Faida Za Kusoma Siyrah

 

Muhammad Faraj Salem Al Saiy

 

 

Maisha ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) ni somo adhimu sana baada ya somo la Qur-aan tukufu, na hii ni kwa sababu ndani yake tunapata faida nyingi sana, zikiwemo zifuatazo:-

 

1.     Kujuwa sababu za kuteremshwa kwa aayah mbali mbali za Qur-aan jambo litakalotuwezesha kukifahamu vizuri kitabu cha Mwenyezi Mungu pamoja na kuzifahamu hukmu zake na Hadiyth zake, na kuifahamu vizuri Sunnah iliyotakasika ya Mtume wa Mwenyezi Mungu Muhammad (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam).

 

2.     Kufahamu namna gani Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) alivyoshirikiana na Swahaabah zake watukufu (Radhiya Allaahu anhum) walivyoipigania diyn ya Mwenyezi Mungu kwa hali na mali na kuieneza kila pembe ya dunia, na pia mafundisho ya hikmah, pamoja na maarifa mbali mbali aliyowafundisha Maswahaabah wake kwa ajili ya majukumu hata wakaweza kusubiri na kustahamili mashaka na tabu mbali mbali mpaka pale Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Alipowapa yale Aliyowaahidi kwa kuitiisha dunia yote ikawa chini ya amri yao.

 

3.     Maisha ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) ni muujiza katika miujiza ya Mwenyezi Mungu, kwani katika kuidurusu Siyrah yake, tutaona namna gani alivyozaliwa na kulelewa katika mazingara ya kiajabu na ya kimiujiza na pia namna alivyoelimishwa na kulindwa na Mola wake (Subhaanahu wa Taala).

 

4.     Tunapata kuwajuwa zaidi watu wa nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) na namna gani walivyoshirikiana na Maswahaabah wake watukufu (Radhiya Allaahu anhum), tokea siku za mwanzo, wakahuzunika na kufurahi pamoja, na wakati huo huo msomaji wa Siyrah anafurahi kwa furaha zao na anahuzunika kwa huzuni zao.

 

5.     Katika somo hili, tunaweza kujuwa namna gani Maswahaabah walivyojifunza katika Madrasah ya Mtume wao mtukufu (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam), akawalea vizuri na kuwafanya wawe Ummah bora kuliko Ummah zote zilizowahi kuteremshiwa watu. Kwani wao ndio walioisimamia diyn hii na kupiga mifano mema katika kujitolea nafsi zao mhanga kwa ajili ya kuutetea Uislamu, kupigana jihadi na kuwalingania watu katika njia ya Mwenyezi Mungu, kuonyesha ushujaa, ustahamilivu na uadilifu mbele ya adui, pamoja na mapenzi na huruma na ukarimu na kila sifa njema mbele ya wenzao.

 

6.     Katika kuyadurusu maisha ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) tutaweza pia kuona na kuonja ladha ya jihadi na namna gani Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na Swahaabah zake watukufu (Radhiya Allaahu anhum) walivyosimama kidete katika kuipigania diyn hii tukufu na namna walivyoweza kusubiri mbele ya adui na kuvumilia mateso na shida mbali mbali.

 

7.     Tutaweza pia kuujuwa ucha Mungu wao na namna gani Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) Alivyoweza kuzibadilisha na kuzijenga nyoyo na nafsi zao kwanza, kabla ya kuziendea nyoyo na nafsi nyingine, na hii ni tafisiri ya kauli ya Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) isemayo:

 

 

{{Hakika Mwenyezi Mungu habadili yaliyoko kwa watu mpaka wabadili wao yaliyomo katika nafsi zao.}} [Ar-Raad: 11]