RIBA

Riba katika lugha ya kiarabu maana yake ni ziada.

Ama katika lugha ya elimu ya fiq-hi maana ya neno 'Riba', ni ile ziada anayolipwa mdai juu ya rasilamali yake.

Mwenyezi Mungu anasema;

"Na mkiwa mmetubu, basi mtapata rasilmali zenu ; msidhulumu wala msidhulumiwe.

Na kama mkopi ana dhiki, basi (mdai) angoje mpaka afarijike".

Al Baqarah - 279 - 280

Riba imeharimishwa katika dini ya Manasara na Mayahudi pia, isipokuwa Mayahudi wao wanaamini kuwa kuchukuwa riba kwa asiyekuwa Myahudi mwenzao ni halali.

Mwenyezi Mungu anasema;

"Na kwa (sababu ya) kula kwao riba, na hali wamekatazwa wasiile".

Annisaa - 161

Katika dini ya Kiislam, hukmu ya kuharamisha Riba iliteremshwa kwa ukamilifu wakati wa Madina pale ilipoteremka kauli yake Subhanahu wa Taala aliposema;

"Enyi milioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu na acheni yaliyobakia katika riba, ikiwa mmeamini.

Na kama hamtafanya (hivyo) basi fahamuni mtakuwa na vita na Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na mkiwa mmetubu, basi (mdai) angoje mpaka afarijike. Na kama nyinyi (mnaodai mkizisamehe deni zenu) mkazifanya sadaka, basi ni bora kwenu. Ikiwa mnajua haya (basi fanyeni)".

Al Baqarah - 278-279

Mtume (SAW) ameitaja Riba kuwa ni miongoni mwa madhambi saba makubwa yanayoangamiza;

Mtume (SAW) amesema;

"Jiepusheni na mambo saba yanayoangamiza".

Masahaba (RA) wakamuuliza;

"Ni yepi hayo ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?"

Akasema;

"Kumshirikisha Mwenyezi Mungu, na Uchawi, na Kuiuwa nafsi iliyoharamishwa na Mwenyezi Mungu isipokuwa ikiwa kwa ajili ya haki (kwa aliyefanya makosa yanayostahiki kuhukumiwa auawe), na Kula Riba, na Kula mali ya yatima, na Kurudi nyuma katika vita (ukawaacha wenzako peke yao), na kuwasingizia uongo wanawake wema wasio na makosa walioamini (kuwa eti wamezini)".

Bukhari na Muslim

Na Mtume (SAW) amewalaani wote wanaoshiriki katika kitendo hicho cha kula Riba.

Mtume (SAW) amesema;

"Mwenyezi Mungu amemlaani anayekula Riba na anayelisha na mashahidi wake".

Bukhari- Muslim na Imam Ahmed

Mwenyezi Mungu anatuhimiza kuwa ikiwa mtu anataka kumkopesha mwenzake mwenye shida, basi amkopeshe mkopo mwema bila ya kumuongezea mwenzake dhiki, na kwamba kufanya hivyo ndiyo mali yake mtu inaongezeka baraka itokayo kwa Mola wake, ama unapomkopesha mwenye shida kisha ukachukua faida ya Riba, basi huko ni kumzidishia dhiki mwenzio na pia ni kuiangamiza mali yako na kuiondolea barka.

Mwenyezi Mungu anasema;

"Na zile (pesa za kukopeshea) riba mtoazo (katika kuwakopesha watu) ili zizidi katika mali ya watu, mbele ya Mwenyezi Mungu hazizidi (pesa hizo; bali zinaingia nuhusi na shakawa); lakini (mali) mnayoyatoa kwa ajili ya Zaka kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu , basi hao (wenye kufanya haya) ndio wazidishao (mali zao)".

Ar Rum- 39

Riba ziko aina mbili;

Ya kwanza ni zile pesa zaidi anazolipa mtu aliyekopeshwa kwa kuhsurutishwa na mdai.

Yaani kwa mfano mtu akitaka kukopa shilingi elfu, anashurutishwa kulipa shilingi elfu na zaidi. Sasa zile zaidi ndiyo Riba yenyewe.

Ya pili ni Riba ya kufadhilisha

Nayo ni ile ya kubadilishana pesa kwa pesa au chakula kwa chakula na kuchukuwa zaidi.

Kwa mfano mtu anapokwenda kubadilisha dhahabu yenye uzito wa gram kumi kwa ajili ya kupata dhahabu nyengine iliyomvutia zaidi, akalipwa badala yake dhahabu yenye uzito wa gram saba. Hiyo inahesabiwa ni Riba.

Inavyotakiwa kwanza mtu aiuze dhahabu ile kwa thamani yake, kisha ainunue dhahabu anayoitaka.

Mtume (SAW) amesema;

"Msiuze Dirham moja kwa Dirham mbili, kwani nakuogopeeni Riba".

Na akasema;

"Dhahabu kwa dhahabu, fedha kwa fedha, ngano kwa ngano, chumvi kwa chumvi, mkono kwa mkono, atakayechukua zaidi au kutaka zaidi, kesha kula Riba".

Ahmed na Bukhari

Mtu mmoja alikwenda kwa Mtume (SAW) akiwa amebeba tende.

Mtume (SAW) akamwambia;

"Tende hii haipatikani kwetu hapa?"

Mtu yule akasema;

"Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, tumebadilishana tende yetu pishi moja kwa pishi mbili za tende hizi".

Mtume (SAW) akamwambia;

"Hiyo ni Riba, zirudishe, kisha uza tende yetu, halafu nunua tende hizi".

Muslim