SIFA ZA MUISLAMU

 Na Omar Rijal

Kujiepusha na chuki
Chuki na uadui ni kazi ya shetani. Penye chuki na uadui hapana jema lolote linalofanyika na ni furaha kwa shetani. Chuki inayoruhusiwa kwa Waislamu ni ile ya kuchukia uovu na maadui wa Allah (s.w.) - maadui wa Uislamu na Waislamu.

Waislamu wanakatazwa kuwa na urafiki na maadui wa Allah.

Enyi mlioamini! Msiwafanye adui zangu na adui zenu kuwa marafiki, mnaowapelekea (habari zenu) kwa ajili ya urafiki hali yakuwa wameishaikanusha haki iliyokujieni..." (60:1).

Enyi mloamoni! Msifanye urafiki na watu ambao Mwenyezi Mungu amewakasirikia; na wamekata tamaa ya kupata malipo ya Akhera
kama walivyokata tamaa makafiri walio makaburini... (60:13).

Enyi mloamoni! Msifanye urafiki na wale walioifanyia mzaha na mchezo dini yenu miongoni mwa wale waliopewa kitabu kabla yenu na miongoni mwa makafiri. Na mcheni Mwenyezi Mungu
kama nyinyi na wenye kuamini. (5:57).

Pamoja na hivyo haina maana Waislamu wasiwafanyie uadilifu hawa maadui wa Allah na maadui wa Uislamu, bali Waislamu wataendelea kuwatendea wema na kuishi nao kwa wema iwapo watataka amani.

Kuwa mwenye Kusamehe
Muislamu anatakiwa ajenge tabia ya kuwavumilia wengine.
Awe na tabia ya kujihesabu. Ajione kuwa naye
kama binaadamu wenzake ni mkosaji na angependa asamehewe na wale aliowakosea kwa makusudi au kwa bahati mbaya. Kitendo cha kuwasemehe wale waliokukosea ni kitendo cha uchaji Mungu chenye malipo makubwa mbele ya Allah (s.w.) Kama inavyobainishwa katika aya zifuatazo:

Na yaendeeni upesi upesi maghufira ya Mola wenu na Pepo (yake) ambaye upana wake (tu) ni (sawa na) mbingu na ardhi. (Pepo) iliyowekewa wamchao Mungu. Ambao hutoa katika (hali ya) wasaa na katika (hali ya) dhiki, na wazuiyao ghadhabu na wanasamehe watu (na wawafanyiao ihsani); na Mwenyezi Mungu anawapenda wafanyao ihsani. (3:133-134).

Basi vyote hivi mlivyopewa ni starehe ya maisha ya dunia tu, lakini kilichoko kwa Mwenyezi Mungu ni bora na cha kudumu (milele). Watakistahiki wale walioamini na wakawa wanamtegemea Mola wao. Na wale wanaojiepusha na madhambi makubwa na mambo mabaya, na wale ambao wanapokasirika husamehe. (42:36-37).

Mwenye kuwasamehe wengine husamehewa makosa yake na Allah (s.w.):

Na wasiape wale wenye mwendo mzuri (wa dini) na wenye wasaa (katika maisha
yao) miongoni mwenu (wasiape kujizuia) kuwapa walio jamaa na maskini na waliohama kwa njia ya Mwenyezi Mungu; na waachilie mbali, (wapuuze yaliyopita. Linalopita hupishwa); Je, nyinyi hampendi Mwenyezi Mungu akusameheni? Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha (na) mwingi wa rehema. (Basi nyinyi sifikeni kwa sifa hizi). (24:22).

Naye Mtume (s.a.w.) Anatufahamisha ubora wa kusamehe katika hadithi zifuatazo:

U'qbah bin Amir (r.a.) Ameeleza kuwa Mtume wa Allah amesema: "Ee U'qbah! Je, nikufahamishe juu ya watu wema kuliko wote katika dunia hii na akhera?" Alijibu Ndio, Akasema (Mtume): "Utaendeleza uhusiano mwema na mtu aliyevunja uhusiano kati yako na yeye; utampa yule aliyekunyima; na utamsamehe yule aliyekudhulumu". (Baihaqi).

Abu Hurairah (r.a.) Ameeleza kuwa Mtume waallah amesema kuwa Musa (a.s.), mwana wa Imran, aliuliza: Ee Mola wangu! Nani, katika waja wako anayeheshimika (Mwenye hadhi) zaidi mbele yako? (Allah) alimjibu: Yule anayesamehe japo ana nguvu au uwezo (wa kutosamehe) (Baihaqi).

Hivyo Allah (s.w.) Anatuusia:

"Shikamana na kusamehe na amrisha mema na wapuuze majahili:. (7:199).

Kukataa kusamehe baada ya kuombwa msamaha na yule aliyekukosea ni jambo ovu. Allah (s.w.) Hamsamehe yule asiyesamehe wanaadamu wenzake. Ukweli ni kwamba wanayotukosea wanaadam wenzetu hata tuyaone ni makubwa vipi, ni madogo
sana ukilinganisha na makosa yetu kwa Allah (s.w.). Inakuaje sasa tushindwe kusamehe haya makosa madogo madogo na wakati huo tunatamani kusamehewa milima na milima ya makosa yetu?

Hivyo, yule anayetaka kusamehewa na Allah, basi awe mwepesi wa kuwasamehe wanaadamu wenzake. Kuhusu uovu wa kukataa kuwasamehe wale waliokiri makosa
yao na kuomba msamaha, anasema Mtume (s.a.w.):

"
Kama mtu, anakiri makosa yake kwa mwingine na kutaka msamaha, na yule akatakaa kutoa msamaha, basi hatanyweshwa maji ya kawthar (huyo aliyekataa, kusamehe). (Tabrani).

Kujizuia na Hasira
Kujizujia na hasira ni tabia njema inayoambatana na tabia ya kusamehe. Hasira humpata mtu anapooudhiwa. Wakati mwingine huja ghafla na kumnyima mtu wakati wa kufikiri. Hasira zinaongozwa na shetani, hivyo humnyima mtu nafasi ya kutumia akili, hekima na busara. Hivyo humpelekea mtu kufanya matendo ambayo hugeuka kuwa majuto baadaye. Hasira hasara.

Kujizuilia na hasira ni kitendo cha ucha Mungu chenye malipo makubwa mbele ya Allah (s.w.). Rejea Qur'an (3:133-134) na (42:36-37).

Pia ubora wa kujizuilia na hasira unadhihirika katika Hadithi zifuatazo:

Abu Hurairah amesimulia kuwa mtu mmoja alimuomba Mtume(s.a.w.):"Niwaidhi'.Mtumeakasema: "Usighadhibike". Kisha akarudia mara nyingi akisema" Usighadhibike. (Bukhari).

Abu Hurairah ameeleza kuwa Mtume wa Allah amesema: "Mtu mwenye nguvu si bingwa wa mieleka bali mtu mwenye nguvu ni yule anayejizuilia na hasira". (Bukhari na Muslim).

Ibn Umar amesimulia kuwa Mtume wa Allah amesema: "Hapana mja aliyemeza kidonge kichungu mbele ya Allah (s.w.) Kuliko kidonge cha hasira alichokimeza, huku akitaraji radhi ya Allah (s.w.)." (Ahmad).

Mbinu za kujizuia na hasira zimebainishwa katika Qur'an
kama ifuatavyo:

Shikamana na kusamehe na amrisha mema na wapuuze majahili (wajinga). Na
kama wasi wasi wa shetani ukikusumbua basi (sema:Audhubillah) jikinge kwa Mwenyezi Mungu. Bila shaka yeye ndiye asikiaye na ajuaye. (7:199-201).

Kutokana na aya hizi tunajifunza kuwa mbinu za kujizuilia na hasira ni hizi zifuatazo:

(i) Kushikamana na kusamehe.

(ii) Kushikamana na kuamrisha mema.

(iii) Kuwapuuza majahili.

(iv) Kujikinga kwa Allah (s.w.) na uovu wa shetani.

Pia Mtume (s.a.w.) Anatupa mbinu nyingine za kupambana na hasira katika hadithi zifuatazo:

Atiyyah bin Urwah Ba'id ameeleza kuwa Mtume wa Allah amesema: "Hakika hasira zinatoka kwa Shetani, na Shetani ameumbwa kutokana na moto na hakika moto huzimishwa na maji. Kwa hiyo yoyote miongoni mwenu atakayepandwa na hasira, na atawadhe". (Abu Daud).

Abu Zarr (r.a.) Ameeelza kuwa Mtume wa Allah amesema: "Wakati wowote mmoja wenu atakapopandwa na hasira akiwa amesimama, na akae chini.
Kama (kwa kufanya hivyo) hasira itamtoka ni vyema; lakini kama haitatoka, na alale chini." (Ahmad, Tirmidh).

Kutokana na Hadithi hizi Mtume (s.a.w.) anatuelekeza tupunguze hasira zetu kwa:

(i) Kutia udhu

(ii) Kukaa chini iwapo tumesimama.

(iii) Kulala chini.

Kuwa na subira na Uvumilivu
Subira ni kitendo cha kuwa na uvumilivu na utulivu baada ya kupatwa na matatizo au misuko suko mbali mbali katika maisha ya kila siku. Muislamu anatakiwa awe ni mwenye kusubiri baada ya kupata shida au matatizo
kama tunavyoamrishwa katika Qur'an.

"Enyi mlioamini! Jisaidieni (katika mambo yenu) kwa kusubiri na kuswali. Bila shaka Allah yupo pamoja na wanaosubiri." (2:153).

"Enyi mlioamini!
Subirini na washindeni wengine wote kwa kusubiri na kuweni imara na mcheni allah mpate kufaulu". (3:200).

Suala la kupatwa na matatizo, misiba na misukosuko mbali mbali ni jambo la kawaida katika maisha ya hapa duniani. Hatuna budi kufahamu kuwa ulimwengu huu haukusudiwa na Mola Muumba uwe pepo.
Bali umekusudiwa uwe uwanja wa kumtahini mwanaadamu. Hivyo viumbe vyote vilivyomzingira pamoja na matukio na miondoko yote ya maisha viko pale kama vifaa vya kumtahini mwanaadamu. Suala la kutahiniwa mwanaadamu limewekwa bayana katika Qur'an:

Kwa hakika tumemuumba mtu kutokana na mbegu ya uhai iliyochanganyika: (ya mwanamume na mwanamke), ili tumfanyie mtihani (kwa amri zetu na makatazo yetu) kwa hivyo tukamfanya ni Mwenye kusikia (na) mwenye kuona. Hakika sisi tumemuongoa, (tumembainishia) njia (zote mbili hizi; kuwa hii ndiyo ya kheri na hii ndiyo ya shari). Basi (mwenyewe tena) atakuwa mwenye shukurani au awe mwenye kukufuru, (kukanusha). (76:2-3).

Ametukuka yule ambaye mkononi mwake umo Ufalme (wote); naye ni mwenye uwezo juu ya kila kitu. Ambaye ameumba mauti na uhai ili kukujaribuni (kukufanyieni mtihani); ni nani miongoni mwenu mwenye vitendo vizuri zaidi. Naye ni Mwenye Nguvu na Mwenye Msamaha. (67:1-2).

Na tutakufanyieni mitihani mpaka tuwadhihirishe (wajulikane) wale wanaopigania dini miongoni mwenu na wanaosubiri; nasi tutadhihirisha habari zenu. (47:31).

Mnadhani kuwa mtaingia Peponi, na hali hamjajiwa na mfano wa (yale yaliyowajia) wale waliopita kabla yenu? Yaliwapata mashaka na madhara na wakatetemeshwa
sana hata Mitime na walioamini pamoja nao wakasema: "Nusura ya Mwenyezi Mungu itafika lini?" Jueni kuwa nusura ya Mwenyezi Mungu iko karibu. (2:214).

Je, watu wanadhani wataachwa (wasitiwe katika misukosuko) kwa kuwa wanasema, "Tumeamini?" Basi ndio wasijaribiwe (wasipate mitihani)? Hapana; bila shaka tuliwatia katika taabu wale waliokuwa kabla
yao, na kwa yakini Mwenyezi Mungu atawatambulisha wale walio wa kweli na kuwatambulisha (wale walio) waongo. (29:2-3).

Ili kukamilisha kusudio hili la kumjaribu (kumtahini) mwanaadamu Mwenyezi Mungu (s.w.) Ameupamba huu ulimwengu kwa machungu na matamu yaliyochanganyika. Uzuri au mazuri hayapatikani kwa urahisi ila mpaka kuvuka vikwazo vingi vya matatizo na misukosuko ya namna kadhaa wa kadhaa. Na uzuri au mazuri yanapopatikana hayabakii milele bali huwa ni ya muda mfupi kwani nayo yamezingirwa na matatizo na mikasa elfu moja na moja. Hii ndio sura halisi ya maisha ya huu ulimwengu. Kwa hiyo wale wanaodhania ulimwengu huu ni mahali pa starehe - kufurahia maisha tu bila ya kuonja machungu yake watakuwa wamejidanganya mno na badala yake wataishi maisha ya huzuni, wasiwasi na kukata tamaa. Kinyume chake, Waislamu wanatakiwa wawe na uhakika juu ya maisha ya huu ulimwengu kuwa ni ya majaribio na mafanikio yatapatikana kwa kutenda wema kwa ajili ya Allah (s.w.) Na kusubiri au kustahamili mazito, matatizo na misukosuko yote ya maisha itakayowakabili.

Kufanya subira si jambo jepesi bali ni jambo linalohitaji jitihada na uzima kubwa
kama Qur'an inavyoatuusia:

Ewe Mwanangu! Simamisha swala, na uamrishe mema, na ukataze mabaya, na usubiri juu ya yale yatakayokusibu (kwani mwenye kuamrisha mema na kukataza mabaya lazima zitamfika tu taabu); Hakika hayo ni katika mambo yanayostahiki kuazimiwa (na kila mtu). (31:17).

Na anayesubiri na kusamehe (atalipwa wema wake). Bila shaka
hilo ni katika mambo makubwa ya kuazimiwa kufanywa (na kila Muislamu). (42:43).

Kufanya subira ni kitendo cha hali ya juu cha Ucha Mungu na Mwenyezi Mungu (s.w.) Ameahidi malipo makubwa kwa yule atakayejitahidi kusubiri
kama tunavyojifunza katika aya zifuatazo:

Sema: "Enyi waja wangu mlioamini! Mcheni Mola wenu. Wale wafanyao wema katika dunia hii watapata wema; na ardhi ya Mungu ina wasaa. Na bila shaka wafanyao subira (wakajizuilia na maasia na wakaendelea watapewa ujira wao pasipo hisabu". (39:10).

Na tutakutieni katika msukosuko wa (baadhi ya mambo haya); hofu na njaa na upungufu wa mali na wa watu na wa matunda. Na wapashe habari njema wanaosubiri. Ambao uwapatapo msiba husema:"Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu, na kwake Yeye tutarejea (atatupa jaza (yake)" . Hao juu
yao zitakuwa baraka baraka zitokazo kwa Mola wao na rehema; na ndio wenye kuongoka. (2:155-157).

Pia Mtume (s.a.w.) Anatufahamisha kuwa malipo ya subira ni Pepo na kusamehewa madhambi
kama tunavyojifunza katika hadithi zifuatazo:

(i) Abu Hurairah (r.a.) Amehadithia kuwa Mtume wa Allah amesema, Mwenyezi Mungu (s.w.) Amesema, "Sina malipo mengine ila pepo kwa mja wangu aliyeamini ambaye anasubiri wakati ninapomchukulia kipenzi chake kutoka miongoni mwa wakazi wa ulimwengu." (Bukhari).

(ii) Anas (r.a.) Amesimulia kuwa amemsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu akisema kuwa allah (s.w.) Amesema, "Ninapomtia msuko suko mja wangu katika vitu vyake viwili vipenzi (macho yake) na akatulia kwa subira, nitamlipa macho yake kwa Pepo." (Bukhari).

(iii) Abu Said na Abu Hurairah wameeleza kuwa wamemsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu akisema: Aslani Muumini hafikwi na makero (matatizo), magumu au ugonjwa, huzuni au hata wasi wasi moyoni, iwe hakusamehewa dhambi zake. (Bukhari na Muslim).

(iv) Imesimuliwa katika mamlaka ya Abu Hurairah kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema Muislamu mwanamume au Muislamu mwanamke ataendelea kuwa katika majaribu juu ya maisha yake,
mali yake na watoto wake mpaka amkabili Mwenyezi Mungu (s.w.) Katika hali ambayo dhambi zake zote zimesamehewa. (Tirmidh).

Hivyo kila Muislamu wa kweli hanabudi kujitahidi kusubiri kwa lolote zito litakalomfika na ajiliwaze kwa maliwazo aliyofunza Mwenyezi Mungu (s.w.) Kwa kusema:

"Innalillaahi Wainnailayhir-Raji'uun".

Tafsiri:

"Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu na kwake yeye tutarejea".

Muislamu hatakiwi achoke kusubiri wala asitamani kufa au kuomba kifo kutokana na mazito yaliyomfikia:

Anas (r.a.) ameeleza kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: "Pasiwe na yoyote miongoni mwenu anayetamani kufa (au anayeomba kifo) kwa sababu ya tatizo lolote lililomfikia.
Kama amefika mwisho wa kuvumilia na aseme: "Ee Allah nibakishe hai iwapo kuishi ni bora zaidi kwangu na nifishe kama kufa ndio bora kwangu". (Bukhari na Muslim).

Maeneo ya Subira:
Katika Uislamu subira inatakiwa ihudhurishwe katika maeneo yafuatayo:

Kwanza: kusubiri unapofikwa na misukosuko au matatizo mbali mbali ya kimaisha miongoni mwa khofu, kufiwa, kuugua, kuuguliwa, kukosa maslahi ya kimaisha na matatizo mengine mbali mbali yanayowafika wanaadamu katika maisha ya kila siku.

Pili: kusubiri au kuwa wastahimilivu katika kutekeleza maamrisho ya Allah (s.w.) katika maisha yetu yote. Maamrisho kama kusimamisha swala tano, kufunga Ramadhan, kuwatendea wema wazi, mayatima, maskini, majirani na wanaadam wengine, kuchunga haki za wengine, (n.k.) ni matendo mja anayotakiwa aendelee kuyafanya mpaka mwisho wa maisha yake. Juu ya kusimamisha swala, tunaamrishwa katika Qur'an:

"Na waamrishe watu wako kuswali, na uendelee mwenyewe kufanya hivyo..." (20:132).

Tatu: kusubiri au kuwa wavumilivu katika kumtii allah (s.w.) Kwa kuacha yale aliyotuharamisha. Movu mengi yaliyoharamishwa na Allah (s.w.), machoni mwa mwanaadamu yanaonekana kuwa mazuri na starehe yenye mvuto mkubwa. Kwa mfano nami asiyeona jinsi ule, uzinifu, muziki, kamari, riba, hongo, nyama ya nguruwe, n.k. vinavyowavutia walimwengu na kuwazamisha humo mamilioni. Mtume (s.a.w.) Amesema:

Pepo imezungukwa na yasiyopendeka (vikwazo) na Moto umezungukwa na vitu vya anasa (carnal desires), Muslim).

Nne: ni kusubiri au kustahimili maudhi kutoka kwa wanadamu wenzetu. Misukosuko na matatizo mengi yanayomkabili mwanadamu ni yale yanayosababishwa na wanaadamu wenzake. Muislamu wa kweli hatalipiza kisasi kwa maovu aliyofanyiwa na mwingine, wala hatamuapiza na kumlaani aliyemfanyia maovu hayo bali atastahimili kwa matarajio ya kupata malipo makubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w.).

Waislamu tunatakiwa mara kwa mara tumuombe Allah (s.w.) Atumiminie subira
kama yeye mwenyewe anavyotuelekeza kuomba:

"... Mola wetu! Tumiminie subira na tufishe hali ya kuwa Waislamu". (7:126).

"Mola wetu!
Tumiminie subira na uithibitishe miguu yetu, na utusaidie juu ya watu hawa makafiri". (2:250).

Kuwa Mkarimu
Ukarimu ni miongoni mwa tabia njema anayotakiwa ajipambe nayo Muislamu. Muislamu anatakiwa awe mwepesi wa kuwakirimu wengine kwa kuwasaidia wakati wanapokuwa katika hali ya kuhitajia msaada bila ya kutarajia malipo yoyote kutoka kwao. Sifa ya wakarimu inabainishwa katika aya zifuatazo:

Na huwalisha chakula maskini na mayatima na wafungwa, na hali yakuwa wenyewe wanakipenda (chakula hicho). (Husema wenyewe katika nyoyo zao wanapowapa chakula hicho): "Tunakulisheni kwa ajili ya kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu (tu) hatutaki kwenu malipo wala shukrani". "Hakika sisi tunaiogopa kwa Mola wetu hiyo siku yenye shida na taabu". (76:8-10).

Pia kumfanyia mgeni takrima ni jambo lililowajibishwa kwa Waislamu, Waislamu kama tunavyojifunza katika hadithi zifuatazo:

(i) Abu Hurairah (r.a.) Ameeleza kuwa Mtume wa Allah amesema,"Yule anayemuamini Allah na siku ya mwisho hatamdhuru jirani yake, na yule anayemuamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho atamkirimu mgeni wake na yule anayemuamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho ataongea mazuri au atakaa kimya". (Bukhari na Muslim).

(ii) Abu Shuraikh Ka'ab (r.a.) Amesimulia kuwa Mtume (s.a.w.) Amesema, "Yoyote anayemuamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho hanabudi kumkirimu mgeni wake, na jukumu lake (la kumhangaikia sana) ni mchana mmoja na ukarimu (kumfurahisha mgeni) ni siku tatu na zaidi ya hapo ni sadaqa. Si vyema kwa mgeni kuendelea kubaikia baada ya siku tatu na kuendelea kumuweka mwenyeji wake katika hali ya uzito". (Bukhari na Muslim).

Kiigizo chetu cha ukarimu ni Mitume wa Allah (s.w.). Tunafahamishwa katika Qur'an juu ya ukarimu wa Nabii Ibrahim:

Je! Imekujia hadithi ya wageni wahishimiwao wa (Nabii) Ibrahimu? Walipoingia kwake wakasema: "Salaam (Alaykum);" Na (yeye Ibrahimu) akasema: "(Alaykumus) Salaam". (Na katika moyo wake anasema): "Ninyi watu nisiokujueni". Mara akaenda kwa ahali yake na akaleta ndama aliyenona. Akampeleka karibu yao. (Walipokuwa hawajanyosha mikono kula alisema: "Mbona hamuli!" (51:24-27).

Katika hadithi, amesimulia Ibn Abbas (r.a.) Kuwa: Mtume (s.a.w.) Alikuwa mkarimu sana kuliko watu wote na alikuwa akizisha ukarimu katika mwezi wa Ramadhan..." (Bukhari).

Malipo haya kuwakirimu watu ni kupata takrima ya allah (s.w.) Huko Peponi kama inavyobainishwa katika aya zifuatazo:

"Basi Mwenyezi Mungu atawalinda (wakarimu) na shari ya siku hiyo na kuwakutanisha na neema na furaha. Na atawajaza Mabustani (ya Peponi) na maguo ya hariri, kwa sababu ya kusubiri (kwao). Humo wataegemea viti vya enzi, hawataona humo jua (kali) wala baridi (kali). Na vivuli vyake vitakuwa karibu yao, na mashada ya matunda yake yataning'inia mpaka chini. Na watapitishiwa vyombo vya fedha na vikombe vya vigae. Vigae vya fedha; wamevijaza kwa vipimo.Na humo watanyweshwa kinywaji kilichochanganyika na tangawizi. Huo ni mto ulio humo (Peponi) unaitwa Salsabili. Na watawazungukia (kuwatumikia), wavulana wasiochakaa, ukiwaona utawafikiri ni lulu zilizotawanywa. Na utakapoyaona (yaliyoko) huko utaona neema (zisizo kuwa na mfano) na kijani kibichi na ufalme mkubwa. Juu yao wana nguo za hariri laini, za kijani kibichi na za hariri nzito. Na watavikwa vikuku vya fedha, na Mola wao atawanywesha kinywaji safi kabisa (Awaambie):"Hakika haya ni malipo yenu; na amali zenu zimekubaliwa". (76!
:
11
-22).

Kujiepusha na uchoyo na ubahili
Uchoyo na ubahili ni kinyume cha ukarimu. Mtu mchoyo ana kasoro katika imani yake. Anaona kuwa chochote alichonacho amekipata kwa jitihada na akili yake tu. Pia anahofu kuwa akitoa kumpa mwingine atapungukiwa au atafilisika. Mtume (s.a.w.) Ametunabahisha hilo katika hadithi zifuatazo:

Abu Hurairah amesimulia kuwa Mtume wa Allah amesema: Mtu anasema: "Hiki changu! Hiki changu! Lakini ukweli ulivyo ni kwamba, vilivyo vyake katika mali yake ni vitu vitatu: "Kile alichokula au kile alichokitoa sadaqa (hakika) amekiweka akiba, na kingine chochote zaidi ya hivi, hakika si vyake (si vyenye kumfaa) na ataondoka awaachie watu". (Muslim).

Abu Hurairah amesimulia kuwa Mtume wa Allah amesema: "Chakula cha watu wawili kina watosha watu watatu, na chakula cha watu watatu kinawatosha watu wanne". (Bukhari na Muslim).

Jabir bin Abdullah (r.a.) Ameeleza: Mtume wa Allah amesema: "Chakula cha mtu mmoja kinawatosha watu wawili na chakula cha watu wawili kinawatosha watu wawili na chakula cha watu wawili kinawatosha watu wanne na chakula cha watu wanne kinawashibisha watu wanane". (Muslim).

Hivyo ukizingatia hadithi hizi, utaona kuwa hapana sababu ya Muislamu kuwa mchoyo au bahili.

Uchoyo na ubahili ni tabia mbaya na malipo yake ni kwenda Motoni kama inavyobainishwa katika Qur'an:

Yule anayetoa (zaka, sadaka na vingnevyo) na kumcha Mwenyezi Mungu. Na kusadiki jambo jema (akalifuata). Tutamsahilishia njia ya kwenda Peponi. Na afanyae ubakhili, asiwe na haja ya viumbe wenzake. Na akakadhibisha mambo mema (asiyafanye). Tutamsahilishia njia ya kwendea Motoni. Na amali zake hayatamfaa atakapokuwa anadidimmia (Motoni humo). (92:5-11).

Kuwa Mwenye Kutosheka
Kutosheka ni kuridhika na neema uliyonayo. Kutosheka ni utajiri kuliko utajiri wote uliopo ulimwenguni.

Abu Hurairah (r.a.) Amesimulia kuwa Mtume wa Allah amesema, utajiri si kuwa na mali nyingi lakini utajiri ni kutosheka". (Bukhari na Muslim).

Muislamu anatakiwa awe ni mwenye kutosheka na kile alichoruzukiwa na Mola wake. Kila mtu amekadiriwa riziki yake na Allah (s.w.). Hakuna mwenye uwezo wa kumpunguzia au kumzidishia mtu riziki. Hili linabainishwa katika Qur'an katika usia wa Mzee Luqman kwa wanawe:

Ewe mwanangu! Kwa hakika jambo lolote lijapokuwa na uzito wa chembe ya hardali, likawa ndani ya jabali au mbinguni au katika ardhi, Mwenyezi Mungu analileta (amlipe aliyefanya); bila shaka Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa mambo yaliyofichikana, (na) Mjuzi wa mambo yaliyo dhahiri. (31:16).

Pia Allah (s.w.) Anatuhakikishia:

"Na hakuna mnyama yoyote katika ardhi ila riziki yake iko juu ya Allah..." (11:6).

Juu ya moyo wa kutosheka Mtume (s.a.w.) Anatuwaidhi katika Hadithi ifuatayo:

Imesimuliwa katika mamlaka ya Abdullah Bin Amr bin Al-'As (r.a.) Kuwa Mtume wa Allah amesema: "Yule aliyeingia Uislamu na akajaaliwa kupata riziki inayotosheleza mahitaji yake muhimu na Mwenyezi Mungu akamfanya kuwa mwenye kutosheka na kila alichotunukiwa, hakika amefuzu kikweli". (Muslim).

Kujiepusha na tamaa na kuomba-omba
Kinyumke cha kutosheka ni kuwa na tamaa au kutotosheka. Kutotosheka ni ufakiri wa moyo. Moyo wa kutotosheka huzaa tabia nyingi mbaya ikiwa ni pamoja na upupiaji
mali, uchoyo, na kuomba omba. Muislamu anatakiwa ajitahidi kutosheka na alichonacho na hata kama anahisi yuko katika dhiki ajitahidi kujizuilia kunyoosha mkono wa kuomba chochote kwa yoyote kwa kadiri iwezekanavyo.

Tumekatazwa katika Qur'an tuwe si wenye tamaa:

"Wala msitamani vile ambavyo Mwenyezi Mungu amewafadhilisha baadhi yenu kuliko wengine. Wanaume wanayo sehemu (kamili) ya vile walivyovichuma; na wanawake nao wanayo sehemu (kamili) ya vile walivyovichuma. Na mwombeni Mwenyezi Mungu fadhila zake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu". (
4:32).

Kuhusu suala la omba omba Mtume (s.a.w.) Ametuuusia katika hadithi zifuatazo:

Abu Hurairah (r.a.) Ameeleza kuwa Mtume wa Allah amesema: "Yule aombaye ili aongezee
mali yake, haombi lingine ila moto wa maisha. (Muslim).

Ibn Umar (r.a.) Ameeleza kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: "
Kama mmoja wenu ataomba bila ya sababu ya msingi atakutana na Allah na uso usiokuwa na nyama." (Bukhari na Muslim).

Ibn Umar (r.a.) Amesimulia kuwa Mtume wa Allah alipokuwa Mimbarini akitoa khutba juu ya kutoa sadaqa na kujizuia na kuomba omba alisema: "Mkono wa juu ni bora kuliko mkono wa chini. Mkono wa juu ni ule unaotoa na wa chini ni ule unaoomba". (Bukhari na Muslim).

Kuomba kunaruhisiwa kwa dharura zifuatazo:
(i) Mtu aliyesimama kumdhamini mtu mwingine ili kuleta suluhu kati ya wagomvi wawili huyu anaruhusiwa kuomba hata akiwa tajiri. Kwa mnasaba huu, wadhamini wa Misikiti, madrasa, na shughuli mbali mbali za Kiislamu wanaruhusiwa kuomba michango ya Waislamu ili kufanikisha shughuli hizo.

(ii) Mtu aliyepata ajali na kuharibikiwa kabisa vitu vyote
kama vile ajali ya moto, mafuriko, n.k.

(iii) Mtu ambaye amepigwa na ufukara na amekosa kabisa mahaitaji muhimu ya maisha
kama chakula, malazi na makazi. Lakini mtu akiwa kama na angalau chakula cha siku moja na malazi na akawa na dirham 50 mkononi mwake haruhusiwi kuomba kama tunavyofahamishwa katika hadithi zifuatazo:

Abdullah bin Mas'ud ameeleza kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: Anayeomba omba watu na ilhali ana mahitaji muhimu ya maisha atakuja siku ya Kiyama na kuomba omba kwake kama mikwaruzo, vidonda au majeraha usoni mwake. Iliulizwa: Ee Mtume wa Mwenyezi Mungu! Ni kiasi gani kinachomtosha mtu? Akajibu: Dirham 50 au thamani yake ya dhahabu. (Abu Daud, Tirmidih, Nasai na Ibn Majah).

Sahl ameeleza kuwa Mtume wa allah amesema: Yeyote yule anayeomba na ilihali anajitosheleza kwa kwa mahitaji muhimu, anaomba moto (Jahannam). Nufali ambaye ambaye ni miongoni mwa wasimulizi wa hadithi hii katika sehemu nyingine aliuliza: Ni yupi mwenye uwezo ambaye kuomba ni haram? Akijibu (Mtume (s.a.w.): Yule mwenye uwezo wa kupata chakula cha asubuhi na usiku. Mahali pengine amesema: Yule mwenye chakula cha siku moja (Usiku na mchana). (Abu Daud).

Kujiepusha na Husuda
Husuda ni miongoni mwa magonjwa makubwa ya moyo. Mtu mwenye husuda anadonda la chuki moyoni mwake, juu ya neema alizoneemeshwa mwingine na Mwenyezi Mungu (s.w.). Kwa maana nyingine anachukia utaratibu wa Mwenyezi Mungu (s.w.) aliouweka katika kugawanya neema zake kwa waja wake. Hasidi kutokana na chuki yake dhidi ya mja aliyeneemeshwa na Mwenyezi Mungu (s.w.), huwa tayari kwa hali na
mali kumdhuru mja huyo asiye na hatia yoyote. Ni kwa msingi huu Mwenyezi Mungu (s.w.) Anatufundisha kujikinga kwake na shari za viumbe vyake, akiwepo hasidi kama tunavyosoma katika Suratul-Falaq:

Sema: "Ninajikinga na Mola wa Ulimwengu wote na shari ya Alivyoviumba, na shari ya giza la usiku liingiapo na shari ya wale wanaopulizia mafundoni na shari ya hasidi anapohusudu:. (113:1-5).

Husuda husababishwa na kutotosheka na kutoridhika na neema za Mwenyezi Mungu (s.w.). Hasidi anataka kila neema aliyotunukiwa mwingine awe nayo yeye au mwingine abakie bila neema hiyo. Anataka awe juu ya mwingine na aonekane wa maana pekee katika jamii. Akihisi kuwa kuna yeyote aliyemzidi kwa cheo, utajiri, elimu, watoto, umaarufu, (n.k.) hupandwa na moto wa chuki moyoni mwake ambao humsukuma kufanya visa mbali mbali dhidi ya huyo anayemhisi kuwa amemzidi au yuko sawa naye.

Muislamu anatakiwa ajitakase na uovu huu wa husuda kwa kutosheka na kile alichonacho akijua kuwa kila neema aliyopewa mwanaadamu imekadiriwa na Mwenyezi Mungu (s.w.) Na hapana yeyote mwenye uwezo wa kupunguza neema ya mtu aliyekadiriwa na Mola wake hata kwa kiasi cha chembe ndogo iliyoje na hakuna yeyote awezaye kumuongezea mtu neema kuliko vile alivyokadiriwa na Mwenyezi Mungu (s.w.).

Pia Muislamu wa kweli anajitahidi kujiepusha na husuda ili asije akaziunguza amali zake njema alizozitanguliza na akawa miongoni mwa watakaohasirika katika maisha ya akhera.

Abu Hurairah (r.a.) Amesimulia kuwa Mtume wa Allah amesema:

"Kuweni waangalifu juu ya husuda, kwani husuda inaunguza
mali njema za mtu kama moto unavyounguza kuni. (Abu Daud).

Husuda au wivu unaoruhusiwa ni ule unaofanywa kwa ajili ya kushindana katika kufanya mema. Wivu wa namna hii sio ule wa kuchukia kuwa kwa nini fulani ameneemeshwa bali ni ule unaomfaya mja ajitahidi zaidi kufanya mema
kama anavyofanya au kumzidi mwingine. Mtume (s.a.w.) Ametufahamisha ni husuda ya namna gani inayoruhusiwa kwa Muislamu katika hadithi ifuatayo:

Ibn Mas'ud (r.a.) Amehadithia kuwa Mtume wa Mwenyezi mungu amesema: Hapana husuda (inayoruhusiwa katika Uislamu) ila kwa watu wawili: "Mtu ambaye Mwenyezi Mungu (s.w.) Amempa mali na akampa uwezo wa kuitumia katika njia ya Mwenyezi Mungu na mtu ambaye Mwenyezi Mungu amempa elimu na hekima akawa anafundisha wengine pamoja na yeye mwenye kuingiza elimu hiyo katika vitendo". (Bukhari na Muslim).

Kumtegemea Mwenyezi mungu (s.w.) na kuwa Jasiri:

Muislamu wa kweli daima humtegemea Mwenyezi Mungu kwa kila kitu. Ana yakini kuwa hapana lolote litakalomfikia, baya au zuri, ila litakuwa linatoka kwa Mwenyezi Mungu ana yakini kuwa ulinzi wa maisha yake na mahitajio yake yote ya kimaisha yako mikononi mwa Mwenyezi Mungu (s.w.). Mwenyezi Mungu (s.w.) Anatuamrisha tumtegemee Yeye tu. Hebu turejee aya zifuatazo:

Na tegemea kwa Yule aliye na uhai wa milele ambaye hatakufa. (25:58).

"... Na kwa Mwenyezi Mungu awategemee Waislamu. Na tuna nini tusimtegemee Mwenyezi Mungu, na hali ametuonyesha njia zetu. Na tutayavumilia maudhi yenu. Basi kwa Mwenyezi Mungu tu wategemee wategemeao". (
14:11-12).

"... Na anayemuogopa Mwenyezi Mungu, (Allah) humtengenezea njia ya kuokoka (na kila balaa); na humpa riziki kwa namna asiyoitazamia. Na anayemtegemea Mwenyezi Mungu yeye humtoshea. Kwa yakini Mwenyezi Mungu anatimiza kusudio lake, Hakika Mwenyezi Mungu amekwisha kiwekea kila kitu kipimo chake".(65:2-3).

Kumtegemea Mwenyezi Mungu kwa kila jambo na hasa wakati wa dhiki na kuhitajia msaada, huzidisha imani na ujasiri kwa waumini. Hebu turejee aya zifuatazo:

Wale ambao watu waliwaambia:"Watu wamekukusanyikieni. Kwa hiyo waogopeni". Lakini (maneno hayo) yakawazidishia imani wakasema: Mwenyezi Mungu anatutosha. Naye ni mlinzi bora kabisa. Basi wakarudi (vitani (na neema za Mwenyezi Mungu na fadhila (zake), hakuna ubaya uliowagusa; na wakafuata yanayomridhisha Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu ni mwenye fadhila kuu". (3:173-174).

Na Waislamu walipoyaona majeshi walisema, 'Haya ndiyo aliyotuahidi Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Mwenyezi Mungu na Mtume wake wamesema kweli, na (jambo hili) halikuwazidishia ila imani na utii. (33:22).

Hakika waumini wa kweli ni wale ambao anapotajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao hujaa hofu; na wanaposomewa aya zake huwazidishia imani na wakamtegemea Mola wao tu basi. (8:2).

Hivyo Waislamu hatuna budi kumtegemea Mwenyezi Mungu (s.w.) Kwa kila hali. Tukifanya hivyo imani yetu itazidi na tutakuwa na moyo wa ujasiri wa kutuwezesha kupambana na hali yoyote ngumu itakayotukabili kwa sababu tunayakini
kama halitufikii lolote, baya au zuri, ila liko katika makadirio ya Mwenyezi Mungu (s.w.). Ni vyema hapa tukumbushe kuwa kumtegemea Mwenyezi Mungu (s.w.) Ni kutekeleza wajibu wetu kwa juhudi na maarifa katika jambo lolote tunalolifanya, kisha matokeo ya jitihada zetu tumuachie Mwenyezi Mungu (s.w.). Hii hasa ndio maana ya kumtegemea Allah (s.w.) Tunayofundishwa katika Qur'an kama inavyodhihirika katika aya zifuatazo:

Naam, wanaoelekeza nyuso zao kwa Mwenyezi Mungu na wakawa ni watendaji mema, basi wao watapata malipo
yao kwa Mola wao, wala haitakuwa hofu juu yao wala hawatahuzunika. (2:112).

Na kwamba, mtu hatapata ila kwa yale anayoyafanya. (53:39).

Kinapokosekana kipengele hiki cha "kumtegemea Mwenyezi Mungu katika kila hali" katika tabia au mwendo wa mja, nafasi yake inajazwa na kipengele cha "woga". Woga na khofu juu ya matukio mbali mbali ya maisha ya hapa ulimwenguni husababishwa na uhaba wa imani juu ya Allah (s.w.) Na sifa zake. Mtu asiyemtegemea mwenyezi Mungu hudhania kuwa mafanikio yote ya kimaisha hupatikana na uwezo wa mwanaadam na kuwa ni mwanadamu pekee mwenye uwezo wa kujikinga na shari zote zinazomkabili. Dhana hii humtia mtu katika wasi wasi na woga atakapohisi kuwa tatizo au dhana fulani linalomkabili litamshinda nguvu kwa kuwa hana uwezo au msaada wa kibinaadam wa kumuwezesha kupambana nalo.

Muislamu wa kweli hapaswi kuwa mwoga wa chochote kwa sababu hapana chochote kinachoweza kumdhuru, ila awe amekadiria hivyo Mwenyezi Mungu (s.w.) na hapana mja awezaye kuepa ajali yake aliyoandikiwa na mwenyezi Mungu. Muislamu anatakiwa awe imara katika kusimamisha Dini ya allah katika kila kipengele cha maisha yake, bila ya kuhofu chochote kwani yeye dima yuko chini ya ulinzi na uangalizi wa Mwenyezi mungu (s.w.) Na halitamsibu ila lile alilomuadikia Mwenyezi Mungu (s.w.).

Sema: 'Halitatusibu ila alilotuandikia Mwenyezi mungu. Yeye ni Mola wetu:. Basi Waislamu wamtegemee Mwenyezi Mungu tu. (
9:51).

Kujiepusha na woga na kukata tamaa
Pia Muislamu hatakiwi kukata tamaa na rehema za Mwenyezi Mungu (s.w.). Hakuna kinachoshindikana kwa Mwenyezi Mungu Muislamu hana budi kufanya jitihada katika kufanikisha jambo muhimu la maisha kwa kufuata njia za hali anazoziridhia Mwenyezi Mungu (s.w.).
Kama jambo hilo lina kheri na Yeye, basi mwenyezi Mungu (s.w.) Atalifanikisha. Mzee Yaquub (a.s.) Akiwausia wanawe wasichoke kumtafuta Yusuf na ndugu yake alipowaambia:

"Enyi wanangu! Nendeni mkamtafute Yusuf na Nduguye, wala msikate tamaa na Rehema ya Mwenyezi Mungu. Hawakati tamaa na Rehema ya Mwenyezi Mungu isipokuwa watu makafiri". (12:87).

Pia iwapo baada ya Muislamu kufanya juhudi na kutumia uwezo wake wote, hakupata mafanikio aliyokusudia, asikate tamaa bali aridhike kuwa matokeo hayo ndiyo yenye kheri mwake kwa kuzingatia Qur'an:

".. Lakini huenda mkachukia kitu nacho ni kheri kwenu. Na huenda mkapenda kitu nacho ni shari kwenu. Na Mwenyezi mungu ndiyeanayejua, (lakini) nyinyi hamjui". (2:216).

Kuwa wenye msimamo thabiti (Istiqama)
Muumini wa kweli anayemtegemea Mwenyezi Mungu (s.w.) Kwa kila hali hana budi kuwa na msimamo thabiti katika kuusimamisha na kuufuata uislamu. Si muumini wa kweli yule anaeyumba yumba (mudhadhabina) kwa kuchanganya haki na batili au utiii na uasi katika kuendesha maisha yake ya kila siku. Mwenyezi Mungu (s.w.) Ametuamrisha wale tutoao shahada ya kweli tuingie Uislamu wote au tuwe Waislamu katika kila kipengele na kila hatua yetu ya maisha na wala tusiingie nusu nusu. Anatuamrisha:

Enyi mlioamini! Ingieni katika Uislamu wote, wala msifuate nyayo za shetani, kwa hakika yeye kwenu ni adui dhahiri. (2:208).

Hivyo, kutamka tu shahada au kusema: "Tunakiri kuwa hapana Mola ila Mwenyezi mungu na Muhammad (s.a.w.) Ni Mtume wake" haitoshi kutufanya kuwa Waislamu wale walioahidiwa malipo makubwa huko akhera; bali tutakuwa wa kweli katika shahada zetu iwapo tutaendesha maisha yetu yote kama alivyotutaka tuishi Mwenyezi Mungu (s.w.) na kama alivyotuelekeza Mtume wake (s.a.w.).Waislamu watakaokuwa imara katika kuutekeleza Uislamu katika maisha yao ya kila siku, ndio walioahidiwa malipo makubwa ya Peponi katika maisha ya Akhera.

Hebu turejee aya chache zifuatazo:

Wale waliosema: Mola wetu ni Mwenyezi Mungu kisha wakabakia imara (wakawa na msimamo), hao huwateremkia malaika (wakawaambia), "Msiogope wala msihuzunike, na furahini kwa pepo mliyokuwa mkiahidiwa. Sisi ni vipenzi vyenu katika maisha ya dunia na katika akhera, na humo mtapata vitu vinavyopendwa na nafsi zenu, na humo mtapata mtakavyovitaka". (41:30 -31).

Hakika wale watasema: 'Mola wetu ni Mwenyezi Mungu'. Kisha wakatengenea (wakawa na msimamo) hawatakuwa na khofu (siku ya kufa kwao wala baadaye) wala hawatahuzunika. Hao ndio watu wa Peponi, watakaa humo (milele); na malipo ya yale waliyokuwa wakiyatenda:. (46:13-14).

Hebu pia tuone jinsi Mtume (s.a.w.) anavyotuwaidhi juu ya kuwa na msimamo katika uislamu wetu:

Sufyaan bin Abdullah (r.a.) Amesimulia kuwa alisema: Ee! Mtume wa Allah niambie neno juu ya Uislamu ambalo sitakuwa tena na haja ya kumuuliza mtu mwingine baada ya hapa. Alisema Mtume; 'Sema:Ninamuamini Mwenyezi Mungu kisha ubakie katika msimamo huo". (Muslim).

Abu Hurairah (r.a.) amesimulia kuwa Mtume wa Mwenyezi mungu amesema: Fuata barabara njia sahihi ya imani na kuwa na msimamo huo, na ujue kwamba hapana yeyote atakayeokoka kutokana na amali yake (nzuri). Mmoja akauliza: Hata wewe Mtume wa Allah? Akajibu (Mtume) Hata mimi, ila mpaka Allah anikunjulie rehema Zake na fadhila Zake. (Muslim).