HUKMU ZA KUWEKA SUTRA MBELE YA ANAYESALI

 

 

Neno 'Sutra' maana yake ni hifadhi, kinga, himaya, sitara, ulinzi nakadhalika Na maana yake ni kuweka kitu mbele yako unapokuwa unasali ili kitu hicho kiwe kama ni sitara baina yako na baina ya anayetaka kupita mbele yako.

 

Hukmu yake

Ni vizuri kwa anayesali kujiwekea 'Sutra' (sitara) mbele yake kwa ajili ya kuzuwia mtu asipite mbele yake na ili asiwe akianglia huku na kule wakati wa kusali.

Imepokelewa kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallahu Llahu alayhi wa Sallam) amesema:

"Mmoja wenu anaposali ajiwekee Sutra na awe karibu nayo."

Abu Daud na Ibni Majah.

Imepokelewa pia kuwa Masahaba (Radhiyallahu 'anhum) walikuwa wakijiwekea mikuki mbele yao wanaposali wakiwa safarini, na waliofuatailia baada ya Masahaba pia walikuwa wakifanya hivyo.

Maulamaa wanasema kuwa ni vizuri kujiwekea Sutra ikiwa unahofia mtu asipite mbele yako, ama ukiwa huhofii basi si lazima, na hii inatokana na hadithi iliyosimuliwa na Imam Ahmad na Abu Daud na Al Baihaqiy kuwa Ibni Abbas (Radhiyallahu 'anhu) alisali mahali penye uwazi na hakuweka mbele yake kitu chochote.

 

Vipi inapatikana Sutra?

Imepokelewa kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallahu Llahu alayhi wa Sallam) amesema:

"Anaposali mmoja wenu basi ajiwekee Sutra mbele yake hata kama ni mkuki."

Ahmad na Al Hakim

Na katika hadithi nyingine:

"Ikiwa hajapata mkuki basi hata fimbo."

Na akasema:

"Anaposali mmoja wenu ajiwekee kitu mbele yake, na asipopata kitu basi hata fimbo, na kama hana fimbo basi achore msitari na hatodhurika na yeyote atakayepita mbele yake."

Ahmad na Abu Daud na wengine

Imepokelewa pia kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallahu Llahu alayhi wa Sallam) amewahi kusali akiielekea nguzo (kama ni Sutra), na amesali kukielekea kitanda huku Bibi Aisha (Radhiyallahu 'anhaa) akiwa amelala juu yake, na amesali kuulekea mti nakadhalika.

 

Sutra ya Imam ni Sutra ya maamuma

Sutra ya Imamu ni Sutra ya maamuma wote walio nyuma yake.

Kutoka kwa Amru bin Shuaib, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa babu yake amesema:

"Tulikuwa safarini pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallahu Llahu alayhi wa Sallam) katika njia iliyonyanyuka karibu na Makkah, na ulipowadia wakati wa Sala akatusalisha akiwa ameuelekea ukuta na kuufanya kuwa kibla na sisi tukiwa nyuma yake. Kondoo akataka kupita mbele yake, na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallahu Llahu alayhi wa Sallam) akawa anamzuwia asipite mpaka akamlazimisha apite nyuma yake."

Imam Ahmad na Abu Daud.

Na kutoka kwa Ibni Abbas (Radhiyallahu 'anhu) amesema:

"Nilikuwa nimepanda punda na wakati huo nilikuwa nishabaleghe na Mtume (Swallahu Llahu alayhi wa Sallam) alikuwa akisalisha watu Mina, nikapita mbele ya baadhi ya safu za watu wanaosali nyuma yake,  nikampumzisha punda na kuingia ndani ya safu na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallahu Llahu alayhi wa Sallam) hakunikataza."

Imepokelewa na maimam wote

Na hizi ni dalili kuwa haijuzu kupita mbele ya imamu, lakini inajuzu kupita mbele ya safu za maamuma kwa sababu Sutra ya imamu ni Sutra ya maamuma.

 

Haramu kupita mbele ya anayesali

Anasema Abu Juhaym kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallahu Llahu alayhi wa Sallam) amesema:

"Lau kama angejuwa malipo yake (dhambi zake) mwenye kupita mbele ya anayesali, basi angehiari kungoja arubaini kuliko kupita mbele yake."

Hakutaja kama hizo 40 ni siku  au miezi au miaka.

Imepokelewa na maimamu wote.

 

Wakiisherehesha hadithi hii, maulamaa waanasema:

"Hii kama anasali akiwa ameweka mbele yake Sutra. Ikiwa hajaweka Sutra basi si haramu kupita mbele yake. Na ikiwa amejiwekea Sutra, basi anayo haki ya kumsukuma na kumzuwia yeyote asipite mbele yake awe ni mwanadamu au mnyama."

Imepokelewa kuwa siku moja Abu Said al Khodari (Radhiyallahu 'anhu) alikuwa akisali na mtu mmoja alijaribu kupita mbele yake, na Abu Said (Radhiyallahu 'anhu) akamzuwia na alipojaribu kupita kwa nguvu akamsukuma.

Alipoulizwa kwa nini alifanya hivyo akasema:

"Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallahu Llahu alayhi wa Sallam) akisema:

"Mmoja wenu akisali na mbele yake amejiwekea Sutra kujisitiri na watu, basi mtu yeyote akitaka kupita baina yake na baina ya Sutra hiyo amzuwie na akikataa apigane naye kwani huyo ni shetani."

Bukhari na Muslim