UDHU NA FAIDA ZAKE

Mara nyingi sana baadhi ya waislamu huitekeleza Ibada hii ya udhu kwa makosa kiasi ambacho huiondolea baraka Ibada hio na wakati mwengine hubatilika kabisa udhu wake kwa kuacha sehemu ya viungo vyake ambavyo vinalazimika kupata maji bila ya kuvifikishia maji ipasavyo. Mfano kama mtu anatia udhu na wakati wa kuosha uso huacha sehemu za uso huo bila ya kupitisha maji au baadhi ya sehemu za miguu yake, jambo ambalo linamharibia udhu wake na pia linamkosesha thawabu na baraka.

Katika kusisitiza jambo hilo Mtume {S.A.W} aliwahimiza sana waislamu juu ya utiaji wa udhu uliokamilika na kwamba kufutiwa kwa madhambi ya mtu pia hutegemea namna anavyoutia udhu wake.

Mtume {S.A.W} anasema:

"Jee sikwambiini juu ya jambo kuwa jambo hili Mwenyezi Mungu hufuta dhambi na hunyanyua daraja zake?"

Wakasema Masahaba:

"Ndio ewe Mtume wa MwenyeziMungu tuambie".

Akasema Mtume {S.A.W}:

"Kutimilisha udhu pamoja na shida zake".

Kwa mujibu wa hadithi hii inaonyesha kuwa udhu uliokamilika una cheo chake maalum mbele ya Mwenyezi Mungu na ule uliokosa ukamilifu huwa na kasoro na kutokua na baraka au kutokamilika mbele ya Mwenyezi Mungu. Na wakati mwengine kukosekana kwa taratibu nzuri hupelekea makosa na kasoro, mfano kutokuwa na nia na azma ya kutia udhu au kutopiga Bismillahi wakati wa kuanza kutia udhu, vile vile utaratibu wa kiislamu ni kwamba kila jambo jema kama hili la udhu hufanywa kwa kutumia mkono wa kulia. Basi udhu kama hapana dharura ni lazima utiwe kwa kutumia mkono wa kulia hapo huwa imepatikana sunna muhimu ya udhu.

Inafaa tuelewe kwamba udhu unakuwa ni lazima kwa mwenye hadathi anaetaka kufanya ibada ya sala iwe sala hio ni faradhi au sunna na vile vile katika sala ya maiti na pia katika sijda ya kisomo, na hasa hasa udhu unalazimika wakati wa kugusa msahafu na japo ni iwe ni aya iliyoandikwa katika karatasi.

 

Inasuniwa na kupendezeshwa udhu kwa muosha maiti au mchukuaji, kwani Mtume {S.A.W} anasema:

"Atakae mkosha maiti basi aoge na atakaemchukua basi atawadhe".

Jambo muhimu katika udhu ni kuondoa kabisa vizuizi ambavyo vitazuia ngozi ya kiungo cha udhu kupata maji, mfano mafuta ya mgando na rangi za kuchani wanazotumia wanawake kujipambia hazifai kabisa. Na kwa wale wenye kuvaa pete vidoleni mwao wanatakiwa wahakikishe zinapata maji sehemu zote zilizozunguka pete hiyo au kuziba na hii na kwa zile pete zenye kubana. Kwa piko na vipodozi vyengine ambavyo vinazuia maji kufika ngozini havifai kwani vitaharibu taratibu za udhu. Ama hina na mafuta mengine mepesi ambayo hayazuii kufika maji kwenye ngozi hayo yanaruhusika kwa masharti yake.

Inafaa tuzingatie kwamba kama hakuna dharura mtu anatakiwa atie udhu yeye mwenyewe bila ya msaada wa mtu mwengine na vile vile kabla ya kutia udhu anatakia asuwaki[apige mswaki] ili kuondoa karaha ya uchafu mdomoni mwake na hii ni kwa yule ambae hakufunga [funga ya ramadhani au ya sunna].

 

Muislamu kuwa na udhu wakati wote ni jambo muhimu sana ambalo linapendezeshwa, kwani udhu ni kinga na ni kisaidizi kikubwa cha Ibada. Kwa hiyo anatakiwa Muislamu kuhakikisha kuwa na udhu wakati wote hasa kabla ya kuingia wakati wa sala ili ajihimu kukimbilia ibada na utiifu kwa Mola wake na hii ni kwa yule mtu ambae hana udhuru. Ama mwenye udhuru basi anaweza kuahirisha kutia udhu hadi wakati wa sala ufike na hii ni kauli ya Jamhuri ya Ulamaa wa Kiislamu.

Kufanya israfu katika jambo la kutia udhu ni jambo la haramu na karaha, na sirafu inakuwa kwa kuzidisha kiwango kinachotakiwa kama vile kuosha viungo mara zaidi ya tatu au kutumia maji mengi sana, hasa ikiwa anatumia mfereji akiwa ameufungua kwa kasi sana.

Jambao la msingi kwa muislamu ni kuelewa kwamba udhu ni kitu muhimu sana katika ibada zake mtu na katika maisha yake yote na ndio maana Mtume [S.A.W] akaupa cheo kikubwa kwa kusema;

"Kujitoharisha ni nusu ya uislamu".

Kwa kutakiwa tuwe na udhu wakati wote hasa hasa tunaposoma Qur’aani na darasa za hadithi na vitabu vya elimu ya kisheria. Na mtu anapoghadhibika kwani udhu unazima chuki za mtu.