IDADI YA WAISLAMU YAONGEZEKA UENGEREZA

23/02/2004

Gazeti la Sunday Times la London limeandika leo kuwa zaidi ya Waingereza weupe elfu 14 wameingia katika dini ya Kiislamu baada ya kuona kuwa mwenendo na tabia za kizungu zinawapotosha.

Gazeti hilo linalotolewa kila wiki limeendelea kueleza kuwa; kutokana na utafiti wenye kuaminika imeonekana kuwa Waingereza wengi wenye kumiliki ardhi na watu mashuhuri na maarufu wameingia katika dini ya Kiislamu jambo linalowafurahisha sana Waislamu wa Uingereza kwa sababu ya himaya watakayoweza kuipata kutokana na mwenendo huo.

 

Gazeti hilo likimnukuu mwandishi wa utafiti huu Yahya Bert aliyekuwa akijulikana hapo mwanzo kwa jina la Jonathan Bert ambaye ni mwana wa Lord Bert aliyekuwa mkurugenzi wa Idhaa ya BBC kuwa amesema:

"Wapo zaidi ya Waingereza weupe 14200 walioingia katika dini ya Kiislamu wakiwemo watu mashuhuri na kwamba katika siku chache zijazo wengi zaidi wanategemea kuingia katika dini hii.

 

Gazeti hilo limeendelea kusema kuwa wengi kati ya walioingia katika dini ya Kiislamu wamevutiwa na makala ya Charles Logan Eton aliyekuwa mwana diplomasi maarufu aliyeandika kitabu kiitwacho 'Uislamu na Ubinadamu'.

 

Sunday Times likimnukuu Eton limeandika kuwa; baada ya kuandika kitabu chake hicho, Eton alipata barua nyingi kutoka kwa watu mbali mbali waliofurahishwa na kitabu hicho.

 

Gazeti hilo limeandika pia kuwa wapo Waingereza wengi walioingia katika dini ya Kiislamu baada ya kufanya urafiki na Waislamu na wengine baada ya kusoma makala mbali mbali juu ya Uislamu mfano wa Ema Clark mjukuu wa waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Herbert.

 

Gazeti hilo limeeleza pia kuwa mchezaji cricket maarufu wa Pakistan Imran Khan na aliyekuwa muimbaji maarufu wa Uingereza Cat Stevens (Yusuf Islam) wamefanya juhudi kubwa katika kuwafanya Waingereza wengi kuingia katika dini ya Kiislamu.

 

Gazeti lingine la Kiingereza limeandika kuwa idadi ya wanawake walioingia katika dini ya Kiislamu kwa njia ya ndoa inakaribia elfu 77

 

Wikala ya habari ya Kiislamu

23/02/2004