SAJDAH YA TILAWA

Muhamma Faraj Salem Al Saiy

 

Mtu anapoisikia aya ya Sajdah ikisomwa anatakiwa akabbir kisha asujudu, kisha pale anapoinuka kutoka kwenye Sajdah akabbir tena bila ya kusoma tahiyatu wala kutoa salaam. - Hii inaitwa Sajdah ya Tilawa.

Kutoka kwa Nafi-i anasema kuwa Abdillahi bin Omar (Radhiya Llahu anhu) amesema;

"Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alikuwa anaposoma Qurani akiifikia aya ya Sajdah anakabbir na kusujudu na sisi tulikuwa tukisujudu (pia)".

Abu Daud - Al Baihaqiy na Al Hakim

FADHILA ZAKE

Kutoka kwa Abu Huraira (Radhiya Llahu anhu) alisema kuwa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema;

"Mtu anapoisoma aya ya Sajdah kisha akasujudu, shetani huondoka akiwa analia huku akisema;

"Ole wangu! Ameamrishwa kusujudu akasujudu na jazaa yake ni Pepo, na mimi niliamrishwa kusujudu nikakataa na jazaa yangu ni Moto".

Ahmed - Muslim na Ibni Majah

HUKMU YAKE

Imam Abu Hanifa amesema kuwa hukmu yake ni Wajib, na Imam Shafi amesema kuwa hukmu yake ni Sunnah.

Maulamaa wengi wamekubaliana kuwa hukmu ya Sajdah ya tilawa ni Sunnah kwa msomaji na kwa msikilizaji. Na hii inatokana na hadithi iliyosimuliwa na Imam Bukhari kuwa Omar bin Khattab (Radhiya Llahu anhu) akiwa juu ya membari mojawapo katika Ijumaa alisoma Suratul Nah'l mpaka alipoifikia aya ya Sajdah akateremka na kusujudu na watu wakasujudu. Ijumaa iliyofuata akaisoma tena sura ile ile na alipoifikia aya ya Sajdah (hakusujudu) akasema;

"Enyi watu! Sisi hatujalazimishwa kusujudu, atakayesujudu atakuwa amesibu (amefanya sawa kama inavyotakiwa) na asiyesujudu hapati dhambi".

Na katika riwaya nyingine alisema;

"Mwenyezi Mungu hakutufaradhishia kusujudu, isipokuwa kwa anayetaka".

Kutoka kwa Zeid bin Thabit (Radhiya Llahu anhu) alisema;

"Nilimsomea Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) siku moja Suratul Najm (yote) na hakusujudu ndani yake".

(Yaani hakusujudu pale alipoifikyia aya ya Sajdah iliyo ndani ya sura hiyo)

Hadithi hii imetolewa na maimam wote isipokuwa Ibni Majah

Imam Addaraqutni akaongeza;

"..Na hapana hata mmoja kati yetu aliyesujudu".

Anasema Sayed Sabeq katika 'Fiq-hi sunnah';

"Hii ni dalili kuwa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) aliacha kusujudu kwa ajili ya kutujulisha kuwa si lazima kufanya hivyo - (si fardhi wala si wajibu - bali ni Sunnah)".

Ipo riwaya nyengine inayosema kuwa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) siku moja aliisoma Suratul Najm na alipoifikia aya ya Sajdah akasujudu, na Masahaba (Radhiya Llahu anhum) wote wakasujudu pamoja naye isipokuwa mzee mmoja wa Kikureshi aliyechota gao la mchanga na kujipangusa nao usoni pake, kisha akasema; "Inatosha mimi kufanya hivi tu". (Yaani haina haja yeye kuporomoka na kumsujudia Mola wake, na badala yake inatosha kujipaka mchanga usoni pake - na hii ni dalili ya kibri)

Anasema Abdullahi bin Masaud (Radhiya Llahu anhu);

"Nilimuona mtu huyo baada ya siku ile akiuliwa akiwa kafir. (akiwa upande wa makafiri)".

Bukhari na Muslim

AYA ZA KUSUJUDU

Aya za Sajdah ni kumi na tano (15). Kutoka kwa Amru bin Al Aas (Radhiya Llahu anhu) kuwa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alimtajia sehemu 15 za kusujudu katika Qurani nazo ni kama ifuatavyo;

1) Al Aaraf - 206. "Hakika wale walioko kwa Mola wako Mlezi hawajivuni wakaacha

kumuabdu, na wanamtakasa na wanamsujudia".

2) Al Raad - 15. "Na viliomo mbinguni na katika ardhi vinamsujudia Mwenyezi Mungu tu vikitaka visitake. Na pia vivuli vyao asubuhi na jioni".

3) Annahl - 49. "Na vyote viliomo katika mbingu na katika ardhi, tangu wanyama mpaka Malaika, vinamsujuidia Mwenyezi Mungu, na wala havitakabari".

4) Al Israa- (Bani Israil) - 107. "Sema: Aminini au musiamini. Hakika wale walio pewa ilimu kabla yake, wanaposomewa hii, huanguka kifudifudi wakasujudu".

5) Maryam - 58. "Wanapo somewa Aya za Mwingi wa Rehema huanguka kusujudu na kulia".

6) Al Hajj - 18. "Je! Huoni kwamba vinamsujudia Mwenyezi Mungu viliomo mbinguni na viliomo katika ardhi, na jua, na mwezi,na nyota, na milima, na miti, na wanyama, na wengi miongoni mwa watu. Na wengi imewastahiki adhabu. Na anayefedheheshwa na Mwenyezi Mungu hana wa kumhishimu. Hakika Mwenyezi Mungu hutenda apendayo".

7) Al Hajj - 77. "Enyi mlioamini! Rukuuni na msujudu, na muabuduni Mola wenu Mlezi, na tendeni mema, ili mfanikiwe".

8) Al Furqan - 60. "Na wanapo ambiwa: Msujudieni Arrahman! Wao husema: Ni nani Arrahman? Je! Tumsujudie unayetuamrisha wewe tu? Na huwazidishia chuki".

9) An Naml - 25. "Na hawamsujudii Mwenyezi Mungu ambaye huyatoa yaliyo fichikana katika mbingu na ardhi, na anayajua mnayo yaficha na mnayo yatangaza".

10) Assajdah - 15. "Hakika wanao ziamini Aya zetu ni hao tu ambao wakikumbushwa hizo, basi wao huanguka kusujudu, na humsabihi Mola wao Mlezi kwa kumhimidi, nao hawajivuni".

11) Surat Saad - 24. "Na Daudi akajua kuwa tumemfanyia mtihani. Basi akamwomba msamaha Mola wake Mlezi, na akaanguka kusujudu na kutubia".

12) Fussilat (Haamiym Sajdah) - 37. "Na katika Ishara zake ni usiku na mchana, na jua na mwezi. Basi msilisujudie jua wala mwezi, bali msujudieni Mwenyezi Mungu aliyeviumba, ikiwa nyinyi mnamuabudu Yeye tu".

13) Annajm - 62. "Basi msujudieni Mwenyezi Mungu, na mumuabudu".

14) Al Inshiqaaq - 21. "Na wanaposomewa Qur'ani hawasujudu?"

15) Al Alaq - 19. "Hasha! Usimt'ii! Nawe sujudu na ujongee!"

SHURUTI ZAKE

Baadhi ya maulamaa wamesema kuwa shuruti za kusujudu Sajdah ya tilawa ni shuruti zile zile zinazotakiwa katika Sala, kama vile kuwa na udhu, kuelekea kibla na kujisitiri mtu utupu wake nk.

Ama Imam Al Shaukani anasema;

"Hapana dalili yoyote ile katika hadithi zinazozungumzia Sajada ya tilawa kuwa mtu anatakiwa awe na udhu anaposujudu Sajdah hiyo, na Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alikuwa akisujudu mbele ya hadhara ya watu (ndani na nje ya msikiti) na watu hao walikuwa wakisujudu pamoja naye na haikunukuliwa kuwa aliwahi kumuamrisha mtu yeyote yule atawadhe, na haingewezekana kabisa kuwa wote waliosujudu naye wawe wana udhu. Imenukuliwa pia kuwa waliwahi kusujudu pamoja naye baadhi ya mushrikina na bila shaka wao ni najsi na hata kama watatawadha basi udhu wao hautosihi."

KUOMBA DUA WAKATI WA KUSUJUDU

Atakayesujudu Sajda ya tilawa anaruhusiwa kuomba dua aitakayo, isipokuwa ipo hadithi ya Bibi Aisha (Radhiya Llahu anhaa) inayosema;

"Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) pale anaposujudu Sajda ya Qurani alikuwa akisema;

"Sajad waj-hiy lilladhiy khalaqahu wa shaqqa sam-ahu wa basarahu bihawlihiy wa quwatihiy, fatabaaraka llahu ahsanul khaliqiyn"

Na maana yake ni;

(Uso wangu umemsujudia Yule aliyeuumba na kuupa masikio na macho kwa uwezo Wake na nguvu Zake, kwa hivyo ametukuka Allah mbora wa kuumba).

Imepokelewa na maimam wote wa hadithi isipokuwa Ibni Majah

Baadhi ya maulamaa wamesema;

"ikiwa mtu atasujudu Sajda ya tilawa katika Sala, basi aseme; "Subhana rabbiya l a-alaa".

KUSUJUDU NDANI YA SALA

Imamu anaweza kusujudu pale anapoisoma aya ya Sajda akiwa ndani ya Sala za kusoma kwa sauti (Magharibi - Ishaa - Alfajiri) au ndani ya Sala za kimya (Adhuhuri na Alasiri), na maamuma anatakiwa amfuate imamu pale anaposujudu hata kama hajamsikia akiisoma aya hiyo katika zile Sala za kimya.

Anasema Abi Rafia kuwa alisali maamuma nyuma ya Abu Huraira (Radhiya Llahu anhu) Sala ya Isha na ndani yake akaisoma sura ya 'Idha ssamaau n shaqat' na alipoifikia aya ya Sajdah akasujudu.

Anasema akamuuliza Abu Huraira (Radhiya Llahu anhu);

"Sajda hii ya nini?"

Akamjibu;

"Nilisali maamuma nyuma ya Abal Qassim (Mtume Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akasujudu alipoifikia aya hii na nitaendelea kusujudu kila ninapoisoma mpaka nitakapokutana naye (Swallah Llahu alayhi wa sallam)".

Bukhari na Muslim

Imepokelewa kutoka kwa Al Hakim kuwa Ibni Omar (Radhiya Llahu anhu) alisema kuwa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alisujudu katika raka-a ya mwanzo ya Sala ya adhuhuri na ikawabainikia baadaye kuwa aliisoma suratul Sajda (Haamiym tanziyl).

Anasema Imam Al Nawawiy;

"Hapana ubaya mtu akisoma sura yenye Sajda akiwa katika Sala ya kimya au akiwa katika Sala ya kusoma kwa kunyanyua sauti."

Ama Imam Malik kwake ni makruh kuzisoma Sura za Sajdah ndani ya Sala.

Imam Abu Hanifa yeye anasema kuwa ni makruh kuisoma sura yenye Sajda katika Sala ya kimya lakini hapana ubaya kuisoma katika Sala ya kusoma kwa sauti.

SAJDA ZIKIWA NYINGI

Mtu akizisoma aya nyingi za Sajdah au akizisikia mara nyingi kwa wakati mmoja ndani ya msikiti au popote pale, anaweza kuiakhirisha na kusujudu mara moja tu pale atakapoisoma kwa mara ya mwisho.

Maulamaa wengine wamesema kuwa ni bora pia kuziakhirisha pia Sajdah hizo ikiwa aya ya Sajdah imesomwa katika zile nyakati zilizokuwa Makruh ndani yake mtu kusujudu kama vile baada ya Sala ya Alasiri hasa pale jua linapozama na na baada ya Sala ya Alfajirihasa pale jua linapochomoz.

KUKIDHI

Maulamaa wengi wanasema kuwa ni bora mtu asujudu pale pale mara baada ya kuisoma aya ya Sajdah au kuisikia, lakini akiiakhirisha na akasujudu baadaye inajuzu ikiwa wakati hautokuwa mrefu.