Uadilifu wa Masahaba na Utatanishi wa hadithi ya Hodhi

Yamekusanywa na kutafsiriwa na Muhammad Faraj Salem Al Saiy

Yaliyomo

Utangulizi 1

Hadithi ya hodhi 2

Daraja yao. 3

Sifa zao ndani ya Qurani 4

Sifa zao ndani ya Sunnah. 5

Katika kauli za maulamaa. 6

Wanafiki 9

Wenye shaka na imani dhaifu. 10

Nani atakayeondolewa?. 11

Alikuwa akiwajuwa. 15

Hitimisho. 18

 

Utangulizi

Zipo baadhi ya hadithi zenye utatanishi au zenye kubeba maana zaidi ya moja, ambazo wakristo katika tovuti zao huzitumia kwa kuzifasiri hadithi hizo kwa maslahi yao, au kwa maana wanayoitaka wao, kinyume na maana yake ya kweli, kwa ajili ya kuupiga vita Uislamu.

 

Kinachoskitisha zaidi ni kuwa wapo baadhi ya Waislamu ambao kwa kutaka maslahi yao, bila kujali athari wanayoiacha, utawakuta wakipoteza wakati wao mkubwa wakifanya utafiti na kunukuu hadithi za aina hizo huku wakitaja baadhi ya makosa ya kibinadamu yaliyowahi kutendwa na baadhi ya Masahaba (Radhiya Llahu anhum), kisha wanayakuza makosa hayo na kuyafanya kuwa ni dalili ya ubaya wa Masahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam).

 

Yareti kama wakati wao wangeliupoteza katika kufanya utafiti juu ya maadui wa Mwenyezi Mungu kama vile Abu Jahal au mnafiki Abdullahi bin Saluul au Firauni au Haaman au Abu Lu'ulua al Majusiy, aliyemuuwa Khalifa wa pili wa Waislamu Umar bin Khattab (Radhiya Llahu anhu). Bali kinyume na hivyo, utawaona wanaunyamazia uadui wao watu hao, juu ya kuwa ukafiri wao umethibiti ndani ya Qurani tukufu na ndani ya mafundisho ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam), na badala yake wanaziunguza juhudi zao katika kujaribu kuwapaka matope Masahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam).

 

Kwa kufanya hivyo wanawapa makafiri silaha kali pamoja na ushahidi wanaoutaka katika kuupiga vita Uislamu na kuwapiga vita waliotuletea dini hii, kwa sababu kwa kuwatuhumu Masahaba bila ya uhakika wala ushahidi ulio wazi, ni kuutuhumu Uislamu waliotuletea Masahaba hao (Radhiya Llahu anhum) baada ya kuupokea kutoka kwa sahibu yao Mtume wa Mwenyezi Mungu, Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam).

Hadithi ya hodhi

Miongoni mwa hadithi wanayoitumia katika ubabaishaji wao huo ni ile hadithi maarufu ya Hodhi, na namna Malaika watakavyowarudisha watu watakaotaka kunywa ndani ya hodhi hilo la Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam), wakidai kuwa hadithi hiyo inawakusudia Masahaba hawa (Radhiya Llahu anhum) sahibu zake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) na marafiki zake na wenzake alioanza nao tokea siku ile ya mwanzo ya kuwalingania watu katika dini hii tukufu.

Imepokelewa katika hadithi hiyo kuwa Siku ya Kiama, wakati Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) atakapokuwa anawanywisha watu maji kutoka katika hodhi lake, watakuja Malaika na kuwaondoa makundi kati yao, na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) atakaposema:

"Hawa ni katika Masahaba wangu."

Malaika watajibu:

"Je Unajuwa waliyoyazuwa baada yako?

 

Na katika riwaya nyingine, Malaika watasema:

"Walirtaddi hawa wakarudi nyuma."

 

Anasema Ibni Abdul Barr: "Maana hasa ya hadithi hizi ni kuwa kila mwenye kuzusha mambo katika dini, atakuwa miongoni mwa watakaofukuzwa penye hodhi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam)."

 

Tukiendelea na kuichambuwa Shubha hii inayowakanganya baadhi ya watu wakadhani kuwa watakao ondolewa penye hodhi ni hawa Masahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) waliosimama naye tokea siku za mwanzo kisha wakaendelea kusimama naye katika shida zake zote na vita vyote dhidi ya makafiri; vita vya Badar, vita vya Bani Qaynuqaa, vita vya Uhud, vita Khandaq, Fathi Makka, Hunayn na vita mbali mbali. Hawa ambao baada ya kufariki kwa sahibu yao Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) waliendelea kuisimamia dini hii kidete na kuipigania kwa hali zao na mali zao mpaka ikaenea ulimwengu mzima.

Daraja yao

Daraja ya Masahaba na heshima yao katika dini ni jambo lisilokubali kujadiliwa na Muislamu yeyote mkweli mwenye kupenda haki, kwa sababu hawa ndio ambao Mwenyezi Mungu aliwahusisha kwa kuwafanya kuwa sahibu zake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam), wakamsadiki na kumfuata na kumnusuru na wakaifuata nuru aliyokuja nayo, na wakafanya kila juhudi kwa kujitolea roho zao na mali zao kwa ajili ya kuipigania dini hii tukufu mpaka ilipokamilika.

Hawa ndio wale waliosifiwa na Mwenyezi Mungu walipoambiwa kuwa wao ni umma bora kupita zote zilizoletwa kwa ajili ya watu. Na Mwenyezi Mungu Akaridhika nao.

 

Masahaba ni waaminifu wa umma huu walioibeba sheria na kuieneza ulimwenguni kote mpaka ikatufikia sisi hivi sasa. Hii Qur'ani tuliyo nayo na haya mafundisho ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) yametufikia kupitia kwao (Radhiya Llahu anhum).

 

Kwa hivyo kitendo cha kuwatilia shaka Masahaba hawa watukufu katika uadilifu wao ni katika kuipiga vita dini na kuwafanya watu wasiamini masdari za dini tulizopokea kutoka kwa Masahaba hao watukufu (Radhiya Llahu anhum). Kwa sababu Qurani tukufu na Mafundisho ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam), yote tumeyapata kupitia kwao.

Ndiyo maana maulamaa wa Kiislamu wanatutaka tuwe na msimamo imara dhidi ya kila mwenye kuwatuhumu Masahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam).

 

Inasikitisha kuona kuwa wapo miongoni mwa Waislamu wenye kuwatuhumu baadhi ya Masahaba, na wanafanya hivyo makusudi kwa ajili ya kukifikia kile wanachokitaka tu, na wakazitumia hizi hadithi za hodhi katika kujaribu kuwapaka matope Masahaba hawa watukufu (Radhiya Llahu anhum).

Katika kujaribu kuharibu sifa za Masahaba (Radhiya Llahu anhum), wakazitumia hadithi mfano wa hii inayosema:

"Wakati mimi nimesimama, litakuja kundi, nitakapowajuwa, atatoka mtu kutoka kwangu na kusema: 'Twendeni', Nitasema: 'Wapi?' Atasema: 'Motoni wallahi.' Nitasema: 'Wana makosa gani?' Atasema: 'Hawa wamertaddi na kurudi nyuma baada yako.."

Bukhari na wengine

Sifa zao ndani ya Qurani

Maulamaa wanasema:

Wa kwanza kutoa hukmu Yake kuwa Masahaba (Radhiya Llahu anhum), ni watu waadilifu ni Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala na Mtume wake (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kama ilivyoandikwa ndani ya Qurani tukufu na kama ilivyokuja kwa njia Mutawaatirah katika Sunnah ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam), na miongoni mwa hukmu hizo ni kauli Yake Subhanahu wa Taala Aliposema:

 

Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na walio pamoja naye wana nguvu mbele ya makafiri, na wanahurumiana wao kwa wao. Utawaona wakiinama na kusujudu wakitafuta fadhila na radhi za Mwenyezi Mungu. Alama zao zi katika nyuso zao, kwa athari ya kusujudu. Huu ndio mfano wao katika Taurati. Na mfano wao katika Injili ni kama mmea ulio toa chipukizi lake, kisha ukalitia nguvu, ukawa mnene, ukasimama sawa juu ya ubuwa wake, ukawafurahisha wakulima, ili kuwakasirisha kwa ajili yao makafiri. Mwenyezi Mungu amewaahidi walio amini na wakatenda mema katika wao msamaha na ujira mkubwa.

Al Fat'h 29

Na Akasema:

Na wale walio tangulia, wa kwanza, katika Wahajiri na Ansari, na walio wafuata kwa wema, Mwenyezi Mungu ameridhika nao, na wao wameridhika naye; na amewaandalia Bustani zipitazo mito kati yake, wadumu humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa.

At Tawba 100

Na Akasema:

Lakini Mtume na wale walio amini pamoja naye walipigania Jihadi kwa mali zao na nafsi zao. Hao ndio watakao pata kheri nyingi, na hao ndio wenye kufanikiwa.

At Tawba 88

 

Na Akasema:

Kwa hakika Mwenyezi Mungu amewapa radhi Waumini walipo fungamana nawe chini ya mti, na alijua yaliyomo nyoyoni mwao. Basi akateremsha utulivu juu yao, na akawalipa kwa Ushindi wa karibu.

Al Fat'h 18

 

 

Sifa zao ndani ya Sunnah

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:

"Kheri ya watu ni wa karne yangu kisha wanaowafuata kisha wanaowafuata."

Bukhari na Muslim

 

Na kauli yake (Swalla Llahu alayhi wa sallam) aliposema:

"Msiwatukane Sahaba wangu. Ninaapa kwa Yule ambaye nafsi yangu imo mikononi mwake, hata mmoja wenu atajitolea katika njia ya MwenyeziMungu kugawa dhahabu ukubwa wake mfano wa jabali Uhud, basi hatofikia gao lao wala hata nusu ya gao lao".

Bukhari na Muslim

 

Na akasema:

"Allah Allah! (nakuusieni) juu ya Sahaba wangu. Msiwageuze kuwa malengo yenu baada ya kuondoka kwangu. Kwani mwenye kuwapenda basi kwa kunipenda mimi (ndiyo) amewapenda, na mwenye kuwachukia basi kwa kunichukia mimi (ndiyo) amewachukia. Na mwenye kuwaudhi ameniudhi (na) mimi, na mwenye kuniudhi mimi amemuudhi Allah, na mwenye kumuudhi Allah, anakaribia Kumnyakuwa."

Attirmidhy

 

Zipo hadithi nyingi za namna hii zenye kuwasifia na kueleza juu ya fadhila zao mbali mbali na mitihani waliyopambana nayo, na kututaka wafuasi wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kuwaheshimu na kuwakirimu na kutowaudhi wala kuwageuza kuwa ni malengo yetu tunayoyatumia kila tunapotaka kuipitisha batil yetu. Na nasaha zote hizi zinatoka kwa Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala na kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam).

Katika kauli za maulamaa

Amesema Imam Ibni Najjar:

"Aliyesifiwa namna hii na Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala, itakuwaje tena asiwe muadilifu. Ikiwa mbele ya mahakama wanatosha mashahidi wawili tu kuthibitisha uadilifu wa mtu, itakuwaje basi ikiwa ushahidi unatoka kwa Muumba wa mbingu na ardhi Subhanahu wa Taala."

Shar'hi ya Kawkab Al Muniyr (2/475)

 

Anasema Al Khatwiyb Al Baghdaadiy

"Usafi wa Masahaba (Radhiya Llahu anhum) na uadilifu wao hauna lazma ya kusifiwa na wanadamu baada ya kusifiwa na Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala Aliyeangalia ndani ya nafsi zao akatujulisha juu ya ukweli wao.

Na hata kama Mwenyezi Mungu asingetujulisha juu ya sifa zao na kuridhika Kwake nao, basi kule kupigana kwao Jihaad kwa mali zao na nafsi zao, wamewaua baba zao na watoto wao waliopigana upande wa makafiri, haya yanatokana na yakini waliyokuwa nayo ndani ya nyoyo zao juu ya nusra ya Mwenyezi Mungu iliyowajia."

Al Kifayah fiy Ilm Annhihaayah 48-49

 

Kwa hivyo kuzichukulia zile hadithi za hodhi kuwa waliokusudiwa ni hawa Masahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) waliomsadiki na kumuamini, wakamsaidia na kumnusuru, kunakuwa ni kuzikataa aya zote na riwaya zote zilizo sahihi zenye kutubainishia fadhila zao na heshima yao mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya Mtume wake (Swallah Llahu alayhi wa sallam).

Kuwatuhumu Masahaba (Radhiya Llahu anhum) ni mfano wa kuukataa ushahidi wa Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala, kwa sababu itakuwaje Mwenyezi Mungu atujulishe juu ya watu Alioridhika nao na kutujulisha juu ya fadhila zao na kwamba atawaingiza katika Pepo Yake, kisha asijuwe kuwa watu hao siku moja watakuja kurtaddi na kubadilisha na kuzuwa nk.

Na huko pia ni kuzikanusha kauli za Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) aliyetujulisha juu ya kuridhika na Sahibu zake na kuwabashiria Pepo aliposema:

"Abubakar (yumo) Peponi, na Umar (yumo) Peponi na Uthmaan (yumo) Peponi na Aliy (yumo) Peponi na Twalha (yumo) Peponi na Az Zubeir (yumo) Peponi na Abdul Rahman bin Auf (yumo) Peponi na Saad (yumo) Peponi na Saeed (yumo) Peponi na Abu Ubaydah (yumo) Peponi"

Muslim na Attirmidhiy na Imam Ahmad na wengine

 

Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alifariki dunia akiwa ameridhika nao.

Na akasema (Swalla Llahu alayhi wa sallam):

"Haingii Motoni aliyeshiriki katika vita vya Badar."

Imam Ahmed na Attabarani na wengine

 

Hivyo kweli inawezekana maneno ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) yapingane yenyewe kwa yenyewe? Leo amuambie kuwa wewe utaingia Peponi, na kesho amkute katika watakaorudishwa mbele ya hodhi?

Huku ni kukanusha wazi wazi maneno ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam). Tutakwenda wapi na ile riwaya ya Attabarani kutoka kwa Abu Dar'daa (Radhiya Llahu anhu) kuwa alimuwambia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam):

"Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, muombe Allah anijaalie nisiwe katika hao"

Akasema: "Wewe si katika hao."

 

Inawezekana kweli Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) asijuwe hali ya Masahaba wengine akaweza kujuwa hali ya Abu Dar'daa alipomjulisha kuwa hatokuwa miongoni mwa watakao ondolewa penye hodhi?

Wanafiki

Waliowahi kuonana na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) hawakuwa watu wa aina moja. Wapo miongoni mwao waliokuwa wanafiki waliokuwa wakijidhihirisha kinyume na walivyo, juu ya kuwa walikuwa wakishiriki vitani.

Mwenyezi Mungu Anasema:

{: 1}.

Wanapo kujia wanaafiki husema: Tunashuhudia ya kuwa wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anajua kuwa wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu anashuhudia ya kuwa hakika wanaafiki ni waongo.

Al Muafiqun - 1

 

Na wanapokuwa vitani huwa wakisema:

{: 8}.

Wanasema: Tukirejea Madina mwenye utukufu zaidi bila ya shaka atamfukuza aliye mnyonge. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye utukufu - Yeye, na Mtume wake, na Waumini. Lakini wanaafiki hawajui.

Al Munafiqun - 8

 

Wenye shaka na imani dhaifu

Walikuwepo pia waliokuwa wakitia shaka, na pia walikuwepo wenye imani dhaifu miongoni mwa mabedui ambao wengi wao walirtaddi baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kufariki dunia.

Mwenyezi Mungu Anasema:

-

Na katika mabedui walio jirani zenu wamo wanaafiki; na katika wenyeji wa Madina pia wapo walio bobea katika unaafiki. Wewe huwajui. Sisi tunawajua. Tutawaadhibu mara mbili, kisha watarudishwa kwenye adhabu kubwa.

At Tawbah 102

 

Hadithi zimeeleza wazi wazi wasfu na sababu za watu watako ondolewa penye hodhi, na wasfu huo haukubaliani na wasfu wa Mashaba (Radhiya Llahu anhum) waliolelewa na kufundishwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam), na mpaka alipofariki dunia alikuwa radhi nao.

Na hii ni dalili kuwa Masahaba (Radhiya Llahu anhum) hawana uhusiano wowote na hadithi hizi, kwani hapana Sahaba hata mmoja aliyertaddi wala aliyezusha.

Umar na Uthmaan (Radhiya Llahu anhum) wanaowatuhumiwa kuwa walizusha, wao walichofanya ni kuhuisha Sunnah ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam), na wala hawajazusha jambo jipya katika dini. na hao tulisema kwamba tumeamrishwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kufuata mwenendo wao.

Anasema Imam Al Khutaaby:

"Hapana hata Sahaba mmoja aliyertaddi, bali waliortaddi ni makabila ya kibedui wasiowahi kuipigania dini, na kwa ajili hiyo haipasi kuwatuhumu Masahaba wale maarufu."

Fathu l Baari 00/385

 

Anasema Imam Al Baghdadiy:

"Wamekubaliana maulamaa wote wa Kisunni 'Ij'maa' kuwa waliortaddi baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kufariki dunia walikuwa ni watu wa kabila la Bani Kindah na Hanifa na Fizaarah na Bani Asad na Bani Bakar bin Wail. Hawa hawakuwa miongoni mwa watu wa Madina wala watu wa Makka kabla ya kutekwa mji wa Makka. Na kisheria wanaoitwa Muhajirin ni wale tu waliohajir kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kabla ya Fat'hi Makka."

Al Farqu baynal Firaq

Nani atakayeondolewa?

Wamekhitalifiana maulamaa juu ya nani atakaye ondolewa penye hodhi la Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) baada ya wote kukubaliana kuwa waliokusudiwa si Masahaba hawa tunaowajuwa sisi.

Amesema Imam An Nawawiy (Mwenyezi Mungu Amrehemu) katika sharhi yake ya Muslim 3/136 -137 katika kuisherehesha hadithi hii ambayo ndani yake imo kauli ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) aliposema: "Unajuwa namna waliyozusha baada yako?" 'Waliokusudiwa ni wanafiki waliortaddi na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) atakapowaita ataambiwa: "Hawa siwo uliahidiwa, kwani hawa walibadilisha."

Na rai nyingine inasema kuwa watu hao ni wale waliokuwa Waislamu wakati wa Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam), kisha wakartaddi baada ya kufariki kwake. Na atakapowaita, ataambiwa kuwa walirtaddi baada yake.

 

Rai ya tatu ni kuwa; hawa ni watu waliotenda maasi makubwa na Bida'h wakafariki kabla ya kutubu, juu ya kuwa walikuwa Waislamu.

Kauli kama hizi pia alizitaja Al Qurtuby katika Al Muf'him 1/503

 

Ikajulikana kuwa Masahaba (Radhiya Llahu anhum) hawamo katika wasfu huu. Na kama mtu atarudi kusoma wasfu wa nani Sahaba uliotajwa na maulamaa mbali mbali atauona uhakika wa hayo.

Maulamaa wanasema kuwa Sahaba ni: "Mtu aliyemuona Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akiwa Muislamu na akafariki dunia akiwa katika hali hiyo."

 

Wasfu huu unawatowa wanafik na waliortaddi, kwani wao si Masahaba aslan. Watakuwaje Masahaba wakati Masahaba ni maadui wa waliortaddi na maadui wa wanafik. Waliwapiga vita mpaka Mwenyezi Mungu Alipowapa ushindi juu yao. Na haya yalitokea baada ya kufariki dunia kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam), wakati waliportaddi makabila mengi ya kiarabu.

Na pia kuhusu kitendo cha Bida'h, ambayo ni sababu mojawapo ya kuondoshwa hodhini. Masahaba (Radhiya Llahu anhum) walikuwa msitari wa mbele kupiga vita kila aina ya Bida'h, bali matendo ya Bida'h hayajaenea isipokuwa baada ya kumalizika zama zao Masahaba hawa (Radhiya Llahu anhum), na dalili ya maneno haya ni kauli ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) aliposema:

"Nyota ndizo zinazolinda mbingu, zitakapo ondoka, mbingu zitajiwa na kile kilicho ahidiwa, na mimi ni mlinzi wa Sahibu zangu, nitakapo ondoka watakuja Sahibu zangu. Na Sahibu zangu ni walinzi wa umma wangu, watakapoondoka, umati wangu utajiwa na kile walicho ahidiwa."

Muslim, Imam Ahmad, Attirmidhiy na wengine.

 

Anasema Imam An Nawawiy:

(Na Sahibu zangu ni walinzi wa umma wangu, watakapoondoka, umati wangu watajiwa na kile walicho ahidiwa.) "Maana yake ni kuwa baada ya kuondoka Masahaba watakuja wazushi na fitan ."

 

Misimamo imara kama hii ya Masahaba (Radhiya Llahu anhum), ambao baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kufariki dunia, walipopambana na maadui, na wakati huo huo walipambana na waliortaddi, na wakati huo huo walifungua nchi nyingi na nyoyo nyingi, yote haya ni dalili kuwa wao ndio hasa wanaostahiki kunywa maji ndani ya hodhi.

Inawezekana pia kuwa watako ondolewa penye hodhi ni watu wenye wasfu ule wa kurtaddi, kwa sababu katika hadithi Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema:

"Nitaambiwa kuwa hawa walirtaddi baada yako."

 

Ikiwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema kuwa sababu ya kuondoshwa penye hodhi ni kwa kurtaddi na kufanya matendo ya Bida'h, kwa hivyo bila shaka yoyote watakao ondoshwa hapo ni wale waliortaddi na waliozusha, na hapana hata mmoja kati ya Masahaba hawa aliyenukuliwa kuwa alirtaddi.

 

Anasema Imam Ibni Abdul Bir:

"Yeyote atakayezusha (atakayeingiza Bida'h yake) katika dini, atakuwa miongoni mwa watakao ondoshwa penye hodhi."

 

Amesema Al Qurtuby katika At Tadhkirah 1/348:

"Maulamaa wetu wote wamesema kuwa; kila aliyertaddi katika dini au aliyezusha Bida'h yake, kile asichokitolea amri Yake Mwenyezi Mungu, huyo atakuwa miongoni mwa watakaofukuzwa penye hodhi."

 

Alikuwa akiwajuwa

Kule kusema kuwa alikuwa akiwajuwa, si lazima kumaanishe kuwa aliwahi kuwaona, bali aliwajuwa kwa alama maalum kama ilivyokuja katika Sahih Muslim kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alisema:

"Watarudishwa katika umati wangu ninaowajuwa kama mtu anavyowajuwa ngamia wake." Wakamuuliza: "Utatujuwa?" Akasema: "Ndiyo, mtakuwa na alama hawana alama hizo wengine isipokuwa nyinyi. Mtarudishwa kutoka kwangu mkiwa weupe hamna madowa kwa athari ya udhu, na wengine miongoni mwenu watazuiliwa hawatoweza kunifikia. Nitasema: "Ewe Mola wangu! Hawa ni sahibu zangu." Atanijibu Malaika: "Unajuwa waliyozuwa baada yako?"

 

Kwa hivyo pale Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) aliposema: "miongoni mwenu", alikusudia 'miongoni mwa umati wake', na maana yake ni kuwa; watafufuliwa umati wake wote kwa alama za udhu, na maana yake ni kuwa watafufuliwa pamoja na Waislamu wenzao, na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) atawajuwa kutokana na athari yao ya udhu.

 

Nne: Riwaya hizi zimepokelewa kutoka vitabu sahih kutoka kwa hao Masahaba (Radhiya Llahu anhum), akiwemo Umar na Abu Hurayrah na Aisha na Ummu Salamah na Hudhayfah na Abu Saeed Al Khodhary na Ibni Masaud na Anas na Sahal bin Saad na Ibni Abbas na Mu'awiyah na wengine (Radhiya Llahu anhum).

Sasa ikiwa hawa ndio waliokusudiwa kuwa ndio watakaofukuzwa penye hodhi, inaingia akili kweli waje kutuhadithia na kutuhakikishia kuwa maneno haya wameyasikia kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam), juu ya kuwa ndani ya hadithi hizi wanatuhumiwa kuwa watakuja kurtaddi na kubadilisha na kuingiza Bida'h?

 

Tano: Wangelikuwa waliokusudiwa katika hadithi hizi ni Masahaba ambao Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alikuwa akiwahutubia na kuwahadithia juu ya matukio haya, asingelikuwa na haja ya kusema: "Watarudishwa makundi ya watu kutoka kwangu." Au "Watu miongoni mwa Sahibu zangu watarudishwa penye hodhi." Au akasema: "Kisha atachukuliwa mmojawapo miongoni mwa sahibu zangu." Badala yake angeliwaambia moja kwa moja bila kuwaficha, akawaambia kwa mfano: "Mtaondolewa penye hodhi, na kupelekwa mbali nami." Au "Fulani na fulani mtaondolewa penye hodhi." Na maneno yenye mfano huo, hii ikiwa ni dalili nyingine kuwa Masahaba sio hawa waliokusudiwa katika riwaya hizi.

 

Sita: Lafdhi zilizokuja katika riwaya hizi kama vile 'Rahat' na maana yake ni kikundi cha watu wasiotimia kumi nk. Ni dalili kuwa watakao ondolewa ni wachache sana.

 

Saba: Wengine wakatowa hata majina ya baadhi ya Masahaba watakaotolewa penye hodhi. Na sisi tunawauliza; Wametowa wapi kauli za kuwahusisha baadhi ya Masahaba kuwa wao ndio watakao ondolewa penye hodhi, na kwamba wao ndio waliortaddi na kuzusha mambo katika dini, kisha wakawapangia wengine kuwa hao hawataondolewa? Wakati hadithi hazikutaja kwa majina yupi ataondolewa na yupi atakayebaki. Ushahidi walioutumia dhidi ya wenzao unaweza pia kutumiwa dhidi ya wanaowataka wao, juu ya kuwa sisi hatusema hivyo, hasa kwa vile hapana nassi inayoeleza kwa uwazi kuwa Fulani ataondolewa na Fulani atabaki. Hadithi sahihi zimetuthibitishia kusifiwa kwa Masahaba wote kwa ujumla, na kututhibitishia pia kuwa wao ni watu wa Peponi.

Kwa hivyo tunasema; Hao Masahaba mnaowadhania kuwa watarudishwa penye hodhi, zipo dalili nyingi sana kutoka kwenye Qur'ani na Sunnah zenye kuwasifia na kuwatakasa kwamba wao ndio walioamini hasa na kututhibitishia kwa dalili isiyokuwa na shaka kuwa wao ni watu wa Peponi.

 

Kutokana na haya, haki inadhihiri, na utatanishi unatoweka kwa sababu ya ushahidi usikuwa na uzito wowote.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala Atupe mwisho mwema na atufufue chini ya bendera ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) pamoja na Masahaba wake watukufu (Radhiya Llahu anhum).

Hitimisho

Kwa kumaliza tunasema:

Kwanza; waliokusudiwa kuwa ni Masahaba katika hadithi hizi ni wanafiki waliokuwa wakijifanya Waislamu mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam).

Mwenyezi Mungu amesema:

-

Na katika mabedui walio jirani zenu wamo wanaafiki; na katika wenyeji wa Madina pia wapo walio bobea katika unaafiki. Wewe huwajui. Sisi tunawajua. Tutawaadhibu mara mbili, kisha watarudishwa kwenye adhabu kubwa.

At Tawbah 102

 

Pili; waliokusudiwa ni wale waliortaddi baada ya kufariki dunia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam). Inajulikana kuwa wengi miongoni mwa makabila ya kiarabu yalirtaddi baada ya kufariki dunia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam), na hawa ndio kwa ajili yao Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) atasema:

"Sahibu zangu hawa." Na ataambiwa: "Hujuwi wewe waliyozusha baada yako. Waliendelea hawa kurtaddi tokea ulipofariki dunia."

 

Tatu; inaweza kumaanisha pia kuwa kila aliyemuona Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) hata kama hakuwa Sahaba kwa maana ya neno hilo, na dalili ni yule mkuu wa wanafiki Abullah bin Ubay bin Salul aliposema:

{: 8}.

Wanasema: Tukirejea Madina mwenye utukufu zaidi bila ya shaka atamfukuza aliye mnyonge. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye utukufu - Yeye, na Mtume wake, na Waumini. Lakini wanaafiki hawajui.

Al Munafiqun - 8