Ukweli Kuhusu Mazishi Ya Kiislamu

Imeandaliwa Na Vijana Wa Kiislamu Musoma-Tanzania

 

Bismillaahir Rahmaanir Rahiim 

 

Kwa hakika kila sifa njema ni Zake Allaah, tunamtukuza Yeye, na tunamtaka msaada Yeye na tunamuomba msamaha Yeye. Tunajilinda kwa Allaah kutokana na maovu ya nafsi zetu na udhaifu wa vitendo vyetu. Aliyeongozwa na Allaah hakuna wa kumpoteza na aliyepotezwa na Allaah hakuna wa kumuongoza. Nashuhudia kuwa hapana apasaye kuabudiwa kwa haki ila Allaah na nashuhudia kuwa Muhammad ni mja Wake na Mtume Wake.

Enyi mlioamini mcheni Allaah (kwa kuyatekeleza yote Aliyowaamrisha na kujiepusha na yote Aliyowakataza) kama ipasavyo kumcha wala msife ila mumekwisha kuwa Waislamu kamili (Qur-aan 3: 102)

 

 ۚ  ۚ

Enyi watu mcheni Mola wenu ambaye Amekuumbeni kutokana na nafsi (asili - Adam) moja. Na akamuumba mkewe katika nafsi ile ile. Na akaeneza wanaume wengi na wanawake kutokana na wawili hao. Na mcheni Allaah ambaye kwaye mnaombana. Na (muwatazame) jamaa. Hakika Allaah ni Mlinzi juu yenu (Anayajua mnayoyafanya). (Qur-aan 4: 1) 

﴿٧٠﴾  ۗ ﴿٧١﴾

Enyi mlioamini mcheni/muogopeni Allaah na mseme maneno yaliyo ya haki (maneno ya kweli). (Allaah) Atakutengenezeeni vizuri vitendo vyenu, na Atakusameheni madhambi yenu. Na mwenye kumtii Allaah na Mtume Wake bila shaka amefanikiwa mafanikio makubwa. (Qur-aan 33: 70-71)

 

Kwa hakika maneno ya kweli kabisa ni yale ya Kitabu cha Allaah, na uongozi ulio bora zaidi ni uongozi wa Muhammad (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake). Na maovu yaliyo mabaya zaidi ni mambo ya kuzua (yaliyo mageni katika mafundisho ya Uislamu), na kila lenye kuzushwa katika dini ni bidaa(uzushi), na kila bidaa ni upotofu na kila upotofu mwisho wake ni katika moto.

 

Ndugu msomaji, Allaah Mtukufu Anasema:

ٰ ﴿١﴾  ۚ ﴿٢﴾

Ametakasika (Ametukuka) Yule ambaye mikononi Mwake upo ufalme na Yeye ni Muweza juu ya kila kitu. Yeye (Allaah) ndiye Aliyeumba umauti na uhai ili apate kuwajaribu ni nani kati yenu mwenye vitendo  vizuri. Na Yeye (Allaah) ni Mwenye nguvu na ni mwingi wa kusamehe. (Qur-aan 67: 1-2)

 

Mtume Muhammad (Rehma na amani ya Allaah iwe juu yake) amesema:

Sikuwa mimi katika hii dunia isipokuwa ni mfano wa msafiri jangwani aliyepumzika katika kivuli cha mti, kisha akaondoka na kukiacha kivuli kile. (Hadiyth sahihi: Al-Albaaniy, namba, 438).

 

Ndugu msomaji, fahamu kuwa kwa mujibu wa mafundisho sahihi ya Uislamu, maiti ana haki nne anazopaswa kutendewa, ambazo ni:

1.     Kuoshwa,

2.     Kuvishwa sanda,

3.     Kuswaliwa, na

4.     Kuzikwa.

Hii ina maana kuwa Waislamu watawajibika kuyafanya haya kwa kila maiti Muislamu na si vinginevyo. Na watakapoacha kumfanyia maiti mambo hayo watapata dhambi Waislamu wote wa sehemu ile.

 

Ndugu msomaji, tunafahamu kuwa una hamu kubwa ya kuyajua kiundani mambo manne tuliyoyataja hapo juu. Shaka ondoa, makala hii iliyo mikononi mwako itakuonesha hayo kadiri utakapozidi kufungua kurasa zake.

 

Awali ya yote tunapenda kukujulisha itikadi ya Uislamu kuhusu maisha na uhai huu wa dunia.

 

Ndugu msomaji, Waislamu wanaitakidi kuwa, kila kilichopo katika dunia kitaondoka (kitakufa). Na hii ni kutokana na kauli ya Allaah Aliposema:

Kila kilicho juu ya ardhi ni chenye kufa (Qur-aan 55: 26)

 

Kama ilivyozoeleka kuwa hakuna mwanzo usiokuwa na mwisho, wala hakuna mchana usiokuwa na usiku, kadhalika hakuna uhai usiokuwa na mauti. Allaah Anasema:

Kila nafsi itaonja umauti (Itakufa) (Qur-aan 21: 35)

Na Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) ameweka wazi katika Hadiyth tuliyoitanguliza hapo nyuma.

 

Ndugu msomaji, waweza kujiuliza kuwa umauti ni nini?

Nasi kwa kulifahamu hilo tuna haki ya kukufafanulia kama ifuatavyo:

Umauti ni mtengano au mfarakano kati ya mwili na roho ya kila kiumbe hai, kama mwanadamu, wanyama, majini n.k. Hapo huwa ndio mwisho wa kazi ya kila kiungo cha aliyekufa; macho, mdomo, sikio, mikono, mguu na mfano wake.

 

Si kama wanavyodai baadhi ya wasiokuwa na ufahamu sahihi na wasio na akili zenye kuwatosha kuwa eti kuna baadhi ya watu ambao huwa wanakufa baadhi ya viungo na baadhi havifi. Huu ni uongo wa wazi kabisa na kila mtu aliye na akili timamu atampa msemaji wa maneno haya moja kati ya sifa tatu zifuatazo:

1.     Mjinga,

2.     Punguani, hajui alisemalo,

3.     Ni mtu aliyeamua kuifanya nafsi yake kuwa pumbavu, mfano wake ni 
kama mtu anayedai mchana kuwa usiku na usiku kuwa mchana.

 

Haiingii akilini kabisa kuwa mtu afe halafu mguu wake usife au mkono wake au macho yake yasife au tupu yake isife. Hii haihitaji Aayah, Hadiyth, wala elimu kubwa wala muujiza, kwani akili inamtosha mwenye nazo na akazitumia. Ama yule asiyekuwa na akili basi Aayah, Hadiyth wala elimu yoyote pia haitamfaa.

 

Ndugu msomaji, katika hili tunaomba mchango wako wa kiakili na kujiuliza kuwa, Je, inawezekana kweli mtu afe baadhi na baadhi abaki kuwa hai halafu aitwe maiti? Jawabu liwe akilini mwako.

 

Mpendwa msomaji, baada ya kupata jawabu, sasa nikueleze yale mambo manne anayopaswa kufanyiwa maiti wa Kiislamu.

 

Jambo La Kwanza Ni Kuosha

Waislamu wanaosha maiti kwa sababu hayo ni mafundisho ya dini, na ni shariah.

Mtume Muhammad (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) ametufundisha hayo katika Hadiyth ya Swahaba (mfuasi wa karibu) mtukufu Ibnu Abbaas (Radhi ya Allaah iwe juu yake) katika kitabu cha Imam Al-Bukhaariy na Muslim kama alivyoeleza Shaykh Al-Albaaniy katika kitabu chake Ahkaamul Janaaiz, na Abuu Nuam katika al-Mustakhraj Hadiyth namba, 139-140:

Maana ya Hadiyth:

Siku moja mtu mmoja alikuwa amesimama Arafah, ghafla mtu huyo akaanguka kutoka katika mnyama wake na yule mnyama akamkanyaga na kufa papo hapo. Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) akasema: Muosheni kwa maji na majani ya mkunazi na mumvishe sanda

Hivyo basi kwa mujibu wa mafundisho ya Mtume Muhammad (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) Waislamu wanawajibika kuosha maiti yao pale linapowezekana, kwa sababu hayo ndiyo mafundisho ya dini yao na si vinginevyo, wala si kama wasemavyo wenye chuki dhidi ya Uislamu kuwa eti Waislamu wanaosha maiti kwa sababu huenda ina janaba (yaani ilizini).

 

Swali la kujiuliza, Je ni kitabu gani kinachozungumzia hayo? Jibu ni hakuna ushahidi juu ya hayo katika kitabu chochote au mafunzo yoyote ya Uislamu wala hakuna ushahidi wowote wa kimazingira. Unaweza kujiuliza, kwa nini basi wanasema wasiyo na ushahidi nayo? Jibu linaloweza kupatikana ni moja tu, nalo ni chuki dhidi ya Uislamu.

 

Ndugu msomaji, ukweli ulio wazi ni kuwa chuki dhidi ya Uislamu imewapelekea watu (maadui) kuuzungumzia Uislamu na kuuzushia mambo ambayo hayapo na hayana ushahidi wowote. Muradi wao ni kuupiga vita Uislamu katika hali yoyote ile iwayo, na hili Allaah Mtukufu Amelitanabahisha katika Qur-aan, Aliposema:

ٰ

Hawataacha kukupigeni kwa chuki walizo nazo mpaka wakutoeni katika dini yenu watakapoweza kufanya hivyo (Qur-aan 2:217)

 

Ndugu msomaji, suala la zinaa limekatazwa katika Qur-aan kuanzia katika hatua zake za mwanzo. Allaah Mtukufu Amesema:

 ۖ

Wala msikaribie zinaa kwani huo ni uchafu na ni njia iliyo mbaya kabisa (Qur-aan 17:32)

 

Haifai kumtazama mwanamke kwa matamanio, imekatazwa pia kupeana mikono na mwanamke/mwanamume ambaye si ndugu yako wa karibu, si hilo tu, Uislamu hauruhusu wanaume kuchanganyika na wanawake katika hali yoyote ile. Kama hilo halitoshi, mwanamke katika Uislamu anatakiwa avae hijabu, vazi lisilo bana mwili wala lisilovutia na linalofunika mwili mzima. Katika hali hii na kwa mazingira haya, iweje Muislamu azini? Hapo ndipo utagundua kuwa aliyesema haya ima alitoka usingizini au hatumii akili.

 

Ndugu msomaji, fahamu kuwa hakuna mfumo au utaratibu wa maisha wenye kumuhimiza na kumuhitaji mtu kuwa mbali na zinaa kama utaratibu wa Kiislamu. Ndio maana Uislamu ukahimiza kuoa na ukakemea vikali uhuni na ukapera (kuto oa). Tunakushauri ndugu msomaji, uusome Uislamu, na hii ndio njia pekee ya kuujua ukweli, badala ya kusikiliza maneno ya watu wenye chuki na uadui dhidi ya Uislamu, ambao wengine wanadai kuujua Uislamu lakini kiukweli ni kuwa wanachotafuta ni kuwadanganya wasiokuwa Waislamu ili kupata muradi wao wa siku.

 

Namna Ya Kuosha Maiti

Ni nani mwenye haki zaidi ya kumuosha maiti? Kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu, mwenye haki zaidi ya kumuosha maiti ni yule mwenye ufahamu sahihi juu ya utaratibu wa kuosha maiti na Sunnah[1] zake, na hasa akiwa ni katika jamaa zake kama vile, mkewe/mumewe, mwanawe n.k.

Waoshaji huwa ni wawili au watatu kulingana na hali halisi. Watu hawa hawana majina maalum kishariah, kama wanavyodai baadhi ya watu kuwa eti kuna kiguzo, kigingi, na mshika kata; huu ni uzushi. Vitabu vinaonesha kuwa, Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) alioshwa na Aliy akisaidiwa na Al-Fadhlu ibnu Abbaas na Usaamah bin Zayd (Radhi ya Allaah iwe juu yao), wala hawakupewa majina maalumu. Haya yameelezwa na Abuu Daawuud kwa mapokezi sahihi juzuu ya pili (2) ukurasa wa 69.

 

Hatua Ya Kwanza:

Maiti itavuliwa nguo kwa upole na kufunikwa shuka ndefu baada ya kumfumba macho kama ilivyopokewa na Imaam Muslim, Ahmad na Al-Bayhaqiy kitabu cha tatu (3) ukurasa wa 334 na kama alivyoeleza Shaykh al-Albaaniy katika Ahkaamul Janaaiz ukurasa wa 12 katika Hadiyth ya Ummu-Salamah amesema:

Aliingia Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) kwa Abu-Salama akamkuta macho yake yapo wazi akamfumba, kisha akasema hakika roho inapotolewa macho huifuata iendapo

 

Huu ni uthibitisho wa mwongozo sahihi wa Uislamu katika kumuosha maiti, si kama wanavyodai maadui wa Uislamu.

 

Hatua Ya Pili:

Baada ya kuvuliwa nguo, haraka iwezekananvyo, maiti itaoshwa. Yataandaliwa maji ambayo yatakuwa yamechanganywa na majani ya mkunazi[2] na kaafuur. Maji si lazima yawe ya moto, ila ikiwa kuna baridi kali maji yawe ya uvuguvugu. Atakayesema kuwa maji lazima yawe ya moto, huyo ni muongo kwani haya yameelezwa katika vitabu vya kishaafiiy kama kitabu cha shekhe Abdullaah bin Abdir-Rahmaan al-Hadharamiy (850-918) ukurasa wa 48 hadi 49, katika mlango wa Al-Janaaiz.

 

Maiti ataoshwa majosho matatu au matano kulingana na hali halisi ya maiti huyo. Hii ni kutokana na Hadiyth iliyosimuliwa na Ummu Atwiyah kuwa:

Aliingia Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) wakati tukiwa tunamuosha binti yake, Zaynab, akasema: Muosheni mara tatu au mara tano au mara saba au zaidi ya hapo ikiwa mtaona haja ya kufanya hivyo....[3]

 

Ikiwa maiti ni wa kiume, nywele zake zitaachwa kama zilivyo ila zitaoshwa vizuri na wala hakitakatwa chochote kwenye mwili wake, si nywele wala kucha. Na ikiwa maiti ni wa kike, nywele zake zitafumuliwa ikiwa zimesukwa, kisha zitaoshwa, halafu zitasukwa tena njia tatu zikielekezwa kisogoni mwake. Na hii ni kutokana na Hadiyth iliyosimuliwa na Ummu Atwiyah.[4]

 

Hatua Ya Tatu:

 

Ndugu msomaji, muoshaji atafunga kitambaa au atavaa kitu chochote mkononi mfano wa glovu, kisha ataosha sehemu za siri za maiti, baada ya kumpapasa tumboni kwa taratibu, ili kuondoa uchafu ulio karibu kutoka. Muoshaji atayafanya hayo bila kuangalia uchi wa maiti. Ni uzushi na ni uongo mkubwa kudai kuwa maiti wa Kiislamu hukamuliwa kwa Nguvu tumboni, kwani kufanya hivyo ni kinyume na mafundisho sahihi ya Uislamu.

 

Muoshaji atatupa kitambaa cha kwanza, kisha atachukua kingine na kuanza kusafisha meno ya maiti, baada ya kulowanisha kitambaa hicho kwa maji. Baada ya hapo, muoshaji na msaidizi wake watamtawadhisha[5] maiti, Wudhuu kamili. Watayafanya hayo yote kwa kuanzia kuliani kwa maiti na kumalizia kushotoni kwa maiti. Kwa mfano, wataosha mkono wa kulia halafu wa kushoto na mfano wa hayo.

 

Ndugu msomaji, fahamu kuwa maiti haitaingizwa maji mdomoni au masikioni au popote pale kwani hakuna ushahidi wowote juu ya hilo katika mafundisho ya Uislamu. Yeyote atakayeleta madai ya namna hii una haki ya kumtaka atoe ushahidi juu ya hilo.

 

Baada ya kutawadhishwa, maiti ataoshwa mwili wote mara tatu, tano, saba au zaidi ya hapo, kamatulivyoelezea hapo nyuma. Atamwagiwa maji upande wa kulia, kisha upande wa kushoto na kuoshwa vizuri kabisa. Na iliyo bora ni kuchanganya maji ya kuoshea kwa majani ya mkunazi kamatulivyokwisha elezea hapo awali katika Hadiyth ya Ummu Atwiyah. Lililo bora katika osho la mwisho ni kuchanganya maji na kaafuur. Hii ni aina ya manukato yanayowekwa kwenye maji.

 

Kufikia hapa ndugu msomaji, tunataraji utakuwa umefahamu usahihi wa kuosha maiti, japo kwa ufupi.

 

Pamoja na hayo, ndugu msomaji, una haki ya kufahamu mambo yafuatayo:

 

Hataoshwa maiti aliyekufa shahidi[6], bali atazikwa na nguo zake hizohizo. Hii ni kutokana na dalili nyingi, miongoni mwazo ni ile Hadiyth ya Jaabir (Radhi za Allaah ziwe juu yake) pale Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) aliposema kuwaelekeza katika kuwazika Maswahaba[7] waliofariki katika vita ya Uhudi kuwa, Wazikeni na damu zao[8]

 

Fahamu pia kuwa, aliyekufa hali ya kuwa amehirimia (ameshakuwa tayari na amekusudia) kufanya hija, mtu huyo naye hatapakwa manukato wala hatafunikwa kichwa chake.

 

Ikiwa maiti itaharabika kutokana na namna ya kifo chake, kama vile kutokana na ajali ya gari, kuungua moto, kuangukiwa na nyumba, n.k, basi maiti huyo atatayamamishwa (yaani badala ya kutumika maji utatumika udongo ulio safi na twahara), na kama itashindikana basi, uwajibu (ulazima) wa kufanya hivyo  utaondoka. Allaah, Mtukufu, anasema katika Qur-aan 2:286:

 

Allaah Haikalifishi (hailazimishi) nafsi ila kwa yaliyo sawa na uwezo wake

 

Pia Wanachuoni wa kanuni za Fiqh (Usuul al-Fiqhi) wana msemo usemao:

 Hakuna uwajibu endapo hauwezekani (hautekelezeki) (La waajiba maal ajzi). Na Allaah ni Mjuzi zaidi.

 

Hutokea baadhi ya nyakati kuwa, mathalani, mtu kafariki na baadhi ya viungo vyake, kama mikono au mguu, vimekosekana. Na maiti huyu ameoshwa, kaswaliwa, na hatimaye kuzikwa akiwa hana viungo vyote. Mara tu baada ya kuzikwa kikaonekana kiungo au baadhi ya viungo vilivyokosekana, Je, kiungo au viungo hivyo vitaoshwa na kuswaliwa? Ndugu msomaji, suala hili aliwahi kuulizwa Shaykh Muhammad bin Swaalih Al-Uthaymiyn[9] (Allaah Amrehemu), akajibu:

Viungo vidogo vidogo kama mikono na miguu vitakapopatikana na maiti ameshaswaliwa, viungo hivi havitaoshwa wala kuswaliwa kwa kuwa ameshaswaliwa.

Akaendelea kusema:

Ama itakapokuwa maiti haikupatikana bali kimepatikana kiungo katika mwili wake kama vile kichwa au mguu au mkono, basi kitaswaliwa na kuzikwa kilichopatikana baada ya kuoshwa vizuri na kuvishwa sanda[10].

 

Mpaka hapa tuna imani kuwa tumeondoa kiu yako juu ya moja kati ya mambo mane anayopaswa kufanyiwa maiti. Hatua inayofuata baada ya hii ni kuvishwa sanda.

 

Kuvishwa Sanda

Baada ya maiti kuoshwa vizuri, hatua inayofuata ni kuvishwa sanda, nguo au shuka ndefu yenye uwezo wa kufunika mwili wote wa maiti. Ni bora zaidi na inapendeza shuka hiyo ikiwa nyeupe. Na hii ni kutokana na Hadiyth sahihi ya Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) aliposema:

Pendeleeni kuvaa mavazi meupe kwani hayo ni katika mavazi bora kwenu na mukafini (muwavishe) maiti wenu kwa hizo sanda.[11]

 

Sanda huwa ni shuka tatu (3) tu, na si zaidi, kutokana na Hadiyth iliyosimuliwa na mama wa Waumini Aaishah (Radhi ya Allaah iwe juu yake) aliyesema:

Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) alikafiniwa (alivishwa sanda) katika nguo tatu[12]

 

Ndugu msomaji, hakuna tofauti kati ya sanda ya maiti mume na sanda ya maiti mke, na hii ni kutokana na kukosekana ushahidi sahihi juu ya hilo, na kama upo, basi ni Hadiyth ambazo hazikusihi upokezi (sanadi) wake. Mfano wa Hadiyth dhaifu inayotumiwa na baadhi ya watu ni Hadiyth ya Layla bint Qaaif Ath-Thaqafiy inayoeleza kuwa sanda ya kike ni nguo tano zikiwa shuka mbili, kikoi, kanzu, na kilemba. Hadiyth hii upokezi (isnadi) yake ni dhaifu. Ndani ya msururu wa wapokezi (isnadi) kuna mtu mmoja, anaitwa Nuuh bin Haakim Ath-Thaqafiy, ambaye hajulikani zaidi ya jina lake tu, kamaalivyoelezea al-Haafidh bin Hajar na wengineo[13]

 

Uandaaji Wa Sanda

Shuka hizo kwa ajili ya sanda zitatandikwa sehemu safi. Kisha zitafukizwa udi na manukato mazuri mara tatu, kama alivyoelekeza Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake):

Mtakapoweka manukato ya maiti basi wekeni mara tatu.[14] Isipokuwa sanda ya aliyehirimia kufanya hija haitapakwa manukato wala haitafukizwa udi.

Hii imeesimuliwa na Ibn Abbaas (Radhi ya Allaah iwe juu yake) kwamba Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) amesema:

Msimpake manukato wala msimfunike kichwa chake kwani huyo atafufuliwa siku ya kiama hali ya kuwa analeta talbiya[15] (Al-Bukhaariy na Muslim).

 

Baada ya kutandikwa sanda, maiti atalazwa juu yake. Itachukuliwa ncha ya upande wa kulia na iletwe hadi kifuani mwake, na ncha ya kushoto itafanywa hivyo hivyo. Utaratibu huo utafuatwa kwa shuka ya pili na ya tatu. Kisha itachukuliwa kuanzia kichwani na itafungwa na miguuni pia itafungwa. Pia itawekwa pamba iliyolowanishwa manukato mazuri na itawekwa juu ya macho yake na mdomoni mwake kama alivyoelekeza Shaykh Ibn Uthaymiyn. Mpaka hapa, maiti itakuwa tayari kwa ajili ya kutekelezewa jambo la tatu ambalo ni kuswaliwa.

 

Kumswalia Maiti

Ndugu msomaji, ni wajibu kumswalia kila maiti wa Kiislamu isipokuwa hawa wafuatao:

1.     Mtoto mdogo ambaye hajafikia kubalehe. Na hii tunaipata katika Hadiyth iliyosimuliwa na bi Aaisha (radhi ya Allaah iwe juu yake) kuwa:

Alikufa Ibraahim mtoto wa Mtume wa Allaah na hali ya kuwa ana miezi minane na Mtume hakumswalia.[16]

2.     Mtu aliyekufa shahidi (aliyekufa vitani) kwani Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) hakuwaswalia waliokufa katika vita vya Uhud.

 

 

Ndugu msomaji, fahamu kuwa tunaposema kuwa si wajibu kuwaswalia watu wa aina hii hatuna maana kuwa ni haraam kuwaswalia, bali tunamaanisha kuwa hakuna ulazima au uwajibu wa hilo. Lakini wakiswaliwa inafaa kwa kuwa kuna ushahidi juu ya hilo kama alivyosimulia Aaishah, mama wa waumini, anayesimulia:

Aliletwa mtoto kwa Mtume wa Allaah (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) miongoni mwa watoto wa answaar (watu wa Madiynah) na Mtume akamswalia.[17]

Ndugu msomaji, ni matarajio yetu kuwa utangulizi huu utakuwa ni mwanzo wa kuifahamu vizuri Swalah ya Jeneza.

 

Namna Ya Kumswalia Maiti

Maiti huswaliwa kwa kufuata utaratibu huu:

Atasimama Imaam (kiongozi wa Swalah) upande wa kichwa, kama maiti ni mwanaume, na hii imethibiti katika Hadiyth ya Abu Ghaalibi al-Khayyaat, amesema:

Nimemshuhudia Anas bin Maalik akiswalia maiti ya kiume akasimama usawa wa kichwa chake.

Pia Imaam atasimama usawa wa katikati wa ikiwa maiti ni mwanamke, kama ilivyothibiti katika Hadiyth ya Samurah bin Jundub, anasema:

Nimeswali nyuma ya Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) naye akimswalia mama wa Kaab.akasimama katikati yake.

Kisha, Imaam ataleta takbira kwa kusema, Allaahu Akbar, (Allaah ni mkubwa) mara nne au tano au tisa, kwani aina zote hizi zimethibiti kutoka kwa Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake). Lakini mara nyingi Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) alileta takbira nne (4).

Katika takbira ya kwanza, itasomwa suratul-Faatihah, baada ya kumlaani Shaytwaan, bila kudhihirisha sauti.

Katika takbira ya pili, itasomwa Swalah ya Mtume kwa ukamilifu wake.

   

Katika takbira ya tatu itasomwa duaa ya kumuombea maiti, nazo ni nyingi zilizothibiti kutoka kwa Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake).

Katika takbira ya nne, ambayo ni ya mwisho, itasomwa duaa yoyote au atanyamaza (anayeswali) na kisha atatoa salamu. Namna zote hizi mbili zimethibiti.[18]

 

Ndugu msomaji, ni muhimu ufahamu kuwa kuna nyakati tatu muhimu ambazo haifai kuswali ndani yake ila kwa dharura. Nyakati hizo zimebainishwa katika Hadiyth ya Uqbah bin Aamir (Radhi ya Allaah iwe juu yake) anayesimulia:

Alikuwa Mtume (Rehma na amani za Allaah iwe juu yake) anatukataza kuswalia au kuzika maiti katika nyakati tatu:

Kwanza - wakati wa kuchomoza jua mpaka linyanyuke juu,

Pili wakati anaamka aliyelala qayluulah (yaani saa 6:00 mchana wakati jua linapokuwa utosini au katikati mpaka lihame kuelekea upande wa Magharibi).

Tatu wakati jua linapokaribia kuzama mpaka lizame kabisa.[19]  

NB: Suala hili lina mitazamo tofauti miongoni mwa wanachuoni wa Ahlus Sunnah wal-Jamaah[20] juu ya kufaa kuswalia jeneza na kuzika katika nyakati hizi. Lakini wengi kati yao wanaliona hilo halipendezi kishariah (makruhu) nao ni kama vile Atwaa, An-Nakhaiy, Al-Awzaiy, Ahmad, Is-haaq, na Ath-Thawriy. Ash-Shaafiiy yeye anaona kuswalia wakati wowote na kuzikwa inafaa[21] Kauli ya jamaa (ya kwanza) ni bora kwa kuwa imeafikiana na Hadiyth.

 

Kuzikwa

Jambo la nne analopaswa kutekelezewa maiti ni kuzikwa. Kaburi ni lazima liwe refu kwenda chini na liwe pana. Kina cha kaburi kiwe sawa na kimo cha mtu mzima na kunyoosha mkono, na litachimbwa kiasi maiti akilazwa kwa ubavu wa kulia atakuwa anaelekea Qiblah[22]

Kaburi likiwa tayari, maiti atachukuliwa katika jeneza na kuwahishwa katika kaburi. Wakati wa kusindikiza jeneza (kumpeleka maiti kaburini), mambo yafuatayo yanapaswa kuchungwa:

Kwanza, lisifuatwe jeneza kwa sauti wala kwa moto. Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) amesema katika Hadiyth iliyosimuliwa na Abu Hurayrah:

Msifuate jeneza kwa sauti wala kwa moto.[23]

Hapa inamaanisha sauti yoyote ya mwanadamu. Pia haifai kubeba chetezo cha ubani chenye moto wakati wa kusindikiza jeneza.

Pili, jeneza lisifunikwe na chochote. Kufunika jeneza au kaburi wakati wa kuzika ni miongoni mwa mambo yasiyokuwa na ushahidi[24]. Baada ya maiti kuwasilishwa kaburini, watatakiwa watu baadhi washuke ndani ya kaburi, na iliyo bora zaidi ni kuwa watakaoingia ndani ya kaburi wawe ndugu wa marehemu.

Allaah Mtukufu Anasema:

ٰ  ۗ

Na jamaa wa nasaba wanastahikiana wenyewe kwa wenyewe zaidi (katika kurithiana na mambo mengineyo) katika Kitabu cha Allaah. Hakika Allaah ni Mwenye kujua kila kitu[25]

 

Maiti atalazwa kama tulivyoelezea katika uandaaji wa kaburi, huku wakisema wanaomlaza maiti kwenye mwana-ndani:

Kwa jina la Allaah na juu ya mila ya Mtume wa Allaah au Kwa jina la Allaah na juu ya Sunnah ya Mtume wa Allaah. Haya yamethibiti kwa riwaya zote.

Wanaotakiwa kuyasema maneno haya ni wale wanaomuweka maiti katika mwanandani (sehemu ndogo inayochimbwa ndani ya kaburi kwa ajili ya kumlaza maiti kwa ubavu wake wa kulia) na sio walio juu ya kaburi. Haya yameelekezwa na Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) katika Hadiyth iliyosimuliwa na Swahaba mtukufu Al-Bayadhi kuwa:

Maiti anapolazwa katika kaburi basi aseme yule anayemuweka katika kaburi wakati wa kumuingiza katika mwanandani; Kwa jina la Allaah na kwa ajili ya Allaah na juu/kwa kufuata mila ya Mtume wa Allaah.[26]

Baada ya maiti kulazwa katika mwanandani, kaburi litafukiwa na mwisho litainuliwa kiasi cha shibri[27]moja tu. Na hili linathibitika kutokana na Hadiyth ya Jaabir (Radhi ya Allaah iwe juu yake) amesema:

Kwa hakika Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) aliwekwa katika lahdi (mwanandani) na yakawekwa nyuma yake matofali na likanyanyuliwa kaburi lake kiasi cha shibri moja.[28]

 

Kujengea Kaburi

Kwa taratibu na mafunzo sahihi ya Kiislamu, kaburi halitajengewa. Haikupata kuonekana zama za Mtume (Rehma na amani ya Allaah iwe juu yake) kaburi likajengewa na yeye akiwa hai, bali alionekana na kusikika kwa kinywa chake akilikemea vikali suala hili. Dalili juu ya hili zipo nyingi, mojawapo ni Hadiyth hii ambayo ameisimulia Abuu Yaala akisema,

Amekataza Mtume wa Allaah kujengwa juu ya kaburi na kukaa au kukanyaga juu yake na kuswali kwa kuyaelekea makaburi.[29]

Ndugu msomaji, jua ya kwamba makaburi ya Baqiy (sehemu walikozikwa Waislamu wa mwanzo, Maswahaba) mpaka sasa yapo na Waislamu wanaendelea kuzikwa katika eneo hilo. Waliojaaliwa kwenda Hijja ni mashahidi kwani huwa wengi wanayazuru makaburi haya na hayajajengewa. Suala la kujiuliza ni Je, kama makaburi hayo yangekuwa yanajengwa ingewezekana leo kuwepo eneo la kuzikia hadi sasa? Hasa ukizingatia kuwa kutoka Mtume (Juu yake rehma na amani ya Allaah) alipokufa mpaka sasa ni zaidi ya miaka 1400 imeshapita? Ni wazi kuwa kusingekuwa na nafasi tena ya kuzikia.

Kwa msingi huu tunatumia fursa hii kumuusia kila asomaye Makala haya kuwa maiti hanufaiki na na wala hana haja na vitu vya duniani, si vigae, marumaru, wala jengo la aina yoyote katika kaburi, bali anachohitaji zaidi maiti ni duaa yako. Mkumbuke, kisha muombee msamaha kwa Allaah Ampunguzie adhabu za kaburi bila kutumia utaratibu maalum, hapo utakuwa umemfanyia jambo kubwa sana. 

Kutokana na Hadiyth tuliyoinukuu punde tunajifunza mambo kadhaa ambayo huwa tunayafanya bila kujua ubaya wake. Mfano wa hayo ni kama kukalia na/au kukanyaga makaburi. Haya tunayashuhudia wakati maiti anapofikishwa katika eneo la makaburi, watu husimama juu ya makaburi na wengine huyakalia. Hili ni suala la kuwa makini nalo na kujichunga wakati tukiingia makaburini tusiyakanyage wala kuyakalia.

 

Kuzika Maiti Msikitini

Ndugu msomaji, miongoni mwa makatazo ni kuzika maiti Misikitini. Imekuwa kasumba ya baadhi ya watu kuacha wasia kuwa wakifa wazikwe Misikitini kwa kuwa pengine wao ndiwo waliotoa maeneo yaliyojengwa Misikiti hiyo au vinginevyo. Hii inawapelekea watu kuswali kwa kuyaelekea makaburi, jambo ambalo limekatazwa na shariah ya Kiislamu. Jambo hili limekuwa ni fitna kubwa miongoni mwa Waislamu kwani miongoni mwa madhara makubwa yatokanayo na jambo hili ni kwa watu kuanza kuomba na kufanya tawassul (kumuomba Mola kupitia makaburi hayo) na hatimaye kuabudiwa kabisa makaburi hayo. Haya ni masikitiko makubwa.

Aliulizwa mmoja wa wanachuoni, Shaykh Ibn Uthaymiyn kuwa ni ipi hukumu ya Swalah kwenye Msikiti wenye kaburi?

Akajibu akasema,

Ikiwa kaburi limeutangulia Msikiti (yaani kaburi lilikuwepo kabla Msikiti haujajengwa) basi ni wajibu kuuhama Msikiti huo na ubomolewe na liachwe kaburi. Na kama Msikiti umelitangulia kaburi basi ni wajibu kufukuliwa (kuhamishwa) kaburi hilo na maiti akazikwe makaburini.

 

Pia Shaykhul Islaam amesema,

Wala haitaswihi (haitafaa) Swalah kwenye makaburi au kwa kuyaelekea makaburi, na katazo hili ni kwa kuziba mianya ya shirki[30]

 

Kuhusu Kaburi La Mtume (Rehma Na Amani Ya Allaah Ziwe Juu Yake)

Maswali huja kuwa mbona kaburi la Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) liko ndani ya Msikiti na limejengewa? Katika kulifafanua hili inahitajika kwa wewe msomaji kuzingatia kwa umakini, kwani jambo hili linatatiza wengi katika watu.

Historia inaonesha kuwa Msikiti wa Madiynah haukujengwa juu ya kaburi lolote kwani Msikiti ulijengwa mwaka wa kwanza wa Hijrah (mwaka wa Kiislamu) na wakati huo Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) akiwa hai.

Pia haikushuhudiwa kuwa Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) aliwahi kumzika yeyote katika Maswahaba zake katika Msikiti.

Tatu, Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) hakuzikwa ndani ya Msikiti, na yeye mwenyewe alikemea hilo la kuzika watu Misikitini kwa kusema katika Hadiyth iliyosimuliwa na ibn Masuud (Allaah amuwie radhi) kuwa,

Hakika miongoni mwa viumbe waovu ni wale ambao kitafika Qiyamah hali ya kuwa wapo hai na wale ambao wameyaweka makaburi Misikitini (wamezika watu ndani ya Misikiti).[31]

Maswahaba ni mfano bora wa kuigwa kwani wao waliyazingatia vilivyo na kuyafanyia kazi maneno na mafunzo ya Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake), kiasi waliweza kufikia kutoa mali zao na nafsi zao kwa ajili yake. Unaweza kujiuliza, inawezekana kweli watu hawa (Maswahaba) wakakiuka maelekezo ya Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) na hatimaye wamzike Msikitini?Kama hawakumzika Msikitini, je ni nani aliyeliingiza kaburi la Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) Msikitini, na wapi lilikuwa kabla?

Jawabu ni kuwa aliyeliingiza Msikitini kaburi la Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) ni Umar bin Abdil-Aziyz kwa amri ya mtawala wa zama hizo aitwaye Al-Waliyd bin Abdil-Malik katika mwaka wa 88 H.

Inafahamika kuwa nyumba ya Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) ilikuwa inapakana na Msikiti kwa kutengwa na ukuta mmoja upande wa kushoto na hasa chumba cha Bibi Aaishah (Allaah awe radhi naye) ambacho ndiko alikozikwa Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake), pamoja na Maswahaba zake wawili, Abu Bakr na Umar (Allaah awawie radhi wote wawili). Baada ya Msikiti kupanuliwa, makaburi hayo yakaingia/yakaingizwa Msikitini, na hii ni kwa sababu Al-Waliyd bin Abd-l-Malik alikuwa hana elimu juu ya hilo. Baadhi ya wafuasi wa Maswahaba (Taabiiyn) walipojaribu kulipinga hilo walionekana hawana kauli. Miongoni mwao ni Saiyd bin al-Musayyib, yeye alijaribu kushauri kuwa basi chumba cha Bibi Aaishah (Allaah awe radhi naye) (mke wa Mtume), ambako alizikwa Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) kisiingizwe ndani ya Msikiti, bila mafanikio. Kwa kuwa Al-Waliyd alikuwa ndiye mwenye mamlaka, akamlazimisha Umar bin Abdil-Aziyz kubomoa ukuta uliokuwa unatenganisha makaburi hayo na Msikiti na kwa hiyo makaburi yakajumuishwa ndani ya Msikiti. Kwa ufafanuzi huu mfupi, ni wazi kuwa hakuna hoja ya kudai kuwa inafaa kuzika au kujengea makaburi.[32]

 

Kuwekea Alama Makaburi

Je, ni namna gani unaweza kulitambua kaburi au kuliwekea alama kaburi? Hilo linajibiwa katika Hadiyth iliyosimuliwa na Swahaba mtukufu Al-Muttwallib bin Abi Wadaa (Allaah amuwie radhi) kuwa, pindi alipokufa Uthmaan bin Madhuun, ndugu wa Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) kwa kunyonya ziwa moja, baada ya kumaliza kufukia kaburi, Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) alibeba jiwe na akaliweka upande wa kichwani kisha akasema,

Nimeliweka jiwe hili ili nipate kulijua kaburi la ndugu yangu na nizike pembeni yake atakayekufa katika jamaa zangu[33]

 

Baada Ya Kuzika

Ndugu msomaji, kinachofuatia baada ya kufunika kaburi ni kukaa kwa ajili ya kuwakumbusha waliohudhuria mazikoni, kama alivyofanya Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) katika Hadiyth ya Al-Baraa bin Aazib iliyopokelewa na Jamaah.[34]

Fahamu kuwa hakuna kitu kinachoitwa talaqini baada ya maziko, kwani mapokezi juu ya jambo hilo ni dhaifu na hayakusihi kabisa. Hadiyth inayozungumzia talaqini ni dhaifu na haifai kuitumia katika hoja, na yeyote anayefanya talaqini anahesabika kuwa ni mzushi[35].

 

Mtume (Rehma Na Amani Ya Allaah Ziwe Juu Yake) Alikuwa Akifanya Nini Alipomaliza Kuzika?

Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) akishamaliza kuzika (yaani baada ya kufukia kaburi) alikuwa akisimama na kisha husema maneno haya:

Muombeeni msamaha ndugu yenu na mumuombee uthabiti, kwani hakika sasa hivi anaulizwa maswali[36] kama ilivyokuja katika Hadiyth ya Uthmaan bin Affaan.

 

Pia ifahamike kuwa, haifai kwa Muislamu kuzikwa katika makaburi ya wasiokuwa Waislamu, wala wasiokuwa Waislamu kuzikwa katika makaburi ya Waislamu[37].

 

Kufikia hapa mpendwa msomaji, tunataraji kuwa, kwa mapenzi ya Allaah, utakuwa umefahamu, japo kwa ufupi, ukweli kuhusu mazishi sahihi ya Kiislamu.

 

Tunataraji pia kuwa, utakuwa umebaini uzushi na uongo kuhusu mazishi ya Kiislamu. Utaufahamu uongo huo pale utakapoona au kusikia watu wanasema au kufanya kinyume na haya tuliyoeleza, halafu yakawa hayana ushahidi, au ushahidi upo lakini ni dhaifu.

 

Tukupe changamoto ndugu msomaji, pindi ikitokea unahudhuria muhadhara wake, fanya kumuomba akupe ushahidi kutoka katika Qur-aan au katika Hadiyth za Mtume, kama ambavyo tumekuwa tukibainisha katika makala hii. Hapo ndipo utakapogundua hila yake yeye pamoja na wengine wanoupaka matope Uislamu.

 

Fahamu pia kuwa, ibada yoyote utakayoona inafanywa na Muislamu lazima iwe na uthibitisho kutoka kwa Mtume (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake), kinyume chake huo utakuwa ni uzushi katika dini.

 

Tunamuomba Allaah Ajaalie Makala hii iwe chachu ya Waislamu kuipenda dini yao na kujifunza na kuyatekeleza yaliyo sahihi katika dini.

 

Tunamuomba Allaah Atusamehe madhambi yetu na walio kufa kabla yetu katika Imani.

 

Na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi.

 

   

  

[1] Sunnah ni matendo aliyoyafanya Mtume Muhammad (Rehma na amani ya Allaah ziwe juu yake) au aliyoyashuhudia yakifanywa.

[2] Aina ya majani yanayochanganywa katika maji

[3] Al-Bukhaariy (3/99-104), Muslim (3/47-48), Abuu Daawuud (2/60-61), An-Nasaaiy (1/266-267)

[4] Shaykh Al-Albaaniy katika Ahkaamul Janaaiz uk. 48, Shaykh Bin Uthaymiyn katika Min Ahkaam Al-Fiqhiyah, uk. 68.

[5] Kutawadha (Wudhuu) ni utaratibu maalum wa kuosha viungo vya mwili, viganja vya mikono, kusukutua, kusafisha pua, kuosha uso, kuosha mikono miwili mpaka vifundoni, kupaka maji kichwani na kusafisha masikio, kuosha miguu miwili mpaka kwenye kongo za miguu, pale Muislamu anapotaka kutekeleza ibada yoyote maalum.

[6] Shahidi ni mtu aliyekufa katika Jihaad, vita takatifu ya kuupigania Uislamu. Kujilipua kwa kujitoa muhanga haifai katika Uislamu na anayekufa katika hali hii si shahidi, wala si katika Jihaad kujihusisha na vitendo vya kigaidi.

[7] Maswahaba ni wafuasi wa mwanzo waliomkubali Mtume na ni wa mwanzo kuukubali na kuueneza Uislamu.

[8] Al-Bukhaariy 3/165, An-Nasaaiy 1/277,

[9] Alizaliwa nchini Saudi Arabia sehemu iitwayo Unayzah tar. 27 Ramadhaan 1347H na kufa 15 Shawwal 1421H.

[10] Fataawa Arkaanil Islaam uk. 406.

[11] Imepokelewa na Jamaa: Abuu Daawuud 2/176, At-Tirmidhiy 2/132, na wengineo kama Bin Maajah, al-Al-Bayhaqiy na Al-Haakim.

[12] Imepokelewa na maimamu sita na Al-Bayhaqiy na Ahmad katika Hadiyth namba, 93. Imesahihishwa na Al-Albaaniy.

[13] Nisbur Raayat 2/258

[14] Al-Albaaniy katika Ahkaamul Janaaiz uk 64 chapa ya Beirut ya mwaka 1406H sawa na 1966AD.

[15] Talbiyah ni matamshi maalum ayasemayo anayehiji wakati wa kuhiji.

[16] Abuu Daawuud 2/166, Bin Hazm 5/158, Ahmad 6/267 na wengineo.

[17] Muslim 9/55, An-Nasaaiy 1/476, Tazama pia kitabu Ahkaamul-Janaaiz uk. 80 82.

[18] Ahkaamul Janaaiz Uk. 123.

[19] Muslim 2/208, Abu Awaanah ameisahihisha, 1/396.

[20] Ahlus Sunnah: Waislamu wenye kufuata mafundisho ya Uislamu kulingana na Qur-aan, Sunnah, na (wakafuata njia ya) ufahamu na walivyouelewa Maswahaba na wafuasi wao kutoka katika watangulizi wetu wema.

[21] Ahkaam uk. 131 katika maandishi madogo chini ya ukurasa.

[22] Qiblah ni muelekeo ambao Waislamu huelekea wanapokuwa wanaswali au kuchinja, nao ni mwelekeo ulipo mji mtukufu wa Makkah.

[23] Ahmad 2/427,528,532

[24] Abu Shaamah katika kitabu Al-Baaithu alaa inkaari al-Bidah uk. 67

[25] Qur-aan 8:75

[26] Al-Haakim na ameipa daraja ya Hasan katika Ahkaam uk 152.

[27] Shibri ni kipimo cha kiganja kimoja

[28] Ibn Hibbaan katika sahifa yake uk.2160, Al-Bayhaqiy 3/410, na isnadi ya Hadiyth ni hasan (nzuri).

[29] Amepokea Imam Al-Haythamiy katika Majmu Az-Zawaaid 3/61 na amesema wapokezi wa Hadiyth hii ni waadilifu.

[30] Ikhtiyaarat al-Ilmiyya uk. 25

[31] Ibn Uthaymiyn katika Fataawa uk. 302. Ahmad 1/405-435.

[32] Fataawa uk. 301

[33] Abu Daawuud 2/69, Al-Bayhaqiyy 3/412, Ahkaam uk. 155.

[34] Ahkaam uk. 156 - 159

[35] Tazama kitabu Zaadul-Maaad cha bin-al-Qayyim 1/206, tazama pia kitabu Subulus Salaam cha Imaam Asw-Swanaaniy 2/161.

[36] Abu Daawuud 2/70, Al-Haakim 1/370, na Adh-Dhahabiy ameikubali.

[37] Ahkaam uk. 136