kuifasiri aya hii anasema Sayed Qutub katika tafsiri yake iitwayo 'Fiy Dhilal al Quraan';

"Muitikieni Mola wenu kwa kumtii kwa hiari zenu juu ya kuwa akitaka anao uwezo wa kukulazimisheni kumtii."

Sayid Qutub akaendelea kusema;

"Mwenyezi Mungu anasema; 'Na jueni ya kuwa Mwenyezi Mungu huingia kati ya mtu na moyo wake'. Na hii ni picha tukufu adhimu ya uwezo wa kuzitiisha nyoyo, kwani Mwenyezi Mungu anaingia kati ya mtu na moyo wake na kuutenga moyo wake mbali na nafsi yake. Anaweza kuuzuwia na kuufanya atakavyo na kuugeuza atakavyo wakati mwenye moyo huo hana uwezo wowote, juu ya kuwa moyo huo ni wake na umo ndani ya kifua chake.

Fundisho hili linamtaka mtu awe macho wakati wote, na awe na tahadhari wakati wote asije akateleza, na pia awe wakati wote akimchunga Mola wake usije moyo wake ukageuzwa, ukaghafilika na kupotoka.

Ikiwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) mwenyewe alikuwa mwingi wa kutamka maneno haya; "Allahumma Ya muqallibal qulub thabbit qalbiy alaa diynika." Na yeye ndiye yeye, kipenzi cha Mola wake (SAW), itakuwaje basi sisi watu wa kawaida tusiokuwa mitume wala si katika waliokingwa?

Na maneno haya wanaambiwa walioamini. Mwenyezi Mungu anasema;

"Enyi mlioamini! Muitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume wake anapokuiteni katika yale yatakayokupeni uhai mzuri."

Na maana yake ni kuwa; 'Mwenyezi Mungu anao uwezo wa kukulazimisheni mkamtii – angetaka – lakini anakukirimuni kwa kukuiteni katika uongofu kwa hiari zenu ili mupate ujira mwema kutoka Kwake.

Kisha akasema; "Na jueni ya kuwa kwake Yeye mtakusanywa."

(Mwisho wa maneno ya Sayed Qutub)

Kwa hivyo ndugu zangu Waislam; Nyoyo zenu zimo mikononi Mwake, kisha baada ya hapo mtakusanywa kwake, kwa hivyo hamna pa kukimbilia isipokuwa kwake, hapa duniani na huko Akhera. Na juu ya uwezo Wake wote huo, bado anakuiteni kwake kwa hiari zenu na kwa  uhuru wenu bila kukulazimisheni, na hataki chochote kutoka kwenu isipokuwa kitu kimoja tu. Nacho ni kuja kwake kwa Moyo Safi."

Maymun bin Maharan;

Ucha Mungu wa kweli ni ucha Mungu wa Moyo na si ucha Mungu wa viungo,  kwa sababu Mwenyezi Mungu haangalii nyuso zenu wala hatizami miili yenu, bali anaangalia ndani ya nyoyo zenu.

Mwenyezi Mungu anasema;

"Namna hii; anayezihishimu alama za (dini ya) Mwenyezi Mungu, basi hilo ni jambo katika utawa (Ucha Mungu) wa nyoyo."

Al Hajj – 32

Na akasema juu ya wanyama wanaochinjwa katika Hija;

"Nyama zao (wanyama hao wanaochinjwa) hazimfikii Mwenyezi Mungu wala damu zao. Lakini inamfikia ta-a yenu (ucha Mungu wenu)."

Al Hajj – 37

Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) amesema;

"Ucha Mungu upo hapa." Akaashiria kifuani pake.

Muslim

Kwa ajili hii lengo kubwa la Ibilisi ni kuushambulia na kuuharibu moyo wa Muislamu, na akeshafanikiwa hayo anakuwa keshalifikia lengo lake.

Na katika hadithi Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) anasema;

"Katika mwili mna kipande cha nyama, kikitengenea, mwili wote unatengenea, na kikiharibika, mwili wote unaharibika. Kitu hicho ni Moyo".

Bukhari na Muslim na wengine

Mwenyezi Mungu ametufundisha namna ya kujikinga Kwake kutokana na shari ya Ibilisi mwenye kuingiza wasiwasi ndani ya nyoyo, Akasema;

"Sema najikinga kwa Bwana Mwenye kuwalea watu.

Mfalme wa watu.

Na shari ya mwenye kutia wasiwasi mwenye kurejea nyuma.

Atiaye wasiwasi nyoyoni mwa watu.

(Ambaye ni) Katika majini na watu."

Suratun Naas

Na katika hadithi yenye udhaifu kidogo ndani yake, imepokelewa kuwa Ibilisi hushika hatamu za moyo wa mwandamu, na (mwanadamu) anapomkumbuka (akamdhukuru) Mwenyezi Mungu, hapo (ibilisi) hurudi nyuma.

Na hadithi hii inapata nguvu kutokana na kauli ya Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala isemayo;

"Wale wanaomuogopa (Mwenyezi Mungu) zinapowagusa pepesi za Shetani (wakasahu) mara hukumbuka (wakamdhukuru Mwenyezi Mungu), tahamaki wamekwishaona njia."

Al Aaraf – 201

 

Kwa ajili ya yote hayo, watu wema waliotangulia walikuwa wakijishughulisha sana na kuzitakasa nyoyo zao na kuzitafutia dawa kila wanapoona athari ya kupungua kwa imani au kupungua kwa hima ya kufanya ibada, au inapopungua ile raha wanayoipata wanapokuwa katika Sala zao au wanaposoma qurani nk.

Imepokelewa kuwa mmoja katika wacha Mungu wa wakati wake, na jina lake ni Maymun bin Maharan aliyekuwa mwandishi na mshauri wa Omar bin Abdul Aziz (RA) alipohisi kuwa imani yake inaanza kupungua na hapati tena ule utulivu alokuwa akiupata katika Sala zake wala haioni tena ile raha alokuwa akiiona anaposoma qurani, akaamua kufuatana na mwanawe kuifunga safari ndefu ya kwenda kwa Al Hassan al Basry  akamshitakie hali yake, na Al Hassan ni katika maulamaa wakubwa wa At Tabiina (waliokuja baada ya Masahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW)), na wakati huo Maymun alikuwa na umri mkubwa sana.

Hebu tumsikilize mwanawe Amr akituhadithia juu ya safari yao hiyo;

'Safari ilikuwa ndefu sana, na ilikuwa tunapoufikia msingi na baba yangu akishindwa kuuruka, nilikuwa nikilala juu ya msingi huo mfano wa daraja, kisha baba yangu hupita juu yangu na kuvuka.

Tuliendelea hivyo mpaka tulipowasili Basra na tulipoifikia nyumba ya Al Hassan al Basry, baba yangu akanitaka nigonge mlango, nikagonga na mtumishi akatufungulia mlango na Al Hassan alipomuona baba yangu akafurahi sana na kumlaki vizuri.

Baada ya kusalimiana, baba yangu akamwambia;

"Ewe Al Hassan! Hakika moyo wangu umekuwa dhaifu (imani yangu imepungua), Nifunge au nifanye nini?"

Al Hassan akaisoma kauli ya Mwenyezi Mungu;

"Unaonaje kama tukiwastarehesha kwa miaka. Kisha iwafikie (adhabu) waliyokuwa wakiahidiwa? Yatawafaa nini yale waliyostareheshwa."

Ash Shuara – 205-207

Baada ya kuisikia aya hiyo baba yangu akaanguka na kuzimia, na miguu ya Al Hassan ikaanza kutetemeka mfano wa mbuzi anayetaka kuchinjwa.

Nikamuuliza baba  yangu tulipokuwa tukiondoka;

"Baba! huyu ndiye Al Hassan? Nilidhani atakuwa kupita hivi"

Akanambia;

"Mwanangu! Amezisoma aya, lau kama utazingatia maana yake basi zingeacha jeraha moyoni mwako."

Maharan akaifunga safari ya kurudi kwao akiwa mwenye furaha baada ya kusomewa aya zilizoutakasa na kuuzindua moyo wake.

Na hivi ndivyo ilivyo kwa kila mwenye moyo ulio na uhai wenye kufahamu. Wale ambao nyoyo zao zishachanganyika na qurani, utawaona zikiwaathiri mara wanaposomewa aya, wanakuwa kama kwamba yote yashaandikwa ndani ya nyoyo zao. Na hawa ndio Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala aliosema juu yao;

"Kwa yakini katika jambo hili mna ukumbusho kwa mwenye moyo au kwa ategaye siko, naye mwenyewe awe hadhiri."

Qaf

Kumbuka kwamba kwa moyo wako unasafiri kuelekea kwa Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala, na si kwa viungo vya mwili wako.

Anasema Ibnu l Qayim katika 'Al Fawaid';

"Na kumbuka kwamba mwaka ni mfano wa mti, na miezi ni matawi na siku ni mfano wa mashada yake, na saa ni mfano wa majani na pumzi ni mfano wa matunda yake. Basi mwenye kuzivuta pumzi zake katika ta-a ya Mwenyezi Mungu, huyo matunda ya mti wake yanakuwa mema, ama yule mwenye kuzivuta katika maasi, matunda yake ni maovu, na kuvuna kwake matunda ya mti huo ni siku ya Kiama, na siku hiyo itabainika wapi mtu alikuwa akivutia pumzi zake.

Adhabu za nyoyo;

Wakati mwengine Mwenyezi Mungu humtia adabu mtu asi kwa kumpa mali nyingi na umri mrefu akadhani kuwa hiyo ni neema itokayo kwa Mola wake.

Mwenyezi Mungu anasema;

"Je! Wanafikiri yakuwa yale tunayowapa (nayo ni) mali na watoto ndiyo tunawatangulizia katika kheri (zao)?  (Wapi hayo!) lakini wenyewe hawatambui."

Al Muminun – 55 – 56

Kuwa na umri mrefu huwa kuzuri kwa watu wema kwa sababu huongezeka wema wao na huongezeka pia thawabu zao, lakini kwa watu waovu hiyo ni adhabu itokayo kwa Mola wao.

Mwenyezi Mungu anasema;

"Wala wasidhani wale wanaokufuru kwamba huu muda tunaowapa (wakaishi kwa satarehe) ni bora kwao. Hakika tunawapa muda na wanazidi madhambi. Na itakuwa kwao adhabu ya kuwadhalilisha."

Aali Imran - 178

Ajabu ya wanadamu ni kuwa nyoyo zinakufa huku adhabu zinateremka juu yao na wala hapana anayejali wala kuhisi.

Anasema Ibni l Qayim katika kitabu chake ' Sayd al khatir';

"Adhabu kubwa kupita zote ni kule mtu asihisi kuwa anatiwa adabu, na kubwa zaidi ni kuwa utamuona akifurahi anapokuwa katika adabu hiyo akidhani kuwa ananeemeshwa, hasa anapotiwa ndani ya mtihani kwa kupewa mali na kuneemeshwa katika hali"

(Mwisho wa maneno ya Ibnul Qayim).

Mwanadamu anaponeemeshwa akajaaliwa kuwa na mali nyingi au elimu  huona kuwa hiyo ni haki yake anayoistahiki na wala hahisi kuwa yumo ndani ya mtihani akingoja jaza yake ikiwa hakuitumia mali au elimu hiyo ipasavyo. Na tatizo kubwa ni kuwa anawaona wale wasiokuwa na mali wala elimu kuwa Mwenyezi Mungu anawatesa na kuwapa adhabu wanayoistahiki.

Kwa nadharia hii anauona mtihani alokuwa ndani yake kuwa ni neema na anayaona majaribio waliopewa wenzake kuwa ni mtihani utokao kwa Mwenyezi Mungu.

Fikra zote mbili hizo ni makosa, kwani Mwenyezi Mungu humneemesha mja wake apate kumshukuru na kuitumia neema hiyo katika mambo ya kheri, na humpunguzia mwengine katika riziki yake au katika dunia yake ili apate kusubiri na kupata jaza itokayo kwa Mola wake, na wote hao wamo ndani ya mtihani. Usidhani kuwa anachotowa Mwenyezi Mungu katika mambo ya kidunia kuwa yana uzito wowote katika mezani Yake Subhanahau wa Taala, kwani Mwenyezi Mungu humpa mtu mwema na humpa muovu pia kwa ajili ya kuwapa mitihani, lakini moyo usiokuwa na imani hauwezi kuidiriki hekima hii.

Mwenyezi Mungu anasema;

"Lakini mwanaadamu, Mola wake Anapomfanyia mtihani Akamtukuza na kumneemesha, basi husema; "Mola wangu amenitukuza. Na Anapomfanyia mtihani akampunguzia riziki yake, husema; Mola Wangu Amenidhalilisha . Sivyo hivyo! Bali nyinyi hamuwatazami mayatima kwa jicho la huruma. Wala hamujihimizi kulisha maskini. Na mnakula urithi kwa ulaji wa pupa. Na mnapenda mali pendo la kupita kiasi."

Al Fajr – 15 – 20

Kuhusu kauli ya Mwenyezi Mwenyezi Mungu; 'Bali nyinyi hamuwatazami mayatima kwa jicho la huruma. Wala hamujihimizi kulisha maskini', anasema Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW);

"Nyumba ya Kiislamu yenye kheri kupita zote ni ile anayoishi ndani yake yatima mwenye kutizamwa kwa wema. Na nyumba ya Kiislamu yenye shari kupita zote ni ile anayoishi ndani yake yatima mwenye kudhalilishwa."

Na akasema;

"Mimi na mwenye kumlea yatima tuko kama hivi viwili Peponi," akalinganisha kwa kidole chake cha kati na cha shahada.

Kheri haipatikani isipokuwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na mtu mwema haridhiki na jambo lisilo na kheri ndani yake, na shari haipati isipokuwa mtu mwenye nafsi ovu mwenye kuikimbilia shari hiyo kutokana na udhaifu wa kuona kwake na udhaifu wa imani, Na mwenye kuikimbilia shari akaicha kheri ni mtu mwenye kuchaguwa kilichokuwa duni akaacha kilichokuwa bora, kwani kilicho duni hawezi kuridhika nacho mwenye Moyo Safi.

Kuutakasa Moyo;

Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala anasema;

"Siku ambayo hayatafaa mali wala watoto. Isipokuwa mwenye kuja kwa Mwenyezi Mungu na Moyo Safi."

Ash Shuaraa – 88 – 89

Maulamaa wanasema kuwa 'Moyo Safi' (Qalbin Saliym) ni Moyo usiokuwa na uchafu wala dhambi. Na baadhi yao wakasema kuwa hapana moyo usiokuwa na dhambi, bali Mwenyezi Mungu hapa anakusudia Moyo uliotakasika na Shirki. Na wengine wakasema; Ni moyo usiotia shaka, na wengine wakasema kuwa ni moyo wenye uhakika kuwa Mwenyezi Mungu Ndiye Haki.

Maulamaa wanasema;

"Imani huongezeka na kupungua".

Inaongezeka kwa kufanya mema na inapungua kwa kufanya maasi.

Mwenyezi Mungu anasema;

"Na wanaposomewa Aya zake huwazidishia imani."

Al Anfal – 2

Na akasema;

"Ama wale walioamini inwazidishia imani nao wanafurahi."

At Tawaba – 124

Muislamu lazima azifahamu sababu zinazopunguza imani na zinazoizidisha ili aweze kuutakasa moyo wake uweze kukabiliana na mitihani.

Siku moja mfalme wa Luqman mwenye hekima "Luqman al Hakiym" alichinja mbuzi wawili kisha akamtaka Luqman amtolee kutoka katika kila mbuzi hao vipande viwili vibaya kupita vyote na viwili vizuri kupita vyote.

Luqman akachagua moyo na ulimi kutoka katika kila mbuzi. (yaani alikata kutoka katika mbuzi wa kwanza moyo na ulimi, na katika mbuzi wa pili pia akakata moyo na ulimi).

Mfalme akamuuliza;

"Nilikwambia uchague kutoka KILA mbuzi sehemu mbili, lakini wewe umechagua kutoka katika mbuzi wote viwili hivi tu (Moyo na ulimi)?"

Luqman akasema;

"Hakuna vibaya kuliko hivi vinapoharibika, na hakuna vizuri kuliko hivi vinapotengenea".

Baadhi ya watu hujipangia minasaba maalum kwa ajili ya kuanzisha upya maisha yao, wakasema kwa mfano;

'Nitakapotimia umri fulani nitabadilisha mwenendo wangu."

Na mwengine huchaguwa unapoingia mwaka mpya kwa mfano akasema;

"Kuanzia mwaka huu nitaubadilisha mwenendo wangu."

Na wengine hujiwekea minasaba mbali mbali kwa ajili hiyo. Hili ni jambo jema, lakini muhimu zaidi ni kuibadilisha nafsi yako kwanza, kubadilisha ndani yako, kuubadilisha moyo wako. Maana moyo ukeshakinai unakuwa ushapiga hatua kubwa mbele katika kujibadilisha kutoka katika hali na kuingia katika hali nyingine.

Mtu baadhi ya siku hupekuwa pekuwa ndani ya meza yake akatowa vijikaratasi asivyohitajia na kuvichanachana, akatowa pini pini asizozihitajia na kuzitupa,  akapanga upya kila kinachohitaji kupangwa. Ikiwa meza ina umuhimu wa kushughulikia na kupangwa namna hii, basi nafsi ya mtu inastahiki zaidi kupewa umuhimu huo.

Mwenyezi Mungu anatuhimiza kuzisafisha na kuzitakasa nafsi zetu kila siku.

Imepokelewa kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) amesema;

"Inapoingia nusu ya mwisho ya usiku au theluthi ya mwisho, Mwenyezi Mungu hushuka mpaka katika mbingu za dunia akasema; 'Yupo mwenye kuomba nikampa? Yupo mwenye kuomba dua nikamkubalia? Yupo mwenye kuomba maghfira nikamghufiria?', mpaka alfajiri inapoingia.

Muslim

Na katika riwaya nyingine;

'Mtu anakuwa karibu zaidi na Mola wake wakati wa usiku mzito."

Huu ni ule wakati usiku unapoanza kutoweka na alfajiri inapoanza kujisogeza, ni ule wakati watu wote wamelala wakakoromeana isipokuwa watu maalum, watu mahsusi tu wanaoziinua mbavu zao kutoka vitandani ili kumuabudu Mola wao kwa kuogopa Moto na kutaraji Pepo.

Ianze kazi hiyo ndugu yangu Muislamu, kwani imani inapunguwa na nafsi inadhoofika kwa wingi wa kupambana na matamanio ya dunia pamoja na mitihani mbali mbali, na utakapoiacha nafsi bila kuiwaidhi na kuipambanisha na nuru ya Mwenyezi Mungu, basi itaachana na kupotea. Ni wewe peke yako unayeweza kuiokoa.

Rudi haraka kwa Mola wako usije ukaingia katika wale Mwenyezi Mungu anaosema juu yao;

"Wale ambao tumezighafilisha nyoyo zao wakafuata matamanio yao, na mambo yao yakawa yamepita mipaka."

Al Kahf – 28

Na katika hadithi l Qudusiy, Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala anasema;

"Ewe mwanadamu! Utakaponiomba na kurudi kwangu nitakusamehe yote uliyonayo wala sijali.

Ewe mwanadamu! Lau kama madhambi yako yatafika mbinguni, kisha ukaomba kwangu maghfira, nitakusamehe wala sijali.

Ewe mwanadamu! Lau kama utanijia ukiwa na madhambi yaliyoijaza ardhi, kisha ukakutana nami ukiwa hujanishirikisha na lolote, na Mimi nitakujia na maghfira yaliyoijaza ardhi."

Attirmidhiy

Na kumbuka siku zote kuwa Mwenyezi Mungu amekuumba kwa ajili ya kukukirimu na si kwa ajili ya kukudhalilisha, ndiyo maana akawaamrisha Malaika wakusujudie.

Kuwa mbali na Mwenyezi Mungu hakukuongezei isipokuwa machungu, upungufu wa raha ndani ya moyo, hata uhodari wa mtu na uerevu wake unageuka kuwa masaibu pale unapokosa baraka za Mwenyezi Mungu.

'Mwenyezi Mungu wewe ndiye Mola wangu. Umeniumba na mimi ni mja wako, na mimi nitatimiza ahadi yako na waadi wako kiasi niwezavyo. Najikinga kwako kutokana na kila shari uloumba. Nakiri juu ya neema zote ulizonineemesha nazo. Na ninakiri juu ya dhambi zangu. Kwa hivyo nisamehe, kwani hapana mwenye kusamehe madhambi isipokuwa wewe'.

Kuishi ndani ya siku yako

Katika makosa makubwa wanayofanya wanadamu ni kuishi ndani ya ndoto wanazojipangia za kesho yao.

Na mtu anapojipangia kesho yake, akaanza kuingia katika bahari ya ndoto isiyo na mwisho na kujiingiza katika wahka na wasi wasi na mawazo yasiyo na upeo, huku akiendelea kujitia dhiki na mashaka nafsini mwake, huyo anaingia katika makosa makubwa sana.

Kwa nini basi mtu haishi ndani ya siku yake hii akamuachia Mwenyezi Mungu kesho yake?

Si vibaya mtu kujipangia kesho yake, lakini vibaya ni kule kuzama ndani ya fikra na mawazo yasiyokuwa na mwisho; 'Itakuwaje kama nikiachishwa kazi? Nitafanya nini meli ikizama na mali yangu ikapotea? Nikifa ghafla nani atanitizamia wanangu? Mwanangu akiumwa? Akifa? Mke wangu? Mume wangu? Nk.

Hizi ni fikra ambazo haijuzu mtu kujishughulisha nazo.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) amesema;

"Atakayeamka akiwa yupo katika amani, mwenye afya njema, anacho chakula cha kumtosha kwa siku moja, huyo ni sawa na aliyemiliki dunia na kila kilichokuwemo ndani yake."

Attirmidhiy

Mtu kama huyu anatakia nini tena kujitia dhiki akafikiria kuachishwa kazi au kupoteza mali au kujiharakishia mitihani?

Imepokelewa kuwa Nabi Ibrahim (AS) anapoamka asubuhi alikuwa akisema;

"Mola wangu hiki ni kiumbe kipya (hii ni siku mpya), kwa hivyo nifungulie siku hii kwa ta-a yako na unikhitimishie kwa maghfira yako na radhi zako, na uniruzuku mema utakayonikubalia na unitakasie wema huo na unizidishie, na nitakapofanya ovu unisamehe, kwani Wewe ni mwingi wa kusamehe, Mpole, Mwenye kurehemu, Mkarimu."

Imepokelewa kuwa Abi Hazim alikuwa akisema;

Tofauti baina yangu na wafalme ni siku moja tu.

Jana yetu, ishapita, hawaionei raha tena wao wala mimi.

Kesho yetu, haijafika, kwa hivyo mimi na wao ni sawa katika kuisubiri.

Tofauti yetu ni siku ya leo. Itakuwaje leo?

Unapoambiwa uishi ndani ya siku yako, haina maana kuwa uipuuze kesho yako, au uache kuifanyia hesabu, kwani mtu kujipangia kesho yake ni dalili ya ukamilifu wa akili. Lakini ipo tofauti baina ya kujipangia na kuifikiria, na baina ya kuwaza na kuingiza wahka moyoni kwa ajili ya kesho isiyo na uhakika, na ipo tofauti baina ya kuitayarisha na kuzama ndani yake, baina ya kuamka na kuitumia leo yako, na baina ya kulala na kuiota kesho hiyo.

Sufyan Al Thauri ambaye ni katika maulamaa wakubwa wa Attabiina, alikuwa mtu mwenye mali nyingi, na alikuwa kila anapoamka akiashiria mali yake huku akisema;

"Tumeamka na ufalme upo mikononi mwa Mwenyezi Mungu asiye na mshirika, na Kwake tutafufuliwa."

Attirmidhiy

Na alikuwa unapoingia usiku akirudia kusema maneno hayo hayo kisha akiomba kwa kusema;

"Allahumma inniy asbahatu minka fiy niamatin wa afiyatin wa sitrin. Faatmim niamatika alayya wa aafiyatuka wasitruka fi ddunya wal akhirah."

Abu Daud

Na maana yake;

"Mola wangu kwa  uwezo wako niko katika neema na afya na sitara. Kwa hivyo nikamilishie neema Yako juu yangu na afya Yako na sitara Yako duniani na akhera."

Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) amesema;

"Juwa halipandi isipokuwa Mwenyezi Mungu huwatuma Malaika wake wakasema; "Enyi watu! Rudini kwa Mola wenu. Hakika kidogo chenye kutosheleza ni bora kuliko kingi chenye kubabaisha."

Na halichi juwa isipokuwa Mwenyezi Mungu atawatuma Malaika waseme;

"Mola wetu mlipe mema kila mwenye kutoa (katika mali yake) na mharibie haraka kila mwenye kuacha kutoa katika mali yake."

Attarghiyb wal Tarhiyb

Anasema Sheikh Al Ghazali katika 'Jaddid Hayatak';

"Hapana baya kuliko mtu kuiba katika maisha yake. Unajuwa vipi mtu anaiba katika maisha yake?

"Anapokuwa mtoto mdogo husema; Nitakapokuwa kijana nitafanya hivi na vile.

Na anapokuwa kijana husema; Nitakapokuwa mtu mzima nitafanya hivi na vile.

Na anapokuwa mtu mzima husema; Nikeshaowa nitafanya hivi na vile.

Akishaowa atasema; Nitafanya nitakapokuwa na nafasi nzuri.

Akeshazeeka akayatizama maisha yake tokea hukoo alikotoka anaona kuwa ameyapoteza buree. Tatizo letu ni kuwa hatusomi kuwa thamani ya maisha ni ile siku yako. Hatuyajuwi hayo mpaka wakati unapopita na kumalizika".

Siha ni Ufalme

Huenda mtu akawa anaishi katika amani na afya njema bila kuhisi wala kuithamini neema hiyo tukufu aliyotunukiwa na Mola wake Subhanahu wa Taala, na wakati huo huo fikra na mawazo yake yote yapo katika mali na utajiri bila kuelewa kuwa kuidharau neema hii ya afya ni dhambi na ni kwenda kinyume na ukweli.

Waarabu wanasema;

"Afya njema ni taji ipo juu ya vichwa vya wenye siha, hawaioni taji hiyo isipokuwa wagonjwa."

Yaani mgonjwa anamuona mwenye afya yake kama ni mfalme.

Imepokelewa kuwa mtu mmoja alimuuliza Abdullah bin Amru bin Aas (RA);

"Mimi si mmoja katika masikini wa watu wa Makka?"

Abdullah (RA) akamuuliza;

"Unaye mke?"

Akajibu;

"Ninaye."

Akamuuliza tena;

"Unayo nyumba ya kulala?"

Akasema;

"Ninayo."

Akamwambia;

"Basi wewe ni miongoni mwa matajiri."

Akasema;

"Ninaye na mtumishi pia."

Abdullah (RA) akamwambia;

"Babi wewe ni katika wafalme."

Sisi ni matajiri, Alhamdulillah! lakini hatuijuwi thamani ya neema tuliyo ndani yake. Mmoja wetu anapoumwa na jino tu au kichwa au homa, dunia yote anaiona chungu.

Imesimuliwa kuwa mfalme mmoja aliyekuwa tajiri sana alikuwa na maradhi tumboni mwake, na alikuwa anapoletewa vyakula vizuri vizuri vya kila aina akishindwa kula. Siku moja alipokuwa akichungulia dirishani alimuona mtia maji wa bustani zake akila mkate mkavu huku akijishindilia chembe za zaituni mdomoni mwake moja baada ya nyingine, akatamani mfalme yule awe kama mfanya kazi wake huyo.

Imesimuliwa pia kuwa mtu mmoja alipotea jangwani akashikwa na kiu na baada ya kutembea siku nyingi akaona kwa mbali guduria, akafurahi akidhani kuwa ndani yake mna maji, lakini mara baada ya kulifikia guduria hilo na kutizama ndani yake alirudi nyuma kwa huzuni huku akiwa amevunjika moyo alipoona kuwa limejaa dhahabu na hamna ndani yake hata tone ya maji.

Impokelewa kuwa siku moja mfalme aliyekuwa katika safari zake za kuwinda alipotea njia akaishiwa na maji. Akamtuma mtumishi wake amtafutie maji, na baada ya kuhangaika sana na juwa lilikuwa kali sana siku hiyo, mtumishi akarudi akiwa na kikombe kimoja tu cha maji, na kabla ya kumpa mfalme wake maji hayo akamuomba amuulize suali, na mfalme aliyekuwa na kiu sana akamwambia;

"Uliza lakini fanya haraka maana nina kiu sana."

Mtumishi akasema; "Iwapo duniani hapana maji mengine isipokuwa haya tu, utakuwa tayari kuyanunua kwa thamani gani?"

Mfalme akasema; "Nusu ya ufamle wangu."

Mtumishi akampa mfalme maji, na baada ya kunywa akamuuliza tena;

"Kama maji haya uliyokunywa yatafungika tumboni mwako yasiweze kutoka, utakuwa tayari kumlipa kiasi gani atakayeweza kuyatoa?"

Mfalme akasema; "Nusu ya pili ya ufalme wangu."

Mtumishi akasema; "Ufalme thamani yake sawa na kikombe cha maji."

Hiyal qanaatu tahfadhuha takun malikan - Walaw la alaa raahatul badani

Undhur liman malaka dduniya biakmaliha – Hal raaha minha bighayri l qutni wal kafani?

Tafsiri; Ni kukinai tu, ukiweza ushakuwa mfalme -  hata kama huna isipokuwa afya ya mwili wako.

Mtizame aliyemiliki dunia na kila kizuri ndani yake -  Aliondoka na nini hapa duniani isipokuwa pamba na sanda?

Siku zote usiitizame nafsi yako, wala usiwatizame walio juu yako, bali watizame walio chini yako.

Ikiwa unayo kazi, wapo wasio na kazi. Ikiwa afya yako ni njema, wapo wagonjwa kwa mamilioni. Ikiwa unaumwa wapo wasioweza kutembea. Ikiwa upo kitandani wapo wasioweza kuvuta pumzi mpaka wasaidiwe kwa vifaa vya hospitali, nk.

Anasema Sh. Muhammad Al Ghazali katika 'Jaddid Hayatak';

Madaktari wanasema kuwa mmoja katika kila watu ishirini wanaoishi Marekani watakuwa wagonjwa katika hospitali za maradhi ya akili, na katika ukweli unaotia uchungu ni kuwa kati ya kila vijana sita waliokwenda kujiandikisha jeshi wakati wa vita vya ulimwengu vya mwisho walikataliwa kwa ajili ya kuwa na maradhi ya mwili au upungufu wa akili.

Alipokuwa akiwahutubia madaktari katika hospitali ya Mayo huko Marekani, Dr. Haroldsin alisema;

"Tumedurusu hali za wafanya biashara vijana mpaka wenye kufikia umri wa miaka arubaini, ikatubainikia kuwa si chini ya watu wawili katika kila watatu wanapata mojawapo ya maradhi aina tatu yenye asili ya dhiki ya nafsi. Na maradhi hayo ni; kukumtika kwa moyo 'palpitation', donda la tumbo 'gastric ulcer' au hypertension, na haya ni baada ya kufikia umri wa miaka arubaini na mitano."

Je, hii ndiyo thamani ya mafanikio? Ivo anahesabiwa kuwa amefanikiwa yule aliyenunua mafaniko kwa maradhi ya donda la tumbo na mapigo ya haraka ya moyo wake? Na maradhi yatamfaidia nini hata kama ataimiliki dunia yote akaipoteza afya yake? Mtu hata aimiliki dunia yote haweza kulala isipokuwa juu ya kitanda kimoja tu, na hawezi kula zaidi ya mara tatu kwa siku. Sasa pana tofauti gani baina yake na mfanya kazi mwenye kuchimba mitaro? Bali huenda mchimbaji akapata usingizi mzuri zaidi na akakifaidi zaidi chakula chake kuliko tajiri mwenye jaha na uwezo.

Anasema Dr. W. S. Alvares;

"Imebainika kuwa maradhi manne katika kila maradhi matano hayatokani na mwili, bali yanatokana na hofu na dhiki ya nafsi, chuki au wasi wasi usiokuwa na msingi."

(Mwisho wa maneno ya Sh. Al Ghazali)

Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) anasema;

"Atakayezielekeza juhudi zake zote katika jambo moja tu, basi Mwenyezi Mungu atamuondolea dhiki za dunia. Na atakayezielekeza juhudi zake katika mambo mengi tofauti na wala asimjali Mwenyezi Mungu popote alipo, basi ataangamia."

Al Hakim.

 

 

Dhiki ya Nafsi

Anasema Sheikh Al Ghazali katika 'Jadid Hayatak' akimnukuu Dil Carington kuwa anasema;

"Nimeishi New York zaidi ya miaka thelathini na saba, na haikutokea hata siku moja mtu akanigongea mlango na kunitahadharisha juu ya maradhi yanayoitwa 'dhiki ya nafsi'. Na maradhi haya katika miaka thelathini na saba iliyopita yamesababisha vifo vingi kupita vifo vilivyosababishwa na maradhi ya tetekuwanga 'chicken pox' kwa mara elfu nyingi.

Naam! Hapana aliyenigongea mlango kunitahadharisha kuwa mtu mmoja katika kila watu elfu kumi wanaoishi Marekani wana hatari ya kupata maradhi ya ugonjwa wa akili wa 'nervous breakdown' unaoletwa na mashaka au kazi nyingi au dhiki ya nafsi, kwani inajulikana kuwa kila dollar inapoteremka thamani yake katika masoko ya pesa 'stock market' basi sukari inapanda na kuongezeka katika mikojo na katika damu ndani ya miili ya wanaokula hasara katika masoko hayo."

Dawa gani iliyo bora ya kutibia maradhi haya kuliko mafundisho ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) aliposema;

"Mwenye kujishughulisha na akhera, Mwenyezi Mungu humuingizia kukinai moyoni mwake, na dunia itamjia mbio. Na mwenye kujishughulisha na dunia, Mwenyezi Mungu humuingizia ufakiri, na hatopata katika dunia isipokuwa kile kile kichache alichokwisha andikiwa?"

Attirmidhiy

Na katika riwaya nyingine;

"Mwenye kuipa umuhimu akhera yake, Mwenyezi Mungu atampa yote mawili (akhera na dunia) na atampa kinaa ndani ya moyo wake. Na mja anapojisogeza kwa moyo wake mbele ya Mola wake, basi Mwenyezi Mungu atazijaalia nyoyo za Waislamu zimpende na kumuombea rehma, na Mwenyezi Mungu atamharakishia kila la kheri."

Al Baihaqy

Mafundisho haya yanatujulisha juu ya uhaba wa thamani ya dunia hii ambayo ingelikuwa mbele ya Mwenyezi Mungu ina uzito hata wa kisasi cha ubawa wa mbu, basi Mwenyezi Mungu asingemnywisha kafiri hata fundo la maji.

Hata hivyo hii isichukuliwe kuwa tunatakiwa tuiache dunia moja kwa moja na kujishughulisha na akhera peke yake kama walivyofahamu baadhi ya wacha Mungu. Bali kinyume na hivyo tunatakiwa tuifanyie kazi na kuchuma tunachoweza kuchuma kwa njia za halali, ili tuweze kuyaendeleza maisha yetu na kutumia uchumi tutakaoupata ndani yake kwa ajili ya kunyanyua hali za maisha.

Lakini juhudi hii isitufanye tukazisahau nyoyo zetu tukajishughulisha na mali, kwani mali tutakayoichuma ni kwa ajili ya matumizi na si kwa ajili ya kurimbika, ni kwa ajili ya kunyanyua hali zetu na kujikinga na balaa, na si kwa ajili ya kuwa nayo tu, kisha tukaacha muongozo mwema tulowekewa na Mtume wetu Muhammad (SAW) aliposema;

"Amestarehe aliyechuma mali ya halali, ukatengenea moyo wake na akawa mkarimu kwa watu huku akiwaepusha watu na shari yake. Amestarehe atakayetenda kwa elimu yake akatoa na kusaidia katika mali yake."

Attarghiyb wal Tarhiyb

 

Anasema Dil Carington;

"Utafiti umethibitisha kuwa dhiki ya nafsi ni muuwaji nambari moja katika nchi ya Marekani. Katika vita vya mwisho vya ulimwengu wameuliwa katika vijana wetu waliokwenda vitani kiasi cha laki tatu unusu, wakati watu wapatao milioni mbili walikufa kwa maradhi ya dhiki ya nafsi katika wakati huo huo. Na hii ndiyo sababu iliyomfanya Dr. Alex Karel aseme kuwa; 'Matajiri na wafanya biashara wasiojuwa namna ya kujiepusha na dhiki ya nafsi wanakufa wakiwa na umri mdogo..'

Wanaokufa kwa maradhi haya miongoni mwa Wamarekani wenye asili za Kiafrika na wenye asili za Kichina ni wachache sana ukilinganisha na wenye asili za kizungu, na hii ni kwa sababu wao wanayachukulia mambo kwa wepesi."

Jadid Hayatak uk. 41-42

Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) amesema;

"Enyi watu! Hakika ya utajiri si utajiri wa mali, bali utajiri wa kweli ni utajiri wa nafsi, na Mwenyezi Mungu Azza wa Jalla humpa mja wake kile tu alichokwishamuandikia katika rizki yake. Kwa hivyo ombeni kwa wema na muchukuwe vya halali na muache vya haramu."

Abu Yaala

Imepokelewa kutoka kwa Ibni Omar (RA) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) alikuwa mara nyingi anapoondoka katika kikao akiomba dua ifuatayo;

Na maana yake ni;

"Mola wetu! Tujaalie tuwe na uoga utakaotuwezesha kujikinga na kukuasi, na tuwe watiifu ili tuweze kuingia katika Pepo yako, na (utugawie) katika yakini itakayotusahilishia katika kupambana na masaibu ya dunia.

Mola wetu tudumishie kusikia kwetu na kuona kwetu na nguvu zetu tunapokuwa hai, na utubakishie mpaka kufa kwetu, na ujaalie visasi vyetu viwe kwa wenye kutudhulumu, na utunusuru juu ya adui zetu, na usijaalie masaibu yetu yakawa katika dini yetu, na usiijalie dunia ikawa ni kubwa lenye kutushughulisha, wala (dunia) isiwe lengo la elimu yetu, na wala usitusalitishie asiyeturehemu."

Attirmidhiy

 

Dua za namna hii na zipo nyingi sana, zinazosaidia katika kuzilainisha nyoyo na kuingiza ndani yake tumaini na kutujulisha nani wa kushikamana naye wakati wa shida na wakati wa masaibu.